Ramadhan Semtawa na Exuper Kachenje
SIKU moja baada ya mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kutaka Tume huru ya majaji kuchunguza upya kashfa ya Richmond; Spika wa Bunge, Samuel Sitta amesema maamuzi ya Bunge yaliyofikiwa juu sakata la kampuni hiyo, hayawezi kuchunguzwa na mhimili mwingine wa dola.
Juzi Rostam alijitokeza kuzungumzia msimamo wake huo na gazeti hili, baada ya taarifa zisizo rasmi kumnukuu kwamba, alitoa hoja hiyo mbele ya Kamati ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ilipokutana na wabunge wa CCM mjini Dodoma.
Akizungumzia msimamo huo wa Rostam ambaye Kampuni yake ya Caspian inatajwa kufanya mawasiliano na Richmond, Spika Sitta alisema mwa mshangao: "Aaa...hakuna kitu kama hicho kinachoweza kufanyika!"
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge chini ya Dk Harrison Mwakyembe, haikuwataja Rostam na Edward Lowassa kuwa wamiliki wa Richmond, isipokuwa Caspian ya Mbunge wa Igunga, anuani yake ilitumiwa katika mawasiliano wakati wa mchakato huo.
Baada ya taarifa hiyo bunge lilipitisha maamuzi kufuatia ushauri wa kamati hiyo teule na kumpa Lowassa kujipima mwenyewe kuhusiana na madai yanayomhusisha na mchakato wa zabuni ya Richmnond.
Lowassa alijipima na kuangalia nafasi yake ya Uwaziri Mkuu; kisha akatangaza kujiuzulu huku Rostam akiwa kimya. Lakini siku za hivi karibuni aliibuka na kuishutumu ripoti ya Dk Mwakyembe kwamba ilipotosha ukweli.
Spika Sitta alisisitiza kuwa haingii akilini, kwa Rostam kutaka uchunguzi wa suala hilo ufanywe na majaji.
"Kwanza, labda nikwambie tu, maamuzi yaliyofikiwa na Bunge katika Richmond hayawezi kuchunguzwa upya na mhimili mwingine wowote wa Dola," alisisitiza na kuongeza:
"Tunazungumzia kumaliza suala la Richmond si kuanza upya, kama ana pesa zake (Rostam) za kulipa majaji, ni huko huko, lakini hilo haliwezekani".
Spika alisema ushahidi mbalimbali ulionyesha uhusiano wa mawasiliano ya mbunge huyo na Richmond kisha Dowans.
"Hivi mnataka ushahidi upi zaidi, ushahidi wa mawasiliano ulionyesha jinsi mtu huyu alivyokuwa akiratibu Richmond kisha Dowans," aliongeza Spika.
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki ambaye aliingia katika kiti cha uspika na kauli mbiu ya Kasi na Viwango, alisema: âKwanza serikali pia haina pesa za mchezo. Yaani sasa hivi zitoke pesa nyingine kuchunguza Richmond wakati wananchi wana matatizo makubwa kiuchumi na kijamii".
Alihoji kwamba; Richmond ilichunguzwa na watu wakapewa nafasi kujitetea, lakini hawakufanya hivyo sasa wanataka nini?
Kuhusu tuhuma za kuileta Richmond, alisema ni upuuzi kwani zipo barua hata 20,000 ambazo aliziandika akiwa Mkurugenzi Mtendaji (TIC), kuhusu wawekezaji mbalimbali.
"Haingii akilini hata kidogo, hivi wewe (alimtaja mwandishi) kama tulikutana mwaka 2000, halafu tukaachana, ukija kufanya ujambazi leo na mimi nitakuwemo?" alihoji. (somo katika mantiki-MM)
Alikiri ni kweli aliwahi kuandikia barua Richmond kwa ajili ya kufunga bomba la mafuta la Mwanza, kwa ushirikiano na akina Elisante Muro, lakini kampuni hiyo ilibainika kuwa haiwezi kazi.
Richmond iliwahi kukataliwa na Wizara ya Nishati na Madini kufunga bomba hilo mwaka 2004, msimamo ambao ulitolewa na Kamishna wa Nishati, Bashir Mrindoko.
Spika alifafanua zaidi akisema: "Ningeweza kuhusika au kuwajibika kama kashfa hiyo ingetokea katika mradi wa bomba la mafuta," alisema na kuongeza:
"Kampuni ilikwishabainika kuwa haina uwezo, wakaileta tena, wakaipokea na kuipigia debe ipate tenda wakati ilishakataliwa katika mradi wa bomba la mafuta. Eboo..!"
Alipoulizwa kuhusina na hoja ya Rostam ya kutaja achanguzwe na majaji watatu, Wakili wa Mahakama Kuu, Bob Makani, alisema anashangazwa na kauli yake (Rostam) kutaka kuundwa tume ya majaji kuchunguza upya kashfa hiyo.
"Namshangaa Rostam, yeye ni nani mpaka anataka achunguzwe na majaji? Jamani tuheshimu Bunge, tuheshimu kamati za Bunge na maamuzi yake," alisema Makani.
Makani ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Chadema alisisitiza jana akisema: "Yeye (Rostamu) ajitetee tu, hawezi kusema iundwe kamati ya majaji. Majaji ni watu wazito, hawawezi kumchunguza yeye."
Alisisitiza kuwa, mbunge huyo anapaswa kuheshimu maamuzi ya Bunge.
"Lazima kamati za Bunge ziheshimiwe, ninachosema yeye ajitetee tu kwa tuhuma zake na si kutaka iundwe kamati ya majaji," alisema Makani alisisitiza.
Juzi Rostam, akijibu maswali ya gazeti hili kuhusu taarifa hizo alizozitoa mbele ya kamati ya mzee Mwinyi, alithibitisha na kusema mbali na kuchukuliwa hatua za kisheria, endapo tume hiyo huru ya majaji itabaini kuwa anahusika na ufisadi wowote wa Richmond; afukuzwe katika nafasi zote anazoshikilia katika chama (CCM) na Bunge.
Rostam ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM; lakini amekuwa akitajwa kama mmoja wa vigogo walioleta kampuni ya Richmond yenye taarifa tata za kutoka Costa Rica na Marekani na kuwezesha kusainiwa kwa mkataba kati yake (Richmond) na Tanesco Juni 23, 2006.
Lakini baada ya kusakamwa kwa muda mrefu, alipopata nafasi katika kikao cha kamati ya Mzee Mwinyi na wabunge wa CCM, ilidaiwa kuwa Rostam alizungumzia kuundwa kwa tume huru kuchunguza kashafa nzima ya Richmond kwa madai kumba, Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk Mwakyembe ilipotosha.
Hata hivyo, katika majibu yake kwa gazeti la Mwananchi, baada ya kuwasiliana naye kwa kumtangulizia maswali kuhusu ukweli na mantiki ya kauli hiyo, alisema hawezi kuzungumzia ya kikao cha CCM, lakini ana maoni ya kuhusu sakata la Richmond.
"Msimamo wangu tangu Tume Teule ya Bunge itoe taarifa yake bungeni uko pale pale. Ripoti ilijaa upotoshaji na uongo. Nilitaka kuzungumza bungeni nikazuiwa," alisema.
Tangu sakata hilo litokee bungeni Februari 2008, kumekuwa na mvutano kati ya Bunge na Serikali katika utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa, ikiwa ni pamoja na kuwachungulia hatua maafisa wote wa serikali walioshiriki kwenye uzembe wa kupisha zabuni ya Richmond.
Source: Mwananchi