*KCWW RAM/XXV 1438*
Darsa ya Maswali ya Ramadhani, Jumamosi tarehe 29 Ramadhani 1438, sawa na 24 Juni 2017
SWAUMU YA SITA NA DENI LA RAMADHANI
Nimeulizwa kuhusu kufunga Sita, NANUKUU:
Naomba kuuliza, Habib Abdulqadir. Je, inajuzu kwa mtu mwenye deni la Ramadhani kufunga Sita kabla ya kulipa deni lake?
JIBU
BISMILLAH
Naam inajuzu iwapo kuna muda wa kutosha wa kufanya yote hayo mawili, kabla ya kumalizika mwezi wa Shawwal. Hivyo, iwapo mtu anadaiwa siku kadhaa za Ramadhani, tuseme siku 7, na umeingia mwezi wa Shawwali, basi anaweza kulipa deni lake la siku 7 za Ramadhani, na kisha akaendelea kufunga siku Sita, ndani ya Shawwal, na kwa kufanya hivyo, atakuwa amepata thawabu kamili za Hadithi isemayo:
( مَنْ صَامَ رَمَضَانَ ثُمَّ أَتْبَعَهُ سِتًّا مِنْ شَوَّالٍ كَانَ كَصِيَامِ الدَّهْرِ) ، رواه مسلم
“Mwenye kufunga Ramadhani, kisha akafuatiliza kwa siku za Sita katika Shawwali, atapata thawabu za mtu aliyefunga milele.” Riwaya nyengine, “ …thawabu za kufunga mwaka mzima”–maana atakuwa amekamilisha KWANZA kufunga Ramadhani, kisha akafuatiliza kwa swaumu ya siku sita, ndani ya Shawwal. Kwa vile kuna sharti la kukamilisha Ramadhani kwanza, kisha kufuatiliza kwa swaumu ya Sita, basi atakuwa amekamilisha kufunga Ramadhani, kwanza, na kisha kufunga sita ndani ya Shawwal.
Ama ikiwa hakuna muda wa kutosha kufunga Sita, kutokana na wingi wa deni lake halali la Ramadhani, kama kuumwa kwa muda wa siku 25 katika Ramadhani, basi kuna khilafu ndogo. Wapo wanaosema kuwa anatakiwa kulipa kwanza deni lake la Ramadhani, na kisha afuatilize kufunga siku Sita, hata kama itapindukia kuingia mwezi wa mfungo pili–ilimradi ameanza funga ya Sita ndani ya Shawwal, na funga ya Sita iwe ni kawaida yake kuifunga kila mwaka. Venginevyo–yaani kama SI kawaida yake kufunga Sita kila mwaka–basi itakuwa Sita imempita, na asubiri mwakani, in shaa’Allah. Huu ndio msimamo wa wanazuoni wengi sana wenye kuonelea dharura ya kulipa deni la Faradhi haraka iwezekanavyo– wanaona kuwa faradhi haiwezi kucheleweshwa nje ya wakati wake, kwa kufanya kwanza ibada ya kujitolea.
Wanazuoni wengine–na hawa ndio wengi zaidi–wanaona hakuna ulazima wa kulipa deni la Ramadhani mara tu baada ya kumalizika Ramadhani, hivyo, deni la Ramadhani linaweza kulipwa wakati wowote ule, kabla ya kuingia Ramadhani nyengine. Hivyo, hakuna junaha kuanza kufunga Sita, baada ya kumalizika Ramadhani na kuswali Idi, ili aweze kuipata Sita–siyo tu, katika muda wake ndani ya mwezi wa Shawwal–bali pia kwa kuifuatiliza baada ya Ramadhani. Ilimradi udhuru wa deni lake ni udhuru wa kisheria.
Mwenyezi Mungu amesema:
ومن كان مريضاً أو على سفر فعدّة من أيام أخر
(البقرة:185)
_“Na atakayekuwa mgonjwa, au yumo safarini, basi aweke idadi siku nyengine.”_
Mwenyezi Mungu Hakusema: “aweke idadi mara moja”, bali _“siku nyengine”_. Siku nyengine ni siku nyengine yoyote isiyokuwa siku ya Ramadhani. Hivyo, hakuna ulazima wa kulipa mara moja. Huu ndio msimamo unaoungwa mkono na wanazuoni wengi sana.
Hata hivyo, kuna msimamo wa kati na kati, wenye kuunganisha misimamo hiyo miwili: i) Ulipaji wa haraka na ii) Kujaribu kupata fadhila za Sita, bila ya kupoteza fadhila moja dhidi ya nyengine.
Msimamo huo ni ule wa wanazuoni wanaoona kuwa mtu anaweza kukusanya yote mawili hayo, kwa wakati mmoja, kwa kutia nia ya kulipa Ramadhani kwanza, na kisha kuongezea nia ya kufunga sita wakati mmoja. Yaani nia mbili kwa swaumu moja–ilimradi nia ya kulipa faradhi itangulie ili iweze kuibeba nia ya Sunna ya kujitolea. Hakuna khilafu kuhusu kujuzu nia zaidi ya moja, kwa Ibada moja–ilimradi Faradhi ndiyo iwe yenye kubeba Sunna ya kujitolea na SI kinyume chake. Huwezi kutia nia ya kufunga Sita, na kuongezea nia ya kulipa deni la Ramadhani. Haiwezekani. Nyepesi haiwezi kubeba nzito: Faradhi haiwezi kubebwa na Sunna, ila Faradhi inaweza kubeba Sunna.
Ndiyo maana, ukiingia msikitini ukakuta watu wanaswali jamaa swala ya Faradhi, basi huwezi kuanza kuswali Sunna ya Qabliyya ya faradhi hiyo, wala huwezi kuswali Tahiyyatul-Masjid, ukaacha kujiunga na swala ya faradhi inayoswaliwa jamaa.
Mtume ﷺ amesema, Ikikimiwa Swala ya jamaa hakuna swala nyengine kuswaliwa.” Hivyo, ni budi ujiunge na Swala hiyo ya Jamaa. Ila ukipenda, unaweza kuongezea nia ya Tahiyyatul-Masjid, na vile vile nia ya Qabliyya ya swala hiyo, baada ya nia kuswali faradhi hiyo jamaa; na hapo utakuwa umepiga ndege watatu kwa jiwe moja. Umeswali Faradhi, umeongezea nia ya Tahiyyatul-Masjid, na nia ya Qabliyya ya faradhi hiyo. Hakuna khilafu katika hilo. Vivyo hivyo basi, kuhusu Swaumu ya faradhi na swaumu ya kujitolea. Deni la Ramadhani linaweza kubeba Sunna ya kujitolea ya Sita, pamoja na Sunna ya kujitolea ya Siku nyeupe–endapo utataka kulipa deni la Ramadhani, katika masiku meupe, ndani ya Shawwal. Hakuna junaha.
والله أعلم وبالله التوفيق
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
**********
2. Naomba kuuliza Sharif wangu. Mimi nina kawaida ya kufunga kila Jumatatu na Alhamisi. Je, naweza kufunga Sita ndani ya funga yangu ya Jumatatu na Alhamisi, na nikapata fadhila zote mbili: Fadhila za kufunga Jumatatu na Alhamisi, na fadhila za kuzifunga siku hizo ndani ya Shawwal? Shukran.”
JIBU
BISMILLAH
Naam unaweza. Hakuna junaha. Zote hizo ni Sunna za kujitolea. Moja ni Sunna ya majira–Sita katika Shawwal, na nyengine ni Sunna ya masiku–Jumatatu na Alhamisi: Zinabebana. Lau kama una kawaida vile vile ya kufunga masiku meupe–tarehe 13, 14 na 15 za kila mfungo, na swaumu zako zinaingiliana katika siku hizo ndani ya Shawwal, basi unaweza kupata fadhila za swaumu zote hizo–kwa pamoja–kwa nia ya swaumu zote tatu kwa kila siku husika. Hakuna junaha. Na hii ndiyo faida kubwa ya kudumisha ibada ya kujitolea. Ukidumisha ibada ya kujitolea, ukatokewa na udhuru usiweze kuitekeleza katika wakati wake, basi unapata thawabu kana kwamba umeitekeleza katika wakati wake. Na papo, iwapo unataka kuchelewesha kufunga Sita, hadi kuanzia siku nyeupe ndani ya Shawwal, na ikawa ndani ya siku hizo mna siku za Jumatatu na Alhamisi, basi hakuna junaha kuanza kufunga Sita katika masiku hayo, na hivyo unapiga ndege watatu kwa jiwe moja. Maqbuul in shaa'Allah.
والله أعلم وبالله التوفيق
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
**********
3. Alhabib naomba kuuliza: Je, mwenye kufunga Sita kisha akafungua katikati ya siku, anawajibika kulipa? Akiwajibika kulipa, je kuna fidia au kafara ya kutoa?
JIBU
BISMILLAH
Swaumu ya kujitolea haina wajibu kulipwa, ndiyo maana ikaitwa Sunna ya kujitolea. Lakini hakuna junaha iwapo umefungua kwa udhuru kuilipa siku nyengine, kwa kufunga tu, pasi na kuweko fidia wala kafara. Huo ndio msimamo wa jumhuri ya wanazuoni.
Hadithi ifuatayo inafafanuwa vizuri zaidi:
عن عائشة رضي الله عنها قالت : ( أهدي لي ولحفصة طعام وكنا صائمتين فأفطرنا ثم دخل رسول الله صلى الله عليه وسلم فقلنا له يا رسول الله إنا أهديت لنا هدية فاشتهيناها فأفطرنا فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم : لا عليكما صوما مكانه يوما آخر ) رواه أبو داود 2457 ، والترمذي 735
Imepokewa kutoka kwa Bi ‘Aisha رضي الله عنها akisema: Tulitunukiwa zawadi ya chakula, mimi na Hafsa, na tulikuwa tumefunga. Basi tukafungua. Baadaye akarudi nyumbani Mtume ﷺ tukamwambia, “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Tuliletewa chakula, tukakipenda, basi tukafungua kwa kukila!” Mtume ﷺ akasema, “Hakuna junaha juu yenu. Fungeni siku nyengine badala yake.” Ameipokea Abu Daud na At-Tirmidhi.
Fidia ni kwa kutoweza kutimiza wajibu, na kafara ni adhabu ya kuvunja sharia, kwa makusudi. Mwenye kufungua swaumu ya kujitolea, hakuvunja jukumu la kutekeleza wajibu, na wala hakuasi kwa kuvunja sharia. Isipokuwa ni makuruhu kufungua–pasi na sababu ya msingi–swaumu ya kujitolea. Ni sawa na kujitolea mbele ya Mwenyezi Mungu kisha ukatoweka na kuacha kujitolea kwako Kwake! Kama una sababu ya msingi, basi hakuna junaha, unaweza kufunga siku nyengine iwapo swaumu hiyo si swaumu ya tarehe maalumu, kama ‘Arafa, au ‘Ashuura.
والله أعلم وبالله التوفيق
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
Imejibiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim.
NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, na kuweka kwenye FB yako, WhatsApp, na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com