Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, amepiga marufuku kutozwa fedha kwa wananchi wanaotumia vyoo vilivyopo katika eneo la mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha-Mount Meru kufuatia malalamiko ya wananchi kwamba wamekuwa wakitozwa shilingi 200 kwa kila matumizi.
Akizungumza Agosti 12, 2025 wakati wa ziara yake fupi katika hospitali hiyo, Kihongosi ametembelea eneo la mochwari na kushuhudia mazingira ya utoaji huduma, kabla ya kutoa agizo la kusitishwa mara moja kwa malipo hayo
Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya wananchi kulalamikia gharama hizo, wakieleza kushangazwa na kutozwa kiasi hicho cha fedha katika taasisi ya umma
Mnamo Agosti 11, 2025, wakizungumza na Jambo TV nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, baadhi ya wananchi walisisitiza kuwa hawapaswi kulipia huduma hiyo kwa kuwa hospitali ni mali ya serikali
“Serikali ituangalie. Leo nimeshangazwa mtu kutozwa shilingi 200 kutumia choo cha mochwari kwenye hospitali ya serikali? Hapana, kwa kweli si sawa,” alisema Elizabeth Joseph, mkazi wa Arusha
Kihongosi ameagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha huduma ya vyoo inatolewa bure kwa wananchi na kuwataka wasimamie kwa ukamilifu utekelezaji wa agizo hilo, akisisitiza kuwa taasisi za umma hazipaswi kuwa kero kwa wananchi wanaohitaji huduma za msingi
Chanzo: Jambo TV