Ramadhan Special Thread

Ramadhan Special Thread

Kugawa Usiku Sehemu Mbili; Tarawiyh Na Qiyaam al-Layl - ´Allaamah Muqbil al-Waadi´iy

 
Kwa hakika masiku yaliyobaki ni machache. Kwa Jicho yakinifu watu wengi wamechoka, na hata idadi ya waswaliji imeanza kupungua. Basi Fahamuni kuwa huenda katika kumi hili na siku hizi zilizobaki mwisho wako ukawa mwema kwa kuupata ule Usiku wenye cheo. Hivyo jihimize umalize kwa nguvu kama ulivyoanza kwa nguvu. Ubora wa A'amal tunaungalia mwisho wake upoje. Ndio maana tunaambiwa kuna wale ambao huweza kufanya maovu maisha yao yote lakini Qadar ikamtangulia na akarejea kwa mola wake kwa matendo machache ya mwisho yenye ikhlaas na akawa ni katika watu wa peponi. Siku zilizobaki si haba, juzuu kumi unaweza kumaliza, Laylatul Qadr unaweza kuidiriki, Swadaka unaweza kuendelea kutoa. Jiombee zaidi dua na magh**** huku ukiuombea umma zaidi na zaidi upate kuongoka. Tushikane mkono kwa mkono kuitafuta pepo. Pepo ambayo jicho la bin-Adam na Majini hayajapatapo kuiona wala akili kufikiria uhalisia wake haijawahi kamwe. Pepo ambayo Jibreel alipooneshwa aliapa kwa Allaah kumuambia kuwa, hakuna yoyote atakaehadithiwa kuhusu mfanano wa pepo na mtu huyo akaacha kuingia Peponi. Pepo ipo chini ya utiifu, uchaMungu, kujitakasa na Rehma ya Allaah. Ewe Mola wetu, kwa Rehma yako tunakuomba pepo yako tukufu na utuepushe na adhabu ya moto.
Aamiyn...
 
Msijibu wewe na nani?

Hayo mamlaka ya kukataza kujibu umeyatoa wapi?[/QUOTE)
Mimi ni msomi ninaeielewa dini Yangu. Nimetumia kipote cha muda wangu kutafuta ilmu, na kama unapotosha lazima nikuonye. Kama unataka kuleta ubishani mi nakuacha uendelee kutoa maoni yako. ila ujue dini ya kiislamu sio porojo, maoni ya watu, wala sio mabishano ya Mpira. Toa vitu kwa ilmu.....
 
*KCWW RAM/29 1438*

Darasa ya Ramadhani, Jumatatu tarehe 24 Ramadhani 1438, sawa na 19 Juni 2017

WAJIBU WA ZAKA YA FITRI

Zakatul-Fitr ni zaka/sadaka ya lazima inayotolewa baada ya ‎kumalizika Ramadhani, na kuingia tarehe mosi, Shawwaal/Mfungo Mosi: ‎mara tu baada ya kuandama mfungo wa Shawwaal, na hivyo kumalizika ‎Mfungo wa Ramadhani.‎

Inaitwa Zaka ya Fitri, kwa sababu ni Zaka inayotolewa baada ya ‎kufuturu/kumaliza Wajibu wa kufunga Ramadhani. ‎

Kama ilivyokuwa Sijdatus-Sahw, inayo sujudiwa mwisho wa ‎Swala–ni mfano wa raba au fidia ya kusahau kufanya Sunna maalum ndani ‎ya Swala, basi na Zakatul-Fitri ni kitakaso cha vijimakosa vidogo vidogo ‎vya Saumu, vilivyochumwa kwa kujua au kutokujua wakati wa kufunga ‎Ramadhani. Yaani ni kirekibisho cha palipoharibika kidogo katika Swaumu.‎

Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas ‎رضى الله عنهما‎ akisema: ‎Amesema Mtume ‎ﷺ‎,
زكاة الفطر طهرة للصائم من اللغو والرفث وطعمة للمساكين. فمن أداها فبل الصلاة فهي ‏زكاة مفبولة ومن ‏أداهابعد الصلاة فهي صدقة من الصدقات (رواه أبو داؤد ,ابن ماجه والدار قطنى)‏

‎“Zaka ya Fitri ni kitakaso cha aliyefunga kutokana na mambo ya ‎upuuzi na maneno machafu, na ni lishe kwa masikini. Hivyo, atayeitoa ‎kabla ya Swala, itapokewa kama Zaka, na atayeitoa baada ya Swala basi ‎ni sadaka kama sadaka yoyote ile nyengine.”‎

Wanachuoni wa Fiqh, huielezea na Zaka ya Fitri kwamba:‎

‏ زكاة الفطر: ‏صدقة معلومة بمقدار معلوم، من شخص مخصوص، بشروط مخصوصة، ‏عن ‏طائفة مخصوصة، لطائفة ‏مخصوصة، تجب بالفطر من رمضان، طهرة للصائم: ‏من اللغو، ‏والرفث، وطعمة للمساكين، ‏

‎“ Zaka ya Fitri ni Sadaka ya wajibu maalumu, ya kiwango ‎maalumu, ‎‏kutoka kwa mtu maalumu, kwa masharti maalumu, kwa niaba ya ‎watu maalumu, kupewa watu maalumu, kwa lengo maalumu, nalo ni ‎Kikataso cha Swaumu na chakula kwa masikini.”‎

Zaka ya Fitri imefaradhishwa mwezi wa Shaabani, mwaka wa pili ‎Hijriyya, kama ‎kitakaso cha mwenye kufunga Ramadhani.‎

Zaka ya Fitri imethibiti kwa Qu’aani na Sunna ya kauli na vitendo. ‎

Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالى‎ amesema, kwa wenye kujitakasa nafsi ‎zao kwa kutoa sadaka:
‎قَدْ أَفْلَحَ مَنْ تَزَكَّى* وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّى * بل تؤثرن الحياة الدنيا * ‏واللآخرة خير وأبقى

‎“ _Hakika amekwishafaulu aliyejitakasa na akakumbuka kutaja Jina la Mola ‎wake na akaswali. Ila ‎nyinyi mna hiari maisha ya dunia! Na ya Akhera ni ‎bora na yenye kudumu zaidi._” (Al-A‘la 87:14-15).‎

Wamesema Imam At-Tabari, Ibn Kathir na wengine, kuwa Sa‘id bin Al-‎Musayyib na ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziz (khalifa) na maswahaba wengine ‎wamesema Aya hizo zinazungumzia Zakatul-Fitr. _Tafsir At-Tabari_ 24/374, pia _‎Muswannaf ‘Abdurrazaaq,_ Hadithi [HASHTAG]#5795[/HASHTAG].‎

Kwa upande wa Sunna:‎

Zimepokewa kutoka Mtume ‎ﷺ‎ Hadithi mbali mbali kuhusu wajibu ‎wa Zaka ya Fitri. Miongoni mwa Hadithi hizo ni:

‎1. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar ‎رضي الله عنهما‎ akisema: ‎Amefaradhisha Mtume ‎ﷺ‎ Zakatul-Fitr juu ya binaadamu, katika Mwezi wa ‎Ramadhani. Nayo ni pishi moja ya tende au shayiri kwa kila mja, awe huru ‎asiwe huru (mtumwa) mwanamume au mwanamke, miongoni mwa ‎Waislamu.” _Muttafaq ‘alayhi_.
‎2. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar ‎رضي الله عنهما‎ akisema: ‎‎Amefaradhisha Mtume ‎ﷺ‎ Zakatul-Fitr katika Mwezi wa Ramadhani, nayo ‎ni pishi moja ya tende, au pishi moja ya shayiri, juu ya mja aliye huru, ‎mwanamume au mwanamke, mkubwa au mdogo, miongoni mwa Waislamu. ‎Na akaamrisha itolewe kabla ya watu kwenda kuswali Swala ya Idi.” ‎Ameipokea Bukhari.‎

Hivyo, Zaka ya Fitri ni Zaka ya kiwiliwili SI zaka ya Mali. Inatolewa ‎kutakasa nafsi ya mja na kuisafisha, hata kama haina makosa au uchafu. ‎Na hiyo inamaanisha ni wajibu kutolewa kwa kila kiumbe Mwislamu, hata ‎aliyezaliwa leo, mwamume au mwanamke, mdogo au mkubwa, ‎muungwana au mtumwa.
3. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas ‎رضي الله عنهما‎ akisema: ‎Amefaradhisha Mtume ‎ﷺ‎ Zakatul-Fitr kuwa ni kitakaso cha Swaumu ‎kutokana na makosa madogo madogo na mambo machafu, na kuwa ni ‎chakula kwa masikini. Hivyo basi, atayeitoa kabla ya Swala (ya Idi), Zaka ‎yake ya Fitr itakubaliwa, lakini atayeitoa baada ya Swala (ya Idi) basi hiyo ‎itakuwa ni sadaka tu kama sadaka yoyote nyengine.” Ameipokea Abu Daud.
‎4. Imepokewa kutoka kwa Abu Sa‘id Al-Khudriyy ‎رضي الله عنه‎ ‎akisema: Tulikuwa tukitoa sadaka ya Zakatul-Fitr (wakati wa Mtume ‎ﷺ‎) ‎pishi moja ya chakula, au shayiri, au pishi moja ya tende, au pishi moja ya ‎samli, au pishi moja ya zabibu.” _Muttafaq 'alayhi_. Na imepokewa vile vile na ‎Tirmidhi, Nasaa'i, Ibn Maajah, Abu Daud na Ahmad. ‎

*UFAFANUZI*

Zaka ya Fitri ni wajibu kwa kila nafsi ya Mwislamu anayetweta–yaani anaepumua. Ni Zaka ya kiwiliwili, si Zaka ya mali. Hivyo, midhali kiwiliwili ‎kipo basi lazima kitolewe Zaka ya Fitri. Ni wajibu. Ni Faradhi. Haiepukiki, ‎isipokuwa kwa yule ambaye hana uwezo kabisa. Hapo ‎لايكلف الله نفسا إلا وسعها‎.‎

Ama mwenye kipato, au mwenye wajibu wa kumtunza mtu mwengine, ‎kama mke, watoto, wazazi wake wawili wasiojiweza, watumishi wa ‎nyumbani na kadhalika, na kipato chake kikawa kinazidi wajibu wake wa ‎kuwatunza anaowatunza, basi ni wajibu KWAKE kujitolea yeye mwenyewe, ‎kwanza, na kisha kuwatolea wote wale anaowajibika kuwatunza, kwa hali na ‎mali. Yaani, lazima awe na chakula cha ziada ya kula yeye na familia yake, ‎siku ya Idi. Hicho kitachozidi ndicho kinachotolewa Zaka ya fitri. Kikiwa ‎hakitoshi kulisha familia yake hiyo siku ya Idi, basi hana jukumu la kutoa ‎Zaka ya Fitri.‎

Kwa maneno mengine, iwapo baba mwenye nyumba ni masikini, hana ‎cha kumtosha yeye na familia yake siku ya Idi, basi huyo hana wajibu wa ‎kutoa Zaka ya Fitri. Wala hana wajibu wa kumtolea mkewe, hata kama mke ‎huyo ni mwenye uwezo kutokana na kipato chake mwenyewe. ‎

Lakini mke mwenye kipato chake mwenyewe, anaweza kujitolea ‎kumtolea mumewe na watoto wake akipenda. Maana hana wajibu wa ‎kujitunza, wala kumtunza mumewe wala watoto wake. Ni hiari yake, na ni ‎fadhila kubwa, sana, kufanya hivyo. Ila SI wajibu juu yake. ‎

Zaka ya Fitri ni chakula, SI pesa. Na kiwango cha kutolewa ni ‎pishi moja ya chakula kinacholiwa sana katika jamii husika. Hivyo, vyakula ‎vinavyoingia hapa ni nafaka zote, kuanzia ngano, shayiri, mchele, unga wa ‎ngano, sembe, maharage, ulezi, nk. Ni chakula kinacholiwa sana ‎na watu wengi katika jamii ya mtoa Zaka hiyo.‎

Kiwango cha Zaka ya Fitri ni pishi moja, ambayo ni sawa na kilo mbili ‎na gram 400; kwa pishi ya Mtume ‎ﷺ‎ (ambayo ni sawa na vibaba ‎vine vya Mtume ‎ﷺ‎, na kibaba kimoja ni ujazo wa nafaka kwenye viganja ‎viwili–kwa pamoja–vya mtu wa kawaida). Hivyo, ni kama kilo mbili na ‎nusu za chakula kinachopendwa sana na jamii husika. Kiwango hicho ni kwa ‎kila kiumbe chenye uwezo wa kujitolea chenyewe. ‎

Iwapo hakina uwezo basi ni juu ya mwenye jukumu la kumtunza ‎kiumbe huyo, ilimradi ana uwezo wa shibe yake na shibe za watoto wake ‎wote, siku ya Idi. Kitachozidi ndicho kitachotolewa Zaka. Kama hakitoshi, ‎basi akigawe kwa utaratibu aliouweka Mtume ‎ﷺ‎ kama ifuatavyo: ‎

عن جابر رضي الله عنه قال قال رسل الله صلى الله عليه وسلم: ((ابدأ بنفسك فتصدق عليها، فإن ‏فضل شيء فلأهلك، فإن فضل عن أهلك شيء فلذي قرابتك، فإن فضل عن ذي قرابتك شيء فهكذا ‏وهكذا)) يقول: فبين يديك، وعن يمينك، وعن شمالك.(رواه مسلم) ‏

‎“Anza kujitolea mwenyewe. Kikizidi kitu watolee watu wako wa nyumbani ‎‎(anza na mke, kwanza, kisha watoto). Kikizidi kitu, watolee ndugu na jamaa ‎zako (anza na ndugu na jamaa wa karibu, kisha wa mbali). Kikizidi basi ‎watolee wa huku na huko, na kule na hapa (walio karibu zaidi nawe na ‎ambao si watu wa ukoo wako, kama majirani wa karibu).” Ameipokea ‎Muslim. ‎

*SUNNA ZA KUTOA ZAKA YA FITRI*

a) Kuitoa mara baada ya kuandama mwezi wa Shawwaal–yaani usiku wa ‎kuamkia Sikukuu, au kabla ya kwenda kuswali Swala ya Idi, au siku moja au mbili kabla ya kumalizika Ramadhani.
b) Kumtolea hata mtoto aliye tumboni, kama alivyokuwa akifanya ‎Sayyidina ‘Uthman bin ‘Affaan ‎رضي الله عنه‎. Ameipokea Ahmad na Ibn Abi ‎Shayba.
c) Kuigawa kwa mikono yako mwenyewe, badala ya kuwapa watu ‎wengine waitoe kwa niaba yako. Mtume ‎ﷺ‎ alikuwa akifanya hivyo, na ‎kuwausia Maswahaba nao wafanye hivyo.
d) Ukiwapa watoto wako nyumbani kuitoa, ni sawa na kuigawa ‎mwenyewe.
e) Kuwapa masikini jamaa zako, wenye kustahiki na ambao huna wajibu ‎wa kuwatunza.
f) Kuigawa kwa masikini wa mahali ulipo, ila ikiwa kuna wanaohitaji ‎zaidi, na ni jamaa zako, nchi nyengine.
‎g) Iwapo chakula unachotoa kina viwango mbali mbali, basi chagua ‎kiwango cha juu: Mwenyezi Mungu amesema: _“Hamtaipata Pepo ‎mpaka mtoe mnavyovipenda.”_
h) Kutoa nafaka kavu, inayoweza kuhifadhika kwa siku kadhaa bila ya ‎kuharibika, ni bora kuliko chakula kisichoweza kuhifadhika kwa ‎muda mrefu.
i) Kwa upande wa Wazazi wako wawili, ni Sunna kumtolea Mama ‎mzazi kwanza, kisha ndiyo Baba mzazi–iwapo wanakutegemea ‎kuwatunza.
j) Kuwapa majirani zako masikini, ni bora kuliko masikini wa mbali.‎

*YALIYOMO NA YATOKANAYO*

Kutokana na Aya za Qur’aani na Hadithi za hapo juu, maulamaa wema ‎waliotutangulia wamefafanua YALIYOMO NA YATOKANAYO kama ‎ifuatavyo:

‎1. Zakatul-Fitr ni wajibu, kwa kila mwenye kuweza, na ambaye ana ‎chakula cha ziada ya chakula chake cha Sikukuu ya mwanzo.
‎2. Asiye na uwezo, na ambaye yumo chini ya kukimiwa na mtu ‎mwengine, kama vile Baba mzazi, au hata mlezi wake tu, basi wajibu ‎wa kutolewa upo juu ya mabega ya mwenye kumkimu. Kwa maana ‎hiyo, Mume anamtolea mkewe, watoto wake, wazee wake–iwapo ‎wamo chini ya himaya yake–mtumishi au watumishi wake, bila ya ‎kujali umri au jinsia. Hata mtoto aliyezaliwa saa moja kabla ya ‎kuandama mwezi wa Shawwaal, anapaswa kutolewa sadaka ya Zakatul-Fitr.
‎3.‎ Zakatul-Fitr ni Zaka ya kutakasa mwili wa aliyefunga, kwa upande ‎mmoja, na hata asiyekuwa na wajibu wa kufunga, kwa upande wa pili, ‎ilimradi umeingia Mwezi wa Rehema na yeye yupo hai. Kwa maana ‎hiyo, Zakatul-Fitri ni Zaka ya NAFSI, SI ZAKA ya mali. Ndiyo maana inampasa kila mtu, mwanamume kwa mwanamke, ‎mdogo kwa mkubwa, muungwana na asiye muungwana.
‎4. Zakatul-Fitr inapaswa kutolewa kwa aliyoko karibu na aliyoko mbali, ‎ilimradi matunzo yake yapo juu ya mabega ya mzee wake. Hivyo, ‎mwanafunzi anayesoma ugenini–na anayetunzwa na wazee wake–‎anapaswa kutolewa Zaka yake ya Fitri.
‎5. Zakatul-Fitr ni mfano wa Sijdatus-Sahw kwenye Swala. ‎Imefaradhishwa ili kuziba mapengo yatayotokea, bila ya kujua, wakati ‎wa kufunga mwezi wa Ramadhani, kwa aliyefunga, au makosa ‎madogo madogo mengine, kwa aliyeruhusiwa kutokufunga–yaani ‎makosa madogo madogo yanayoweza kuchumwa katika mwezi wa ‎Ramadhani. Kwa lugha nyengine ya kisasa: Zakatul-Fitr ni RABA ya ‎kufuta makosa madogo madogo.
‎6. Kwa maana hiyo, Zakatul-Fitr anatolewa vile vile mtumishi Mwislamu, ‎kwa vile wajibu wa Swaumu upo juu yake kama Mwislamu yeyote ‎mwengine. Ama asiyekuwa mwislamu hatolewi Zakatul-Fitr, maana ‎wajibu wake kwanza, ni kuwa Mwislamu kabla ya kuanza kufunga.
‎7. Inaitwa Zakatul-Fitr kwa sababu ni Sadaka iliyokusudiwa kumlisha ‎masikini katika siku ya Idi. Yaani ni Zaka ya kumsaidia masikini ‎aweze kufungua kinywa Sikukuu ya Idi, na afurahike kama wanavyofurahika Waislamu wenziwe wenye kujiweza.
‎8. Kutokana na sababu hiyo kuu, ndiyo maana inatakiwa itolewe ‎KABLA ya Swala ya Idi. Na kama itatolewa mwishoni mwa ‎Ramadhani ni bora zaidi. Hivyo, mwezi mzima wa Ramadhani, hadi ‎kabla ya kuswaliwa Swala ya Idi, ni muda halali wa kutoa Zakatul-‎Fitr.
‎9. Kwa vile lengo la Zakatul-Fitr ni kumlisha masikini, basi ‎kinachotolewa ni chakula kinacholiwa sana katika jamii. Hivyo basi, ‎ama ni ngano, shayiri, tende, kitoweo kikuu (samli) na kadhalika. Kwa ‎jamii zetu, ni mchele, sembe, maharage, ulezi nk.
‎10. Kwa sababu kumetajwaa “Kumlisha” au “Chakula” kwa masikini, ‎basi maulamaa wengi, wanashurutisha kutolewa chakula chenyewe na ‎si mbadala wa chakula. Huu ndio msimamo rasmi, wa Imam Shafi, ‎Malik na Ahmad.
‎11. Hata hivyo, Imam Abu Hanifa–na anaungwa mkono na maulamaa ‎wengi kutoka madhehebu zote nyengine–inajuzu kutoa mbadala, yaani ‎thamani ya chakula kikuu cha jamii–maana lengo ni kumwezesha ‎masikini kujipatia chakula siku ya Idi, na siyo kumlazimisha kula ‎chakula kinacholiwa na watu wengi kwenye jamii. Amejenga hoja ‎yake kwamba siku ya Idi, mtu hupenda kula kile ambacho ni nadra ‎kukipata. Hula chakula tunu. Kwa hivyo, anaweza kupewa thamani ya ‎kiwango kinachotakiwa kutolewa.
‎12. Kiwango cha wastani ni pishi moja ya chakula cha kawaida–sawasawa ‎na kilo mbili na nusu.
13. Kwa nchi kama zetu za Afrika ya Mashariki, mchele wa kawaida ‎huuzwa mfuko wa Kilo TANO kwa bei ya baina ya shilingi 10,000 hadi 12,000. Hivyo, kilo mbili na nusu ni sawa na 5000 hadi 6000 ‎kwa kila mtu mmoja (sijui bei za sasa ni kiasi gani. Ila kigezo ni hicho ‎cha mfuko wa kilo tano). Bila ya shaka, bei ya sembe itakuwa ‎tofauti na bei ya mchele, ila kwa vile sembe ni kitu kinacholiwa sana ‎na watu wengi wasiojiweza, na hula wali nyakati za furaha na nadra, ‎basi ni bora kutoa mchele kuliko sembe. ‎

*INAENDELEA …* ‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎
الحقير إلى الله تعلى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka “Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi ‎wa ‎Umma”, kitabu ‎ambacho ni tafsiri kamili ya ‎رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإمام ‏النووي ‏‎ ‎kilichotungwa na Imam An-Nawawi na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili na ‎Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com
 
*KCWW RAM/XX 1438*

Darsa ya Maswali, Jumatatu tarehe 24 Ramadhani 1438, sawa na tarehe 19 Juni 2017

MASWALI YA SWAUMU: ZAKA YA FITRI

Nimekuwa nikiulizwa maswali mengi sana kuhusu Zaka ya Fitri hivi karibuni, na kuwaahidi wasubiri darsa ya Zaka ‎ya Fitri. Leo Darasa ya Zaka ya Fitri imetoka na in shaa'Allah naanza kujibu ‎maswali mbali mbali niliyoulizwa kuhusu Zaka ya Fitri.‎

Nimeulizwa faraghani, NANUKUU: (makosa ya uchapaji–typos–yamesahihishwa)

‎1. Alhabib! Nimesikia kuwa Zaka ya Fitri ni Sunna, si wajibu. Je, ni ‎kweli? Na kama ni Sunna, basi si itakuwa jambo la hiari tu? Naomba ‎ufafanuzi na dalili. Shukran.‎

JIBU

BISMILLAH

Zaka ya Fitri ni FARADHI, si Sunna. Huo ndio msimamo wa ‎wanazuoni karibu wote, kwa sababu ya Hadithi Swahihi mbali mbali, ‎ambazo baadhi yake nimezinukuu katika Darsa yangu ya Zaka ya ‎Fitri. Na katika Hadithi zote hizo, imesemwa wazi wazi kuwa, ‎‎“Amefaradhisha Mtume ‎ﷺ‎ Zaka ya Fitri kwa watu, kwa ajili ya ‎Ramadhani, nayo ni pishi moja ya shayiri kutolewa kwa kila mtu, ‎muungwana au mtumwa, mwanamume au mwanamke, miongoni mwa ‎Waislamu.” _Muttafaq 'alayhi._

KILICHOFARADHISHWA hakiwezi kuwa Sunna. Faradhi maana yake ‎wajibu, lazima, sharti, takalifu, kalifisho: Utake usitake, upende ‎usipende, ilimradi una uwezo wa kuitoa.

Ila, kama kawaida ya mambo kama haya, hutokeza watu wakajaribu ‎kutoa tafsiri zao wenyewe za kutaka kukwepa au kijivua uwajibikaji. ‎Miongoni mwa watu hao ni baadhi ya wafuasi wachache sana, wa ‎madhehebu ya Malik walioishi karne ya nne Hijri, kusema kwamba ni ‎Sunna, wakaungwa mkono na watu wachache kule Iraq, kwa hoja ya ‎kwamba, kuna Hadithi Swahihi kutoka kwa Mtume ‎ﷺ‎ ambayo alikuwa ‎akimfunza Bedui mambo ya dini, ambaye alimuendea kumuuliza ‎mambo mbali mbali ya Dini. Mtume ‎ﷺ‎ akamueleza kuhusu Shahada, Swala, ‎Swaumu, Hija na Zaka. Alipomueleza kuhusu wajibu wa Zaka, na ‎kumaliza, Bedui alimuuliza, ‎‎“Je, kuna ziada isiyokuwa Zaka?”
هل علي غيرها؟
Mtume ‎ﷺ‎ akamjibu, ‎‎“Hapana! Isipokuwa ukijitolea!”
إلا أن تطوع‎.
Hivyo ‎wanadai kuwa Mtume ‎ﷺ‎ amesema wazi wazi katika Hadithi hiyo kuwa ‎‎“Hakuna! Isipokuwa kama utajitolea!” _Muttafaq 'alayhi._

Ni upotovu ‎na upotoshaji!

Bedui alikwenda kuuliza mambo makuu ya Dini, nguzo za Dini, ‎Mambo ya msingi ya Dini. Ndiyo akamueleza kuhusu Nguzo za ‎Uwislamu. Na kila alipoelezwa nguzo moja, kama Swala, au Hija, ‎alikuwa akiongeza kuuliza, “Je, kuna wajibu mwengine zaidi kuliko ‎hilo?” Mtume ‎ﷺ‎ akimjibu, “Hapana! Isipokuwa ukijitolea.”‎

Vivyo hivyo kuhusu Zaka, Hija, na Swaumu. Alikuwa akimfunza ‎Nguzo za Uwislamu. Ndiyo maana yule Bedui alipomaliza alisema ‎kwa kuapa, “Wallahi nitafanya yote hayo, lakini sitazidisha chochote ‎cha ziada.” Akashika njia na kwenda zake.

Mtume ‎ﷺ‎ akacheka na kusema, “Akitenda hayo kama alivyoahidi, ‎basi naam, atafaulu!”

Riwaya nyengine inasema, akasema: “‎Anayetaka kumuona mtu wa peponi, amuangalie huyu!”‎

a) Alikuwa akimfunza utekelezaji wa Nguzo za Uwislamu, maana ‎alianza na Shahada.‎
b) Alikuja kwa nia ya kusilimu.‎
c) Alikuwa akimueleza kuhusu Nguzo ya ZAKA, na hiyo ni zaka ya ‎mali.‎
d) Haikusemwa ilikuwa mwaka gani; kabla au baada ya Zakatul-‎Fitr.‎
e) Maswahaba wote, na waja wema waliowafuatia, wameelewa ‎kuwa Zaka ya Fitri ni WAJIBU. Je, walielewa kimakosa? ‎
Hivyo, ni wazi kuwa si uelewa swahihi hata kidogo.‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

‎********** ‎

‎2. Je, ni wajibu vile vile kumtolea mtoto mchanga ambaye hana ‎wajibu wa kufunga? Maana umesema kuwa ni kitakaso cha kufuta ‎makosa madogo madogo ya Swaumu.‎

JIBU

BISMILLAH

Naam ni kitakaso cha mwenye kufunga, kama alivyosema Bwana ‎Mtume ‎ﷺ‎, ila amesema vile vile katika Hadithi hiyo hiyo kuwa, “Na ‎Chauka (takrima) kwa masikini.” Hivyo, si Zaka ya aliyefunga tu, bali ‎ni Zaka ya utakaso wa mwili na kiwiliwili cha kila Mwislamu, mdogo ‎kwa mkubwa, mwanamume kwa mwanamke, muungwana au ‎mtumwa, ilimradi ni Mwislamu. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar na ‎Ibn ‘Abbaas na Abu Hurayra na Maswahaba wengine kuwa, ‎“Amefaradhisha Mtume ‎ﷺ‎ Zaka ya Fitri, kuwa ni pishi moja ya tende ‎au pishi ya shayiri, juu ya muungwana au mtumwa, mwanamume au ‎mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislamu. Na ‎ameamrisha itolewe kabla ya kutoka kwenda Swala ya Idi.”

Kwa maana hiyo, Zaka ya Fitri ni jukumu juu ya kiwiliwili, dhimmi ya ‎kiumbe aliye hai, anatweta, katika mwezi wa Ramadhani. Hivyo, ‎haina umri, wala jinsia, wala cheo, wala rangi. Kila mwanadamu ‎Mwislamu anapaswa kutoa au kutolewa Zaka ya Fitri, iwapo yeye ‎mwenyewe hana uwezo wa kutoa. Na jukumu hilo linaaanguka juu ‎ya mabega ya mwenye wajibu wa kumtunza na kumuangalia, kwa ‎hali na mali.‎

Ndiyo maana Maswahaba kama Sayyidina ‘Uthman bin ‘Affan ‎رضى الله ‏عنه‎, na wengine, wakasema: Hata mtoto aliye tumboni anatolewa ‎Zaka ya Fitri, maana tayari ni kiumbe tumboni mwa mama yake. Ila ‎wanazuoni wanachukulia hilo kuwa ni jambo jema, yaani Mustahabb ‎‎(Inafaa). Lakini, akizaliwa KABLA ya kuchwa jua la mwezi-‎mwandamo, basi SASA ni wajibu kutolewa Zaka ya Fitri.‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
‎********** ‎

‎3. Je, ni wajibu kumtolea Zaka ya Fitri mwenda wazimu, au taahira?‎

JIBU

BISMILLAH

Naam, ni wajibu kumtolea, ama kutokana na mali yake mwenyewe, ‎iwapo anayo mali, au amerithi mali, au kutolewa na anayemtunza ‎kwa hali na mali. Hakuna kukwepa Zaka ya Fitri. Ikiwa hakuna wa ‎kumtunza, wala kumuangalia, yaani ni mzururaji tu, akiomba omba, ‎basi sasa YEYE ndiye anayetakiwa kupewa Zaka ya Fitri. ‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم ‏‎ ‎

‎********** ‎

‎4. Je, kuna nia maalum kutia wakati wa kutoa Zaka ya Fitri?‎

JIBU

BISMILLAH

Naam ni lazima pawepo nia; maana Zaka ya Fitri ni Ibada, na kama ‎zilivyo Ibada zote, katika Dini, haiwezi kuswihi na kupokelewa mpaka ‎utie nia ya kuifanya Ibada hiyo:
إنما الأعمال بالنيات
Hadithi mashuhuri ‎iliyopokewa na Sayyidina ‘Umar ‎رضي الله عنه‎.

Nia ndiyo inayotofautisha baina ya zawadi na Zaka, baina ya kutoa ‎kitu kwa lengo la kutimiza wajibu wako aliokuwekea Mwenyezi Mungu, ‎na kujionesha au kuonesha wengine kuwa wewe ni mkarimu. Baina ‎ya amali swahihi na amali isiyo swahihi kisheria.

Ila hakuna nia maalum, kwa maana kuomboleza kwa kusema, “Mimi ‎nanuwia kutoa kitu fulani kuwa ni zaka yangu ya Fitri.” Hapana. Nia ‎mahali pake ni moyoni; kuitamka ni utashi wako, hakuzidishi kitu, ‎wala hakupunguzi kitu, katika kusihi amali yako.

Zaidi, siyo lazima kutia nia hiyo pale unapotoa. Inatosha pale ‎unapoenda kununua chakula fulani, kwa nia ya kukitoa kuwa Zaka ‎yako au yenu ya Fitri, basi imetosha, in shaa’Allah. ‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

‎********** ‎

‎5. Nimewaona baadhi ya watu wanapokuwa na chakula cha kutoa ‎Zaka ya Fitri, basi hutia mkono kwenye chakula hicho, au kuweka ‎mkono juu ya chakula hicho na kutia nia kuwa chakula hicho ni Zaka ‎ya Fitri. Je, ni Sunna au wajibu kufanya hivyo?‎

JIBU

BISMILLAH

Ni uzushi wao wenyewe, hauna asili wala fasili katika Dini. Hakuna ‎dalili yoyote kwamba ni sharti uweke mkono wako juu ya chakula ‎cha Zaka ya Fitri, kwa kuamini kwamba kufanya hivyo ndiyo ‎unajisogeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo, haya ni mambo ‎ambayo ni vyema kuyaepuka kabisa, maana ni uzushi mbaya. ‎Mwenyezi Mungu hahitaji kuoneshwa kwa kauli wala kwa kitendo ‎kuwa chakula ulichonacho ndio chakula cha kutoa Zaka ya Fitri. ‎Mwenyezi Mungu anaona na kujua hata yaliyomo na kufichika ndani ‎ya nyoyo. Inatosha nia yako moyoni kuhusu chakula hicho, in shaa’Allah. ‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم ‏‎ ‎

‎********** ‎

‎6. Sharifu! Ninaelewa kuwa Zaka hailazimu kutolewa mpaka ifike ‎nisabu, yaani iwango maalum, na kwa muda maalum. Je, zaka ya ‎Fitri nayo ina nisabu na muda maalumu? Ahsante sana.‎

JIBU

BISMILLAH

Zaka ya Fitri haina kiwango maalum wala kupitiwa na muhula ‎maalum. Kilicho muhimu ni kuwa una chakula cha ziada ya kujikimu ‎wewe na kuwakimu wanaokulazimu, kwa siku ile ya Idi–mchana ‎wake na usiku wake. Kitachozidi lishe yenu kwa siku hiyo kamili, ndicho kinachotolewa Zaka ya Fitri. Kama kilichozidi hakitoshi ‎kuwatolea wote, basi anza kujitolea wewe mwenyewe kwanza, kikizidi, ‎mtolee mkeo, kikizidi watolee watoto wako nk.

Kama hakitoshi, basi kigawe kwa utaratibu aliouweka Mtume ‎ﷺ‎ ‎kama ifuatavyo: ‎
عن جابر رضي الله عنه قال قال رسل الله صلى الله عليه وسلم: ((ابدأ بنفسك فتصدق عليها، فإن فضل ‏شيء ‏فلأهلك، فإن فضل عن أهلك شيء فلذي قرابتك، فإن فضل عن ذي قرابتك شيء فهكذا وهكذا)) يقول: ‏فبين ‏يديك، وعن يمينك، وعن شمالك.(رواه مسلم) ‏
‎“Anza kujitolea mwenyewe. Kikizidi kitu watolee watu wako wa ‎nyumbani (anza na ‎mke, kwanza, kisha watoto). Kikizidi kitu, ‎watolee ndugu na jamaa zako (anza na ‎ndugu na jamaa wa karibu, ‎kisha wa mbali). Kikizidi basi watolee wa huku na ‎huko, na kule na ‎hapa (walio karibu zaidi nawe na ambao si watu wa ukoo ‎wako, ‎kama majirani wa karibu).” Ameipokea Muslim.

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

**********

‎7. Alhabib! Jazaaka Allahu khayran, kwa ilmu unayotupa. Nina swali ‎dogo, ila linanitia wasi wasi mkubwa sana. Mimi nadaiwa. Nimekopa ‎kwa mtu, ananidai. Je, inajuzu kwangu mimi kutoa Zaka ya Fitri, ‎badala ya kulipa deni langu? Yaani siwezi yote mawili. Lazima ‎nichague moja tu. Nifanye nini?‎

JIBU

BISMILLAH

Deni halikuzuwii kutoa Zaka yako ya Fitri, katika siku yake, katika ‎muda wake. Maana Zaka ya Fitri ni Zaka ya nafsi, si Zaka ya Mapato. ‎Ni Zaka ya kiwiliwili. Ndiyo maana wanachuoni wengine huiita: زكاة البدن‎ ‎

Hivyo, ilimradi una CHAKULA cha ziada cha kukutosha wewe na ‎familia yako kula siku ya Idi, kilichozidi kinatolewa Zaka ya Fitri, ‎hata kama una deni la pesa au mali.

Hapa nataka kufafanua jambo moja muhimu sana, ambalo watu ‎wengi hawalielewi au wanalielewa lakini wanalipuuza.

Masikini ambaye hana uwezo wa kutoa Zaka ya Fitri, siku ya Idi, ‎Lakini akapokea Zaka za Fitri za watu wengine kiasi kwamba alicho‎nacho hivi sasa ni ziada ya chakula chake kamili kwa siku ile ya Idi, ‎ANAPASWA kutoa Zaka yake ya Fitri kutoka katika chakula alichonacho cha ziada. Hawezi kujivua wala kujitoa katika uwajibikaji wa ‎kutoa Zaka yake ya Fitri, kutokana na chakula cha ziada alichonacho. Wajibu wa Zaka ya Fitri ni juu ya NAFSI, tajiri au masikini. ‎Hivyo, masikini aliyepokea chakula cha kutosha kwa siku yake ya Idi, ‎yeye na watoto wake, hana budi kutoa Zaka yake ya Fitri, kwa nafsi ‎yake na watoto wake, kutokana na ziada ya chakula alichonacho ‎kwa siku hiyo.

Na wale wasiotaka ‎kujituma hata kidogo–bali kugeuza omba omba kuwa ndiyo KAZI ‎yao–wanapata dhambi kubwa sana. Kwanza, dhambi za kuomba omba ‎‎(Mtume ‎ﷺ‎ amesema: Mwenye kuomba omba kupindukia dharura ya ‎chakula chake cha siku, anaomba makaa ya Moto!) Pili, dhambi za ‎kuomba ziada ya mahitaji yao halisi ya siku moja (ili siku inayofuata ‎wakatafute kibarua cha kujipatia pato).

Hivyo, wasidhani kwamba kwa vile wao ni omba omba basi ‎hawapaswi kutoa Zaka ya Fitri yao na ya watoto wao. Hapana! Ni ‎wajibu. Ni Faradhi watoe Zaka yao ya Fitri, kama mtu yeyote yule ‎mwingine mwenye ziada ya chakula chake cha Siku ya Idi.

Zaka ya Fitri ni wajibu juu ya kila mtu, juu ya nafsi yake, na nafsi za ‎anaopaswa kuwakimu, sawa sawa awe tajiri au masikini, ‎mwanamume au mwanamke, mkubwa au mdogo, muungwana au ‎mtumwa. Hakuna anayevuka. Huna kitu basi huna wajibu. Lakini ‎ukeshapata cha ziada tu, basi wajibu unarudi juu ya mabega yako. ‎Na utapatilizwa kwa kutotoa. ‎

*INAENDELEA …* ‎

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

Imejibiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza ‎chochote, ‎na kuweka kwenye FB yako, WhatsApp, na kwenye ‎Makundi ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha Dini. ‎Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com
 
Kwa hakika masiku yaliyobaki ni machache. Kwa Jicho yakinifu watu wengi wamechoka, na hata idadi ya waswaliji imeanza kupungua. Basi Fahamuni kuwa huenda katika kumi hili na siku hizi zilizobaki mwisho wako ukawa mwema kwa kuupata ule Usiku wenye cheo. Hivyo jihimize umalize kwa nguvu kama ulivyoanza kwa nguvu. Ubora wa A'amal tunaungalia mwisho wake upoje. Ndio maana tunaambiwa kuna wale ambao huweza kufanya maovu maisha yao yote lakini Qadar ikamtangulia na akarejea kwa mola wake kwa matendo machache ya mwisho yenye ikhlaas na akawa ni katika watu wa peponi. Siku zilizobaki si haba, juzuu kumi unaweza kumaliza, Laylatul Qadr unaweza kuidiriki, Swadaka unaweza kuendelea kutoa. Jiombee zaidi dua na magh**** huku ukiuombea umma zaidi na zaidi upate kuongoka. Tushikane mkono kwa mkono kuitafuta pepo. Pepo ambayo jicho la bin-Adam na Majini hayajapatapo kuiona wala akili kufikiria uhalisia wake haijawahi kamwe. Pepo ambayo Jibreel alipooneshwa aliapa kwa Allaah kumuambia kuwa, hakuna yoyote atakaehadithiwa kuhusu mfanano wa pepo na mtu huyo akaacha kuingia Peponi. Pepo ipo chini ya utiifu, uchaMungu, kujitakasa na Rehma ya Allaah. Ewe Mola wetu, kwa Rehma yako tunakuomba pepo yako tukufu na utuepushe na adhabu ya moto.
Ameeen Thumma Ameeen....
Allah aitakab'al dua yako
 
Alipofariki Mtume wetu Muhammad ( s.a.w )
kipenzi cha Allah (SWT)
Maswahaba walipata tabu sana kutangaza msiba
wa
Mtume kwa waislamu, Omar bin Khatab (r.a)
alisema;

"Atakayetangaza kuwa mtume (s a w ) amekufa
shingo
yake halali yangu"

Lakini Aboubakar bin Swidiq (r. a) alisema
maneno
haya ya busara kuwaambia waislamu:-

"Ndugu zangu kama kuna mtu alikua akiswali na
kufanya ibadat mbali mbali kwa ajili ya
MUHAMMAD (s a w ) basi MUHAMMAD
hatunaye
tena,
Lakini kama ulikua ukiswali na ukifanya ibada
kwa ajili ya ALLAH basi ALLAH yuko milele"

FUNZO KWETU;- Kama ndugu yangu umekua
ukifunga na kusali kwa ajili ya mwezi huu
mtukufu wa ( RAMADHANI ) basi Ramadhan hiyo
yaanza kuondoka taratiiibu,

Lakini kama ulikua ukiswali nakufunga kwa ajili
ya kutaka radhi za ALLAH basi ALLAH yupo siku
zote,

Tudumu na tushikamane wote katika kamba
ya mwenyezi mungu hata baada ya
( Ramadhani ) kuisha,huu ni
UKUMBUSHO na ukumbusho huwafaa wenye
kuamini,

Tunamuomba mwenyezi mungu atujalie tuwe ni
wenye kudumu ndani ya swala mpaka mwisho
wa uhai wa maisha yetu Ameeeeen!!!
 
Assalamualaikum,
Ndugu zangu katika Iman ni kwamba Ramadhan inaisha na katika hizi za Ramadhan za mwisho tunajisahau sana. Watu wanaanza kupanga promise na kusahau kwamba tulitoka katika mwezi wa toba.
Nawaasa tujitahd kutunza swaumu zetu tusiziharibu kwa jambo la mara moja.
Inshallah Mungu ataqabbal swaumu zetu, wabillahittawfiiq
 
*﴿ ﺑِﺴْﻢِ ﺍﻟﻠﻪِ ﺍﻟﺮَّﺣْﻤﻦِ ﺍﻟﺮَّﺣِﻴﻢِ ﴾*

*☪ LEO KATIKA FUNGA ☪*
*( 27 )*

*Allah ﷻ Anasema:*

*{إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ}*
*Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.*
-Sura At-Tawbah, Ayah 60
"""""""""""""""""""""""""""""""""""""

*[emoji383]---ﺯﻛﺎﺓ ﺍﻟﻔﻄﺮ--- (٢)[emoji383]*
*---ZAKATUL FITRI--(2)*

*■ TUKIWA TUNAENDELEA NA DARSA YETU KWA NJIA FUPI KABISA INAYO HUSU ZAKATUL FITRI.*


*LEO TENA TUFAHAMU MINGONI MWA MAELEKEZO YA ZAKATU FITRI.*

*● JE NINI KITOLEWACHO?*

_Zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazoweka wazi alichowaamrisha mtume(ﷺ)-maswahaba wake kukitoa kwa ajili ya *Zakaatul-Fitri.*_

_Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa Abuu Saaid Al-khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema:_

*“Tulikuwa wakati alipokuwa miongoni mwetu Mtume(ﷺ)-tukimtolea Zakaatul-Fitri kila mkubwa na mdogo.*
*Kibaba cha chakula, au kibaba cha shayiri, au kibaba cha zabibu au kibaba cha maziwa ya unga.”* Bukhaariy.

Abdillah Ibn Tha’alabah-Allah amuwiye radhi-amesema: *“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie alihutubia siku moja au mbili kabla ya Eid".*

*“Toeni kibaba cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (Mtoleeni) kila muungwana au mtumwa, mkubwa au mtoto.”* Abuu Daawoud.

_[emoji843]Wanachuoni wamesema mazingatio katika kutoa ni kuangalia chakula rasmi cha mahala husika, chakula kitumiwacho katika dhifa na shughuli zao mbalimbali._

*Na kibaba kwa kipimo cha kilogramu ni sawa na ¾ ya kilogramu moja. Hiki ndicho kipimo kinachopaswa kutolewa kwa kila kichwa kimoja.*

*● WAKATI GANI ITOLEWE?*

_Wakati bora kabisa wa kutoa Zakaatul-Fitri ni ule usiku wa kuamkia siku ya Idd. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Idd._

ﻋﻦ ﺍﺑﻦ ﻋﺒﺎﺱ ﺭﺿﻲ ﺍﻟﻠﻪ ﻋﻨﻬﻤﺎ ﻗﺎﻝ : *"ﻓﺮﺽ ﺭﺳﻮﻝ ﺍﻟﻠﻪ ﺻﻠﻰ ﺍﻟﻠﻪ ﻋﻠﻴﻪ ﻭﺳﻠﻢ ﺯﻛﺎﺓ ﺍﻟﻔﻄﺮ ﻃﻬﺮﺓً ﻟﻠﺼﺎﺋﻢ ﻣﻦ ﺍﻟﻠﻐﻮ ﻭﺍﻟﺮﻓﺚ ﻭﻃﻌﻤﺔً ﻟﻠﻤﺴﺎﻛﻴﻦ، ﻣﻦ ﺃﺩﺍﻫﺎ ﻗﺒﻞ ﺍﻟﺼﻼﺓ ﻓﻬﻲ ﺯﻛﺎﺓ ﻣﻘﺒﻮﻟﺔ، ﻭﻣﻦ ﺃﺩﺍﻫﺎ ﺑﻌﺪ ﺍﻟﺼﻼﺓ ﻓﻬﻲ ﺻﺪﻗﺔ ﻣﻦ ﺍﻟﺼﺪﻗﺎﺕ"* . ﺭﻭﺍﻩ ﺃﺑﻮ ﺩﺍﻭﺩ ﻭﺍﺑﻦ ﻣﺎﺟﻪ.

_Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi kwamba yeye amesema:_

*“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie, alifaradhisha Zakaatul-Fitri ili kumtwaharisha mfungaji kutokana na maneno na matendo machafu. Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo.”*

*[emoji383] HIVO MUDA WA KUTOA ZAKATUL FITRI KABLA SWALA YA EDI HAIJASWALIWA.*

*● MWISHO KABISA, JE NANI APEWE ZAKATUL FITRI.*

_Wanaopaswa kupewa Zakaatul-Fitri ni wale wale wenye sifa ya kupewa Zaka ya faradhi ambao wametajwa katika kauli yake Allah._

*Allah ﷻ Anasema:*

*{إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ}*
```Sadaka hupewa (watu hawa); maskini na wanaozitumikia nyoyo zao juu ya Uislamu na katika kuwapa uungwana watumwa na katika kuwasaidia wenye deni na katika kutengeneza mambo aliyoyaamrisha Allah hasa kwa kupewa wasafiri walioharibikiwa, ni faradhi inayotoka kwa Allah na Allah ni mjuzi na mwenye hekima.”```
Surat At-Tawbah 60

*[emoji840] UKUMBUSHO:*

*IKIWA MTU ATAPOKEA ZAKATU FITRI NA IKAMTOSHELEZA KULA SIKU YA EDI, BASI KINACHOBAKIA NAE ATAWAJIBIKA KUKITOA ZAKATUL FITRI, BALI ASIKUSANYE TU NA KUKIWEKA NDANI.*
================
Asalam alaykm

*الدعوة اﻹسلامية.*
 
Kwa hakika masiku yaliyobaki ni machache. Kwa Jicho yakinifu watu wengi wamechoka, na hata idadi ya waswaliji imeanza kupungua. Basi Fahamuni kuwa huenda katika kumi hili na siku hizi zilizobaki mwisho wako ukawa mwema kwa kuupata ule Usiku wenye cheo. Hivyo jihimize umalize kwa nguvu kama ulivyoanza kwa nguvu. Ubora wa A'amal tunaungalia mwisho wake upoje. Ndio maana tunaambiwa kuna wale ambao huweza kufanya maovu maisha yao yote lakini Qadar ikamtangulia na akarejea kwa mola wake kwa matendo machache ya mwisho yenye ikhlaas na akawa ni katika watu wa peponi. Siku zilizobaki si haba, juzuu kumi unaweza kumaliza, Laylatul Qadr unaweza kuidiriki, Swadaka unaweza kuendelea kutoa. Jiombee zaidi dua na magh**** huku ukiuombea umma zaidi na zaidi upate kuongoka. Tushikane mkono kwa mkono kuitafuta pepo. Pepo ambayo jicho la bin-Adam na Majini hayajapatapo kuiona wala akili kufikiria uhalisia wake haijawahi kamwe. Pepo ambayo Jibreel alipooneshwa aliapa kwa Allaah kumuambia kuwa, hakuna yoyote atakaehadithiwa kuhusu mfanano wa pepo na mtu huyo akaacha kuingia Peponi. Pepo ipo chini ya utiifu, uchaMungu, kujitakasa na Rehma ya Allaah. Ewe Mola wetu, kwa Rehma yako tunakuomba pepo yako tukufu na utuepushe na adhabu ya moto.
Ameen thumma ameen.
 
Back
Top Bottom