RIWAYA; URITHI WA GAIDI
NA; BAHATI MWAMBA
SIMU; 0758573660
SEHEMU YA KUMI NA SABA
****
Remi alikuja kuzinduka akiwa amelala sakafuni na alikuwa na maumivu nyuma ya kisogo chake, maumivu ambayo hakujua yalisababishwa na nini.
Alitulia na kurejesha kumbukumbu zake na ndipo alipokumbuka vizuri kitu cha mwisho kumkumba ilikuwa ni maumivu kama ya kuchomwa sindano nyuma kidogo ya kisogo chake na pia alihisi anadondokea mikononi mwa mtu.
Alinyanyuka chini alipokuwa amelala na kujaribu kuangaza ila hakuona mwanga zaidi ya kidirisha kidogo kilichokuwa juu kabisa ukutani.
Pua zake zilinusa harufu nzito iliokuwa mle chumbani.
Akajaribu kupapasa ukutani labda ataona sehemu ya kuwashia taa, ila hakuona.
Hakujua alipoteza fahamu kwa muda gani hadi wakati huo alipojikuta akiwa amelala sehemu ngeni kabisa.
Akakaa chini na kuegemea ukuta, kisha akatulia na kuacha kichwa kiwaze yanayomsibu.
Wala hakufikiria sana, mlango ukafunguliwa na wakaingia wanaume wawili waliokuwa na kamba mikononi mwao na walipomfikia bila kumuuliza wakamfunga mikono na miguu kisha wakambeba mzegamzega na kwenda nae sehemu nyingine bila kusema kitu.
Kwa makadirio walikuwa wamekata kona za korido kama nne hivi na kwa kudhania alihisi yupo kwenye nyumba ya horofa.
Wakaingia kwenye chumba kilichokuwa na taa kali na wakambwaga chini bila huruma kisha wakatoka na kumwacha akijizoazoa kunyanyuka.
Akanyanyuka!!
Hakuwa peke yake mule ndani.
Kulikuwa kuna mtu amekaa kwenye kiti huku akiwa ameshika kisu kikali akikichezea kwenye vidole vyake.
Mtu yule alikuwa na asili ya watu wa India.
Alikuwa anatabasamu kana kwamba alifurahia uwepo wa Remi pale ndani.
"Kaa kwenye kiti tafadhali" yule mtu alisema.
"Naitwa Sultani" Akijitambulisha bila kusuburi Remi akae kwenye kiti.
Remi alikaa!
"Nambie wataka nini kwangu" Alihoji Remi.
"kwani unajua u wapi hapa?" Alisema Sultani.
"Ni mtoto tu ndo anaweza asijue alipo ila sio mimi. Kwanini mmeniteka?" Alihoji Remi.
Sultani alicheka.
"Ni kweli umetekwa, ila unaweza kuwa huru ukionesha ushirikiano" Alisema Sultani.
"wewe usivyojua alipo hata mimi sijui" Alijibu Remi.
"Remi;tatizo huwa unajiona shujaa sana wewe ila ushujaa ukizidi hugeuka kuwa upumbavu" Alisema Sultani huku akipitisha kisu kwenye mdomo wake.
Remi hakujibu!!
"Sikia,kutwambia alipo mumeo ni safi sana mana si wewe ama mumeo watakaoendelea kuteseka na haya masahibu" Alisema Sultani huku akiwa analamba kisu kwa ulimi wake.
"Nimekwabia vile usivyojua alipo, hata mimi sijui alipo aisee" Remi alizidi kushikilia msimamo wake.
.
Sultani alicheka kinafiki.
"Ok tuachane na mumeo, vipi kuhusu ukurasa wa Bombay?" Alisema Sultani.
Remi alitumbua macho, lilikuwa jambo geni kwake kulisikia.
"Ndo nini hicho?" aliuliza Remi.
"Hizi ni karatasi nne zenye maneno ya kiarabu, na zilipotea miaka kadhaa nyuma na inasadakika zipo hapa nchini" Alisema Sultani.
"Hebu usinichanganye tafadhali, mara mume wangu mara karatasi, sasa mimi nahusika na lipi hapo eti" Alisema Remi huku akionekana dhahiri akiwa amepagawa kwa maneno hayo.
"Yote unahusika nayo, kwa sababu mumeo alionana na Ahmed; Gaidi ambae ndie aliepotea na vitu hivyo" Sultani alisema huku sasa macho yake yakiwa yameanza kubadilika kama mtu aliekula pilipili.
Remi aligwaya!
"Ninyi watu mwanifurahisha sana aisee, yani kila siku maigizo na sijui kabisa uhusika wangu katika hizi show" Alisema Remi.
"Sio tena muda wa showtime bali ni muda wa event kabisa na bado uhusika wako upo" Alisema Sultani na hapo Remi akabutwaika baada ya kusikia showtime.
Hapo alijua kabisa bado yuko mikononi mwa watu wale wale wanaompa tabu kila siku.
"Kwa sasa hatutakuumiza, ila wakati mwingine hatutakuwa na swalia mtume juu ya jambo hili, lakini pia kwa usalama wako, endapo ukiona karatasi yoyote usioielewa basi toa taarifa" Alisema Sultani
"Nitoe taarifa kwa nani" Alihoji Remi.
"Mwanamke mjanja kama wewe nani akwambie pa kutoa taarifa? Ukiziona sisi tutajua umeziona na tutazifuata" Alisema Sultani huku akinyanyuka.
Aya!!
Yakoje mambo haya, mara nitoe taarifa mara watajua, duh! Sasa kwa nini hawakuniacha hadi wajue nimeziona ndo watokee? Alijihoji Remi na alipokuja kutazama alipokuwa sultani hakumuona tena.
"Kapita wapi bwege huyu?" Alijihoji Remi huku akigeuka huku na huko pasi kumuona Sultani.
Akiwa bado na taharuki, mara akaanza kuhisi baridi sana ndani ya chumba kile huku kila dakika ikiongezeka.
Mara ukaanza kutoka na mvuke wenye harufu nzuri sana na Remi alipovuta akaanza kupoteza fahamu taratibu.
**
Saa sita baadae Remi alizinduka kutoka kwenye koma ya kifo na usingizi
.
Akashangaa kuona akiwa amelala kwenye sofa, akaamka haraka na kutulia.
Dakika moja mbele akarudiwa na ufahamu wake na ndipo alipotupia macho kwenye ukuta.
Lahaula!!
Alikuwa yupo ndani kwake na alikuwa akimtizama mumewe kwenye picha.
Alipagawa!!
Alijua kabisa pale sio sehemu sahihi kwake na alihitaji kuondoka pale haraka iwezekanavyo.
Kitu ambacho hakujua ni kuwa ile ilikuwa imepangwa iwe vile.
Alipotaka kufungua mlango ili atoke, alikutana na domo la bastola huku polisi kama sita wakifungua mlango na kuingia ndani harakaharaka na yeye kubaki akiwa kama kapigwa sindano ya ganzi.
Mbele yake alikuwa amesimama ofisa mwenye cheo cha Inspekta na alikuwa na tabasamu lisiloeleweka kama ni chafya alitaka kupiga ama alikuwa anataka kucheka ama kulia.
Usoni alipachika miwani ya macho na kufanya aonekane kama Mr Bean.
"Niite Inspekta Kibe Kengeleo; au wengi hupenda kuniita Kenge na upo chini ya ulinzi kwa tuhuma za mauaji na kuwakimbia polisi, lakini pia unatuhumiwa kutaka kuhujumu uchumi wa nchi na pia kuishi nchini kinyume cha sheria" Kenge alimsomea makosa yake mtuhumiwa wake ambae alikuwa ameganda kama sanamu la posta akiwa hajui ni vipi yametokea hayo yanayomtokea.
Kilichofuata ni kupigwa pingu kisha wakatoka nae na kumpandisha kwenye karandinga na kutimua nae kuelekea kituo cha polisi kwa taratibu zaidi.
Remi alikuwa mikononi mwa polisi.
***
Habiba alimtumia ujumbe mfupi Kobelo akiwa ameambatanisha na namba mbili za simu ambazo pia kila namba aliweka jina la mmiliki wake.
Namba ya kwanza ilioonekana kuwa eneo hilo, mmiliki wake alikuwa ni Davis Minja. Huyu alimtambua kama mwandishi alietekwa.
Na namba ya pili ilikuwa na jina la mmiliki ambae ni Seki Zayd.
Kobelo akatuma tena ujumbe kwa Habiba ya kuwa alihitaji kujua ilipo namba hiyo wakati huo.
Habiba alijibu ujumbe ule kwa kusema namba ile inaonekana ipo posta kwenye jengo la mamlaka ya mapato.
Sajenti Kobelo aliharakisha kutoka na kuelekea nje kulikokuwa na gari lake kisha akaingia na kutia moto kuelekea posta huko.
Kwa kutumia uzoefu wake wa kuishi ndani ya jiji la Dar; alikatisha njia zisizo rasimi na hatimae aliingia posta akiwa ametumia saa moja na nusu tu.
Aliegesha kwenye maegesho ya wafanyakazi wa ofisi zile na kumtumia ujumbe Habiba ambae nae alijibu kwa kumwelekeza kuwa mtu yule bado alikuwa maeneo yale.
Kobelo aliendelea kungojea hadi nyakati za jioni ambapo ofisi zilikuwa zinafungwa.
Akapokea ujumbe wa Habiba ya kuwa mtu yule alikuwa anatoka na amekaribia alipo.
Kweli Kobelo aliona bwana mmoja mrefu wastani akiwa ameshika vitabu akifungua mlango wa gari jeupe.
Kobelo alijaribu kumpigia.
Bwana yule alipokea na Kobelo akakata.
Alipata hakika ya mtu wake anaemfuatilia.
Akaunga msafara kumfuata bwana yule ambae alikuwa na kitambi cha kuzugia umasikini.
Safari yao ilikuwa ni ya mdogomdogo kwa sababu ya foleni, lakini hatimae walifika walikokuwa wanaenda.
Mtu yule aliegesha gari kando ya barabara na kushuka kuelekea kilipo chuo huria Kinondoni.
Kobelo nae alishuka na kuelekea huko.
Bwana yule hakuingia chuoni ila alizunguka na kuwa kama anafuata ofisi za kuchapa na kurudufu karatasi zilizokuwa kule na hatimae safari yake iliishia kwenye gari moja la kifahari.
Bwana yule hakuingia, bali kioo kilishushwa na bwana yule akapokea bahasha fulani na kuanza kurejea kwenye gari lake.
Kobelo nae alifuata.
Alipanda kwenye gari na kutokomea kuelekea njia ya kawe.
Kobelo nae alikuwa nyuma.
Bwana yule aliingia kwenye nyumba moja nzuri iliokuwa na geti zuri la kisasa.
Kobelo hakuwa na namna, alipaki mbele kidogo kisha akangojea giza liingie ili akwee ukuta.
**
Giza lilitamalaki na ni wakati huo ambao Kobelo nae alikuwa amevaa kofia yake pana na kuvaa gloves mikononi huku akiwa ameshika kisu kidogo mkononi mwake.
Akatumia ukuta wa nyumba ya pili kupata msaada wa kuingia ndani ya nyumba ile.
Na hatimae alidondoka kistadi pembeni kidogo ya kichaka cha maua.
Na alipotaka kusimama, alisikia silaha kubwa ikikokiwa nyuma yake.
"Tulia Kanga wewe"
Sauti ya jitu ilikoroma.