The Financials ; Mahesabu:
Baada ya mji wetu kujenga miundombinu ambayo mpaka sasa mikopo mingi tumeshalipa mji wetu ni endelevu na unajiendisha ingawa mji wetu una wakazi elfu Hamsini mji ungeweza kuwa na watu hata laki 5 ni kwamba miundombinu ingejengwa kulingana na wakazi husika.
Katika watu elfu 50, mji wetu una wazazi kama elfu 20 ambao wanafanya kazi na kulipwa pesa 500USD, (tunaweza kuziita units lakini kwa kufanya andiko hili lieleweke vizuri tutaziita Dollars) ; Hii inagharimu mji 10M USD kama malipo ya wakazi, tukichukulia familia nyingi zina wastani wa watu wanne Mama; baba na Watoto wawili pato la familia ni kama 1000USD kwa mwezi.
Elimu: Kila Mzazi analipia watoto wake elimu 100USD kwa mwezi (Yatima wanasomeshwa bure) kwahio (watoto 20,000 x 100USD) inamaanisha 2M USD zinakwenda kwenye Elimu kila Mwezi.
Chakula; Kila mtu ana uhakika wa kupata chakula bora (milo mitatu kwa siku) kutoka kwenye migahawa minigi iliyopo katika mji, ambapo wazee wanapata chakula bure, kila mtu analipa 80USD kwa ajili ya Chakula Bora (Milo Mitatu kwa Siku); kwahio mji wa watu elfu Hamsini ukiondoa wazee elfu 10 unakusanya (40,000 x 80USD) 3.2M USD kwa ajili ya kuhakikisha kila mtu anatapa variety ya chakula bora.
Afya: Huduma za afya zinapatikana kwa kila raia na mji wetu unajikita zaidi kwenye kinga kuliko kuponya; kwahio tumejikita zaidi kwenye uchunguzi wa Tiba asilia na elimu ya afya kwa watu wote; na sababu tunajua wazee ni sehemu ya jamii yetu na ni hatima ya kila mmoja wetu watu wa uangalizi (social care) ni muhimu sana na hii ni moja ya ajira za kudumu ambazo tunajua hata tukifanya automation kiasi gani bado itahitajika. Ili kugharamia afya ukiondoa wazee kila mtu anatoa 20USD kwa mwezi kwahio (watu 40,000 x 20USD) mji unakusanya 800,000USD kwa ajili ya Afya kwa wote kila mwezi.
Marekebisho / Ukarabati; ili kufanya watu waweze kuishi vizuri ndani ya mji na katika mji safi na unaopendeza kuna kazi katika kapu la kazi za ukarabati, usafi na recycling; kwa kufanikisha hili kila nyumba inatoa 10USD kwa mwezi (nyumba 10,000 x 10USD) jumla ya 100,000USD zinakusanywa kila mwezi kwa ajili ya Usafi.
Usafiri: Kuna usafiri wenye ufanisi ndani ya mji na wa kwenda kwenye sehemu za kazi (eco - industrial parks) usafiri huu mbali na kuwa fanisi ni rafiki kwa mazingira. Na kutokana kwamba usafiri huu ni wa kutumia nishati ya umeme na sio mafuta kwahio uendeshaji wake ni wa gharama nafuu ukizingatia gari la mafuta lina sehemu nyingi za injini tofauti na umeme kwahio service yake ni gharama nafuu. Kwa wale wanaotaka kwenda nje ya mji wanaweza wakakodisha magari kutoka mradi wa kukodisha wa mji. Ili kufanikisha usafiri na usafirishaji kila mtu ukiondoa wazee anapewa ticket ya kusafiri bila kikomo ndani ya mji na kwenda kwenye sehemu za kazi, ticket hiyo itamgharimu kila mkazi ukiondoa wazee 10USD (kwahio mji utakusanya watu 40,000 x 10USD jumla ya 400,000 USD kwa mwezi kuhudumia usafiri (kumbuka hapo nishati inakusanywa bure kwahio gharama ya uendeshaji ni ndogo sana)
Makazi; Pamoja na uhakika wa ujira kila mkazi kila mtu ana uhakika wa Makazi; Makazi bora ya gharama rafiki ambayo mkazi analipia kwa muda mrefu bila riba. Wamiliki hawa wa nyumba wanalipa 100USD kila mwezi ili kutunisha mfuko wa nyumba. Pia nyumba hizi zinaweza kutumiwa kama mafao ya uzeeni mara nyingi wazazi hawa wakizeeka wanauza nyumba kwa Jiji na kuhamia kwenye nyumba za wazee ambapo kuna msaada na uangalizi mzuri zaidi. Kwahio ada ya Makazi kutoka kwenye nyumba elfu 10 Mji unakusanya (nyumba 10,000 x 100USD) jumla 1M USD kila mwezi.
Mafao ya Uzeeni; Kwa kusaidia watu wakistaafu wapate mafao ya uzeeni ingawa huduma nyingi ni bure kwa wazee kila mtu katika maisha yake ya ufanyaji kazi anachangia 20USD kwa mwezi kwa ajili ya mfuko wa Mafao; Hivyo mji unakusanya kutoka kwa wazazi 20,000 x 20USD jumla ya 400,000USD kwa ajili ya mfuko wa mafao ya uzeeni.
Kwahio kwa ufupi; Mji utatumia 10M USD kwa ajili ya mishahara kila mwezi; na ukiondoa pesa ambazo mji utazipata katika mauzo ya starehe, na bidhaa nyinginezo ambazo watu watanunua kutoka kwenye pesa yao inayobaki baada ya matumizi mji utakusanya 2M kutoka kwenye Elimu; 3.2M kutoka kwenye Chakula kwa wote; 800,000 USD kwa ajili ya Afya; 100,000 USD kwa ukarabati wa mji. 400,000 USD kwa usafiri na usafirishaji; 1,000,000USD kwa ajili ya Makazi na 400,000 USD kwa ajili ya mafao ya Uzeeni; kwahio mji utakusanya 7.9M moja kwa moja na pesa nyinginezo kutoka kwenye Starehe na manunuzi mengine.
Tukiangalia kwa upande wa mtumiaji yaani Kaya; familia ya watu wanne yenye mama na baba ambao wanafanya kazi kwenye mshahara wao wa 1000USD kwa mwezi baada ya kila mmoja wao kufanya kazi kwa muda mchache iwezekanavyo; matumizi yatakuwa kama yafuatavyo:-
- 200 USD kwa elimu ya watoto wao wawili (Baki 800USD)
- 320 USD kwa chakula bora kwa mwezi mzima - watu wanne (Baki 480USD)
- 80 USD kwa ajili ya Afya (20USD x watu wanne) (Baki 400USD)
- 40 USD kwa ajili ya Usafiri (watu wanne) (Baki 360)
- 20 USD mafao ya Uzeeni (watu wawili) (Baki 320)
- 10 USD kwa ajili ya Usafi (Baki 310)
- 100 USD kwa ajili ya Makazi (Baki 210)
Kwahio hawa wazazi wawili watakuwa na angalau 105 USD kila mwezi kwa kila mmoja kuweza kutumia anavyotaka kwa matumizi mengine ukizingatia matumizi muhimu mengine yote yametekelezwa.
Nakumbuka wakati tunapiga mahesabu haya wakati bado tunaishi kwenye mabanda yetu katika kijiji kabla hakijawa mji; Nilimuuliza Busara..., Vipi kuhusu watu ambao hawapo kwenye Mpango wa Mji na wanataka kutembelea huu mji, ni nini kitakachowazuia kufisadi bei nafuu za vitu vinavyouzwa ndani ya mji au kununua vitu ndani ya mji kwa bei nafuu na kuviuza pengine ? Najua kwenye nyumba tuna sheria ya kulinda kwamba mmiliki anaweza kuuza wakati wowote ila kuuza kwake atauzia mji kwa bei ya gharama za wakati huo hii itazuia watu kununua nyumba nyingi ili kupangisha wengine..., lakini ni kipi cha kuzuia watu kununua bidhaa nyingine na kuzifanyia magendo ?
Rafiki yangu akadakia huenda Busara anataka kuanzisha pesa yake mwenyewe yaani pesa ya mji tofauti na pesa nyingine......
Busara alijibu haraka hapana kutengeneza pesa yenu wenyewe ni kinyume cha sheria na kwa kufanya hivyo tunaweza kujikuta mikononi mwa sheria..., Kumbuka hizi Pesa nimesema tu pesa ili kuweza kueleweka zaidi tunaweza kuziita units / tokens au hata credits... kumbuka mji utakuwa cashless na bidhaa, manunuzi mshahara na kila kitu kitakuwa kinafanyika electronically kwa kutumia mfumo wa Block Chain..., Fulani akilipwa mshahara na akinunua kitu inaonekana kabisa kwamba unit hii imetoka hapa imekwenda pale na ikirudi tena kwenye mji hapo tutakuwa tumetengeneza utajiri (creating wealthy from productivity) tofauti na mifumo ya sasa ambapo pesa / wealthy inatengenezwa kutoka hewani na mabenki yanavyotoa mikopo....
Na kwa kujibu swali la rafiki yangu kuhusu watu wa nje ambao watataka kununua bidhaa au kufurahia maisha tutawapokea kwa mikono miwili na kwa ukarimu na kuwahudumia....
Eeehh ?!!! Nilijikuta nauliza kwa mshangao, kivipi ?
Busara aliendelea kama nilivyoshaelezea miamala yote ndani ya mji itakuwa ni ya ki-elektroniki kwa kutumia mfumo wa block chain; na kama nilivyosema kuwa na mfumo wa cashless utafanya miamala kuwa rahisi. Kwahio kila mgeni anayeingia kwenye mji atabadilisha pesa zake kwa kununua tokens / credits za kwenye mji ili aweze kufanya manunuzi ndani ya mji.
Anabadilisha kwa Exchange Rate...., Kiwango gani cha pesa ? niliendelea kudadisi....
Swali zuri sana...., kama ulivyoshagundua bidhaa ndani ya mji zitakuwa na gharama nafuu sana zenye faida ndogo sana na bidhaa ambazo hazitengenezwi ndani ya mji zitanunuliwa kwa wingi na kwa bei za jumla kwa ajili ya matumizi ya mji...., hivyo basi kwa mji kuhakikisha inapata fedha ya kuweza kununua bidhaa ambazo haitengenezi ndani ya mji na pia kuzuia watu kutumia mianya ya bei nafuu kujinufaisha..., mambo mawili makuu yatafanyika;
Moja:
Kubadilisha pesa kutoka currency / pesa moja kwenda kwenye tokens / credits za mji itazingatia bidhaa ambazo mji unatakiwa kununua kwa wakati huo kutokana na mahitaji yake na ni kiasi gani pesa hio inaweza kununua bidhaa hio...., mfano kama tuna uhaba wa mchele na kubadilisha pesa kukazingatia kilo moja ya mchele, na tuseme kwa wakati huo kilo moja ya mchele ni 1USD; mji unaweza kuamua kilo kumi za mchele ni sawa na Credit/Token Moja ya Mji yaani sawa na 10USD. Kwahio kwa kipindi hiki mtu mwenye US Dollars atapewa City Credit 1 akitoa 10USD. Na hii inatafanyika kwa watu ambao hawapo kwenye program ila kwenye miji ambayo inashirikiana na ipo kwenye mpango huu wataweza kutumia credit za miji yao bila haja ya kubadilisha.
Nilijikuta nasema..., kinadharia inapendeza lakini utendaji wake na mafanikio yake bado yananitia shaka..., enhee nini jambo la pili;
Mbili:
Utakuwa umeshagundua kwamba kwa watu waliopo kwenye huu mfumo bei ya bidhaa ni nafuu sana na mfumo huu umehakikisha unapata faida finyu sana ili kuhakikisha watu wake wanabudu bei na kubakiwa na pesa ya kufanya mambo mengine...., Hivyo basi vitu kama Afya, vyakula vya ziada, vinywaji na vilevi n.k. vitakuwa na bei ya juu kidogo kwa watu ambao hawapo kwenye mfumo na wamepata credit zao kutokana na kubadilisha pesa zao..
Nakumbuka yule jamaa mtata aliyekuwa amechoshwa na maisha yetu ya kijijini kipindi kile aliuliza kwa dhiaka..., Ngoja kidogo Mzee...., tuseme kwamba mimi ni kinyozi....
Kwa usahihi zaidi tuseme wewe ni mkazi wa mji mwenye ujuzi wa kunyoa....
Sawa..., tuseme ujuzi wangu ni wa kiwango cha juu duniani hakuna mwingine na naweza kwa kichwa kimoja kulipwa dollar 10..., hii inamaanisha nikiwahudumia watu 10 kwa siku naweza kupata 1500USD ambayo ni mara tatu ambacho takipata kwenye mji wenu...., kwanini nibakie kwenye mji wenu badala ya kujiajiri kwa kuwa na banda langu la kunyoa.
Busara alimuangalia kwa muda wa kama dakika tano...., nikaanza kuwaza huenda leo Busara ameshikika, Naam kwanini usiwe na duka lako mwenyewe..., Ni kweli ni bora na faida zaidi ufanye hivyo, na sisi kama mji kama tunaweza kuiga ujuzi wako tutafanya hivyo na kufundisha wengine ili waendelee kufanya ulichokuwa unafanya wewe...
Jamaa alitoa kicheko na kutoa tabasamu la kejeli...., kwahio pamoja na kufanya yoote uliyofanya mwisho wa siku mnaweza mkajikuta wajuzi, wabunifu na watu wenye vipaji wanaondoka kwenye mji wenu...
Polepole kijana, aliendelea Busara...., nimekubaliana na wewe kwamba unaweza ukatengeneza banda lako mwenyewe lakini nina uhakika hauwezi kupata manufaa sawa na manufaa ambayo ungeyapata kama ungebakia kwenye mji, kwa pesa ya ziada ambayo utaipata.
Kwanini ?!! jamaa aliuliza....
Kwanza kabisa kuwa na miundombinu ya kisasa kwenye jengo la kisasa na la kifahari na wahudumu wanaojali na kupenda kazi yao utahitaji uwekezaji mkubwa sana jambo ambalo litapunguza faida yako.., bila kusahau gharama ya pango.... Pia kumbuka hii ni package (kifurushi) ambacho pesa ni sehemu ndogo sana ya mpango mzima; Kwahio unaweza ukawa na dollar zako 1500 bila nyumba, mafao ya uzeeni, mpango wa afya, elimu kwa watoto wako, uhakika wa chakula bora, uhakika wa usafiri n.k.
Jamaa alicheka kwa kebehi..., kwani siwezi kuvipata hivyo sehemu nyingine ?
Busara aliendelea kwa upole..., ni kweli unaweza, lakini nina uhakika huwezi kupata ubora unaopatikana kwenye mfumo na kwa gharama sawa ya mfumo..., bila kusahau kutokuwa na msongo wa mawazo kwa kufahamu fika kwamba maisha yako yote yana uhakika tangia siku unazaliwa mpaka siku unapoaga dunia, na wapendwa wako wote utakaowaacha watakuwa kwenye mikono salama. Vilevile utakuwa umeondokana na sintofahamu ya kutokujua lini wateja watakuja au utaendelea kuwa kinyozi bora mpaka lini au ushindani utakuondoa pindi akija mtu bora kuliko wewe....
Nina uhakika atakuwa hana anasa ya kufanya kazi kwa masaa machache iwezekanavyo...., niliongezea...
Kweli kabisa, alisema Busara mwisho wa siku anaweza kujikuta anafanyia kazi pesa badala ya pesa kufanya kazi kwa ajili yake... (anakuwa mtumwa wa pesa)
Nakumbuka tulipotoka..., nikiona tulipofika kweli ni makubwa yamefanyika, na haya yaliweza kufanikiwa kwa kutumia nguvu na kuwa na Dira, yaliweza kufanikiwa sababu wote waliofanikisha mafanikio hayo walikuwa na kiu, walikuwa na uduni waliotaka kuondokana nao na mafanikio hayo yalifanyika kwa juhudi zao wenyewe...
Kwa mfano mimi nisingekuwa mbangaizaji na nina shughuli zangu za kufanya mtu angekuja na kuniambia niachane na kidogo nilichonacho ili niende kutafuta kingi ambacho hakina uhakika...., kwa hakika nisingemsikiliza na ningempuuza, lakini sababu maisha yangu na waliotuzunguka yalikuwa duni na tulikuwa hatuna pa kukimbilia pindi tukatapo tamaa tulihakikisha tunafuata hatua kwa hatua kuelekea kwenye kesho yetu tuliyoitamani.
Kweli Maisha Matamu Sana Haya.....
MWISHO