Riwaya: Jina langu ni Pheady

Riwaya: Jina langu ni Pheady

KAZI IENDELEE...


Nyumba ya Patrick ilikuwa kando ya ziwa hivyo ningeshukia nyuma yake kwa upande wa ziwani. Tuliendelea taratibu mpaka nilipofika ninapopahitaji na kumuambia rafiki yangu asimamishe mtumbwi. Maeneo yale yalionekana kutokuwa na umeme siku hiyo, nafikiri ni kutokana na mgao wa umeme uliokuwa ukiendelea kote nchini. Nilijiweka sawa tayari kwa shughuri pevu iliyombele yangu, nilichomeka visu sita kwenye viatu, vitatu kila upande, nikachukua kishoka kidogo na kukichomeka nyuma ya mgongo alafu nikahitimisha kwa kuchukua upinde uliokuwa umefungiwa kifuko cha mishale yenye sumu pamoja na sime ndefu.
"Kwa heri rafiki yangu Mungu akipenda tutaonana." Nilimuambia.
"Sawa Mr Pheady, lakini inabidi nikusubiri nione mwisho wako" Alisema kwa huzuni.
"Okay, utasogeza mtumbwi mbali alafu subiri nusu saa kama hutaona mlipuko wa nyumba ndani ya huo muda basi wewe ondoka nenda zako lakini ukiona mlipuko nisubiri naweza kurudi ila uwe makini." Nilisema. Baada ya hapo tuliagana kwa kumbatiana alafu mimi nikajitosa makini(ziwani).

Haikuwa mbali kutoka tulipokuwa mpaka ufukweni na mie maji nilielewa kuyakata maana ndio yaliyotuzunguka kisiwani Ukerewe na michezo ya majini ndio iliyotukuza. Nilihisi maumivu makali sehemu ya kifuani baada ya kuingia majini, nilijua hii ilitokana na maji kugusa sehemu nilizoungua lakini aikujali ili nia na lengo langu litimie.
Nilifika ufukweni mwa ziwa na kujikuta nimetokea hatua chache tu kutoka kwenye ua wa nyumba ya Patrick kwa nyuma kupakana na ziwa Victoria. Nilianza kunyata kuelekea ua wa hiyo nyumba huku huku nikisaidiwa na giza lililokuwepo ili nisionekane. Nilivuka ule ua kwa kupita pembeni ya ya ziwa na kuwa naangalia kwa mbele yangu nyuma ya nyumba ambayo ilionyesha mwanga wa taa katika chumba kimoja ambacho nilijua ni sebule kutokana na nilivyoona siku ile tulipokuja kumuokoa Kikakika.

Nilitembea kwa kunyata huku nimeinama usawa wa ua mithili ya ninja. Nilifika nyuma ya ile nyumba iliyokuwa mahabusu ya Kikakika na kuchungulia usawa wa nyumba kubwa ambapo niliona gari imepaki pembeni ya nyumba. Nilitulia na kuvuta hisia zote mahali pamoja Ili kama kuna mtu au dalili za ulinzi hapo nje niweze kuzing'amua lakini sikuhisi au kuona dalili ya mtu yeyote. Nilisogelea gari na kulifanyia ukaguzi hakukuwa na mtu ndani yake. Nilinyaya mpaka kwenye ukuta wa nyumba chini ya dirisha lililokuwa linaonyesha mwanga, mambo yote niliyafanya kwa haraka na tahadhari kubwa. Nilichungulia ndani kwa chati kwani lilikuwa dirisha la vioo na ndani kuna pazia lililokuwa limesukumwa kwa pembeni kidogo, niliweza kuona ndani bila pingamizi. Ndani kulikuwa na mtu mmoja aliyekaa kwenye sofa na huku mbele yake kukiwa na meza iliyokuwa na chupa ya pombe na bunduki aina ya machine gun ikiwa imelazwa pembeni juu ya hiyo meza, Mtu mwenyewe alikuwa amepitiwa na usingizi. Nilipiga akili namna ya kuingia humo ndani nikaona kwa kupitia mlangoni naweza kushtukiwa na kunaswa kirahisi. Hivyo nilichomoa sime kwenye ala yake mgongoni na kuanza kupenua polepole kwenye maungio ya kioo na chuma cha frem ya dirisha huku macho yakiwa makini na yule mtu aliye ndani kama ataonyesha dalili ya kushituka.
Yule mtu aliye ndani pale si mwingine bali ni yule mzulu aliyekuja na Wanna See kutoka South Africa, alikuwa kachukua nafasi ya ulinzi wakati wenzie wakiwa wamepumzika. Hiyo ilikuwa ni baada ya kuwa wamekuja kunifanyia unyama nyumbani na kurudi zao Mwanza wakiwa na uhakika kuwa wameniua. Kwani ile jana baada ya kuwa wamepata habari zangu kwa Magesa, asubuhi Patrick alikuja Nansio kufuatilia nyendo zangu na ndio siku na mimi nilifika Nansio. Aliweza kunasa nyendo zangu vizuri sana mpaka na kujua wakati niliolala baada ya kutoka kule Bondeni Bar. Hivyo akawasiliana na wenzie waliokuja na ule mtumbwi wao wa kujaza upepo huku wakiwa wamefunga injini ya nguvu kubwa. Waliungana naye katika kutekeleza unyama wao na baada ya kufanya huo ushenzi Patrick alibaki kusikilizia alafu Wanna See na yule Mzulu wakarudi Mwanza.

Kwa hiyo kusalimika kwangu pale nyumbani na kutoroka kwangu hospitali na gari ya polisi Patrick alipata habari akawa amepanda boti ya jioni kurudi Mwanza. Kufika Mwanza akakutana na mchumba wa Zuberi ambaye ni Mtuli, Mtuli alimtishia kumpeleka polisi kutokana na kifo cha mchumba wake ambaye alikuwa ni rafiki wa Patrick na maiti yake ilikutwa kule kwa Magesa. Mtuli alienda kutambua miili ya maiti kule Bugando hospitali na kuhisi Patrick ambaye ni rafiki ya mchumba wake atakuwa anajua kilichotokea. Alimsaka mpaka akawa amempata jioni ile aliporudi kutoka Ukerewe na akawa amemsakama kwa maswali huku akimtishia kumpeleka polisi kuhusiana na tukio hilo. Kitendo hicho kilifanya Patrick atumie mbinu zake za kijasusi na kumteka Mtuli, kwa hiyo usiku huu ninapoingia hapa ndani yumo Mtuli huku akiwa amefungwa kamba kwa nyuma na kupigwa sindano ya usingizi alafu yupo Patrick, Wanna See na yule Mzulu aliye pale sebuleni.
Nilimaliza kupenua ile sehemu ya maungio ya kioo na kupata nafasi ya kushika vidole vyangu kabla yule mtu wa ndani hajashituka. Nilipachika vidole na kuanza kuvuta kwa akili ili nikipachue kile kioo bila kumshitua. Wakati nafanya hivyo ghafla kioo kilikatika na kutoa mlio uliomshtua yule mtu. Ulikuwa ni mlio hafifu uliomchanganya asijue ulipotokea alionekana kuwa na wenge la usingizi na kuangaza huku na huku. Akinyanyuka na kuchukua ile bunduki alafu akaelekea mlangoni, alifika mlangoni na kugeuka kuangaza sebuleni na akafungua mlango na kutoka sebuleni kuingia kwenye korido.
Alipotoka mlango ulijifunga nyuma yake nikasikia nyayo zikitembea kwenye korido. Nilipitisha mkono kwenye ile sehemu iliyobaki wazi baada ya kioo kukatika na kufungua komeo la dirisha. Nilitumbukia ndani bila kelele yoyote, hayo yote yalifanyika kwa muda mfupi sana. Nilivuta pazia na kuziba uwazi wa dirisha alafu nikanyata na kujificha nyuma ya sofa ambalo mwanga wa taa ulikuwa haufiki vizuri kwani walitumia taa ya kuchaji kutokana na kukatika umeme. Nilipokuwa nimeishachukua mafichoni yangu nilisikia mlango ukifunguka na kujifunga alafu nikasikia nyayo kutoka chumba cha jirani kuja sebuleni nilipokuwa. Nilikaa kwa tahadhari huku akili na macho yangu yote yakiwa kwenye mlango wa kuingilia sebuleni. Ndipo nilipoona mzungu mmoja aliingia kwa tahadhari kubwa huku akiwa na bastola mkononi, aliangaaza pale sebuleni kwa haraka na baada ya kutomuona mwenzake aliyekuwa pale aligeuka kutoka, lakini kama aliyekumbuka kitu vile aligeuka tena ghafla na kuangalia sehemu nilipojificha. Najua alihisi kitu lakini alikuwa amechelewa kwani wakati ananyanyua bastola kuelekea kwangu niliachia mshale mmoja wenye sumu ambao tayari wakati nilishauweka kwenye upinde. Alishituka na kujirusha kwa namna ya ajabu ambayo sikutegemea nikawa nimekosea shabaha niliyokuwa nimelenga hivyo mshale ukampata begani na kujichomeka hapo begani. Nia yangu ilikuwa umpate kwenye koromeo.
Niwakati alipojirusha na kujiviringisha hewani ndipo na yeye aliacha risasi kuelekea nilipo hukua akiwa hewani. Nilifanya ile sofa kama ngao yangu hivyo zile risasi ziliishia kwenye mbao za sofa huku zikichanachana sponji ya sofa. Kwa jinsi alivyoruka na kuachia risasi nilitambua huyu mzungu hakuwa mtu wa kawaida. Alikuwa mtu na nusu bali nilifarijika kwa mshale uliompata maana sumu itafanya kazi. Alipotua chini alikuwa amechuchumaa na aliuvunja ule mshale kwa halaka na kujiviringisha pale chini akiahamia nyuma ya sofa iliyokuwa pembeni yake. Vitendo vyote hivyo vilifanyika kwa kasi ya ajabu na kimya kimya Kwani bastola yake ilikuwa na kiwambo cha kuzuia sauti. Akiwa pale nyuma ya sofa alichungulia kwa uvunguni na kuniona nami nikiwa nyuma ya sofa jingine nikijiahidi kumpata kwa shabaha ya mshale. Kama unavyojua msomaji ni vigumu kulenga shabaha ya mshale ukiwa umelala. Aliponina tu alivurumisha risasi lakini nilikuwa mwepesi na kuruka kutoka pale na kutua pembeni ya jokofu. Alitulia akinipigia mahesabu nami nilikuwa nampigia hesabu. Nilijua kadri muda unavyokwenda ndivyo sumu inavyosafiri hasa unapojishughurisha damu nayo inasafirisha sumu kwa haraka kwenda kwenye moyo.
Ghafla alisimama kwa haraka na kurusha risasi kwa wingi kuelekea kwenye jokofu nilipo wakati huo huo alijirusha hewani na kujiringisha kuelekea kwenye mlango unaotoka sebuleni. Nilitambua mbinu yake, nami nilisukuma kwa nguvu lile jokovu kwa kutumia miguu yote miwili kumuelekea na wakati huohuo nikahama nilipo huku nikichomoa kishoka kidogo kilichokuwa mgongoni mwangu na kulenga mkono uliokuwa umeshika bastola. Maana mkono mmoja haukuwa na kazi kwani nilishamdunga mshale begani hivyo hakuweza kuutumia. Kile kishoka kilimpata barabara kwenye kiganja cha huo mkono ulioshika bastola na kukata nusu ya kiganja ambapo aliangusha bastola na kiganja kikaning'inia. Ni kutokana na pigo hilo nilililotoa hapo kwenye kiganja ndipo alipotoa yowe la fadhaa huku akitua chini na kujirusha tena tayari akawa ametoka nje ya sebule huku bastola ikiwa imedondoka sebuleni.
Nilijiviringisha kwa haraka na kuiwai ile bastola alafu nikajibanza kwenye kona ya sebule inayoniwezesha kuona milango yote, wa kutokea sebuleni na ule wa kuingilia kwenye korido la vyumbani. Nilipoangalia ile bastola ilikuwa inebakiaza risasi tatu tu. Lile yowe alilotoa lilikuwa limewashitua yule Mzulu aliyekuwa nje na Patrick aliyekuwa amelala chumbani. Yule mzulu alikuja kwa kasi kutoka nje ndio alipokutana na Yule mzungu akiwa katika hali mbaya. Yule mzungu alimueleza kitu yule mzulu na hapo mzulu akaanza kuja kwa kunyata usawa wa dirisha nililopitia. Wakati huo kule ndani Patrick alikuwa anachukua siraha zake anazoziamini na kwa upande mwingine kule stoo alikokuwa amefungiwa Mtuli alikuwa anajitahidi kujifungua kamba kutoka kwenye kiti alichofungiwa.
Yule Mzulu alipofika dirishani aliingiza mtutu wa bunduki na kuanza kuachia risasi kusambaza sebule nzima wakati yeye akiwa meinama. Wakati anaingiza mtutu niliiona nikawahi kulala chini pembeni ya ukuta. Kutokana na yeye kuchuchumaa risasi hazikuweza kupiga chini zilikuwa zinapiga kuanzia usawa wa magoti. Kwa kuwa ile ilikuwa machine gun mlio mkubwa ulisikika na aliendelea kumimina risasi hovyo. Nilitoa yowe la kumzuga kana kwamba nimepatwa na risasi na wakati huo huo nikatembelea tumbo kwa haraka mpaka chini ya dirisha alilokuwa ameingizia mtutu. Lile yowe lilimdanganya asitisha kupiga risasi na kunyanyua kichwa kuchungulia ndani nami wakati huo nilirusha dodo ya kuwekea mishale kwenye sofa iliyokuwa mbali nami na inaweza kuonwa vizuri na mtu anayechungulia dirishani. Alipochungulia na kuona ile podo alivuta kichwa kwa ndani ya dirisha ila apate kuona pembeni huku siraha yake ikiwa tayari tayari mikononi. Wakati huo kule chumbani Patrick alikuwa tayari eshamaliza kuzivaa dhana zake za kazi na likiwa anatoka kwa tahadhari kuja sebuleni. Vilevile nilisikia mtu akipiga mlango wa chumba fulani kwa nguvu huku akitoa sauti ya kama mtu aliyezibwa mdomo.
Mara yule mzulu alipotoa kichwa ili kuona vizuri ndani nilimuona nikiwa nimelala chali chini ya dirisha. Ni pale alipojivuta zaidi kwa ndani ndipo niliposukuma upanga wangu kwa nguvu zote iliompata chini ya kidevu na kutokea utosini, alikufa palepale bila kelele. Kitendo bila kuchelewa nilijiviringisha na kwenda kubana pembeni ya mlango wa korido inayotoka vyumbani ambako nilikuwa nasikia mgongo wa mlango usio wa kawaida. Nilipofika tu pembeni ya huo mlango wa korido taa ya pale sebuleni ilipigwa risasi na kukawa giza. Nilibana kwa tahadhari pale pembeni huku nikiyazoeza giza macho yangu na nikiwa nimefungua milango yote ya fahamu ya mwili wangu.

Ghafla pembeni yangu katika mlango wa kutokea vyumbani pazia lilicheza kidogo, nikawa makini kuangalia niliona kivuli cha mtutu wa bastola ukitokeza kwa chini. Nikajua adui atakuwa amelala kwa chini na anatembelea tumbo, niliendelea kutulia kuangalia Kinachoendelea maana sikujua kuna watu wangapi katika nyumba ile hivyo tahadhari ya kumshambulia yule mtu ilikuwa ni muhimu. Baada ya mda kiwiliwili kilichoshika ule mtutu wa bastola kilijitokeza, kilionekana kama kivuli vile maana ilikuwa giza. Nilipokitazama vizuri niliona mkono mwingine ukiwa umeshikilia kitu kama embe nikajua litakuwa bomu la kutupa kwa mkono. Niliendelea kumuangalia jinsi anavyotembelea tumbo huku nikijaribu kuhisi na kusikiliza kama kuna mwingine nyuma yake. Alipokuwa ametoka mwili mzima ndipo alipojivuta na kuchuchumaa huku akigeuka na kutazama upande nilipo. Sikufanya ajizi palepale niliachia risasi iliyolenga mkono ulioshika bomu la kutupa ikampata na bomu likanguka pembeni. Ile risasi ilipompata alirusha kwa kurudi kinyumenyume huku akiachia risasi hovyo nami nilijiviringisha kutoka nilipokuwepo na kuingia chini ya meza kubwa iliyokuwa pembeni pale sebuleni alafu kukawa kimya. Kila mtu alikuwa anatumia hisia kutambua adui wake alipo. Mimi nilijua alipo kwani kile kivuli kilielekea nyuma ya sofa, katika kuviziana kule mara ukimya ulikatishwa na kelele za mlango kugongwa kwa nguvu kule sehemu ya vyumbani. Mpaka wakati huo nilikuwa nimetumia robo saa na kutokana na nilivyomuahidi rafiki yangu aliyenileta nilitakiwa kutumia chini ya nusu saa.
Bila kutegemea umeyuliwaka, Tanesco walikuwa wamerudisha umeme uliokuwa umekatwa kwa ajili ya mgao. Kitendo cha umeme kurudi kilifanya adui yangu aangaze huku na huku bila umakini kwani hakujua nilipo nami nilitumia fulsa ya kujua alipo na kuruka juu huku nilijiviringisha hewani na wakati huohuo nikaachia risasi moja iliyompata bega la mkono ulioshika bastola na bastola ikaanguka. Mikono yote ikawa haina kazi, sikutaka kumuua maana nilikuwa na mwaswali naye. Nilitua chini pembeni yake huku nimemuelekezea ile bastola niliyoichukua kwa yule mzungu.

Ni wakati huo nilipokumbuka ile milio ya machine gun kuwa itakuwa imesababusha uwezekano wa kuja askari hapo. Hivyo nilimsogelea na kumuuliza; "Wewe ni nani?" Aliniangalia kwa dharau kisha akajibu: "Hata nikikuambia haitakusaidia kitu"
Sikutaka anicheleweshe kwani mahali hapo palishaanza kuwa na hatari ya kukutwa na polisi. Nilishika mkono nilioupiga kwa risasi na kuunyonga kwa nguvu, alipiga yowe na kusema ; "Naitwa Patrick" nilimtazama huku nikipunguza kidogo nguvu za kumnyonga. " "Nafikiri sasa tutaelewana" nilisema huku nikimkazia macho.
"Unafanyia nani kazi na kwa nini unatafuta kuniua? Nilimuuliza.
"Najifanyia kazi mwenyewe na kuhusu kutaka kukuua ni kwa sababu ulichukua dhahabu ambazo sisi tulishazipigia hesabu." Alijibu huku akionyesha uso wa maumivu.
"Sidhani kama suala lilikuwa ni dhahabu tu eleza kila kitu vinginevyo naunyofoa huu mkono" nilisema huku nikizidisha nguvu katika kuunyonga mkono alipiga yowe na kusema; " nasema... Nasemaa... Tafadhari usinitese hivyo niue tu." Nilimpunguzia maumivu na kunwambia haya eleza.
Kabla ya kueleza alinitazama na kusema: "Naomba unijibu swali langu na baada ya hapo uniahidi nitakachokiomba ndipo nikueleze."
Nilimuambia sawa nitakujibu na utakachoomba nitatimiza kama hakuna madhara kwangu.
"Wewe unaitwa Lyampili?" Aliuliza
"Hapana naitwa Pheady." Nilimjibu
"Mbona picha zako zilikuja toka Afrika Kusini na jina la Lyampili?" Aliuliza
Nilimtazama na kumwambia; Jina la Lyampili ni la utu wangu wa zamani katika utu ninaotukia sasa hivi ninaitwa Pheady. Hivyo toa ombi lako alafu unijibu swali langu. Niliongea kwa kuunguruma maana muda haukuwa rafiki tena kuendelea kuhojiana.
"Nimekuelewa ndugu Pheady au Lyampili, ombi langu ni kuwa nikimaliza kujibu uniue bila maumivu na kuna dada huko ndani ya stoo umuokoe akaendelee na maisha yake. Kwani najua ukiniacha hai sitaweza kuhimili adhabu ya serikali kutokana na matendo yangu yatakayodhihilishwa na huyo dada pamoja na rekodi kadhaa zitakazotafutwa na polisi." Nilimuangalia kwa fadhaa alifu nikamwambia ombi lake limekubaliwa. Hapo alimueleza yote kuhusu jinsi alivyokuwa akitumika na kundi la unyan'ganyi lililiongozwa na waafrika Kusini na shughuri zao ilikuwa ni kupola madini aina mbalimbali hapa Tanzania na kwenda kuyauza katika masoko ya Dunia. Vilevile alinieleza suala zima la ujio wa Wanna See na sababu ya mimi kutaka kuuliwa kama ulivyokwisha kusoma ndugu msomaji.
Baada ya maelezo yake nilimuwekea mdomo wa bastola kifuani upande wa kushoto na kuachia risasi iliyomfanya alale usingizi tulivu wa kifo.
 
Back
Top Bottom