SEHEMU YA 45
“Nipo kazini!”
“Aa, msipoteze wakati bwana! Mchinjeni tu!” ilisema sauti nyingine kwa hamaki zaidi kuliko ile sauti ya kwanza.
“Ngojeni, msimwue bure, ngojeni kwanza,” alisema mwingine kwa sauti ya kuamrisha.
Yule askari alikwisha fadhaika haelewi kinachotokea Alihisi amekabiliwa oa mauti na alikata tamaa kabisa kwani kundi lililomzunguka lilikuwa m kundi la watu waliokasirika kila mmoja na silaha mkononi. Bahati yake nzuri kiza cha usiku ule kilificha mandhari ya kutisha ya watu wale ambao nguo zao zilijaa damu na nyuso zimezungukwa na manywele na madevu yasiyoshughulikiwa kwa muda wa siku nyingi sana.
“Wewe nani?” iliuliza sauti katika kundi.
“Mimi askari.”
Pale pale alitoka mtu katikati ya kundi lile na kumpiga kofi hata akaona vimurimuri badala ya shangwe lile lililomzunguka.
“Ebo, sisi tunakuuliza wewe nani tokea saa ile wewe umeshika askari, askari. jina lako nani?”
“Mcha, Mcha Hamadi.” alijibu mbio mbio huku bado maruirui ya kofi alilopigwa yanamtaabisha.
“Ah, Mcha, mwacheni, hawezi kufanya tabu, mlinzi mwenye funguo yuko wapi?”
“Yuko pale! Nyumba ile!” alijibu Mcha huku sauti inamtetemeka kwa hofu na wasiwasi, miguu inamtetemeka, nywele zimemsimama.
“Haji, nenda kachukue funguo halafu..wengine watakwenda kumlafuta fundi mitambo, nani anajua anakokaa?”
“Mimi nakujua! Twendeni nikupelekeni!” Mcha aliruka na kusema haraka haraka.
“Twende, sisi tutakuchukua kwa amani lakini ukijaribu kuleta shari njiani utakiona cha mtema kuni,” ilisema sauti moja kutoka katika kundi lile la watu waliokuwa tayari kufanya chochote kile, kizuri au kibaya.
Kundi lile lilijigawa sehemu mbili, kundi moja lilibaki Raha leo na kundi jingine likafuatana na yule askari na kukiandama kiza cha usiku ule. Mcha bila ya hata kujua njia aliyoipita alijishtukia ameshafika mbele ya nyumba ya fundi wa mitambo, “anakaa hapa, ngojeni nimgongee dirisha.”
“Ngoja kijana, usiwe na pupa, sisi tunamjua zaidi kuliko wewe,” ilisema sauti moja kwa utulivu.
Dirisha liligongwa, kabla ya aliegongewa dirisha hajafungua, dirisha la nyumba ya pili lilifunguliwa na ilisikika sauti ikiuliza, “Nani ana......”
Kabla hajamaliza kusema alilolitaka risasi ya ghafla iliyotoka katika bunduki mojawapo ya watu waliokuwemo kundini mle ilipiga pale pale ilipotokea ile sauti na sauti hiyo haikusikika tena.
“Mwamba!” iliita sauti moja.
“Hallo!” alijibu Mwamba aliyeonyesha yu macho.
“Tayari!”
“Tayari sio? Nakuja.”
Mwamba alifungua mlango wa nyumba kwa haraka na kutoka nje. Vunge la fungilo lilikuwa mfukoni mwake na kutoka hapo walifululiza moja kwa moja mpaka kwenye kituo cha radio.
Zogo lilizidi na makundi ya watu yalianza kumiminika Raha Leo kila mmoja silaha mkononi. Mwamba alipousogelea mlango wa kituo cha radio macho ya watu wote waliokuwa na hasira za siku nyingi yalimwangalia yeye. Mwamba alilifungua lango kubwa lililochongwa kwa nakshi nzuri na bila ya kujali chochote alifululiza moja kwa moja mitamboni. Watu watatu walokuwa na bunduki za aina ya ‘Mark 4’ walimfuata nyuma yake.
ITAENDELEA