SEHEMU YA KUMI NA SABA.
Sikugeuka nyuma wala sikupunguza mwendo.Nilikua natoka kasi kweli kweli. Niliibukia katika eneo nililolifahamu ambapo nililiona jengo la Internationa House likiwa kulia kwangu. Nilikunja kushoto kwenye makutano ya ile barabara niliyotoka nayo na ile ya kuelekea kwenye lile jengo la International House na Holiday Inn na kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka huku nikikimbia kidogo kidogo, nikichukua uelekeo wa jengo la PPF Tower. Jasho lilikuwa likinitirirka vibaya sana na sina hata haja ya kukuambia jinsi moyo ulivyokuwa ukinipiga. Miguu ilikuwa ikinitetemeka na nikahisi maumivu kwenye sehemu ya juu ya mkono wangu wa kulia. Nilipojitazama nikaona kuwa nilikuwa nimejichanja na kipande cha kioo pale niliporuka dirishani. Kioo kilichana mkono wa lile koti langu gumu la jeans na kwa kiasi kikubwa kabisa lile koti lilipunguza makali ya kile kioo na hivyo kupunguza ukubwa wa lile jeraha ambalo lilikuwa likichuruzika damu kidogo, lakini hilo nililiona kuwa ni swala dogo sana. Niliangaza huku na huko, kila mara nikitaraji kusikia mtu akinipigia ukelele kuwa nisimame au akiwapigia kelele wapita njia wengine kuwa wanikamate.
Nililipita duka la Imalaseko na kuongeza kasi kuelekea barabara kubwa ya Azikiwe. Hatua kadhaa mbele yangu niliona daladala kubwa aina ya Isuzu Journey likisimama kwenye makutano ya ile barabara niliyokuwapo na ile ya Azikiwe kuelekea posta ya zamani, na kondakta akinipigia kelele akiniuliza iwapo nilikuwa ni msafiri. Kwa rangi ya mstari wa lile basi, niliona kuwa lilikuwa ni basi linalofanya safari za Mwananyamala-Posta.Sikufikiri zaidi, nilimpungia mkono anisubiri huku nikiongeza mbio.
Kwa wakati ule, basi lolote lingekuwa muafaka kwangu. Niliparamia lile basi kwa pupa nalo likaondoka kwa kasi eneo lile kuelekea maeneo ya posta ya zamani, huku yule kondakta akishangilia na kurukaruka mlangoni, nami nikijibwaga kwenye kiti nikitweta huku nikijifuta jasho kwa mkono wa koti langu. Tulipofika eneo la posta ya zamani nilipatwa na kihoro baada ya kuona tukisimamishwa na askari wa usalama barabarani. Niliangaza huku na huko na nikaona magari yote yaliyokuwa pale barabarani yalikuwa yamesimama, yakifanya foleni kubwa. Nilichanganyikiwa vibaya sana. Niliinuka na kutaka kuteremka, lakini konda alinizuia, akiniuliza iwapo nilikuwa nataka kuwalipisha faini ya elfu ishirini kwa kuteremsha abiria sehemu isiyo kituo, tena mbele ya wana usalama. Niliketi kwenye kiti huku akili ikinizunguka.
Ina maana huu ni msako kwa ajili yangu?
Nilitoa kichwa nje ya dirisha na kutazama kule mbele tulipokuwa tukielekea. Mwili ulinifa ganzi niliposhuhudia askari wa jeshi la polisi zaidi ya sita wakiwa wameshika bunduki aina ya SMG wakiwa wametanda mbele ya barabara, baina yao wakiwamo askari wa usalama barabarani.
Nimekwisha!
Nilimgeukia konda na kumuuliza kwa sauti ambayo nilishindwa kuamini kuwa ni yangu.
“Ni...ni kitu gani? Kuna nini mbona tumesimamishwa?”
Konda alinitazama kwa muda kabla ya kuniuliza. “Anti vipi...? Una haraka sana nini?” Nilimtazama kidogo kisha nikapeleka uso wangu pembeni, asije akanishika sura halafu akaja kuniletea matatizo hapo baadaye.
“Hao ni wenye nchi wanapita dada yangu, eeeh!” Yule konda aliniambia baada ya kuona kuwa sikumjibu hapo awali, kisha akaongezea. “Hii ndio Bongo dadaangu, Ohooo! Namna hii mtu hata umpe nini hakubali kuachia madaraka. We’ watu wote tunasimamishwa ili mkuu apite bwana! Hata ingekuwa mimi siachii ngazi mwanangu!” Abiria waliangua kicheko nami nikabaki nimeduwaa huku nikihisi moyo ukinipiga kwa nguvu.Kwa hakika nilikuwa nimeshikwa na woga mkubwa.
Kumbe ni msafara wa kiserikali tu!
Nilishusha pumzi za faraja kwani nilijua kama ule msako ungekuwa kweli ni kwa ajili yangu basi nisingekuwa na namna ya kujiokoa. Muda si mrefu ving’ora vilisikika na msafara mrefu wa magari ya kifahari ambayo hayakuwa na shaka kuwa ni ya serikali ulipita, nasi tukaruhusiwa kuendelea na safari yetu muda mfupi baadaye. Nilitahamaki kuona lile basi likikunja kuelekea maeneo ya feri badala ya kule posta ya zamani kama nilivyotarajia. Kumbe lilikuwa ni basi la Mwananyamala-Kivukoni. Hii ilikuwa ni mbaya kwangu, kwani nilitaka nipotee lile eneo la mjini haraka iwezekanavyo. Sasa hii ya kuelekea Kivukoni tena si ndio ninazidi kujizamisha ndani ya mji kabisa. Nilitaka kumpigia kelele konda aniteremshe, lakini nikachelea kuonekana kituko bila sababu.
Niliamua kutulia kufuata safari ya lile basi. Potelea mbali.
Nilipofika Kivukoni niliteremka baada ya kuona lile basi lilikuwa linaendelea kusubiri abiria wajae ndio lianze safari yake ya kuelekea Mwananyamala. Niliamua kutafuta basi lolote litakalonitoa katika yale maeneo ya katikati ya mji na kunirudisha uswahilini ambapo ningeweza kupotea kirahisi, ingawa sikuwa na wazo nielekee wapi hasa. Nilianza kuangaza huku na huko pale kituoni nikitafuta basi lolote ambalo lilikuwa liko tayari kuondoka eneo lile wakati niliposhituka kwa kihoro baada ya kuona umma wa watu ukinijia mbio kama kwamba walikuwa wanamkimbiza mwizi.
Moyo ulinilipuka na woga ukanitawala.
Ni nini tena? Wamenijuaje?
Nilianza kukimbia kidogo kidogo huku akili ikinizunguka kwa woga na mwili ukiniingia baridi.
Lakini mbona walikuwa wananikimbiza kimya kimya? Au...?
Na hata pale nilipokuwa nikijitahidi kukimbia kwa wasiwasi na woga mkubwa, nilishuhudia wale watu wakinipita bila hata kunijali na badala yake wakiendelea kutimua mabio kuelekea mbele.
What is happening...?
Niliendelea kukimbia huku nikiangaza huku na huko, nikijaribu kuwatazama wakimbiaji wenzangu kwa mshangao nisijue kinachoendelea, halafu nikaelewa.
Wanakimbilia pantoni!
Kama mwehu nami nikakaza msuli na kutimua mbio kwa nguvu zangu zote kuikimbilia ile pantoni. Niliiwahi nikiwa miongoni mwa watu wa mwisho kabisa, na muda si mrefu ile pantoni ikauacha ukingo wa bahari na kuanza safari ya kuelekea Kigamboni. Nilijiegesha kwenye kona moja mle ndani na kujikunyata nikilitazama jiji la Dar es Salaam likirudi nyuma taratibu wakati ile pantoni ikikata maji kuelekea upande wa pili wa bahari ya Hindi.
Mwili wote ulikuwa ukiniuma na miguu ilikuwa ikinivuta kuliko kawaida. Nikiwa ndani ya pantoni nilitoa kitambaa changu cha kichwa na kujifunga kichwani, nikizificha kabisa zile nywele zangu za rasta.
Niliteremka upande wa pili wa bahari na kujiunga na msururu mrefu wa wasafiri wenzangu kuelekea katikati ya kitongoji kile cha Kigamboni. Sikuweza kabisa kuiruhusu akili yangu iyatafakari matukio ya asubuhi ile, kwani nilihisi kuwa ningeweza kulipuka wazimu ghafla. Nilipitia kwenye maduka ya pale karibu na kipando cha pantoni na kununua nguo za kubadili kwani zile nguo zangu zilikuwa zimeanza kutoa harufu ya jasho, na pia nilijua kuwa kufikia sasa nilikuwa najulikana nguo nilizovaa, hivyo polisi wangekuwa wanamsaka mwanamke aliyevaa suruali na koti la jeans, kijitopu chekundu kwa ndani, akiwa amesuka nywele katika mtindo wa rasta. Kwa kuwa bado nilikuwa na pesa za kutosha, nilinunua nguo kadhaa za kubadili na kuongeza begi jingine dogo ambamo niliweka zile nguo zangu mpya. Niliingia duka la dawa na kununua dawa ya kidonda, bandeji, mswaki na dawa ya meno.
Kisha nilikodi teksi na kumuambia dereva anipeleke kwenye nyumba nzuri ya wageni iliyotulia. Alinipeleka kwenye nyumba moja ya wageni ambayo niliafikiana naye kuwa ilikuwa imetulia. Nikijiandikisha kwa jina la Nuru bint Shaweji, nilikodi chumba cha self contained kwa muda wa siku tatu. Kazi yangu nilijiandikisha kama mwanafunzi wa chuo cha elimu ya sayansi ya bahari cha Zanzibar. Sababu ya ujio wangu pale Kigamboni ikiwa ni kuandika juu wa mwenendo wa pwani ya Kigamboni. Maelezo yote haya nilijua kuwa ni upuuzi na uongo mtupu, lakini ilikuwa ni vigumu kwa yule jamaa wa mapokezi, ambaye alionekana kuwa hakwenda shule kiasi cha kuweza kuelewa mambo kama yale, kuyatilia maanani na kuyafuatilia.
Nilijifungia chumbani kwangu na kuelekea moja kwa moja bafuni ambapo nilioga kwa muda mrefu. Kisha niliosha na kufunga kidonda changu, kabla ya kujibwaga kitandani na kuchapa usingizi mzito.
v.
J
ambazi lauawa na pingu mkononi.
Kilikuwa ni kichwa cha habari kilichochukua uzito wa juu kabisa katika moja ya magazeti ya kila siku yanayotoka jioni. Moyo ulinilipuka na kuanza kunienda mbio, huku nikishuhudia lile gazeti likitetemeka mikononi mwangu wakati nikikodolea kwa kutoamini kichwa kile cha habari.
Ilikuwa ni majira ya saa moja za jioni wakati nikiwa napata mlo wa jioni kwenye mgahawa wa ile nyumba ya wageni wakati nilipoona kile kichwa cha habari kutoka kwenye moja ya magazeti yaliyokuwa yakitembezwa na kijana mmoja ndani ya mgahawa ule. Nilinunua haraka lile gazeti huku hamu ya kula ikiniisha. Niliinamia sahani yangu ya chakula na kukichezea chezea kwa muda kile chakula, kisha nikarudi chumbani kwangu upesi na kuanza kuisoma habari ile.
Macho ya Nyoka ameuawa!
“Haiwezekani! Haiwezekani auawe kirahisi namna hii! Macho ya Nyoka! Labda ungeniambia Dokta Martin Lundi, ningeweza kuamini, lakini sio Macho ya Nyoka!” Nilikuwa nijisemea peke yangu mle ndani huku nikitikisa kichwa kukana habari ile huku nikiiona kwa macho yangu pale gazetini.
Hapana bwana, kwangu hilo lilikuwa haliwezekani kabisa. Yule mtu ni muuaji wa kuzaliwa. Yaani yeye ndiye mwenye kazi ya kuua watu, sasa iweje tena yeye ndio auawe kirahisi namna hii?
Sio Kweli. Hii ni mbinu yao tu ya kutaka kunilaghai ili nijiamini kuwa niko salama halafu wanikamate kirahisi. Macho ya Nyoka ndiye mtu niliyemuhofia kuliko wote miongoni mwa wale wauaji niliowaona kule msituni, na nilishapata hisia kuwa kama sitanusurika na maisha yangu katika kindumbwendubwe hiki, basi ni Macho ya Nyoka ndiye atakeniua. Sasa tena hii habari...hapana si kweli!
Macho ya Nyoka afe! Sikuamini.
Lakini gazeti ndivyo lilivyoandika!
Macho ya Nyoka aliniahidi kifo cha mateso makubwa kwa macho tu na nikaelewa bila shaka yoyote ni nini alikuwa akiniahidi! Yaani hakutamka hata neno moja! Macho tu, na ujumbe ukafika!
Nilikumbuka yale macho yake jinsi yalivyoniahidi kifo pale aliponitazama kwa chuki huku akininyooshea kidole kabla hajatimua mbio kumkimbia yule afisa wa polisi, pingu ikimning’inia katika mkono mmoja.
Eti amekufa!
Nilikumbuka ule mlipuko wa bastola niliosikia ukitokea kule nje walipokuwa wakikimbizana, baada ya yule afisa wa polisi kuniamuru nisiondoke wakati akimfuata mbio yule muuaji. Nami nikaamua kutimua mbio kutoka eneo lile bila ya kujali kelele za Suleiman Kondo kuwa nisikimbie.
Pamoja na kuona kuwa kile kilichosemekana kutokea kuwa hakiwezekani, sikuweza kujizuia kuisoma ile habari iliyoandikwa gazetini kuhusu tukio lile lililotokea asubuhi ya siku ile pale ofisini kwetu.
Na hata nilipomaliza kuisoma kwa mara ya pili, bado nilibaki mdomo wazi na kujiuliza iwapo nilitakiwa niiamini au nisiiamini habari ile.
Kwa mujibu wa gazeti lile, ni kwamba jambazi hilo ambalo bado jina lake halijatambulika, liliuawa katika mapambano na polisi baada ya kufanikisha kutoroka kwa mwanamke ambaye alikuwa ametiwa mbaroni na polisi kuhusiana na mauaji ya kutatanisha ya watafiti wa Idara ya Makumbusho ya Taifa pamoja na watu wengine huko Manyoni.
Kutokana na maelezo ya gazeti lile, nilielewa kuwa Macho ya Nyoka alipokuwa akikimbizwa na yule askari, aliamua kusimama ili apambane naye, ambapo alitoa bastola (hii itakuwa nyingine, ambayo bila shaka alikuwa nayo – kwani ile bastola yake ndiyo aliyokuwa akiitumia yule askari baada ya kuangushwa chini katika mapambano), lakini kabla hajaitumia, yule askari alimuwahi kwa risasi ya mguu, na alipozidi kujaribu kumtupia risasi ndipo yule askari alipompiga risasi nyingine(sikumbuki kusikia mlipuko wa pili wa bastola, lakini wakati huo mimi ndio nilikuwa nimehamanika nikitafuta namna ya kutokomea kutoka eneo lile) iliyompata kifuani na kumuua.
Just like that...!Yaani hivi hivi tu!
Baada ya hapo gazeti lilielezea tena habari za yale mauaji ya kule Manyoni, na kutaja kuwa mwanamke aliyetoroka katika tukio lile bado anatafutwa na polisi na kutaja jina langu halisi, huku likinukuu taarifa ya polisi kuwa mwananchi yeyote atakayemuona au kuwa na habari zozote za mahala anapoweza kupatikana mwanamke huyo, atoe taarifa katika kituo chochote cha polisi kitakachokuwa karibu naye.
Kwa kuwarahisishia kazi wananchi, wasifu wangu wote ulielezwa gazetini, ikiongezewa na taarifa ya nguo nilizokuwa nimevaa siku ile pamoja na mtindo wa nywele niliokuwa nimeusuka. Nilishukuru mungu kuwa ingawa nilipoingia pale kwenye ile nyumba ya wageni nilikuwa nimevaa zile jeans zangu, nywele zangu za rasta nilikuwa nimezifunga ndani ya kilemba ambacho hadi muda ule nilipokuwa nakula pale kwenye mgahawa bado kilikuwa kichwani mwangu, na nilikuwa nimebadilisha nguo.
Zaidi ya hapo, picha yangu yenye ukubwa wa pasipoti iliwekwa pale gazetini, picha ambayo sikuwa na shaka ilitoka pale ofisini. Ni picha ambayo niliipiga siku chache baada ya kumaliza masomo yangu Chuo Kikuu, niliyoiwasilisha pale ofisini wakati naanza kazi kwa ajili ya kuwekwa kwenye faili langu binafsi la ajira. Katika picha ile nilikuwa naonekana mdogo zaidi, mwembamba zaidi, na zaidi ya hapo nilikuwa nimekata nywele zangu na kuziacha ndogo ndogo sana, ikiwa si siku nyingi tangu nitoke kwenye msiba wa baba yetu, ambapo kutokana na msiba ule, nilinyoa nywele zote.
Haikuwa picha ya kunitia shaka sana, lakini niliogopa kupita kiasi, kwani sasa jina langu lilikuwa hadharani, na wajihi wangu ulikuwa gazetini kwa kila mwenye macho kuuona.
Nitakimbilia wapi sasa?
Bila hata kufikiri zaidi nililitupa pembeni lile gazeti na kuanza kufumua zile rasta.
Hivi ni kwa nini haya mambo yanatokea?Ndilo swali lililokuwa likijirudia tena na tena kichwani mwangu tangu nilipoamka kutoka kwenye ule usingizi mzito ndani ya ile nyumba ya wageni. Na baada ya kusoma zile habari za kwenye lile gazeti, nilijikuta nikizidi kujiuliza lile swali. Na kila nilipojiuliza swali lile,nilijikuta nikijiuliza swali jingine kubwa na gumu zaidi. “Kwa nini mambo yale yanikute mimi katika watu wote?”
Kwa kweli wakati natimua mabio baada ya tukio la pale ofisini, sikuwa na hakika kama nilikuwa nachukua uamuzi wa busara, kwani nilipoyatafakari upya matukio yote yaliyotokea pale ofisini siku ile, nilipata hisia kuwa huenda yule afisa wa jeshi la polisi alikuwa ni askari wa kweli, na kwamba hata kama alikuwa na nia ya kunikamata kwa makosa yale aliyonitamkia pale ofisini kwa Mkurugenzi, kutokea kwa Macho ya Nyoka na matendo yaliyofuatia, kungeweza kabisa kumbadilisha mawazo na labda angeweza kuwa ndiye mtu wa kunisaidia, hasa nikizingatia kuwa yule alikuwa ni afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la polisi.
Lakini kwa wakati ule ningeyajuaje hayo? Ningeweza kuyachezea bahati nasibu maisha yangu? Hapana, bora nilivyokimbia.
Lakini kila nilipozidi kutafakari tukio la pale ofisini na uamuzi niliochukua, ilinifunukia wazi kuwa sasa nilikuwa naendeshwa na hisia zaidi kuliko kitu kingine chochote. Kuwa ujumla wa matukio yote yaliyonikuta huko nyuma hadi kufikia sasa, umepelekea hisia zangu zote kufikia hatua ambapo zilikuwa zinaanza kutekeleza matendo ya kujihami na kujiokoa kwanza, halafu kutafakari juu ya hatua hizo baadaye. Baada ya matukio ya kule kwa mkuu wa wilaya nilipokimbilia kutafuta msaada, na yale ya kule kwa Kelvin na nyumbani kwa mama yangu, nilikuwa nimejitosheleza fika akilini mwangu kuwa sehemu pekee yenye usalama kwangu ni pale nitakapokuwa peke yangu. Na kwamba kila nitakayemdhania kuwa huenda akawa na msaada kwangu, anaondokea kuwa upande wao.
ITAENDELEA