Rais wangu salamu kwako.
Rais wangu, kusema kweli umeniangusha sana na umezidi kuondoa imani yangu kwako. Swali ninalokuuliza: Je, na mwezi huu wa nne utapokea mshahara kama watumishi wengine?
Nimeuliza swali hilo kwakuwa bila ya kuhadaa wala kubwabwaja umenifanya mimi pamoja na Watanzania wengi kukumbwa na majonzi kwa tunayoyaona na kuyashuhudia. Nalia kwa huzuni kubwa na nina mashaka makuu na kesho yangu pamoja na ya wenzangu.
Nakumbuka siku unaondoka Dar kwenda mkoani ukiwa Dodoma ulituambia tusitishane, tuchape kazi, tena ukasema kaugonjwa haka wala siyo tunavyokachukulia. Ni mwepesi kuliko malaria na UKIMWI. Baada ya kauli yako hiyo unajua ni nini kilitokea? Wasaidizi wako walianza kuyaishi yale uliyosema, hawakujiandaa kuchukua hatua. Wakatuzodoa kuwa Corona si chochote wala lolote. Sasa tunalia!
Pengine ungekuwa na kauli tofauti na ile hali ingekuwa tofauti Rais wangu. Pengine ungechukua tahadhari za kimamlaka kama mkuu wa nchi hali ingekuwa tofauti Rais wangu. Lakini ulipuuzia na kutoa kejeli zilizovuka mpaka juu ya ugonjwa huu. Sasa tunalia watu wako.
Ninalia nikishuhudia misafara ya ambulance kama daladala ndani ya jiji la Dar. Ninalia nikiona leo wenzetu wa mikoani wanatukimbia. Wanatukimbia kwa sababu yako Rais wangu. Wanatukimbia kwakuwa jemedari ulifanya mzaha uliopindukia ukauacha ugonjwa ukolee. Ona leo tumebaki wakiwa tukilia na kuomboleza, kukata tamaa na kumuachia Mungu!
Lakini Rais wangu, wewe uliondoka Dar mapema sana , nachelea kusema uliijua hali halisi. Mbona hukutuambia ukweli? Mbona hukutuweka huru? Umeondoka umetuacha na sasa tunatengwa na ndugu zetu na kuteseka kwa ugonjwa. Ukirudi utatueleza nini hasa? Tutakuamini tena kwa lipi zaidi?
Ninalia baada ya kushuhudia nilichokiona Mloganzila, hospitali imejaa na sasa tunatafuta nyingine! Sijui nayo itajaa? Ninalia maana siijui kesho yangu mimi binafsi hasa ninaposhuhudia watu wakitolewa ndani ya nyumba zao hoi kwa Corona. Kilio changu kinakuwa kizito kwakuwa uzembe uliofanya mwanzoni umeendelea kuufanya hata juzi.
Eti hufungi mipaka kwakuwa unategemewa na nchi zingine! Watu wako waliokupa ajira wana thamani kuliko kitu chochote kile. Chonde chonde, ndiyo waliokufanya sasa unaongea ukiwa na mamlaka. Umeshindwa kutumia mamlaka kutoa amri zitakazookoa walau kwa kiasi fulani watu wako.
Swali langu kwako, mwezi huu utapokea mshahara kama watumishi wengine?