Mwakyembe anapoficha mambo kulinda ‘heshima ya serikali'
Chesi Mpilipili Julai 2, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
KUNA mambo kadhaa yanayofanywa na viongozi wa nchi hii ambayo ni kielelezo tosha cha jinsi kulivyo na ombwe la watu wanaostahili kweli kuwa na kuitwa viongozi wa wananchi.
Ni mambo ambayo ni kielelezo halisi cha jinsi viongozi wetu walivyo tayari kuweka kando maslahi ya waliowachagua kushika nyadhifa walizo nazo iwapo kwa kufanya hivyo watakuwa wanapalilia maslahi yao kwa kwa mamlaka za juu zenye nguvu zaidi kuliko wapiga kura wao.
Naomba nizungumzie matukio mawili tu ya hivi karibuni kama mifano hai. Matukio haya yametokea kwenye nyanja mbili tofauti; lakini zinazohusiana na maisha ya kila siku ya Watanzania. Siasa na michezo.
Tuanze na lile la michezo. Siku chache zilizopita kulikuwa na taarifa za mgogoro mdogo wa viongozi kwenye moja ya timu mbili kubwa za soka, ukubwa ambao sio lazima uwe ni kutokana na usakataji wa kabumbu mahiri wa timu hizo.
Mgogoro huu ulianza pale uongozi wa klabu hiyo ulipofanya kilichoelezwa kuwa ni kumsimamisha mweka hazina wa klabu hiyo kutokana na makosa ambayo hayakuwekwa wazi zaidi ya kusemwa kuwa ni 'kuvunja kanuni za uongozi.'
Taarifa hii ya uongozi wa klabu ikafuatwa siku chache baadaye na taarifa kutoka kwa mweka hazina wa klabu ambaye pamoja na mambo mengi alisema kuwa anasubiri barua rasmi kutoka kwa viongozi ili na yeye 'alipue mabomu'!
Kiongozi yule wa karne ya ishirini na moja wa klabu yenye mamilioni ya wanachama, wapenzi na mashabiki akasisitiza kwamba alikuwa na mengi tu ya kuyasema kuhusiana na viongozi wenzake na angeyasema mara tu baada ya kupata barua rasmi ya kusimamishwa!
Kama vile haitoshi, siku chache baadaye katika kile wengi walichoona kuwa ni kutafuta huruma ya wapenzi wa klabu hiyo, kiongozi huyo aliibuka tena na kudai kuwa alikuwa ameandika barua ya kuomba aruhusiwe kukarabati uwanja wa klabu hiyo ambao ulikuwa mahututi lakini alikuwa hajapata jibu kutoka kwa viongozi waliomsimamisha!
Kwangu mimi, na bila shaka kwa wapenzi wengi wa michezo nchini, hiki kilikuwa ni kilele cha unafiki. Huyu alikuwa ni kiongozi wa muda mrefu tu kwenye safu za uongozi za klabu hiyo ya soka na kama angekuwa na nia ya kweli ya kuukarabati uwanja wa klabu yao angeweza kufanya hivyo pengine bila hata kuhitaji kuomba ruhusa kwa mtu zaidi ya kutoa taarifa tu!
Lakini alikuwa amesubiri hadi wenzake walipomsimamisha uongozi ndipo akaona ule ndio ulikuwa muda muafaka si tu wa yeye kukarabati uwanja wa timu yake bali zaidi mno kuwatangazia wanachama jinsi alivyoandika barua kwa viongozi wenzake ili kupewa amana hiyo lakini alikuwa hajajibiwa!
Hilo ni moja. Kubwa zaidi lilikuwa lile la kuwaambia wanachama kuwa alikuwa na mambo mengi ya kusema kuhusiana na uozo uliomo kwenye uongozi uliomsimamisha lakini alikuwa anasubiri kwa hamu uongozi huo umpe rasmi barua ya kumsimamisha ili na yeye alipue mabomu!
Tatizo la viongozi wengi wa nchi hii ni kuwachukulia Watanzania kuwa ni maamuma wasiojua kuchanganua mambo. Haikuhitaji akili za ziada hapa kung'amua kuwa alichokuwa anafanya kiongozi huyu ni kutetea unga wake tu kwa kuwatingishia kibiriti viongozi wenzake na haikuwa kwa ajili ya manufaa ya klabu na wanachama wake.
Kwa maana nyingine, kiongozi huyu aliyechaguliwa na wanachama wa klabu alikuwa anamfahamu uozo uliokuwa ndani ya safu ya uongozi wa klabu yao lakini alikuwa anasubiri atofautiane na viongozi wenzake kwanza ndipo aone umuhimu wa kuwaambia wanachama juu ya uozo uliopo kwenye uongozi wa klabu yao!
Na hii pia iwe mpaka apewe barua ya kusimamishwa kazi kwanza ndio aumwage uozo huo hadharani. Bila barua, uozo huo ungeendelea kuwa siri yake! Hawa ndio viongozi wetu wa michezo.
Tuhamie kwenye siasa. Wakati kashfa ya EPA ilipoanza kushika kasi, taarifa za baadhi ya magazeti zilituambia kuwa kuna kiongozi ambaye alikuwa anasema kuwa iwapo angetajwa tu kuhusika na kashfa hiyo basi asingekubali kwenda na maji peke yake. Angekufa na mtu.
Kwa maana nyingine ni kwamba kiongozi huyu angetaja majina ya wahusika wa kashfa hiyo iwapo tu yeye angetajwa kuhusika. Kama wasingemtaja, basi, naye asingewataja na kwa maana hiyo Watanzania wanaosubiri kwa hamu kubwa majina ya wahusika hao, watasubiri mpaka wachoke.
Kwa vile hizi zilikuwa ni taarifa za magazeti ambazo hakuna jina lililotajwa, naomba tuziache kama zilivyo na badala yake tuhamie kwenye yale yaliyotokea majuzi pale mjini Dodoma kwenye kikao cha Bunge kinachoendelea huko sasa.
Wakati anachangia hotuba ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu, mwenyekiti wa kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza utaratibu uliotumika hadi kampuni ya Richmond kupewa tenda ya kufua umeme, Mh. Dk. Harrison Mwakyembe ametoa kauli tete ambayo kwa hakika imewachanganya watu si haba.
Kwanza, Mh. Mwakyembe alieleza kushangazwa kwake na wabunge waliokuwa wanatoa hoja za kuwasafisha watuhumiwa wa kashfa ya Richmond na kuwataka kama hawakubaliani na uchunguzi wa kamati yake, basi, wavunje kanuni husika za Bunge ili mjadala wa Richmond urudishwe tena Bungeni kujadiliwa upya.
Akaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa iwapo mjadala huo utafunguliwa tena, basi, kamati yake ingeyasema hata yale ambayo kamati yake ilikuwa imeficha kuyasema ili kulinda heshima ya Serikali iliyo madarakani!
Hii kwa hakika ilikuwa ni kauli nzito na ya kushitua kutoka kwa mtu ambaye Watanzania walio wengi wanamuona ni shujaa kutokana na kuongoza kamati iliyotoa taarifa iliyosababisha waziri mkuu na mawaziri watatu kujiuzulu kwa mpigo, 'tetemeko' ambalo halijawahi kutokea nchini.
Binafsi, nimejikuta nikiifananisha kauli hii na ile ya yule kiongozi wa timu kubwa nchini aliyesema kuwa anangoja apewe kwanza rasmi barua ya kusimamishwa uongozi na viongozi wenzake ndipo na yeye ataje uozo ulio kwenye uongozi huo!
Tungeelewa iwapo Mh. Mwakyembe angesema kuna mambo waliamua kuyaficha kwa vile kama wangeyasema yangeweza 'kuhatarisha usalama wa taifa letu'. Hili tungekubaliana nalo. Lakini 'ili kulinda heshima ya serikali'?
Ni kauli ya utata ambayo bado najitahidi kujipa matumaini kwamba pengine ilimtoka tu kwa bahati mbaya Mh. Mwakyembe kutokana na jazba aliyoonyesha kuwa nayo kama hotuba yake ilivyoonyesha na hakufikiria madhara yake pale wananchi watakapoanza kuichambua.
kwa hakika, kauli ya Mheshimiwa Mwakyembe imezua maswali mengi zaidi kuliko majibu miongoni mwa Watanzania wanaomchukulia kama shujaa wao. Ni mambo gani hayo makubwa zaidi ambayo kamati ya Mh. Mwakyembe iliyaacha kuyasema au kuyaweka katika ripoti yao ili ‘kulinda heshima ya serikali'?
Iweje wabunge wetu hawa waone kuifichia serikali yale ambayo yangeweza kusababisha heshima yake ipungue ni muhimu zaidi kuliko kutuwekea wazi kila kitu sisi waajiri wao na kutuacha tuamue wenyewe ni lipi ambalo litaitia aibu serikali na lipi halitaitia aibu?
Je, kwenye hadidu za rejea za kamati yao teule kulikuwa na kanuni inayowataka kuficha mambo ambayo wangeona ni mazito mno kiasi cha kuhatarisha heshima ya serikali? Ni kigezo gani walichotumia katika kuamua kuwa haya ni mambo mazito na yangeweza kuiaibisha serikali na haya sio mazito tuyaweke wazi?
Na baada ya kauli hii ya utata ni kipi sasa kitatufanya tusiamini maneno ya 'majeruhi' mmoja wa kisiasa aliyesema kuwa kama kamati hiyo ilikuwa na uwezo wa kuamua kutosema baadhi ya mambo, basi, pia ilikuwa na uwezo wa 'kuchomekea' baadhi ya mambo ili kuhalalisha makosa ya baadhi ya waheshimiwa waliotuhumiwa na kamati hiyo?
Tunadhani ni vizuri Mheshimiwa Mwakyembe na kamati yake akaharakisha kufafanua kauli tete yake hii. Yeye bado ni shujaa kwa Watanzania walio wengi.
Tusingependa Watanzania wafike mahali pa si tu kumfananisha na yule kiongozi wa klabu anayengoja apewe barua ya kusimamishwa uongozi na wenzake ndipo atuambie uozo wa uongozi wao; bali pia tusingependa tuanze kujiuliza ni upande gani wa kipande chake cha mkate Mheshimiwa Mwakyembe anachoona kimepakwa siagi. Upande wetu wapiga kura au upande wa serikali?