Serikali mkoani Kigoma imeahidi kuendelea kusimamia kwa ufanisi miradi yote ya Maendeleo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora kama ilivyopangwa sambamba na kutosita kuchukua hatua kwa mkandarasi yeyote atakayekiuka makubaliano ya mkataba na kukwamisha miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Kigoma na kuwataka wananchi mkoani humo kuendekea kuiamini serikali katika usimamizi na utekelezaji wa miradi iliyoianzisha kwa lengo la kutatua kero zao.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, mkoa umepokea Shilingi Tril. 11.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo huku baadhi ya miradi utekelezaji wake umekamilika na ambayo haijakamilika ipo katika hatua za utekelezaji na hakuna mradi uliokwama.
Amesisitiza kuwa masuala yote ya ujenzi yanasimamiwa na kanuni na Sheria zinazotokana na mikataba hivyo mkandarasi anapotakiwa kuongeza muda wa utekelezaji mradi, serikali itahakikisha nyongeza ya muda huo itakuwa ni ile inayokidhi matakwa ya kimkataba.