*** Haji na Zedi hawakulala, mana hawakujua ni kitu gani kitamkuta mwenzao huko aliko.
Wakati wao wakimuwazia vile, tayari Honda alikuwa ameiingizwa kwenye chumba cha mateso huku akiwa amevuliwa nguo zote.
Yule kijana wa Kisaudia aliona ile pete ikiwa kwenye uume wa Honda na alipoishika akashindwa kuelewa ni kitu gani kile.
Pete ile ilikuwa imetengenezwa maalumu kwa ajili ya kushikwa na Honda peke yake na kama ikishikwa na mtu tofauti basi sehemu ilipounganishwa hutoa taarifa ya hatari.
Kijana yule akaitazama kwa makini ila akaona ni pete za kawaida tu ambazo huvaliwa na watu wenye mikuyenge mikubwa mikubwa.
Hakuitilia shaka zaidi na akaitupa chini.
Likaletwa dumu la mafuta ya taa na kumwagwa mwilini mwa Honda kisha wakamuuliza zilipo zile karatasi za kile kitabu.
Akashindwa kusema.
Na kitu alichogundua ni kuwa zile karatasi zilikuwa na umuhimu mkubwa sana kwa wale watu kuliko hata uhusika wake katika kuwapepeleza.
Alikaa kimya.
Mafuta yalipomwagwa mwilini yakasalia kidogo kwenye dumu na yakamiminwa chini na kusambaa kisha jamaa mmoja alikaa pembeni na kiberiti.
Leo tutakuchoma moto Ahmed." Alisema yule kijana. ***
Mapambazuko yaliwakuta Haji na Zedi wakiwa wameshajadiliana vya kutosha kuhusu namna ya kufanya ili waweze kusambaza kirusi Maria.
Walijiandaa na kutoka nje ya makazi yao na kuelekea kutega njia ambayo waliamini gari lililombeba binti yule litakuwa linapita.
Kabla ya saa mbili kamili, gari moja la bei mbaya liliwapita njiani, na wao walilifuata kwa nyuma na walipofika makutano ya mnara wa kijeshi, wakafanya hila za kutaka kulipita gari lile likiwa katika mzunguko wa mwanajeshi asiefahamika.
Wakaparazana na kukosa mwelekeo na kwenda kuingia kwenye bustani ya mnara ule.
Walinzi wawili walishuka kwa gadhabu na kuliendea gari la Zed huku wakitukana.
Zedi alishuka!
Kwa makusudi aliongea lugha tofauti na kiingereza huku wale jamaa nao wakiongea lugha tofautitofauti, mara kingereza,mara kisomali ili mradi wapunguze jaziba zao.
Lengo la kuongea Kiswahili ni kutaka mlinzi wa tatu nae ashuke.
Na kweli alishuka, na Haji nae akashuka.
Haji alikifungua kichupa kile na kukiziba mdomo kwa kidole chake kisha akakifumbata mkononi.
Ajabu ni kuwa mlinzi wa tatu alieshuka alikuwa anaongea kiswahili safi kabisa.
Jamaa yule anaezungumza kiswahili aliwatuliza wenzie kisha akaanza kuongea na Zedi na hata Haji alipofika waliendelea kuongea kiswahili.
Walinzi wale ilitakiwa wawahi kutoka pale ili mwanafunzi awahi shule.
Hivyo ilikuwa ni kujitahidi kusawazisha suala lile.
Zedi aligundua wanataka kuondoka, hivyo akaanzishaa tena mgogoro kwa kuonesha yeye ndie amekosewa na wale jamaa.
Zogo likazuka upya!
Haji alikaa makini kwa ule upande ambao aliamini yupo mwanafunzi.
Mwanafuzi nae aliona anacheleweshwa, akashusha vioo vya upande wake.
Kosa!.
Macho makali ya Haji yalikuwa sambamba na na kwa wepesi wa hali ya juu akajifanya nae amaeingiwa na jaziba kwa kurusha mikono hovyo na pale ndipo alipokirusha kichupa kile chenye kirusi Maria.
Mtoto yule alikiona kichupa kile na bila kujua akakichukua na kukinusa kisha akakitupa nje na kuwaita walinzi wake.
Walifanikiwa!
Baada ya kufanikiwa walituliza mashetani yao nao walipanda gari na kuondoka huku wakiwa wametumia dakika saba tu na walijua ndani ya dakika kumi askari wa Mogadishu wangeliwakuta pale.
Waliondoka wakijipongeza huku Haji akitema kidonge alichokuwa amebugia ili kuzuia a athari za kirusi kile wakati alipokuwa amekifungua.
Walirejea kwenye makazi yao na kuanza kupanga mikakati ya namna watakavyoweza kuingilia tiba ya binti yule.
Haji alikaa kwenye kompyuta na kuanza kupika taarifa na wasifu wa mganga bingwa wa magonjwa ya kuambukiza ambae alikuwa anafanya kazi kwenye hospital kubwa pale Mogadishu kama mganga mkuu.
Na hapo walipata mtu mwenye sifa sawa na zile walizozihitaji.
Na waliangukia kwa Dr Azam.
Zedi alichukua vifaa vyake na kukaa kwenye kioo huku Haji akiwa anaendelea kupika taarifa za Dr Azam.
Alibadili maeneo muhimu na hasa mawasiliano,aliweka anuani ya barua pepe na namba za simu za kwao,kisha akaifunga kompyuta na kumgeukia Zedi.
"Aisee! wewe mtu ni hatari yani hutofautiani na sura ya huyu jamaa kabisa."Alisema Haji huku akichukua kamera yake kumpiga picha Zedi ambae alikuwa amefanikiwa kujichongea sura sawa na ya Dr Azam.
"Hii ni raha ya ukomando,kila kitu MI see rahisi kukifanya" Alijigamba Zedi.
"Ila hatuwezi kufanya hii kazi vizuri bila Azam mwenyewe kutoweka mjini" Alisema Haji.
"Upo sahihi, hebu tumtafute mjini na tutoweke nae" Zedi aliafiki. ***
Jioni ya siku ile Zedi na Haji walikuwa na kazi moja tu, nayo ni kuhakikisha wanajua alipo Dr Azam.
Walifanikiwa kujua anapoishi na kwa uzoefu wao wa kuteka watu ambao hawana madhara, walifanikiwa kumchukua na kuondoka nae hadi kwenye makazi yao. Wakati wao wakimteka Azam; Imamu Shafi'I alikuwa anapokea taarifa kutoka kwa tabibu wake ya kuwa mwanae amepata maambukizi ya ugonjwa wa ajabu hajapata kuona na hajui kama aliwahi kusoma popote kuhusu ugonjwa ule.
Ugonjwa ule ulisababishwa na kirusi ambacho kina shambulia seli nyeupe kwa kasi kubwa sana na kupelekea mwili kukosa nguvu na mgonjwa kuwa anastukastuka kila mara.
Imamu alipagawa!
Kwa haraka alituma sampo ya damu ya binti yake kila kulipokuwa na tabibu wanaefahamiana.
Na hadi giza linaingia alikuwa amepata majibu yenye kufanana na kila tabibu alishindwa kujua ni wapi atapa dawa za kuzuia kirusi kile kisifanye kazi.
Na pia wapo waliomtahadharisha ya kuwa siku chache zijazo binti yule anaweza kukosa uhai.
Hali ilizidi kuwa mbaya kupindukia.
Imamu Shafi'I aliita watu wake wa karibu usiku ule na kuwataka ushauri.
Wengi walishauri walivyoweza ila mmoja alishauri aitwe Dr Azam; mganga mkuu wa hospital ya old Mogadishu.
Haraka haraka haraka wasaidizi wake waliingia mtandaoni kutafuta sifa za Dr yule.
Walijiridhisha na taarifa zake,kisha wakampigia simu.
Walikubaliana kuonana ahsubuhi katika mnara wa kanisa katoliki. ***
Zedi na Haji walipongezana baada ya kuona ujumbe wa barua pepe kisha ukafuata ujumbe wa simu.
Makubaliano yalifanyika na wakajipanga kufanya walichokubaliana.
**
Ahsubuhi kama kawaida Dr Azam wa bandia alitumia gari la Dr Azam wa kweli na kuelekea nalo kule kwenye mnara wa kanisa katoliki kama walivyokubaliana.
Ungelimtazama Zedi; basi ungeamini ndie Dr Azam halisi.
Alipofika pale, alipigiwa honi na gari moja lililokuwa limepaki pembeni ya duka moja la vifaa vya baiskeli.
Akaenda na gari lake ila alishuka kijana mmoja na kumwomba ashuke aache pale gari lake na apande kwenye gari lao.
Dr Azam wa bandia alitii.
Alichukua kibegi chake chenye vifaa tiba na kupanda ile gari.
Safari ilianza.