MADRID, Hispania
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho amelilaumu Shirikisho la Soka Barani Ulaya UEFA, marefa wake na kocha Pep Guardiola baada ya timu yake kufungwa mabao 2-0 na Barcelona katika mechi ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, ambapo kichapo hicho kimeiweka Madrid katika hatihati ya kushindwa kuutafuta ubingwa wa Ulaya.
Katika mechi ya juzi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Mourinho alishuhudia timu yake ikicheza pungufu baada ya mchezaji wake Pepe kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 61.
Baada ya Pepe kutolewa, katika dakika 15 za mwisho Lionel Messi aliweza kufunga mabao mawili na hivyo kuiweka Barcelona katika nafasi nzuri wakati timu hizo zitakaporudiana wiki ijayo kwenye uwanja wa Camp Nou.
Akizungumzia pambano hilo Mourinho alisema njama za Barcelona na UEFA zinatakiwa zimalizwe haraka kwa sababu Barcelona inakuwa inapendelewa na waamuzi ambao wanapangwa na UEFA.
"Ni karaha kwangu mimi kuishi katika dunia hii, kila nusu fainali hali hii hutokea, kwa nini?, kwa nini Chelsea haikufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya miaka miwili iliyopita, pia mwaka jana Inter Milan kuingia fainali ilikuwa ni miujiza, kwa nini inatokea tena katika mechi hii,"alihoji Mourinho.
Mwaka 2009 kocha Pep Guardiola aliiongoza Barcelona kuifunga Chelsea bao 1-0 kwa taabu, lakini katika mechi ya fainali ya mwaka jana Barcelona ilifungwa na Inter Milan ambayo ilikuwa ikicheza na wachezaji pungufu uwanjani kwa muda wa zaidi ya saa moja. Katika mechi ya kwanza Inter ilishinda mabao 3-1 na waliporudiana Barcelona ilishinda 1-0, hivyo Inter Kuingia fainali.
"Nashindwa kuelewa, nashindwa kujua kama Barcelona inapendelewa kwa sababu inadhamini UNICEF, au ni kwa sababu ya urafiki wao na Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Hispania Angel Maria ambaye ni mkuu wa kamati ya waamuzi wa FIFA na UEFA, sijui ni kwa sababu ni timu nzuri, lakini Brcelona wana nguvu ya upendeleo ya aina yake, wana nguvu ambayo timu nyingine haina,"alisema Mourinho.
Mourinho ambaye aliwahi kufanya kazi kwa miaka minne katika timu ya Barcelona akiwa kocha msaidizi katika miaka ya 90 alisema," Hauwezi kuficha kwamba hivi sasa Barcelona wanafurahia sana kwamba wanaennda kucheza fainali kwenye uwanja wa Wembley, lakini kushinda kwa staili yao kuna acha radha mbaya."
Mimi nimeshinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na nimeshinda yote kwa timu yangu kutandaza soka uwanjani, tulishinda kwa kufanya kazi, juhudi, kutoka jasho kweli na tulipigana haswa na kufanya kazi nyingi, Josep Guardiola ni kocha mzuri, lakini anatwaa ubingwa wa Ulaya kwa kashfa iliyotokea walipocheza na Chelsea na kama ikitwaa tena ubingwa wa Ulaya kashafa itakuwa ni mechi hii dhidi ya Real Madrid.
Klabu ya Barcelona imesema timu yao ya wanasheria wanazipitia kauli zote za Mourinho kabla hawajaamua kumchukulia hatua.
Akilizungumzia pambano hilo, kiungo wa Barcelona, Xavi Hernandez alisema timu yao imezawadiwa kwa kile walichostahili kwa sababu wanashambulia sana kuliko kujilinda sana kama wanavyocheza Real Madrid.
Katika mechi ijayo ya marudiano Madrid itawakosa Pepe na Sergio Ramos kwa sababu wachezaji hao wamepewa kadi, pia kocha Jose Mourinho hatakaa kwenye benchi la ufundi.
"Nimecheza mechi tatu dhidi ya Barcelona na kila wakati tunacheza tukiwa 10, hicho ndiyo kitu siwezi kuamini, labda Pepe alicheza faulo, lakini siamini kama ile ni kadi nyekundu,"alisema Emmanuel Adebayor.