Riwaya: Kijijini kwa Bibi

RIWAYA : KIJIJINI KWA BIBI.

MTUNZI : ALEX KILEO. .

SEHEMU YA KUMI NA TANO.

______________
ILIPOISHIA
_______________

"sasa si ungenitaharifu nimwambie
mjomba
ako yuko pale ni polisi pia" Mama
kayoza akaongea huku sura yake
ikiwa na huzuni.

"mama bwana, sasa
we si ungenitaharifu kwanza kwamba
una ndugu dodoma" Kayoza alisema
maneno hayo kwa kudeka mbele ya
mama yake.

"mimi nina mambo
mengi mwanangu" Mama kayoza
akajitetea.

"ulisema ni polisi eeh?,
anaitwa nani?" kayoza akamuuliza
mama yake.

"ndio ni polisi, tena ana
cheo cheo, anaitwa Joel Minja, ila
wenzake wamezoea kumuita sajenti
Minja" Mama kayoza akajibu.

"mh, Sajenti Minja!!!!?" Omari akajikuta
anauliza bila kutarajia...

_____________
ENDELEA..
_____________

"ndio mwanangu, kwani
unamjua?", Mama Kayoza akamuuliza
Omary.

"ndio mama, namfahamu"
Omary akajibu.

"si unaona mwenzio
anamjua, ni mtu maarufu pale Dodoma" Mama Kayoza akasema
huku akimuangalia Kayoza.

"kaka umemjuaje hadi mimi nisimjue?"
Kayoza akamuuliza Omary.

"huyo jamaa ndio anaeshikilia kesi yetu"
Omary akajibu.

"ni yule jamaa white
tuliyekutana nae siku zile
hospitali?", kayoza akamuuliza
Omary.

"eeeh, ndio yule yule, na
tena siku ile ya ajali ulitaka kumnyonya damu, ila ulimuacha",
Omary akajibu.

"eh, ulitaka kumnyonya damu?", Mama kayoza
akaingilia kwa swali.

"ndio mama, hayo ndio
matatizo ambayo yananiandama
mama, na sasa tunavyoongea,
tunatafutwa nchi nzima na polisi kwa
kosa la kunyonya watu damu na
mauaji ya polisi" Kayoza akamjibu
mama yake huku akiwa katika sura ya
huzuni.

"ina maana bado hayajaisha
tu?" Mama kayoza akauliza huku
akionekana ana mawazo.

"hayajaisha?, kumbe mama unajua
matatizo yangu?" Kayoza akamuuliza
mama yake huku akimshangaa.

"ni hadithi ndefu
mwanangu", mama kayoza akajibu.

"nisimulie hata kwa kifupi" kayoza
akamchachamalia mama yake amsimulie.

"nitawahadithia baadae,
ngojeni kwanza nikapike chakula cha
mchana, maana nikisema tuongee tu,
tutashinda na njaa
hapa" Mama Kayoza alijibu kisha akanyanyuka na kuelekea jikoni huku akionekana ni mtu mwenye mawazo mengi sana.

**************

Sajenti Minja alikuwa na dhamira ya kuacha kazi, tena alipania haswa kuacha kazi. Aliona bora mjinga alie hai, kuliko kujifanya shujaa alafu mwishowe ufe.

Alipotoka katika mgahawa ambao alikuwa na mkuu wa Polisi, alielekea moja kwa moja kwa secretary wa ofisi ya polisi kwa nia ya kwenda kuchukua ujuzi wa namna ya kuandika barua ya kuacha kazi kabisa. Aliona bora ahache kwa maana akisema aombe aondolewe katika ile kesi ni lazima angekataliwa kwa kuwa hakuwa na sababu za kutosha.

Aliingia pale kwa secretary huku akiwa na mawazo mengi sana,

"Naweza kupata nakala moja ya barua iliyoandikwa mtu aliyeomba kuacha kazi?" Sajenti Minja aliuliza baada ya salamu,

"Zipo nyingi tu, hata ukitaka kumi utapata" Dada aliyepo alimjibu kwa utani lakini Sajenti Minja hakuonekana kuwa katika sura ya utani, badala yake alikuwa mnyonge sana kiasi kwamba yule dada akamshangaa kwa maana Sajenti Minja anajulikana sana pale ofisini kwa kupenda utani,

"Naomba moja tu, tena iliyoandikwa na mfanyakazi aliyeacha kazi muda mfupi baada ya kuanza" Sajenti Minja aliongea huku akiangalia chini,

"Mh...wewe unaitaka ya nini?" Dada alimuuliza huku akitilia shaka hali aliyokuwa nayo Sajenti Minja,

"Kuliko kuendelea na hii kesi, nimeona bora niache kazi" Sajenti Minja alitoa kauli iliyomshangaza yule Dada,

"Kwanini usingeandika barua ya kuomba hiyo kesi apewe mtu mwingine?" Dada aliuliza,

"Nikiulizwa sababu nitajibu nini?" Sajenti Minja aliuliza,

"Dah, kweli mtihani" Dada alijibu baada ya kufikiria kwa muda mfupi,

"Sasa kama wewe uliye mzoefu na kazi hii unaona huo ni mtihani, je mimi ambaye sina uzoefu wa kutosha?" Sajenti Minja aliuliza huku akiamini hawezi kujibiwa,

"Ila hiyo sio sababu ya kuacha kazi, wewe si umeanza kazi juzi tu? Ungeizungusha hii kesi muda mrefu bila mafanikio yoyote ni lazima angepewa mtu mwingine" Dada alijaribu kumshawishi Sajenti Minja,

"Mafunzo niliyopitia mimi sio uliyopitia wewe, mafunzo niliyopitia mimi yananifundisha kusimamia Ukweli" Sajenti Minja aliongea,

"Hakuna mafunzo ya uaskari yanayofundisha kusema uongo, ila mimi nimeona bora utumie hiyo njia kuliko kuacha kazi" Dada aliongea kwa huruma ili kumshawishi Sajenti Minja akubaliane nae,

"Naomba nipatie hiyo nakala ya barua, nitaenda kufikiria mbele ya safari" Sajenti Minja aliongea kuonesha amedhamiria kutekeleza hadhma yake,

"Sawa bwana" Dada aliongea kisha akamtafutia hiyo nakala na kumpatia, Sajenti Minja akapokea na kuondoka.

***************

Mama kayoza
ni jina lake la ukubwani tu, jina
alilozaliwa nalo ni Aika John Minja,
ni mtoto wa tatu kutoka familia ya
watoto wanne, na ni mtoto wa kike
pekee katika familia yao, kaka zake
wawili ni wafanya biashara wakubwa
kiasi katika jiji la Arusha, na mdogo
wake ni afisa wa polisi, anaitwa Joel
John Minja.

Mama Kayoza alipokuwa na umri wa
miaka kumi na saba, alijiingiza katika masuala ya mahusiano ya
mapenzi, ila aliambulia kupata ujauzito na kukataliwa na mwanaume
aliempa huo ujauzito na mbaya zaidi hata nyumbani kwao alifukuzwa.

Baada ya kuangaika na mimba yake mtaani na Maisha kumuendea vibaya, aliamua arudi nyumbani na kuwaomba msamaha wazazi, wazazi wake wakamkubalia kwa hali aliyonayo ila
kwa kuwa alikuwa bado mwanafunzi,
wazazi wake wakamshauri akaitoe ile
mimba, nae akakubali.

Ila katika
utoaji wa hiyo mimba ilipelekea au kile kitendo cha Kutoa mimba kilitaka
kumgharimu maisha yake, kwani alivuja damu nyingi kiasi kwamba
ilimbidi alazwe hospitali takribani mwezi
mmoja na nusu kutokana na damu kumpungukia mwilini.

Alipotoka hospitali
akahapa kutopenda tena
mwanaume na akaahidi kutilia mkazo katika masomo yake.

Baada ya kupona kabisa,
aliendelea na shule na Mungu akamjaalia kumaliza
kidato cha nne salama, ila alama aliyopata haikua salama kwani haikumruhusu kujiunga au kuendelea na madarasa yanayofuata.

Baada ya miaka miwili ya kukaa nyumbani, kwa bahati nzuri akatokea mwanaume, mwenyeji
wa Bukoba, alieitwa Ezekiel Kayoza
Lutashobi na kutoa posa kwa wazazi
wa Aika, wakamkubalia bila kipingamizi kwa sababu ya fedha
alizokuwa nazo na pia waliona binti yao tayari amefikia umri wa kuishi na mume.

Baada ya miezi kadhaa ya kufuata utaratibu wa dini na mila, bwana Ezekiel na bi Aika wakaoana kwa ndoa ya kikristo iliyokuwa na kila aina ya furaha kutoka kwa ndugu wa pande zote mbili, yaani upande wa mwanaune na upande wa mwanamke.

Walikaa miaka miwili bila kupata mtoto, hapo ndipo chokochoko zikaanza kutoka kwa upande wa mwanaume wakidai wifi yao ni mgumba.

Baada ya uvumilivu wa maneno na kashfa nyingi kutoka kwa mawifi, Aika alifanikiwa kupata ujauzito na kujifungua mtoto mmoja wa kiume aliyefuatiwa na wengine wawili wote wakiwa wa kiume na jumla ni kwamba alibahatika kupata watoto watatu.

Wa kwanza aliitwa
Zakaria, wa pili, Buguzo na wa tatu ndiyo huyu bwana mdogo alisebabisha niandike huu mkasa, anaitwa Kayoza.

**********

Mama Kayoza akatayarisha
chakula, akawatengea wanae mezani,
kisha akajumuika nao kula. Wakati wakiwa wanakula hakuna aliyemkumbusha mama Kayoza kuwa awasimulie ule mkasa, wote walikuwa kimya.

Baada ya kula na kuoga, wote walikaa sebuleni
wakawa wanaangalia filamu za
Tanzania, kayoza akavunja ukimya,

"mama, baadae yenyewe si ndio sasa
hivi?, tuadithie basi" Kayoza alimkumbusha mama yake,

"khaa!, nawe
nae usahau?" Mama kayoza
akamwambia mwanae kwa utani
huku anacheka.

"matatizo
yanasahaulika nini?", kayoza akamjibu mama yake.

"haya basi,
nianzie wapi?" Mama kayoza akauliza huku akimuangalia mwanae.

"anzia mwanzo" kayoza
akajibu huku akitega masikio ili kusikiliza kisa kilichopelekea yeye kuwa mtu wa kubadilika na kuwa kama mnyama.

Mama kayoza akaanza
kuwaelezea...

******ITAENDELEA******

the Legend☆
 
RIWAYA : KIJIJINI KWA BIBI.

MTUNZI : ALEX KILEO..

SEHEMU YA KUMI NA SITA NA KUMI NA SABA.

______________
ILIPOISHIA
_______________

Baada ya kula na kuoga, wote walikaa
sebuleni
wakawa wanaangalia filamu za
Tanzania, kayoza akavunja ukimya,

"mama, baadae yenyewe si ndio sasa
hivi?, tuadithie basi" Kayoza
alimkumbusha mama yake,

"khaa!, nawe
nae usahau?" Mama kayoza
akamwambia mwanae kwa utani
huku anacheka.

"matatizo
yanasahaulika nini?", kayoza
akamjibu mama yake.

"haya basi,
nianzie wapi?" Mama kayoza akauliza
huku akimuangalia mwanae.

"anzia mwanzo" kayoza
akajibu huku akitega masikio ili
kusikiliza kisa kilichopelekea yeye
kuwa mtu wa kubadilika na kuwa
kama mnyama.

Mama kayoza akaanza
kuwaelezea...

____________
ENDELEA...
_____________

Alianza namna hii, "mimi
nilipoolewa na baba yako, nilimkuta
ana fedha zake za kutosha, alikuwa
ana magari makubwa ya kubebea
mizigo, alikuwa na daladala pale
Bukoba mjini, alikuwa na gari ndogo
tatu za kutembelea, na nyumba tatu
pia.

Kwa hiyo yeye alitoka Bukoba
mpaka Kilimanjaro kuja kunioa mimi,
kwa madai ya kuwa alinipenda toka
zamani na alikuwa ananifuatilia chini
chini.

Baada ya ndoa nilitoka nyumbani na kuhamia kwenye nyumba ya baba yako ambayo aliijengea Bukoba.

Ila baada ya kuhamia Bukoba,
nilikaa pale nyumbani kwangu wiki
mbili ndani, hakuna hata jirani
mmoja aliyekuja kuniona, mule
ndani nilikaa na wafanyakazi tu, na
baadhi ya ndugu wa baba yako
ambao walikuwa ndio
wananichangamsha changasha, ila
kingine kilichokuwa kinanishangaza ni
kwamba kila ilipofika mwisho wa
mwezi, baba yako alinunua, mbuzi
wawili weusi na kondoo mmoja, alafu
wanaukoo wote walikuja pale
nyumbani, walikuwa wanaingia katika
chumba kimoja kilichopo uwani na kujifungia uko, mimi sikuruhusiwa kuingia.

Na nilipomuuliza, yeye
aliniambia kile chumba ni kitakatifu,
mimi sikuwa mtu wa kuhoji hoji sana,
kwa hiyo sikutaka kudadisi zaidi kwa maana nilipojaribu kufanya hivyo uso wake ulionesha kutofurahishwa na maswali yangu.

Ila niliendelea kujiuliza mwenyewe ni nini utakatifu
wa hicho chumba?.

Wanandugu wa baba yako na baba yako mwenyewe waliendelea kuingiaingia katika
chumba iko ambacho ni kikubwa,
kilikuwa na uwezo wa kubeba watu
mia na zaidi.

Kingine cha kushangaza ni kwamba, wote walikuwa wanavaa
mavazi meusi, iwe shuka au nguo ya
kawaida, ili mradi mwanamke avae
nguo ndefu hadi katika vidole vya
miguu yake.

Na kila siku wanayoingia katika hicho chumba ikifika usiku mkubwa,
walichukua magari makubwa ya
mizigo na kuenda wanapopajua
wenyewe, pamoja na wale mbuzi na
kondoo.

Ila baadae baba yako alikuja
kuniambia kuwa uwa wanaenda
kutoa sadaka katika mzimu wa mababu
zao walikufa miaka iliyopita, na kwa sasa yeye ndio
kaachiwa mamlaka ili autunze mzimu mmoja ambao ni mkuu kuliko mizimu yote wanayoiabudu.

Sikufurahishwa
na hali hiyo, ila sikutaka kumuudhi
mume wangu, baada ya miaka miwili
ya ndoa, nikajifungua mtoto wangu
wa kwanza ambae ni kaka yako", Mama Kayoza aliongea kisha akamimina maji katika kikombe na kunywa,

"mama mbona
huyo kaka yangu simfahamu, au yupo mbali na nchi hii?" kayoza
akahoji.

"Subiri sasa mbona una
haraka hivyo?" mama Kayoza
akauliza huku akimshangaa mwanae,

"Maswali ni lazima, sasa nisipouliza utajuaje kama nimekuelewa?" Kayoza alihoji

"Sikiliza kwanza, maswali utauliza nikimaliza kusimulia" Mama kayoza alijibu kisha akaendelea,

"baada ya kumzaa
kaka yako wa kwanza, furaha
iliongezeka katika familia yetu, ila kitu ambacho
kilikuwa kinanitatiza ni kuwa,
majirani hawakutaka kabisa
kunizoea na wala hawakutaka hata kuja kutujulia hali kipindi nimejifungua, sikujua sababu, ila siku
moja kuna jirani mmoja ndio
akanipasulia sababu, eti kuwa mume
wangu na ukoo wake ni wachawi wa
kutupwa, na kila mke aliyemuoa
hakukaa hata mwaka, alikufa,
wananishangaa mimi nimemaliza
miaka mitatu, na ninae mtoto
mkubwa tu wa mwaka mmoja.

Kiukweli ile habari ya wanawake kufa
iliniogopesha, ikabidi jioni ilipofika
nimuulize mume wangu, kwa kuwa
alinipenda alinieleza ukweli...

_____________________________
SEHEMU YA KUMI NA SABA.
_____________________________

Aliniambia kuwa, kila mwanamke
ambaye alimuoa, alimshauri aachane
na mambo ya mizimu, ilo suala
lilimuudhi na kuwaua kwa njia ya
kuwadhoofisha kiafya, ila mwisho wa
siku, mzimu wenyewe ukamshauri
asioe mwanamke ambae anatokea
Bukoba, ndo akaja kunioa mimi.

Akaendelea kuniambia
"tangu nimekuoa, sijaona hata siku
moja ukifatilia mambo yangu, na leo
ndio umeniuliza kwa mara ya kwanza
kuhusu mambo yangu yaliyopita
kipindi cha nyuma".

Baada ya baba
yenu kuniambia maneno haya,
niliridhika nayo kabisa na wala sikutaka kuuliza tena ingawa nilianza kuishi kwa hofu.

Baada ya miaka miwili nilifanikiwa
kuzaa mtoto wa pili, na hapo tukapanga
tusizae tena, na baba yako kwa mara
ya kwanza akaniambia kuwa
anaachana na mambo ya mizimu, mimi
nilipingana nae, ila hakunielewa.

Mimi niliendelea kupingana nae kwa sababu
nilihisi kuwa ndugu zake wanaweza
kuona mimi nilimshawishi baba yenu kuachana na mambo ya mizimu.

Baada ya
miezi sita tangu aitoe kauli ya
kuachana na mizimu, ni kweli aliacha kununua kondoo wa kuchinjwa kila mwisho wa mwezi, na pia aliwaambia ndugu zake warafute sehemu ya kufanyia ibada zao kwa kuwa yeye hakuwa tayari kuendelea na hizo ibada.

Mwanzo walikuwa wagumu kumuelewa, ila baadae walikubaliana nae ila kwa shingo upande.

Baada ya mwaka mmoja, tulianza kufilisika, gari zilipata ajali
kiutatanishi zikafa, nyingine
alidhulumiwa na ndugu zake ambao
walikuwa wanazisimamia, na hatua
ya mwisho kabisa na ambayo sikuwa
naifikiria kabisa, ni kwamba baba
yako aliamua kuuza nyumba zake
zote, hadi ile tuliyokuwa tunakaa,
kisha akatuchukua mimi na kaka
zako akatupeleka kijijini kwa mama
yake, ambaye ni bibi yako.

Huko sasa ndipo mauza uza yakaanza, Siku moja
wakati natoka kisimani kuchota maji,
nikamkuta kaka yako mkubwa,
amekufa kifo cha ajabu sana,
shingoni alikuwa na alama za meno,
kile kifo hata baba yako
kilimshangaza, tuliomboleza tukalia tukazika, mwishowe tukasahau.

Siku ya harobaini baada ya kile kifo, usiku wakati tumelala
na baba yako, tulishtushwa na
upepo mkali ulioezua paa la nyumba
tuliyokuwa tunakaa, wote tukakurupuka kitandani na kuanza kushangaa hiyo hali, wakati
tunautafakari ule upepo, kilitokea
kiumbe cha ajabu sana, wote tukabaki na mshangao ulioambatana na uoga.

Kile kiumbe hakikuonekana kujali hali tuliyonayo, kilimwambia
baba yako kuwa kinaitwa
NDIFU, ni mzimu wa ukoo, na kimekuja kutaka hifadhi, baba yako
akapata ujasiri na kumuuliza alikuwa
anataka hifadhi ya nini?, kile kiumbe
kikasema kinataka kuishi ndani ya mwili
wa mtu alie hai, baba yako
akamwambia sawa aende tu
akaishi, kile kiumbe kikakataa na
kusema anataka kuishi kwenye mwili
wa baba yako au kaka yako ambae
ndio huyo tu, tuliebaki nae, baba
yako akakataa.

Kile kiumbe kikasema,
kitu kitakachotokea asubuhi
tutakapoamka tusishangae, Kisha
upepo mkali ukakibeba na paa la
nyumba yetu likarudi kama
mwanzo, tukabaki tunashangaa huku kila mmoja akiwaza lake, ila mwisho tukajadiliana na kukubaliana tusubiri mpaka kesho ili tuone hicho kitakachotokea, tukalala.

Kesho tulipoamka ndipo
tukapata kitu kilichotupa mshtuko,
kiasi kwamba nikapoteza fahamu...

******ITAENDELEA******

the Legend☆
 
RIWAYA : KIJIJINI KWA BIBI.

MTUNZI : ALEX KILEO..

SEHEMU YA KUMI NA NANE.

_______________
ILIPOISHIA..
________________

Kile kiumbe kikasema,
kitu kitakachotokea asubuhi
tutakapoamka tusishangae, Kisha
upepo mkali ukakibeba na paa la nyumba yetu likarudi kama mwanzo, tukabaki tunashangaa huku kila mmoja akiwaza lake, ila mwisho
tukajadiliana na kukubaliana
tusubiri mpaka kesho ili tuone hicho
kitakachotokea, tukalala.

Kesho tulipoamka ndipo
tukapata kitu kilichotupa mshtuko, kiasi kwamba nikapoteza fahamu...

____________
ENDELEA..
____________
tulimkuta mtoto wetu wa pekee
amekufa kwa mtindo ule ule aliokufa
nao mtoto wetu wa kwanza.

Ndugu wa mume wangu walikuwa wanajua
chanzo cha vifo vyote vya
wanangu,baada ya mazishi kuisha na
watu kutawanyika, ndugu wa baba
yako wakamuita pembeni na
kumshawishi aurudie ule mzimu na
kuuomba radhi ili mambo yake
yarudi kama awali, ila baba yako
akakataa.

Baada msiba kuisha, ule
mzimu uliendelea kumuandama
baba yako, mi kuona umezidi ikabidi
nimwambie baba yako aukubali ili
aulee kama mwanzo.

Baada ya kauli ile, usiku mzimu ulitutokea tena tukiwa tumelala kitandani na kuongea maneno makali na ya kutisha juu ya msimamo wa baba yako, na kisha mzimu ukaongea maneno mazuri na kunisifia sana juu ya ushahuri niliompa baba yako, kwa ushauri ule niliompa baba yako, kuanzia hapo
ule mzimu ulinipenda mimi na
kuahidi kuwa kamwe hautanidhuru
mimi na mtu yeyote yule ambae ana
damu au nasaba moja na mimi, yaani mwanangu
na ndugu zangu wote tuliochangia wazazi wote, au baba tu, au pia mama tu.

"ndio maana Sajenti Minja haukumdhuru eee!?" Omary akauliza huku akimuangalia Kayoza,

"inawezekana
mwanangu, labda Minja hakudhurika kutokana na ahadi aliyonipa mzimu" Mama kayoza akajibu,

"Duh, hii habari inazidi kunisisimua, inawezekanaje mimi nikawa mzimu?" Kayoza aliuliza huku akijishangaa,

"Je unaamini kuwa nabii Musa aliweza kuipasua bahari ya shamu na akapita na wanaisraeli?" Mama Kayoza alimuuliza mwanae,

"Hiyo naamini" Kayoza alijibu huku akimuangalia mama yake,

"Sasa kwa nini huamini kuwa hata wewe unaweza kuwa mzimu?" Mama kayoza alimuuliza mwanae,

"Sasa utafananishaje mambo ya Mungu na uchawi?" Kayoza alimjibu Mama yake huku akionekana kutofurahia hilo swali,

"Huo uchawi uliumbwa na Mungu na manabii waliutumia ila waliuita muujiza na si uchawi" Mama Kayoza alimfafanulia mwanae,

"Endelea na simulizi yetu mama bwana" Kayoza akamuambia mama yake,

"Ngojeni kidogo" Mama kayoza aliongea kisha akainuka na kuelekea msalani.

****************

Sajenti Minja alienda mpaka nyumbani kwake, akaingia mariwatoni na kuanza kusafi mwili.

Alipomaliza alienda mpaka katika meza na kuanza kuandika barua ya kuacha kazi. Aliindika kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia ile nakala ya barua aliyopewa na yule Dada polisi.

Alipomaliza kuandika aliirudia tena na tena kuisoma na kuona haina makosa.

Akaiweka vizuri katika bahasha na hakuona haja ya kuchelewa kuiwasilisha ofisini kwa mkubwa wake ingawa muda ulikuwa umeenda sana.

Akatoka nje na kuchukua gari iliyomfikisha katika kituo cha kazi, na kwenda moja kwa moja mpaka kwa yule dada aliyempa maelekezo hawali, kwa bahati nzuri alimkuta,

"Umerudi tena? umemaliza nini kuandika?" Yule dada aliuliza huku akiwa anaamini Sajenti Minja kuna kitu kingine kafuata na wala sio kuwasilisha barua ya kuacha kazi,

"Ndio nimeileta barua hivyo" Sajenti Minja alijibu huku akimpatia ile bahasha yenye barua ndani,

"Kha! Wewe mtoto mbona umeandika haraka hivyo, hujajipa hata muda wa kufikiri?" Yule dada alimuuliza huku akimshangaa Sajenti Minja,

"Mpaka nimefikia hatua hii, ujue nimefikiria sana" Sajenti Minja alijibu huku akionekana kutofurahishwa na maswali ya yule dada,

"Wenzako wanatafuta kazi, wewe unaacha" yule dada alimuuliza Sajenti Minja huku akipokea ile bahasha,

"Ni bora nikae bila kazi kuliko kupambana na kiumbe cha ajabu" Sajenti alijibu kijeuri,

"Na kwenye barua umeandika sababu ya kuacha kazi ni kiumbe cha ajabu?" Yule dada aliendelea kuuliza huku akijua anamkera Sajenti Minja,

"Ifungue uisome, ukimaliza utairudishia kwenye bahasha nyingine" Sajenti Minja alijibu,

"Unaona huo ndio utakuwa ustaharabu?" Yule dada nae alimuuliza,

"Nadhani ndio itakuwa nzuri zaidi kuliko kuniuliza maswali ilihali majibu nimekupa ndani ya hiyo bahasha" Sajenti Minja alijibu,

"Okey, unaweza kwenda" Yule dada aliongea huku akiwa amekasirishwa na majibu ya Sajenti Minja,

"Kuna hivi vitu pia" Sajenti Minja alimpa bahasha nyingine ila ilikuwa kubwa zaidi ya ile ya mwanzo na pia haikufungwa,

"Na humu kuna nini?" Yule dada aliuliza huku akiipokea ile bahasha,

"Ipo wazi hiyo bahasha, unaweza tu kuangalia vilivyomo ndani" Sajenti Minja alijibu kisha yule dada akaingiza mkono na Kutoa kitu kimoja moja, ilikuwepo bastola, namba ya uaskari na kitambulisho cha Sajenti Minja mwenyewe.

"Sasa hivi unaniletea vya nini?" Yule dada aliuliza huku akimshangaa Sajenti Minja,

"Unapoacha kazi si unatakiwa kurudisha hivi vyote?" Sajenti Minja aliuliza,

"Hivyo utamkabidhi mkubwa wako, tena atakapokubaliana na maombi yako" Yule dada alijibu huku akivirudisha vile vitu katika mfuko ambao vilikuwepo hawali,

"Sasa kama nimeshawasilisha barua, hivi nikae navyo vya nini" Sajenti Minja aliuliza,

"Zingatia nilichokwambia, tusibishane hapa. Tena ulete mkanda, kofia na buti" Yule dada alimalizia,

"Sikupewa magwanda mimi, narudisha nilichopewa" Sajenti Minja alijibu huku akivipokea vile vitu vikiwa ndani ya ile bahasha,

"Sawa, kesho mchana nenda kwa mkuu, nadhani atakuwa ameshaipitia barua yako" Yule dada alimpa maelekezo Sajenti Minja.

Baada ya hapo Sajenti Minja akaondoka.

*****************

Mamá kayoza alipotoka msalani, akanywa maji kisha akaendelea,

"kuanzia siku ambayo mzimu aliniahidi hatonidhuru mimi na kizazi changu, nikawa najihisi niko tofauti na
mwanzo, kila nilichofanya
nilifanikiwa, nadhani mzimu aliamua kunionesha namna anavyonijali.

Baada ya miezi mitatu toka kaka yako wa pili amefariki, kwa bahati nikashika
mimba.

Siku ambayo niligundua nina mimba, mzimu alitutokea tena usiku na kuniomba sana niendelee na msimamo wangu wa kumshahuri baba yako juu ya kuujali huo mzimu, nami nikaitikia kwa kukubaliana nao.

Mimba ilipofikisha miezi tisa ndipo nilikuzaa wewe,
tena hapo ni baada ya kukaa mwaka mmoja tangu nilipompoteza
mwanangu wa pili.

Baada ya wewe kuzaliwa, sasa hapo yule
mzimu alichachamaa, alitutokea usiku na kusema kuwa anataka
kuingia kwenye mwili wa baba yako, Baba yako hakukubali hilo jambo,
hata baba yako alipokataa yule
mzimu hakuwa na cha kufanya kwa
sababu nilimuomba ampe baba yako muda wa kufikiri kwanza, na kwa kuwa mzimu aliniahidi kutonidhuru mimi
na ndugu zangu na damu yangu kwa
hiyo kazi yake ilikuwa kunilinda mimi
na nasaba zangu, mzimu akaondoka.

Miaka ikasogea na
mzimu haukuchoka kumsumbua
baba yako, ulitutokea kila siku na kuongea maneno ya vitisho juu ya Maisha ya baba yako, ila Baba yako aliendelea kushikiria msimamo wake.

Ikafika kipindi baba yako
akaanza kuumwa, aliumwa wiki
nzima na tulipoenda hospitali ugonjwa ukawa hauonekani, ghafla hali yake ikawa mbaya
zaidi, mwili ukadhohofika na hakuweza hata kuamka
kitandani.

Ule mzimu kuona Baba yako yupo katika hali ile, ukabadilisha
maamuzi ya kumuingia baba yako,
ukawa unataka kuingia ndani ya
mwili wako, ila baba yako
akapinga tena jambo hilo, tena alilipinga kwa nguvu zote ingawa alikuwa mgonjwa.

Kwa mila za kijijini kwa
baba yako mtu anapokuwa anaumwa
sana anatenganishwa na mke au
mme wake. Huduma zote muhimu anakuwa anahudumiwa na
mama yake au ndugu zake, kwa hiyo
baba yako alikuwa anahudumiwa na
mama yake ambaye ni bibi yako.

Sasa siku moja wakati niko nje
nakunyonyesha huku natayarisha
chakula, ghafla upepo ulivuma kwa
nguvu sana, kisha ukaingia katika
chumba alichokuwepo baba yako ambaye pia ndani alikuwa bibi yako.

Baada ya dakika tano za ukimya katika chumba kile, nikasikia mabishano yamezuka kati
ya bibi yako na baba yako, mara ghafla bibi yako akaja kukuchukua
mapajani kwangu, kwa ahadi ya kwamba kuna kazi anaenda kuifanya na
anakurudisha mda si mrefu.

Akaingia na wewe kwenye chumba alichokuwepo
baba yako, kisha yale mabishano
yakaendelea, baada ya muda kidogo
nikaskia baba yako analia kwa sauti
ya juu sana, ndipo nikatoka mbio hadi
katika chumba alichokuwepo Baba yako na
mama yake ambaye ni bibi yako, nikakukuta wewe Kayoza
unamnyonya damu baba yako" Mama kayoza aliongea
maneno haya huku machozi yakianza kumtoka....

******ITAENDELEA******

the Legend☆
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…