Kashfa ya Richmond, Waziri Mkuu,mawaziri wawili waomba kujiuzulu Tanzania
Muhibu Said na Kizitto Noya
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ibrahim Msabaha, wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na kuhusishwa katika kashfa ya zabuni ya Kampuni ya Richmond Development ya Marekani.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti katika Kikao cha Bunge mawaziri hao walisema tayari wameshamwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumtaka aridhie nia yao ya kujiuzulu kwa maslahi ya taifa.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliliambia Bunge kuwa hadi kikao cha Bunge cha jana jioni mawaziri hao bado hawajajiuzulu rasmi kwani Rais hajatoa taarifa rasmi kwake kueleza kuwa ameridhia nia yao hiyo.
Lowassa ambaye ameshika nafasi ya Uwazi Mkuu kwa muda wa miaka miwili sasa alisema amefikia uamuzi huo ili kujenga dhana ya uwajibikaji.
"Mheshimiwa Spika, nimetafakari sana, kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya serikali yangu, nimeamua kumwandikia Rais barua kumwomba niachie ngazi. Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji, lakini na kutokukubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya Bunge wa kumsingizia mtu," alisema Lowassa.
Kabla ya kutangaza uamuzi wake huo, Lowassa alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Harrison Mwakyembe akisema kwamba aliwasilisha ripoti hiyo bungeni kwa mbwembwe.
"Lakini la pili, nimpongeze Dk Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa Kamati Teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli," alisema Lowassa.
Hata hivyo, alisema aliamua kuzungumza bungeni jana ili kuweka kwenye kumbukumbu kwamba hakuridhika na jinsi kamati hiyo ilivyofanya kazi yake.
Alisema katika uchunguzi wake, kamati hiyo iliamua kusikiliza watu wengine, minong'ono ya mitaani na ilisafiri hadi nchini Marekani kwenda kutafuta mashahidi, lakini yeye ambaye ni mmoja katika watuhumiwa, hawakumhoji hata siku moja.
"Mheshimiwa Spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu, Ofisi ya Bunge mpaka ofisini kwangu hata wangeniita ningekwenda kwa miguu kama hamna gari na nilikuwa tayari kufanya hivyo," alisema Lowassa.
Kutokana na hali hiyo, alisema anaona kuwa alichofanyiwa si sahihi, kimemfadhaisha, kumdhalilisha na ameonewa kwa jambo hilo.
"Maana zimechukuliwa tuhuma zikaja zikaelezwa hapa kwamba hivi ndivyo ilivyo. Mimi sijaulizwa. Kulikuwa na shida gani ya kuniuliza, kwa nini muamini minong'ono ya mitaani kuliko maelezo yangu. Sisi wote hapa ni wanasiasa tukianza kuamini minong'ono ya mitaani niambieni mwanasiasa atakayesimama. Hatuwezi, tume imepewa muda wa kutosha, lakini inashindwa kumuona mtu ambaye wanamtuhumu na wanamsema kwa kirefu sana," alisema Lowassa.
Alisema hata aliponong'onezwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta na kumuuliza kama anao ushahidi wowote, alimpa ushahidi huo wa maandishi, lakini katika ripoti ya kamati, hakuna ushahidi hata mmoja uliotoka kwa Waziri Mkuu.
"Kile kitabu cha majedwali kimejaa majedwali mengi pamoja na magazeti ya udaku, lakini maelezo ya Waziri Mkuu hakuna hata moja," alisema Lowassa na kuongeza:
"Mheshimiwa Spika, naamini ngekuwa ni heshima wangeiweka halafu wakasema tunakaa kitambulisho hiki kwa sababu hii na hii, hiyo ndiyo imejengwa hoja. Lakini kujenga hoja na kuja hapa bungeni tunahutubia nchi nzima na kusema Waziri Mkuu amefanya hiki, amefanya hiki bila ya kumsikiliza nachelea kuuliza hivi mtu wa chini itakuwaje?".
Hata hivyo, alisema ametafakari kwa makini jambo hilo na kujiuliza sababu za wajumbe wa kamati hiyo kufikia kuacha jambo la msingi kama hilo.
"Mimi…nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe," alisema
Alimshukuru Rais Kikwete kwa heshima aliyompa ya kutumikia nchi kwa wadhifa huo kwa miaka miwili, pia alimshukuru Spika, mawaziri, manaibu waziri, wabunge na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Spika Sitta alisema tamko hilo la Lowassa ambalo lilijenga wingu zito bungeni na kuzua mkanganyiko na minong'ono miongoni mwa wabunge, ni zito na hakulitegemea.
"Waheshimiwa wabunge tamko hilo ni zito na wala sikulitegemea. Sasa ningeomba ushauri tuendeje. Tuchangie tu hakuna haja ya kunong'ona na kupiga kelele," alisema Sitta.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alikuwa mbunge wa kwanza kuomba mwongozo wa Spika bungeni jana iwapo tamko hilo la Lowassa akiwa ni Waziri Mkuu, linamaanisha kuwa Baraza zima la Mawaziri kuanzia wakati huo limejiuzulu.
Akijibu hoja hiyo, Sitta alisema hajapata mawasiliano yoyote na Rais kumueleza kama amekubali kujiuzulu kwa Lowassa au la na kwamba, kilichofanywa na Waziri Mkuu, ni kuwasilisha tu kusudio lake la kuomba kujiuzulu.
"Sasa hatuwezi kulifanyia kazi kusudio, kwa hiyo tuendelee tutaona mambo kadri yanavyokwenda. Hayo mengine yanayofuata sasa yananguka hayana maana kabisa," alisema Sitta.
Pamoja na Karamagi kutangaza nia yake hiyo, alisema hajahusika na kusainiwa kwa mkataba kati ya serikali na Richmond akisema kwamba, ulisainiwa miezi sita kabla ya yeye hajahamishiwa katika Wizara husika ya Nishati na Madini.
Hata hivyo, alisema kutokuwapo kwa nyaraka yoyote inayoonyesha alihusika na kusaini mkataba huo, hakumuondolei kuwamo katika utaratibu wa serikali wa "Uwajibikaji wa Pamoja".
Alisema akiwa wizarani hapo, waligundua kuwa Richmond ina dalili zote za tapeli na kutaka kufuta mkataba ili kumpata mwekezaji mwingine, lakini kamati katika ripoti yake haikupongeza hatua yake hiyo.
Naye Dk Msabaha akitangaza nia yake ya kujiuzulu wadhifa wake, alisema amefikia uamuzi huo akiamini katika uwajibikaji na utawala bora.
"Mimi si mwoga, ni mwadilifu, si mla rushwa, ni mchapakazi, ninaamini katika uwajibikaji na utawala bora," alisema Dk Msabaha.
Mapema wakichangia mjadala huo baadhi ya wabunge walipendekeza mawaziri wote waliohusishwa katika mkataba huo mbovu kufilisiwa ili kuziba pengo la hasara iliyopatikana.
Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela alisema kimsingi hakuna mtu aliyeonewa katika taarifa hiyo kwani kuna kila ushahidi wa kuborongwa kwa mkataba huo.
Kilango aliyesema kuwa anapotetea maslahi ya wananchi hana urafiki, aliwataka wabunge wenzake kukubaliana na mapendekezo ya kamati hiyo na kuipitisha bila kupoteza muda.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wenzake wa kamati na mwenyekiti wa kamati hiyo Mbunge wa Nzega (CCM) Lukas Selelii alisema mkataba wa Richmond ni mbovu kuliko mikataba yote ambayo serikali imewahi kuiingia na kumtaka Lowassa kufuta kauli yake kuwa taarifa ya kamati hiyo ni ya uwongo au kuithibitisha.
Akitetea hoja yake Lowassa alisema kuwa kauli anayoamini kuwa ya uwongo ni ile inayosema kuwa Kampuni ya Richmond ni yake na rafiki yake, Rostam Aziz.
Naye Mbunge Viti Maalum (Chadema) Anna Maulida Komu, alilaani tabia ya baadhi ya watandaji wa serikali na wabunge kutumia nyadhifa zao kujinufaisha kwa gharama za wapigakura wao.
"Naomba ndugu zangu tuache kuwageuza wananchi Kachumbari bali tufanye kazi waliotutuma kwa maendeleo yao na taifa," alisema Komu.
Wabunge wengine waliochangia hoja ya kushinikiza Mawaziri hao kuwajibika ni pamoja na Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka na Dk Willibrod Slaa, mbunge wa Karatu (Chadema).
Dk Slaa alitaka pia Baraza lote la Mawaziri lijiuzulu kwa kile alichoita uzembe wa kushindwa kufuatilia ukweli wa kampuni ya Richmond kabla ya kukubali kuingia nayo mkataba.
Alitaka pia kufanyika kwa uchunguzi wa kipolisi ili kubaini ukweli wa mambo na kuchukua hatua zaidi kwa watuhumiwa wa sakata hilo.
Naye Mbunge wa Moshi Mjini (CCM) Philemon Ndesamburo alipendekeza rais awawajibishe Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kwamba waondolewa kwenye kamati ya EPA kwa kuwa wameonyesha kutokuwa waandidilifu katika kazi zao.
Mwananchi 08/02/2008