Katika michakato na mapambano ya kisiasa na ya kitabaka,aghalabu huwepo mikingamo juu ya mawazo na matarajio.Kutokana na ukweli huo,si rahisi,na kwa kwa kweli haitarajiwi,pande zinazopambabisha fikra na mawazo kukubaliana ama kutokubaliana katika kila jambo.Sasa,kama tutaitazama Rasimu ya Katiba kwa jicho la kisiasa ,kwa maana ya tofauti za wazi za kiitikadi na kifalsafa,kinadharia,kimtazamo na kimwelekeo,kadiri zinavyowatofautisha washiriki wa kisiasa kimatendo na kimazoea,haitastaajabishi hata kidogo,kuona wanachama,wapenzi na viongozi wa vyama mbalimbali wakiipokea rasimu hiyo kwa hisia na mitazamo tofauti.
Yawezekana kabisa baaadhi ya wanachama,wapenzi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi watapendezwa na kuchukizwa na maudhui ya baadhi ya Ibara fulani za Rasimu ya Katiba,mathalani,''uwepo wa mgombea binafsi'' ama hata ''muundo wa Muungano''.Hali hiyo hiyo,inatarajiwa kujitokeza kwa wanachama,wapenzi na viongozi wa vyama vya UPDP, CHADEMA, NLD nk., katika maeneo hayo na mengine.Hii ni kweli kwa kuwa,mosi,tunayaelewa na kuyatambua mapendekezo na misimamo ya baadhi ya vyama vya kisiasa hapa nchini na pili,tunaelewa na kutambua kuwa hoja za kisiasa katika kipindi cha kati ya 2010 na 2013,kutokana na sababu zinazoeleweka bayana,zilichukua nafasi kubwa katika uwanja wa kisiasa kadiri ya agenda ya Katiba Mpya na kufanya mapendekezo na misimamo ya makundi mengine yaliyopo katika jamii hapa nchini,kama vile tabaka la wafanyakazi na wakulima,wavuja jasho,kutokupata usikivu stahiki ingawa hii si lazima imaanishe kuwa maoni ya tabaka hili muhimu hapa nchini yamezingitiwa ama hayakuzingatiwa.Hali hizo kwa kweli zilitarajiwa na kwa hakika kutaraji vinginevyo ni jambo lisiloshawishi akili na lisilokubalika kimantiki.Hiyo ilitarajiwa kwa kuwa mchakato wa kupata rasimu na hatimaye katiba mpya hauwezi kuzingatia maoni ya wadau wa kisiasa pekee ingawa ushiriki wao hauwezi kupuuzwa.
Ishara ya kutia moyo imejitokeza wazi nayo ni kwamba mara baada ya maudhui makuu ya Rasimu ya Katiba kuwekwa bayana wadau mbalimbali,hasa wa kisiasa,wanaonyesha kufurahia na papo hapo kutofurahia baadhi ya maudhui ya Ibara za Rasimu hiyo.Hii ni hatua muhimu kwa kuwa hatimaye Katiba Mpya ni nyenzo ama taasisi ya kusimika na kuimarisha mwafaka wa Kitaifa,utakaozingatia maslahi mapana na ya muda mrefu ya watu wa taifa letu bila kujali tofauti zinazojitokeza katika itikadi,falsafa,imani,nadharia,maslahi,matamanio na matarajio miongoni mwa wananchi.