RC Dkt. Batilda Burian aipongeza NEMC kupanda miti 2000 Tanga kuelekea maadhimisho ya miaka 40

RC Dkt. Batilda Burian aipongeza NEMC kupanda miti 2000 Tanga kuelekea maadhimisho ya miaka 40

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
1,194
Reaction score
911
IMG-20260520-WA0290.jpg


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kanda ya Bagamoyo, limepanga kupanda jumla ya miti 2000 mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya taasisi hiyo yatakayofanyika Mei 29, mwaka huu.

Kati ya miti itakayopandwa kwenye maadhimisho hayo yenye ujumbe unaosema, “Tunza mazingira, linda Taifa”, 500 itakuwa ya matunda na itapandwa kwenye Shule ya Sekondari Kasera na 1,500 itapandwa kwenye shamba la miti la Halmashauri ya Jiji la Tanga lililopo kata ya Mzizima.

Meneja na Mhandisi wa Mazingira wa NEMC, Kanda ya Bagamoyo, Ndimbuu Joram, na Mhandisi Jerusalem Bagaza, wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Batilda Burian, kujadili maandalizi ya maadhimisho hayo.

Mhe. Balozi Dkt. Batilda, amepongeza hatua zinazochukuliwa na NEMC kuendeleza uhifadhi wa mazingira, na kuhimiza ushirikiano wa wadau ili mazingira yaendelee kuwa salama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Joram, amesema lengo la upandaji miti hiyo ni kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira, na kuongeza juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hatua ya upandaji miti kwenye maadhimisho hayo, inafikiwa ikiwa ni takribani miezi miwili tangu Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipozindua Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa 2026, iliyofanyikia kwenye uwanja wa Ilulu mkoani Lindi Machi 19, mwaka huu.

Mhe. Balozi Dkt.Nchimbi, pamoja na mambo mengine, alisema kasi ya kutekea kwa misitu imekuwa kufikia hekta 460,400 kwa mwaka, hivyo kuwataka Watanzania kuilinda rasilimali hiyo muhimu kwa mazingira na uchumi.

Kwa mujibu wa Afisa Mazingira Mkoa wa Tanga, Ayoub Mrisho, katika kipindi cha kuanzia uzinduliwa kwa kampeni hiyo, jumla ya miti milioni 24 imepandwa kwenye Halmashauri za Jiji, Miji na Wilaya zipatazo 11 mkoani humo.

Mrisho amesema miti hiyo inajumuisha matunda, kivuli, viungo na mikoko ambayo kwa sehemu kubwa imepandwa kwenye maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi katika wilaya za Muheza, Pangani, Mkinga na Tanga.

Pia soma:Prof. Shemdoe aongoza Watumishi TAMISEMI kupanda miti kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Rais Dkt. Samia
 
Back
Top Bottom