RIWAYA: Mume Gaidi

RIWAYA: Mume Gaidi

SEHEMU YA 16


Patrick na kundi lake wakajiandaa kuifanya hiyo kazi hatari.
Kazi yenyewe ilikuwa ni kumteka mzee mmoja mwenye upara aliyeita Ayubu, mzee huyu alikuwa ni mlevi na alisifika kwa ulevi wake ila alikuwa ni mtu makini sana.
Wakamtumia Patrick kuweza kumshawishi mzee huyo ili afatane nae na wakammalize wanapopajua wao, kwavile Patrick alikuwa ni mtu aliyesoma na mwenye muonekano wa ukarimu na upole, ukimuona huwezi kumfikiria kama anaweza kutenda jambo lolote baya.
Patrick akatumia kama siku mbili kumzoea mzee huyo kwenye duka la pombe.
Tusa akiwa ndani ametulia kwani hakuweza kwenda popote kwavile alifungiwa ndani na Patrick, alishangaa siku nzima imepita bila ya Patrick kurudi.
Tusa akajiuliza kuwa Patrick yuko wapi ila hakuwa na jibu wala hakuwa na wa kumuuliza, kwa upande mwingine alishukuru kwa kutokumuona Patrick kwani alikuwa ni mateso mbele ya macho yake.
Siku ya pili jioni tangia Patrick aondoke, Tusa akasikia mlango ukifunguliwa naye akajua kwavyovyote vile atakuwa ni Patrick tu ila ukweli ni kwamba hakuwa Patrick bali ni Maiko.
Maiko aliingia hadi sebleni na kuita 'Tusa'
kwavile Tusa alijua ni Patrick, akaitikia tu kule kule jikoni alipokuwa. Maiko akamfata Tusa hadi jikoni, Tusa akashtuka kuona sura ngeni ambayo hajawahi kuiona kabisa.
MAIKO: Mbona umeshtuka Tusa?
TUSA: Kwasababu sikujui.
MAIKO: Usiwe na wasiwasi, mimi naitwa Maiko ni kama baba mkwe wako. Njoo basi sebleni tuzungumze.
Tusa akatoka jikoni na kumfata Maiko pale sebleni, kwa upande mwingine Tusa alihisi kuwa labda ukombozi wake umefika.
TUSA: Abee.
MAIKO: Usiniogope Tusa, Patrick ni kama kijana wangu hata mahari yako nimemchangia.
Tusa alikuwa anakodoa mimacho tu, wala hakujua cha kujitetea.
MAIKO: Nimekuja tu kukusalimia na kujua unaendeleaje, vipi hali yako lakini?
TUSA: Niko salama, je Patrick yuko wapi?
MAIKO: Patrick ameenda kuchukua mzigo Nairobi, kwahiyo usijari.
TUSA: Atarudi lini?
MAIKO: Siku mbili tu zimepita ndio umemkumbuka hivyo!
TUSA: Hapana, nimeuliza tu.
Muda wote Maiko alikuwa akimuangalia Tusa kwa macho makali sana, macho hayo yalimuogopesha sana Tusa kiasi cha kuingiwa na uoga.
Maiko kuona vile kuwa Tusa anaogopa akaamua kuaga.
MAIKO: Kesho nitakuja tena kukuangalia kwahiyo usijari.
TUSA: Sawa nashukuru.
Maiko akainuka na kutoka, akafunga milango kama ambavyo aliikuta, kwahiyo Tusa akafungiwa ndani vile vile kama kawaida.
Maiko akiwa anaelekea nyumbani kwake sura ya Tusa ilimkaa kichwani bila kutoka, mara akapigiwa simu na Patrick.
PATRICK: Nadhani hii kazi itachukua kama siku tano na sio tatu tena, maana huyu mzee ni mtata sana.
MAIKO: Hakuna tatizo, nyie fanyeni kazi tu.
Maiko alifurahi kusikia hivyo ili na yeye apate wasaa mzuri wa kuzungumza na Tusa.
Kama ambavyo Deborah alihitaji, alimuomba Sele na kwenda kuishi nae nyumbani kwake.
SELE: Nimemkumbuka sana Patrick, hivi yuko wapi?
DEBORAH: Yupo huko kwenye miji ya watu, amepata kazi huko. Na yeye amekukumbuka sana.
SELE: Dah! Bora arudi anifanyie na mimi mpango wa kazi.
DEBORAH: Hilo ondoa shaka, Patrick na wewe mmh!! Lazima atakufanyia tu.
SELE: Ndio mamdogo najua Patrick hawezi kunitupa mimi. Nikikumbuka wakati tuko wadogo ilikuwa raha sana.
DEBORAH: Utoto raha, hata mimi namtamani Patrick wangu arudi utoto ili nikae nae muda wote ila ujana ukifikia mara kutafuta kazi mara kuoa ndio kunikimbia kabisa hapo.
SELE: Hivi Patrick ana mchumba mama?
DEBORAH: Awe nae wapi? Angekuwa nae angeniambia, Patrick anatafuta maisha kwanza si unajua wanawake wanavyofilisi mwanangu.
SELE: Kweli kabisa, ila lazima atakuwa nae wa kuzugia. Mmh ila Patrick na mambo ya mademu yuko mbali nayo kabisa, labda kama atampatia huko kazini.
DEBORAH: Hata kutongoza kwenyewe mwanangu yule hawezi.
SELE: Hahaha, mamdogo nawe loh!
Sele alitamani sana kumuona nduguye Patrick, alikuwa amemkumbuka sana.
Alikuwa akipiga stori nyingi na mamake mdogo za kumuhusu Patrick.
Sele alikuwa anaishi na Deborah kama ambavyo alizoea ila kwasasa hakuwepo Patrick, alingoja zipite siku mbili tatu ili aanze kuzunguka mitaani na kuwasalimia vijana wenzie aliowaacha.
Patrick alitumia lugha nzuri sana kumshawishi mzee Ayubu ili aweze kufatana nae.
PATRICK: Mzee kuna bia mpya imezinduliwa ila tulikuwa tunahitaji watu wa kuonja na kwavile nimekuona mzee wangu hapa ni mkarimu nimependelea uwe mmoja wapo kati ya watu watakaoionja na kutuambia ladha yake.
AYUBU: Hayo ndio mambo ninayopenda kijana, inaitwaje hiyo bia na je kuna malipo?
PATRICK: Hiyo bia bado haijapewa jina ila waonjaji ndio mtakaopendekeza jina la pombe hiyo. Ndio mtalipwa elfu ishirini ila leo nitakupa elfu kumi kama advance.
Mzee Ayubu alifurahi sana alipokabidhiwa hiyo pesa na kuambiwa kuwa atafuatwa badae kwaajili ya hilo zoezi.
Muda ulipofika Patrick alimfata mzee Ayubu na kuondoka nae.
Akampeleka huko kwa wenzake, wenzee huyo alidhania kuwa na wale wapo kwaajili ya kuonja hiyo bia mpya.
Mzee Ayubu akapewa glasi moja tu na kulala hapohapo, wakamfanya watakavyo na kuondoka.
Kwakweli kwa Patrick ilikuwa ndio mara yake ya kwanza maishani kuua mtu, siku zote alijua kuwa kazi haramu afanyayo yeye na Maiko ni madawa ya kulevya tu kumbe kuna kazi mbaya zaidi ya kuchukua baadhi ya viungo vya mwili wa binadamu na kuua kabisa, alitetemeka sana kuuangalia ule mzoga wa mzee Ayubu. Roho ya Patrick ikasinyaa, huruma ikamjaa ila hakuwa na jinsi zaidi ya kulikimbia hilo eneo la tukio.
Walirudi Arusha, na kwenda kwenye hilo jumba ila Patrick hakuweza kuingia kwani mawazo yake yalikuwa kwa Tusa, alihitaji kumuona Tusa, ingawa ilikuwa usiku ila Patrick alishaamua kurudi kwake ili akamuangalie Tusa.
Tusa akiwa katulia ndani kama ambavyo Maiko alimuahidi, na kweli siku hiyo akaenda tena kumuona Tusa. Mida ya jioni mlango ulifunguliwa na Maiko akaingia, Tusa akajiuliza kuwa iweje tena huyo Maiko kuja jioni vile, na hakutaka kuondoka wala nini.
Muda kidogo Maiko akaanza kumsifia Tusa.
MAIKO: Tusa, kweli wewe ni binti mrembo tena unayevutia machoni. Kweli pesa yetu imeenda kihalali kabisa.
Mara Maiko akaanza kumsogelea Tusa, Tusa akawa analia huku akipiga kelele na kumsihi Maiko asimfanye chochote.
MAIKO: Tusa, hata mimi ni halali kuwa na wewe kwani nimekulipia mahari kubwa sana. Kwahiyo hutakiwi kuninyima.
Tusa akawa anakimbia hovyo hovyo mule ndani, ila mwanaume ni mwanaume tu.
Maiko alimkamata Tusa na kumuingilia kimwili kwa nguvu, Tusa akawa analia na kuomboleza.
Mara mlango unafunguliwa, Patrick alikuwa anaingia ndani.
 
SEHEMU YA 17


Maiko alimkamata Tusa na kumuingilia kimwili kwa nguvu, Tusa akawa analia na kuomboleza.
Mara mlango unafunguliwa, Patrick alikuwa anaingia ndani.
Maiko hakuweza kusikia mlango unavyofunguliwa kutokana na kelele za Tusa na pia hakufikiria kama Patrick anaweza kuja muda huo, aliendelea na yake mpaka pale alipohisi amejiridhisha.
Patrick alishangaa kumsikia Tusa akilia na kujiuliza maswali "Hivi huyu Tusa ni chizi nini? Yani anajiliza hata kama sipo." akaanza kufatilia sauti ya Tusa inapotokea na akagundua kuwa ni chumba cha mwisho kabisa, kile chumba ambacho walitumia kumtoa Tusa ujauzito aliobeba.
Patrick alipofika kwenye kile chumba alimuona Maiko kasimama na Tusa amejikunyata chini, Patrick akaelewa kuwa kwa vyovyote Maiko alikuwa amemuingilia kimwili Tusa, Patrick akachukia sana, kwa ghadhabu akamsukumia Maiko pembeni ambapo alikuwa hajafunga suruali vizuri, ile Maiko anainuka akashtukia anapigwa ngumi ya uso, kabla hajajiweka sawa akapigwa ngumi nyingine.
Maiko akaiona kuwa ishakuwa cheche, akaamua kukimbia.
Patrick alikuwa na hasira hadi mishipa ikamtoka usoni, hakuweza kuzungumza zaidi ya kutetemeka tu, alikuwa akimuangalia Tusa kwa macho makali na ya ghadhabu.
Maiko akafanikiwa kutoka na kupanda gari yake na kuondoka.
Sele alikuwa akimuwaza sana Tusa, alikosa raha kila alipomfikiria Tusa. Alijiuliza maswali mengi sana kuhusu Tusa.
"kwanini ulikubali kuolewa Tusa? Inamaana hukunipenda tena? Na vipi mimba yangu uliyobeba Tusa? Natamani nikuone mpenzi wangu ili moyo wangu uridhike"
Deborah akamuangalia Sele aliyejawa na msononeko machoni.
DEBORAH: Tatizo nini jamani? Eti Sulemani, una nini wewe? Kila siku mawazo.
SELE: Mamdogo, nilikuwa na msichana mzuri sana. Niliyempenda kwa dhati ila mapedeshee wamemuiba mpenzi wangu.
DEBORAH: Mmh pole sana, tatizo la mabinti si waaminifu.
SELE: Alikuwa mwaminifu ila wamemlaghai kwa pesa na mali. Mamdogo nikimfikiria moyo wangu unaniuma sana, sijui kama atatokea msichana yeyote nikampenda kama yeye.
DEBORAH: Usiwe na shaka mwanangu, kama ni wako basi ni wako tu. Tambua ipo siku atarudi kwako.
SELE: Natamani hiyo siku hata iwe leo, kwakweli tunanyanyasika sana maskini katika mapenzi.
DEBORAH: Usijari mwanangu, kila kitu kitakuwa sawa.
SELE: Asante mama.
DEBORAH: Uwe unaenda na kuzungukazunguka huko mtaani ukutane na wenzio, wakina Juma, John labda upunguze kidogo mawazo.
SELE: Sawa mamdogo.
Sele akaamua kwenda kutembea tembea kidogo pale mtaani kama alivyoshauriwa na Deborah ili aweze kupunguza mawazo kiasi.
Patrick akiwa na ghadhabu juu ya Maiko na Tusa.
PATRICK: Kwanini Tusa umelala na Maiko?
TUSA: (Huku akitetemeka), alinilazimisha, amenibaka.
PATRICK: Kwanini akubake Tusa? Umeshindwa kujizuia? Nadhani nawe ulipenda.
TUSA: Hapana Patrick, sijapenda.
PATRICK: Unataka na mimi nikuingilie wapi? Huko kwenye uchafu wa Maiko? Nijibu Tusa.
TUSA: Hapana Patrick.
PATRICK: Kiukweli nimekereka sana Tusa, umeichefua roho yangu.
Tusa akawa anatetemeka tu huku machozi yakimtoka.
Kwavile ulikuwa usiku ikabidi waende kulala, Tusa alilala kwa uoga na mashaka yaliyopitiliza.
Patrick akainuka na kumuingilia Tusa kinyume na maumbile, Tusa alitapatapa na kulia sana ila Patrick hakumuacha hadi pale alipojiridhisha.
Tusa hakuweza kulala hadi panakucha, alikuwa akilia tu. Siku hiyo alipatwa na ugonjwa wa kuhara gafla, alikuwa akiendesha tu na tumbo likimsokota.
Patrick alimuacha Tusa akiwa analia na kuondoka zake ile asubuhi.
Sele akiwa mtaani alikutana na marafiki wengi sana na kupiga story za hapa na pale, na ndipo alipotokea John na kukumbushana mambo yao ya zamani na kuambiana ya sasa.
JOHN: Mwenzio Patrick kaukata, maisha yamemnyookea ile mbaya. Ila wewe umechakaa balaa, vipi hata demu bongo hukuopoa?
SELE: Wee nilikuwa na msichana wangu mzuri sana John, yani huwezi amini.
JOHN: Nilitaka nishangae, kukaa kote bongo usiwe na demu. Labda kama uliwataka wa huku Mwanza.
SELE: Wewe, sijaona huku msichana mrembo kama Tusa wangu.
JOHN: Anaitwa Tusa? Ngoja nikuonyeshe mrembo mwingine mwenye jina hilo kwenye facebook.
John akafungua picha ya Tusa na kumuonyesha Sele.
Sele akashtuka kuiona picha ya Tusa.
SELE: Ndio huyuhuyu Tusa wangu, naye alikuwa anaipenda sana facebook.
JOHN: Mmh! Kaka, yani wewe ndio ulikuwa na huyu mrembo? Aliwahi kuniambia kuwa mpenzi wake anaitwa Sele, sasa wewe Sulemani na Sele wapi na wapi?
SELE: Mimi ndio huyo Sele, kule Dar wamezoea kuniita Sele jamani.
JOHN: Basi una bahati sana kama huyu mrembo ni wako.
SELE: Sipo nae tena, kuna pedeshee mmoja ameniibia mrembo wangu.
JOHN: Kivipi? Au ndomana siku hizi simuoni facebook.?
Sele akaamua kumueleza John kinagaubaga ilivyokuwa kwake na Tusa hadi pale alipokuta Tusa kaolewa na huyo pedeshee Patrick.
Stori hiyo ikafungua akili ya John na kumfanya afikirie kwa kina kama awazacho ndicho au sicho.
Safari ya Patrick asubuhi hiyo ilikuwa ni moja kwa moja kwa Maiko.
PATRICK: Kwanini umenifanyia hivi Maiko?
MAIKO: Mmh! Hata ubaba umekufa sababu ya mwanamke!
PATRICK: Sina baba kama wewe, na bora wewe si baba yangu wala ndugu yangu. Binadamu mwenye roho mbaya kama ya simba.
MAIKO: Jamani Patrick, tusameheane tu ni mambo ya kupitiwa.
PATRICK: Unayajua maumivu ya mke wewe? Umenituma kufanya kazi ya kinyama na bado unanisaliti na mke wangu, kwanini Maiko?
Patrick alikuwa na hasira sana, wakati anaongea alimsogelea Maiko na kumkunja.
MAIKO: Tafadhari Patrick usinitende vibaya, najua wewe ni kijana jasiri. Usiniumize tafadhari, ila kumbuka hata mimi mahari ya Tusa nimechangia tena nimetoa pesa nyingi kushinda wewe.
PATRICK: Kwani nilikuomba unichangie pesa? Kumbe ulikuwa unatoa kwa shingo upande? Dah najuta kukufahamu Maiko.
MAIKO: Niachie Patrick, tuzungumzie kazi niliyokutuma.
PATRICK: Sina muda huo.
Akatoka nje na kuingia kwenye gari yake na kuondoka.
Maiko akawa anajisemea,
"alitaka afaidi peke yake yule binti mrembo! Hajui kuwa kizuri kula na nduguyo, toto choyo kama mama yake loh! Mke kitu gani wakati nimechangia mahari!!"
Maiko kazi yake ni kuharibu tu, kwanza huwa hapendi kuona mtu anaishi kwa furaha mwanzo mwisho.
Akajiandaa na yeye ili akaone kazi yake aliyowatuma wakina Patrick.
Nyumbani kwa kina Tusa, mama yake bi.Pamela akiwa anafua, mara akamuona Tina akija mbio mbio huku anahema kwa kasi ya ajabu.
PAMELA: Tina kuna nini?
TINA: Kuna tatizo mama.
PAMELA: Tatizo gani?
TINA: Tumepatwa na msiba mama.
Pamela alihisi kuchanganyikiwa kabisa kwani hakujua ni msiba wa nani.
 
SEHEMU YA 18


Pamela alihisi kuchanganyikiwa kwani hakujua ni msiba wa nani.
PAMELA: Jamani Tina, nani tena?
TINA: Mamdogo, ni babu yao na wakina Tusa.
PAMELA: Wee Tina wewe, unamaanisha mzee Ayubu? Nani amekupa taarifa?
TINA: Ndio mzee Ayubu, nimeona kwenye taarifa ya habari. Tena amekufa kifo cha kusikitisha sana.
Pamela alishapagawa kusikia habari za huyo mkwe wake, ikabidi aende kumtaarifu mumewe na wajaribu kuwapigia ndugu zao ili kujua ukweli wa habari hiyo.
Pamela akaamua kumpigia simu wifi yake aliyeitwa Amina, ambaye naye alimwambia kuwa ndio wamepata habari muda huo.
Ilikuwa ni huzuni sana kumpoteza mtu mcheshi kama mzee Ayubu.
Patrick alirudi nyumbani kwake na kumkuta Tusa yupo palepale alipomuacha asubuhi.
Patrick akamuangalia Tusa na kukaa kwenye kochi, Tusa akamtazama Patrick na kumfata pale alipokaa, Tusa akaanza kuongea kwa maombolezo na kwa uchungu.
TUSA: Hivi Patrick, wewe ni mume wa aina gani? Mume usiyemjali mkeo na unasema unampenda? Hivi ulinioa ili unitese? Nimekukosea nini mimi jamani?
Patrick alimuangalia Tusa kwa jicho kali ila lililojaa huruma.
TUSA: Nasema ya moyoni, kiukweli natamani kufa kuliko kuishi na wewe Patrick. Kukupa namba yangu ndio kosa kubwa la kunifanya niteseke hivi? Unanifanya kama mbwa jike nisiye na thamani, kila anayetaka anachukua tu. Patrick umeniharibia maisha yangu, pesa zako ndio za kunitesa kiasi hiki!! Nimewahi kukuomba pesa mimi?
Tusa akainama na kuendelea kulia.
PATRICK: Nisamehe Tusa mke wangu, kiukweli nimejaribu kufanya mambo mengi ili unipende cha kushangaza huna mapenzi nami kabisa, kama vile sio mumeo. Hata mimi inaniuma Tusa, lini utajifunza kunipenda?
TUSA: Sikupendi na sitakupenda kamwe hadi naingia kaburini.
PATRICK: Kwani Tusa nina kasoro gani mimi? Kwanini usinipende kama yule bwanako?
TUSA: Siwezi kukupenda Patrick, wewe ni gaidi uliyejificha. Nampenda Sele na sikuzote nitaendelea kumpenda, najua sitaweza kuwa nae tena ila nitampenda milele. Nani akupende wewe Patrick? Mwanaume mwenye roho mbaya, usiyejali wengine, mtu mwenye roho ya shetani.
PATRICK: Ni kweli nina roho mbaya ndiomana nimeua.
TUSA: (Akashtuka sana) umeua?
Patrick hakumjibu Tusa ila akaenda chumbani, Tusa akaona maisha yake hapo ni ya mashaka, akabaki anajisemea.
"Eeh Mungu, naomba unitetee katika maisha haya"
Baada ya kutafakari sana, John akaamua kumfata Sele ili amwambie anachofikiria yeye.
JOHN: si uliniambia kuwa huyo pedeshee aliyemchukua Tusa anaitwa Patrick?
SELE: Ndio anaitwa Patrick.
JOHN: Mmh! Hivi sio Patrick ndugu yako kweli?
SELE: Acha masikhara bhana John, kwanini umuhisi yeye?
JOHN: Sikia nikwambie, Patrick ana hela sana kwa sasa halafu anaishi Arusha.
SELE: Hata kama, hawezi kuwa yeye.
John akaamua kumueleza Sele kuwa kwanini amemuhisi Patrick.
JOHN: Sikia nikwambie, kipindi Patrick amerudi hapa alinishangaa kuona nashinda facebook.
SELE: Kwani kukushangaa kuna tatizo John?
John akamueleza Sele ilivyokuwa, na jinsi Patrick alivyotaka kufunguliwa akaunti ya facebook na jinsi alivyomuulizia Tusa.
JOHN: Aliniuliza kwa makini jina analotua Tusa, nikagoma kumtajia ila akaomba kuona picha yake nadhani hapo ndipo alipojua jina lake na kumuomba urafiki.
SELE: Hayo uyasemayo John yananiingia sana halafu inaonyesha kama kuna uhusiano, ila kiukweli nakataa. Patrick hawezi kufanya vile, majina yanafanana John tena hayo majina ya Patrick wako wengi sana duniani.
JOHN: Kwahiyo haiwezekani kuwa ni yeye ingawa alimuulizia Tusa?
SELE: Kumuulizia mtu ni jambo la kawaida John, sidhani kama anaweza kuwa Patrick huyu.
Sele alipinga kabisa hisia za John za kudhania kwamba Patrick wanaemjua ndio muhusika.
Wakiwa msibani, hadi wanazika kila mmoja alisikitishwa na kifo cha mzee Ayubu, kwani kilikuwa ni kifo cha kusikitisha sana.
Mzee Ayubu alikutwa ametolewa upara na kunyofolewa sehemu za siri, kila mtu alihuzunika kwa kifo cha mzee huyo.
Hata baada ya mazishi habari ilikuwa ni hiyo hiyo ya juu ya kifo cha mzee Ayubu, hakuna aliyetambua mtu aliyemfanyia unyama mzee huyo, watu walikuwa wakisikitika tu.
Amina kama mtoto mkubwa wa kike wa mzee Ayubu akaamua kumuulizia Tusa kwani Tusa ndie mjukuu mkubwa wa mzee huyo na hakuonekana msibani.
AMINA: Wifi, Tusa yuko wapi?
PAMELA: Tusa yupo kwa mumewe, ameolewa.
AMINA: Yani mnamuoza mtoto bila ya kutushirikisha na wengine?
PAMELA: Ilikuwa ni haraka wifi, naomba utusamehe.
AMINA: Na mbona hajaja msibani au hamjampa taarifa? Unajua Tusa ni mtu muhimu sana kwa babu yake, angepaswa kuwepo mahali hapa.
PAMELA: Kwakweli Tusa hapatikani kwenye simu, huwa tunawasiliana na mumewe tu. Ila tangu msiba utokee naye hapatikani.
AMINA: Mmh! Wifi mmeuza mtoto nyie, yani hapatikani na hata kumfatilia hamumfatilii?
PAMELA: Mumewe kasema wanaendelea vizuri, hata hivyo mtu mwenyewe ana pesa.
AMINA: kupenda pesa uache wifi dada, ila mfanye juu Tusa apate habari na aje kutembelea kaburi la babu yake.
PAMELA: Sawa tutafanya hivyo.
Baadhi ya maneno yalimuingia vizuri Pamela, akawaza sana moyoni kuhusu mtoto wake Tusa kwani ilikuwa kama amemtupa vile.
Patrick alikuwa nyumbani kwake kama vile mtu aliyepagawa.
Akaitazama simu yake na kugundua kuwa alibadilisha laini ya simu, aliweka laini inayojulikana na watu wachache ili kuepuka usumbufu, wakati anatazama simu yake, ilianza kuita muda huo na mpigaji alikuwa Maiko.
PATRICK: Sema.
MAIKO: Mbona umekuwa hivyo Patrick? Unataka kuharibu kazi mwishoni? Uje kufanya kazi, kesho asubuhi nakuhitaji kuna mpango flani wa pesa uje tupange.
PATRICK: Poa.
Bado Patrick hakujisikia raha kuzungumza na Maiko ni kwavile tu ameshakula kiapo cha kufanya kazi ya Maiko hadi mwisho.
Tangia Patrick aropoke kwa Tusa kuwa aliua, Tusa alijikuta akimuogopa zaidi Patrick.
PATRICK: (Kwa ukali), una nini wewe Tusa? Unaniogopa mimi nimekuwa jini? Nakusemesha hujibu, umekaa kama sanamu. Nina hasira zangu hapa naweza nikakubutua ukiendelea kuwa kimya.
Tusa hakuweza kujibu zaidi ya kujipeleka kulala tu, ndipo Patrick nae alipoamua kulala.
Patrick akiwa usingizini, akamuona mzee Ayubu akimjia kwa sura ya huruma, na kuanza kuongea.
"kwanini umeniua Patrick?"
 
SEHEMU YA 19


Patrick akiwa usingizini, akamuona mzee Ayubu akimjia kwa sura ya huruma, na kuanza kuongea.
"kwanini umeniua Patrick?"
Patrick akabaki akimtazama na kukosa jibu, mzee Ayubu akasema tena,
"Laiti ungelijua mimi ni nani yako! Usingethubutu kuniua."
Patrick akashtuka na kupiga kelele, "mzee Ayubuuu..."
Tusa nae akashtuka na kujisemea.
TUSA: Mzee Ayubu!!
PATRICK: (Huku akihema sana), nilikuwa naota Tusa.
TUSA: Huyo mzee Ayubu ni nani na ana mahusiano gani na wewe?
PATRICK: Ni rafiki yangu tu.
TUSA: Kivipi?
PATRICK: Aaargh, hayo mengine hayakuhusu bhana. We endelea kulala tu, nishakwambia ni rafiki yangu inatosha.
TUSA: Sawa bhana.
Tusa akaamua kujilaza tena, ila muda ule ule Patrick akaanza kumlazimisha Tusa kuwa anataka kumuingilia kimwili, kwakweli kile kitendo kilikuwa ni kero kwa Tusa kwani hakuwa na la kufanya, na siku zote Patrick huwa anamuingilia Tusa kwa kumlazimisha tu kitu kinachomfanya Tusa aumie na kulia sana kwani hakupewa maandalizi yoyote.
Kulipokucha Patrick aliwaza sana juu ya mzee Ayubu, na akajiuliza kuwa ana mahusiano yapi na mzee huyo kwani ile sauti kuwa angejua ni nani yake asingemuua ilimrudia mara kwa mara.
Alipoamua kwenda kwa Maiko alihitaji kumuuliza baadhi ya maswali ili apate kujua kwanini Maiko alimtuma kwenda kumuua mzee Ayubu, na pia aweze kujua kuwa yeye na mzee Ayubu wana mahusiano gani.
Sele aliendelea kuichuja kauli ya John katika akili yake, alishindwa kuamini kabisa kuwa inawezekana akawa ni Patrick ingawa kuna uthibitisho wa kutosha kuwa ni yeye.
Sele aliwaza sana bila ya kupata majibu, akawa anajiuliza tu,
"Hivi ni kweli Patrick anaweza kunitenda vile? Mmh!! Hapana, hata kama angekuwa mtu mwingine Patrick hawezi kuwa na roho mbaya ya kiasi kile"
Akamfata alipokaa Deborah ili amuulize maswali mawili matatu kuhusu Patrick.
SELE: Hivi mamdogo, ulisema kuwa Patrick yupo mkoa gani?
DEBORAH: Patrick yupo Arusha.
SELE: Anafanya kazi gani?
DEBORAH: Alisema yupo mgodini.
SELE: Ana pesa sana eeh!
DEBORAH: Mbona leo maswali mengi kama polisi? Ana hela ndio, nadhani kazi yake ina kipato sana.
SELE: Maswali kawaida tu mamdogo, mpigie basi nimsalimie.
DEBORAH: Yani ni kama wiki mbili sasa simu yake haipatikani, ngoja nimjaribishe.
Deborah akaamua kuchukua simu na kumpigia Patrick ila napo hakupatikana.
SELE: Vipi hapatikani?
DEBORAH: Ndio hapatikani, hata sijui amepatwa na matatizo gani maana sio kawaida kabisa.
SELE: Basi tungoje siku atapiga mwenyewe.
DEBORAH: Ndio ila nitaendelea kumjaribisha mara kwa mara kama nitampata hewani.
Sele hakuweza kumwambia mamake mdogo juu ya maneno ya John kuwa uenda Patrick ndio muhusika kwani aliona ni kumpa presha mamake mdogo na pia hakuwa na uhakika bado.
Patrick alienda kwa Maiko na kufanya nae shughuli za hapa na pale, baada ya hapo akaamua kutulia nae na kumuuliza maswali aliyoyakusudia.
PATRICK: Hivi kwanini ulinituma kumuua mzee Ayubu? Kwani unamfahamu au unamahusiano naye?
MAIKO: Kiukweli simfahamu kabisa huyo mzee Ayubu, ila haya ni mambo ya biashara. Kuna mtu alitoa oda ya kufanya hivyo na tumeingiza pesa nyingi sana.
PATRICK: Huyo mtu ni nani na ana mahusiano gani na wewe?
MAIKO: Huyo mtu ni ndugu yangu ila haishi hapa, yupo nje ya nchi ni huko hufanya hiyo biashara ya viungo vya wanadamu. Hapa anakujaga mara moja moja sana.
PATRICK: Viungo vya wanadamu vina kazi gani?
MAIKO: Akija tena nitakutambulisha kwake umjue halafu utamuuliza hayo maswali yako.
PATRICK: Je, kuna uhusiano wowote kati ya mimi na mzee Ayubu?
MAIKO: Acha kuota Patrick, wewe mtu wa Mwanza, mzee Ayubu wa Morogoro huo uhusiano wenu unatokea wapi? Una ndugu Morogoro wewe?
PATRICK: Hapana.
MAIKO: Ndugu zako wako Mwanza, mzee Ayubu hakuhusu wewe wala mimi.
PATRICK: Unajua nini? Mi najiuliza, kwanini iwe mzee Ayubu na si mwingine yeyote?
MAIKO: Hayo maswali utamuuliza mwenye kazi, labda ana kisasi nae.
Patrick aliondoka kwa Maiko na kutambua kwamba mtandao wa Maiko ni mkubwa sana kwani hata yeye ana bosi wake, yote hayo yalimchanganya Patrick.
Walipomaliza matanga ya kwenye msiba, Pamela na mumewe walirudi kwao wakiwa na mwanamke mmoja wa makamo akidai kuwa yeye ni mama mzazi wa Adamu.
Mwanamke huyo aliitwa Rehema, hata Adamu alimshangaa kwani hakuweza kumuona tangia alipokuwa mdogo na yote hayo ilitokana na kwamba Adamu aliachwa na mama huyo akiwa na miaka miwili.
PAMELA: Mama, kwanini ulimuacha mwanao akiwa mdogo hivyo?
REHEMA: Nilijifungua mapacha, wazazi wangu hawakutaka niolewe na Ayubu ila Ayubu alihitaji watoto wake ikabidi tugawane mmoja nikawa nae na mwingine akaondoka na Ayubu. Kwa kipindi kirefu nimemtafuta Ayubu bila mafanikio mpaka pale nilipoona taarifa ya kifo chake kwenye luninga. Kwakweli nimesikitishwa sana, nikaamua kufunga safari hadi Morogoro.
PAMELA: Kwahiyo umetokea mkoa gani?
REHEMA: Kigoma mwanangu, kwakweli ilikuwa safari ndefu sana.
PAMELA: Pole sana mama.
REHEMA: Asante, na mbona kule wanapenda kukuita wifi dada?
PAMELA: Mama, kuna kaundugu flani hivi kapo kati yangu na Adamu ila mwanzo hatukugundua hadi tumeoana na kufunga ndoa. Ila undugu wenyewe hauna nguvu sana, ni undugu wa mbali.
REHEMA: Undugu gani tena?
PAMELA: Nitakwambia tu mama usijari ila kwanza turekebishe tofauti yako wewe na Adamu. Natumaini kuna muda atakuelewa mama yetu, hata usijari.
Pamela alipatana sana na huyu bi.Rehema kutokana na ucheshi wa bibi huyo hata akashangaa kwanini hakuweza kuishi na mzee Ayubu.
Patrick kabla ya kurudi nyumbani kwake alipitia baa kwanza ambako alikunywa pombe hadi akaridhika.
Aliporudi kwake alimkuta Tusa amelala, akaanza kumuamsha kwa nguvu, tofauti na walevi wengine ambao wakilewa wanakuwa legelege ila Patrick alikuwa na nguvu sana.
Akawa anamsumbua Tusa hadi akafanikiwa kumuingilia anakokutaka yani kinyume na maumbile, Tusa hakuweza kulala tena zaidi ya kulia tu.
Patrick akaanza kumwambia Tusa.
PATRICK: Unajua ile siku ya kwanza nimekufaidi sana huko nyuma na nimeona kutamu zaidi, siku hizi itakuwa hukohuko na safari hii hadi utapata mimba ya mgongo.
Halafu akalala, Tusa alilia sana na kuombea ukombozi wake ufike.
Kulipokucha Patrick aliamka kama kawaida ila alijikuta akimkumbuka sana mama yake, akaamua kuchukua simu yake na kumpigia ila iliita kama mara tatu bila ya kupokelewa.
Patrick akaweka simu mezani na kwenda kuoga, kwakweli siku hiyo alijisahau kwani huwa haachi simu yake, kila mahali anakuwa nayo.
Patrick akiwa bafuni ile simu yake ikaanza kuita, Tusa aliposikia akasogea kuitazama akaona jina 'mama' Tusa akaona kuwa kwa vyovyote vile huyo lazima atakuwa mama yake na Patrick, akaamua kuipokea ili amueleze matatizo yake.
 
SEHEMU YA 20


Patrick akiwa bafuni ile simu yake ikaanza kuita, Tusa aliposikia akasogea kuitazama akaona jina 'mama' Tusa akaona kuwa kwavyovyote vile huyo lazima atakuwa mama yake na Patrick, akaamua kuipokea ili amueleze matatizo yake.
Tusa akaipokea ile simu na kuisikia sauti iliyosema 'hallow' kuwa ni ya mwanamke wa makamo.
TUSA: Mama, mimi ni mke wa Patrick. Ananitesa na kuninyanyasa sana.
DEBORAH: Patrick kaoa?
TUSA: Ndio na mimi ndiye mkewe.
DEBORAH: Unaitwa nani binti?
Mara Patrick akatoka bafuni na kumkuta Tusa yupo na ile simu sikioni, akaenda na kumpokonya halafu akaiweka sikioni mwake.
Deborah aliendelea kuongea kwani kilio cha Tusa kilimuingia masikioni mwake vilivyo.
DEBORAH: Niambie binti, halafu niambie anachokufanya hadi ulie hivyo.
Patrick akaikata ile simu na kumgeukia Tusa.
PATRICK: Nani kakutuma upokee simu yangu? Hujui mama yangu ana presha, akifa je? Nijibu, nani kakutuma?
Tusa aliendelea kulia bila ya kutoa jibu, Patrick akamuuliza tena.
PATRICK: Kitu gani kinakuliza sasa wakati umeshafanya makosa?
TUSA: Unanionea Patrick, unaninyanyasa, unanitesa. Nini kosa langu jamani?
PATRICK: Kosa lako ni kupokea simu isiyo kuhusu.
Patrick akamsogelea Tusa akiwa anahitaji la kumzabua kibao, mara simu yake ikaita tena. Patrick akashindwa kupokea kwani hakujua cha kumjibu mama yake kwa muda huo.
PATRICK: Unaona sasa Tusa, mimi namwambia nini mama? Unadhani atanielewa? Yani we Tusa una akili mbovu sana.
Patrick alikuwa na hasira sana akaona kuwa akiendelea kukaa hapo atamuumiza huyo Tusa, akaamua kuvaa na kuondoka zake.
Tina alimkumbuka sana ndugu yake na rafiki yake kipenzi Tusa, kama kawaida yake alikuwa mara kwa mara nyumbani kwa kina Tusa ili kujua kama kuna taarifa yoyote kuhusu Tusa.
Akiwa amekaa na mamake mdogo wanaongea.
PAMELA: Hivi Tina dadangu bado hajarudi?
TINA: Anarudi leo mamdogo, halafu amesikitishwa sana na kifo cha babu. Kama angewezaa kupaa kutoka china basi angekuja msibani.
PAMELA: Kwakweli kifo chake kimetushtua wengi.
TINA: Vipi kuna taarifa yoyote kuhusu Tusa?
PAMELA: Hakuna mwanangu, tuzidi kumuombea tu.
TINA: Sawa mamdogo, mi naenda ila akija mjomba msalimie.
PAMELA: Sawa usijari.
Bi. Rehema akajikuta akiwa na maswali mengi kichwani.
REHEMA: Huyo mjomba wa Tina hapa kwako ni yupi?
PAMELA: Adamu mama ndio mjomba ake.
REHEMA: Adamu si mumeo na Tina wewe ni mamake mdogo iweje mumeo awe mjomba ake?
PAMELA: Utajua tu mama kwanini imekuwa hivyo, hata usijari.
Bi. Rehema alikuwa akishangaa tu bila kuelewa.
Deborah alishindwa kuelewa kabisa, akabaki anajisemea mwenyewe.
"Hivi kweli Patrick anaoa bila hata ya kunitaarifu? Dharau gani hii?"
Sele alimuona mamake mdogo huyo akiwa anajisemesha mwenyewe.
SELE: Nini tena mamdogo?
DEBORAH: Kwakweli nashindwa kumuelewa Patrick.
SELE: Kafanyaje tena?
DEBORAH: Asubuhi nilipotoka kuoga nikakuta kwenye simu yangu kuna missed call tatu, ile kupiga sasa mmh.
SELE: Kwani ikawaje?
Deborah akamsimulia Sele alichoambiwa kwenye simu.
SELE: Mmh! Yani Patrick kaoa? Kamuoa nani? Na kwanini hakusema?
DEBORAH: Hayo yote sijui, najaribu kumtafuta kwenye simu hapatikani halafu ile namba haipokelewi, nadhani ni namba yake anaogopa kupokea kwavile mimi nimeshajua ukweli.
SELE: Sasa itakuwaje mamdogo?
DEBORAH: Usijari Sele, mimi namjua Patrick. Natambua wapi pa kumkamatia, atanitafuta mwenyewe.
SELE: Sawa mamdogo.
Akili ya Sele ikawaza mengi sana, akaanza kuhisia kuwa huenda huyo binti akawa Tusa ila tu hakuwa na uhakika.
Deborah hakuacha kumtafuta Patrick kwenye simu ila simu yake haikupokelewa. Akaamua kumtumia ujumbe, alijua utafika na atausoma tu.
Mama yake na Tina aliyeitwa Fausta alienda nyumbani kwa mdogo wake Pamela ili kumsalimia bi. Rehema.
FAUSTA: Karibu sana mama.
REHEMA: Asante ingawa nimefika kipindi cha majonzi.
FAUSTA: Kwakweli huu msiba wa baba umetugusa sana, ingawa sijaishi nae sana ila namkumbuka sana baba alikuwa mcheshi na mpenda watu. Yeyote aliyemfanyia hivi baba na alaaniwe milele.
REHEMA: Inaonyesha unamjua sana mzee Ayubu.
FAUSTA: Ndio namjua, ni baba yangu mzazi kwakweli nimeumia sana.
REHEMA: Mmh!! Baba yako mzazi? Wewe na Pamela si mtu na mdogo wake? Iweje mzee Ayubu awe baba yako mzazi?
FAUSTA: Mama, sijui kama utanielewa.
REHEMA: Nieleweshe tu nitakuelewa.
FAUSTA: Mama, mimi na Pamela tumechangia mama halafu mimi na Adamu tumechangia baba kwahiyo Pamela ni ndugu yangu na Adamu ni ndugu yangu.
REHEMA: Mmh! Ndiomana Pamela wanamuita wifi dada!! Sasa nimeanza kuelewa, kwamaana hiyo Adamu na Pamela ni kama ndugu.?
FAUSTA: Wenyewe wanakataa kuwa si ndugu, ila walioana bila kujua. Hata hivyo undugu wao hauna nguvu sana.
REHEMA: Yani umenielewesha kwakweli, ndomana mwanao anamuita Adamu mjomba. Mmh! Kazi ipo. Eeh na wewe ulikuwa wapi kwani hadi msiba umeisha?
FAUSTA: Nilikuwa China, huwa naenda mara kwa mara kuna mizigo naitoaga kule naileta huku.
REHEMA: Hongera kwa hiyo kazi, kila siku namngoja Adamu kumwambia kuhusu pacha wake ili aende akamtafute huko Mombasa.
FAUSTA: Mombasa? Alienda kutafuta nini huko?
REHEMA: Aliondoka na kaka yangu ila hawajarudi hadi leo halafu huyo kaka yangu mwenyewe ana akili mbovu huyo balaa hadi kuna kipindi alipelekwa Milembe halafu akatoroka.
FAUSTA: Mmh! Kazi ipo, ila hakuna tatizo mama tutampata tu.
REHEMA: Eeh! Na huyo mama yenu yuko wapi?
FAUSTA: Alishakufa na hivi baba nae amekufa basi tumebaki yatima.
Rehema na Fausta wakaongea mambo mengi ya maisha na kuweza kutambuana kwa undani zaidi.
Patrick akiwa kwa Maiko huku akiendelea kuzipotezea simu anazopiga mama yake.
Mara akaona meseji imeingia kwenye simu yake kutoka kwa mama yake.
"Patrick mwanangu, hutaki kunitafuta, simu zangu hupokei! Nashukuru sana najua hiyo ndiyo fadhira yako kwa malezi yote niliyokupa. Umeona maisha ya huko Arusha ni bora kuliko mimi, basi endelea na maisha hayo ila usahau kabisa kama una mama anayeitwa Deborah"
Patrick alisoma ujumbe huo mara mbili mbili, neno la mwisho likawa linamrudia mara kwa mara kuwa asahau kabisa kama ana mama anayeitwa Deborah. Patrick akajihisi ni mkosaji, akatambua alichofanya hapo hakipendezi, akaamua kwenda sehemu iliyotulia na kumpigia simu mama yake ili amwombe msamaha.
Patrick aliongea kwa kutubu kwa mama yake ambapo Debora alimpa chaguo moja tu.
DEBORAH: Ukitaka nikusamehe basi chagua moja kati ya haya.
PATRICK: Yapi hayo mama? Niko tayari kwa chochote ilimradi tu nipate msamaha wako mama.
DEBORAH: Mlete huyo binti uliyemuoa Mwanza aje nimuone au mimi nije huko Arusha kumuona.
Patrick akajikuta anawaza jibu la kumpa mama yake.
 
SEHEMU YA 21


Patrick akajikuta anawaza jibu la kumpa mama yake.
Deborah akamuuliza tena Patrick na kumsisitiza ampe jibu.
PATRICK: Mama, naomba kama masaa mawili nifikirie majibu ya kukupa.
DEBORAH: Kwani ni mtihani huo?
PATRICK: Hapana mama ila nahitaji muda kidogo.
DEBORAH: Kwahiyo utanipa jibu saa ngapi?
PATRICK: Nimekwambia baada ya masaa mawili mama.
Patrick akajikuta akiwaza sana na kujiuliza maswali mengi, kuwa akimwambia mama yake aende Arusha itakuwa msala kwa Maiko na akiamua kwenda yeye Mwanza atamuagaje Maiko kipindi hicho wakati walikuwa na kazi nyingi za kufanya, akajikuta akijiuliza sana. Akaamua kurudi kwake ili akatafakari kwa kina.
Bi. Rehema alikuwa akitafakari mara kwa mara juu ya mtoto wake Adamu na mkewe Pamela.
REHEMA: Hivi Pamela mwanangu hukujua kabisa kama una undugu wa mbali na Adamu?
PAMELA: Tulijua wakati tumeshapendana sana ila hata hivyo undugu wetu hauna nguvu sana.
REHEMA: Hata kama, nyie ni sawa na dada na kaka ila ndo hivyo maji yashamwagika. Vipi huyo binti yenu atarudi lini?
PAMELA: Hata sijui mama, maana tangu ameolewa huko Arusha hatujapata kuzungumza na yeye hadi leo. Mwanzoni tulikuwa tunazungumza na mumewe ila sasa kimya.
REHEMA: Hivi mnajua kama Arusha kuna ujangili sana? Mnajua wanapoishi?
Akatokea Adamu nae na kuchangia.
ADAMU: Na huko Mombasa alipoenda mwanao je? Unadhani atakuwa mzima? Kama akiwa mzima basi shoga.
REHEMA: Sina maana mbaya, ila nyie kama wazazi mlipaswa kutambua kwanza anapoenda mtoto wenu kabla hajaenda. Mlipaswa kuwatambua ndugu wa mkwe wenu, mlipaswa kuwa na mawasiliano nao. Ila hapo mlipo hamjui chochote.
PAMELA: Usemayo mama ni kweli kabisa, tumefanya makosa sana kumuozesha mwanetu kwa mtu tusiyemfahamu vizuri. Ila hakuna la kufanya sasa, labda tungoje arudi tu.
REHEMA: Cha msingi ni kumuomba Mungu arudi salama, sinamaana kwamba mji wa Arusha ni mbaya hapana. Ila Arusha ina watu flani ambao hupenda sana kufanya mambo ya ajabu.
ADAMU: Sio Arusha tu, hata Mbeya kuna wachuna ngozi. Shinyanga kuna machinjachinja.
PAMELA: Mmh!! Na wewe Adamu unataka kuleta mada zako za mikoa hapa.
Adamu alipenda sana kumpinga mama yake huyu kwani alimuona ni mwenye upendeleo, kwa kumchukua pacha mmoja kumlea yeye na kumuacha yeye kwa baba yake ambapo alilelewa na mashangazi.
REHEMA: Unanichukia bure mwanangu, ila ni baba yako aliyetaka tugawane watoto. Sio kwamba sikukupenda mwanangu.
Pamela alimuhurumia bi. Rehema aliyejaribu kumuelekeza Adamu kila leo japo amuelewe.
Patrick akiwa nyumbani kwake na kuendelea kutafakari, akamuita Tusa, naye Tusa alishajiandaa kwa majibu yaliyonyooka iwapo akiulizwa chochote na huyo mumewe.
PATRICK: Hivi siku ile ulipopokea simu yangu ulimwambia nini mama?
TUSA: Sijamwambia chochote zaidi ya kujitambulisha tu kuwa mimi ni mkeo.
PATRICK: Na kwanini ulipokea Tusa?
TUSA: Kwanza sikujua kama ni mama yako, nilihisi ni mwanamke wako ndomana nikapokea nisikie atasemaje.
PATRICK: Inamaana Tusa umeanza kuwa na wivu na mimi?
TUSA: Ndio ninao, wewe ni mume wangu lazima nikuonee wivu.
Kauli ya Tusa ilimfanya Patrick ajisikie vizuri sana.
PATRICK: Vipi ukionana na mama yangu utamwambiaje?
TUSA: Sitamwambia chochote zaidi ya kufurahi kumuona.
PATRICK: Eeh ungependa mama yangu aje hapa umuone au nikupeleke alipo ukamuone?
TUSA: Nadhani itakuwa vizuri tukimfata yeye, kwani itanifanya hata mimi kutambua miji mingine.
PATRICK: Sawa sawa Tusa, naona leo umekuwa mke mwema. Usijari tutapanga safari hivi karibuni.
TUSA: Sawa mume wangu.
PATRICK: Aaaah! Umeniitaje Tusa?
TUSA: Mume wangu.
PATRICK: Umenifurahisha sana, siku zote ungekuwa hivi ningenenepa jamani.
Patrick aliona kuwa ameanza kupendwa na Tusa na hiyo ndio ikawa furaha yake.
Deborah bado alitafakari kwa kina mambo ya Patrick. Alimuona Patrick kuwa mtoto wa ajabu tofauti na malezi aliyompa.
Alipoona muda umepita sana akaamua kumpigia simu tena Patrick ili ajue jibu lake.
PATRICK: Mama usijari, nitakuja nae Mwanza.
DEBORAH: Kweli Patrick?
PATRICK: Kweli mama, nitakutajia siku ya kuja. Ni hivi karibuni kati ya siku mbili tatu mama.
DEBORAH: Mungu akutangulie mwanangu ili muweze kufika salama huku wewe na mkeo.
PATRICK: Asante mama.
Deborah akafurahi kwani akahisi ni yule Patrick aliyemzoea kwani amejirudi sasa.
Sele akatokea na kumuuliza mama yake mdogo.
SELE: Mama, Patrick amekutajia jina la mkewe?
DEBORAH: Hapana ila anakuja nae huku Mwanza.
SELE: Lini hiyo?
DEBORAH: Kasema ataniambia hiyo siku.
Sele akabaki na lindi la mawazo huku maswali lukuki yakimuelemea kuwa je kama huyo mwanamke akiwa Tusa wake atafanyaje. Alikosa jibu kabisa.
Patrick akaamua kwenda kumuaga Maiko ila Maiko alitokea kuipinga safari ya Patrick.
MAIKO: sikia nikwambie Patrick, huyo binti ukimpeleka kwa Deborah sahau kabisa kurudi nae Arusha.
PATRICK: Haiwezi kuwa hivyo bhana, hata hivyo si atakuwa kwa mama yangu?
MAIKO: Kumbuka kuna kazi kubwa sana ambayo inatakiwa aifanye huyo Tusa. Labda tuifanye kwanza ndio uende nae.
PATRICK: Mama anataka kwenda kumuona mara moja tu, hakuna tatizo nitarudi nae.
MAIKO: Hapana Patrick, nimekataa. Namjua Deborah alivyo, tutamkosa kabisa huyo Tusa.
PATRICK: Mama yangu hayupo hivyo.
MAIKO: Hujui tu Patrick, Deborah kanipotezea mademu zangu wengi sana. Anajifanya mshauri wa wanawake kwavile tu yeye mambo yamemuharibikia. Usiende na Tusa hadi kazi yetu itakapokamilika.
Hayo majibu hayakumpendeza kabisa Patrick ukizingatia kashamwambia mama yake kuwa karibia anarudi.
Patrick aliporudi kwake akaamua kufanya kitu cha haraka, akaamua kupanga safari ya haraka bila kumshirikisha Maiko alitaka Maiko ashtukie tu kuwa alishaondoka.
PATRICK: Tusa jiandae kesho tuna safiri.
TUSA: Ndio ile safari uliyosema?
PATRICK: Ndio tunaenda kumuona mama.
Kesho yake mapema alfajiri wakaondoka na kwenda kupanda mabasi yaendayo Mwanza. Wazo la Tusa ni kumtoroka Patrick tu wakiwa safarini.
 
SEHEMU YA 22


Kesho yake mapema alfajiri wakaondoka na kwenda kupanda mabasi yaendayo Mwanza. Wazo la Tusa ni kumtoroka Patrick tu wakiwa safarini.
Wakati gari inakaribia kuondoka, Tusa akaanza kuhangaika huku amejishika tumbo.
PATRICK: Nini wewe?
TUSA: Tumbo Patrick, nimebanwa vibaya sana.
PATRICK: Mambo gani hayo Tusa jamani? Haya fanya haraka basi uende chooni.
TUSA: Kiko wapi?
PATRICK: (Akimuelekeza kwa mkono) nyuma ya lile bus la bluu, fanya haraka mi nitakuwa hapa kuwazuia ili watusubiri.
TUSA: Sawa mume wangu.
PATRICK: Uwahi kurudi maana hizo haja zako zisije zikatuchelewesha hapa.
Tusa aliposhuka ndani ya lile bus, alikuwa na mpango mmoja tu kichwani nao ni kutoroka.
Akaenda kama alivyoelekezwa na Patrick, kufika karibia na choo akazunguka nyuma yake huku akichungulia chungulia pa kuelekea, mara gafla akatokea mtu nyuma yake na kumziba mdomo, Tusa akaanza kuangaika, akafanikiwa kumpiga teke la nyuma mtu yule, lile teke lilimfanya yule mtu amwachie Tusa ila Tusa kabla hajapiga hatua zaidi akadakwa tena na yule mtu halafu yule mtu akampiga Tusa ngumi za dabodabo tumboni kitu kilichofanya Tusa alegee kabisa halafu akambeba begani na kwenda kumuweka kwenye gari.
Patrick akiwa ndani ya basi akashangaa kuona Tusa harudi na basi ndio limeanza kutoka, aliwazuia mwishowe akachoka na kuamua kushuka kabisa.
Kitu cha kwanza alichofanya Patrick ni kwenda chooni, akatazama vyoo vyote lakini hakumkuta Tusa, hofu ikaanza kumuingia Patrick, akatoka na kuzunguka nyuma ya choo akashangaa kuona gari la Maiko linaishia, wasiwasi ukamjaa kuwa Maiko amemteka Tusa.
Akaamua kuchukua bodaboda na kuifatilia gari ya Maiko.
Pamela akiwa amelala na mumewe alijikuta akishtuka gafla na kusema kwa nguvu.
"Tusaaaaaaa......"
kitendo hicho kilimshtua na Adamu pia.
ADAMU: Vipi mama Tusa, umepatwa na nini?
PAMELA: (Huku akitetemeka na kuonyesha hofu), nimeota vibaya kuhusu Tusa.
ADAMU: Umeota kafanyaje?
PAMELA: Ameumia sana halafu anapiga kelele za kutaka msaada, maskini mwanangu jamani (akaanza kulia).
ADAMU: Nyamaza mama Tusa, haya ni makosa kweli tumeyafanya. Sasa tujadili namna ya kutatua maana kulia hakutasaidia.
PAMELA: Naelewa hilo mume wangu, namuhurumia mwanangu Tusa. Binti yangu ni mpole sana, kama anapata mateso si haki yake kwakweli. Mwanangu Tusa si mkorofi, ni mcheshi, mpole, mkarimu na anapenda watu wote. Mbona niote anateseka vile, halafu hakuna wa kumsaidia! Roho inaniuma kwakweli, naumia sana nikimkumbuka Tusa, inakuwa kama tumemtupa jamani.
ADAMU: Sio hivyo mke wangu, tumuombe Mungu tu mtoto wetu arudi salama.
PAMELA: Kwakweli ipo siku nitaenda Arusha kumtafuta mwanangu, roho inaniuma sana Adamu.
Pamela alihuzunishwa sana na ndoto mbaya aliyoota juu ya Tusa.
Alikosa raha na amani kila anapo mfikiria mwanae.
Patrick alimfatilia Maiko hadi nyumbani kwake na kumuona akimshusha Tusa kama mzigo toka katika gari yake halafu akaingia nae ndani, Tusa alikuwa kapoteza fahamu, hakuweza kujielewa kabisa.
Patrick aliingia kwa Maiko akiwa na ghadhabu sana.
MAIKO: Nilijua tu kuwa utakuja mwenyewe baada ya mkeo kuwa huku.
PATRICK: Kwanini umemteka mke wangu Maiko?
MAIKO: Tumekubaliana nini mimi na wewe? Si mpaka Tusa atakapokamilisha kazi yangu? Sasa kwanini uliamua kutoroka nae, unanisaliti Patrick?
PATRICK: Sikuwa natoroka Maiko.
MAIKO: Ila ulikuwa unafanya nini?
PATRICK: Nilitaka Tusa akamfahamu mama tu basi.
MAIKO: Namjua Deborah, Patrick huyu Tusa angeenda huko asingerudi tena.
PATRICK: Angerudi tu.
MAIKO: Mimi ndio ninaemjua Deborah, kumbuka amewahi kuwa mke wangu yule.
PATRICK: Na ulijuaje kama nimeondoka.
MAIKO: Sikia Patrick, mtandao wangu ni mkubwa sana. Ulidhani kuondoka na basi sitojua? Mimi ndio Maiko bhana, Tusa lazima afanye kazi yangu ili milioni kumi yangu irudi, ulidhani nimetoa bure?
PATRICK: Maiko wewe ni mtu mbaya sana, umembaka Tusa, umeona haitoshi sasa umemteka eti umfanyishe kazi. Mbona una roho mbaya hivyo jamani?
MAIKO: Sina roho mbaya ila mfanya biashara yeyote hutarajia faida sio kutoa kitu kwa hasara. Nilitoa milioni kumi kuchangia mahari ya Tusa, sasa nitamtumia Tusa kuingiza pesa zaidi.
Patrick alishindwa kuelewa kuwa ni kazi gani ambayo Maiko alitaka kumfanyisha Tusa, roho ya Patrick ilipatwa na hofu sana.
Tusa akawekewa ulinzi wa kutosha, aliposhtuka akaanza kutapika damu, Patrick akamuhurumia Tusa, akamsogelea na kuanza kumbembeleza Tusa ambaye alikuwa akilia tu.
Wakati Patrick akiendelea na hiyo kazi ya kumbembeleza Tusa, mara akaitwa na Maiko, ikabidi aende kumsikiliza.
MAIKO: Patrick, yule mtu uliyekuwa unamuulizia ameshawasili na muda mfupi ujao atakuwa hapa nyumbani.
PATRICK: Nani huyo?
MAIKO: Anaitwa Mashaka ndio huyo ambae ataenda na Tusa kwenye kazi.
Moyo wa Patrick ukalia paaaa baada ya kusikia mtu huyo ataenda na Tusa kwenye kazi.
Deborah alishangaa sana kuona mida inazidi kukatika bila kuwasili Patrick.
DEBORAH: Kwakweli nashangaa sijui mwanangu amepatwa na nini njiani jamani!
SELE: Hata me nimeshangaa ila tujipe moyo tu kuwa atafika.
DEBORAH: Ndio hivyo yani hadi akili haikai.
Muda ukaenda, usiku sana ukafika wakaamua kulala tu.
Hadi kesho yake hakuonekana Patrick wala mfano wake kitu ambacho kilizidi kumuumiza Deborah na kumtia simanzi moyoni.
DEBORAH: Simu yake haipatikani, sijui hata kapatwa na nini?
SELE: Mamdogo tumuwazie mema tu aweze kurudi, mawazo mabaya tuyaweke kando.
SELE: Sawa mwanangu.
Deborah aliendelea kujiuliza maswali mengi sana bila ya majibu.
Patrick akawafata baadhi ya vijana wa Maiko ili awaulize kuhusu huyo Mashaka.
Akamfata moja kwa moja kijana aliyeitwa Talo.
PATRICK: Eti Talo, huyu jamaa Mashaka anajishughulisha na nini huku?
TALO: Inamaana hujui? Huyu ndio hununua viungo vya binadamu.
PATRICK: Binadamu wa aina gani?
TALO: Mauaji mengi tunafanya kwaajili yake, kama la yule mzee mwenye upara.
PATRICK: Sasa yeye anafanyia nini hivyo viungo?
TALO: Huwa anapeleka Nigeria huko na kwingineko, ni jamaa mwenye pesa sana.
PATRICK: Mmh! Kwahiyo huwa anawapangia watu wa kuwaua?
TALO: Ni yule mzee tu ndio alitoa maelekezo ila mara nyingi huwa anaagiza tu labda nataka shingo ya mtu mnene basi sisi tunamzia yeyote mnene tunafyeka tu, malipo yake ni makubwa sana ndomana hatukaukiwi na pesa kwa ajili yake.
Patrick akapata picha ya kitu na kuanza kuingiwa na hofu kuhusu Tusa.
Maiko alimuita Patrick ili wazungumze kuhusu Tusa.
MAIKO: Sasa Patrick, huyu ndugu yangu ataondoka na Tusa kwaajili ya kazi.
PATRICK: Kwanini jamani? Mbona wanifanyia hivyo Maiko?
MAIKO: Usijari, nitakupatia milioni mia moja kwaajili ya hiyo kazi Patrick. Tunatengeneza pesa ya maana hapa.
PATRICK: Hapana bhana.
MAIKO: Hivi kazi gani Patrick ikupatie pesa yote hiyo? Tena hiyo milioni mia moja ni kianzio tu, kazi ikikamilika utapata milioni mia tano. Patrick hupendi utajiri wewe? Fikiria mambo mazuri hayo.
Moyo wa Patrick haukuafikiana kabisa na swala hilo kwani Tusa alikuwa na hali mbaya sana, halafu akatambua kwamba thamani ya Tusa ni zaidi ya hiyo milioni mia tano na pia ni zaidi ya pesa yoyote, huruma ilimjaa Patrick dhidi ya Tusa.
Patrick akaamua kupambana kwaajili ya kumtetea Tusa.
 
SEHEMU YA 23


Patrick akaamua kupambana kwaajili ya kumtetea Tusa.
Wakati Patrick anajipanga kupambana huku Mashaka na Maiko nao wanapanga namna ya kuondoka na Tusa.
Patrick akamfata tena Maiko.
PATRICK: Kwahiyo umedhamiria kabisa Tusa aende na Mashaka?
MAIKO: Tatizo liko wapi Patrick? Fikiria mambo ya pesa kwanza.
PATRICK: Hapana, nampenda sana Tusa siko tayari kumpoteza kizembe hivyo.
MAIKO: Sasa unataka kufanyaje Patrick? Unataka kupambana? Unajua wazi huna la kufanya sababu unataka ataenda hutaki ataenda tu.
PATRICK: Lakini huo ni uonevu Maiko, Tusa ndiye binti pekee nimpendaye.
MAIKO: Duniani kuna wasichana warembo maelfu kwa maelfu, na ukiwa na pesa unampata yeyote umtakaye, sasa wewe kinakushinda nini kumtoa Tusa mmoja na kuingiza pesa nyingi zitakazofanya uwapate kama hao zaidi ya kumi! Fikiria mara mbili Patrick, mwanamke si ndugu yako ikitokea tenda uza mmoja uwapate wengi zaidi bila ya shida.
PATRICK: Mmh! Na mama yangu ulitaka kumuuza nini?
MAIKO: Deborah nilimpenda ila alitiwa uwaruwaru na wewe, alikuthamini wewe tu hadi kuniibia na kutoroka nawe.
PATRICK: Ila ingetokea kama hivi ungemuuza?
MAIKO: Patrick, weka hili kwenye akili yako, pesa kwanza mapenzi baadae. Mwanamke si chochote kwenye pesa, hawa ni viumbe dhaifu huwa tunawatoa sadaka tu kwanza wapo wengi sana humu duniani.
PATRICK: Kwahiyo nisimtetee Tusa?
MAIKO: Wazo lako la kumtetea Tusa lifute kabisa kwenye kichwa chako, Mashaka ni mtu hatari sana anaweza kukumaliza ingawa bado mimi nakuhitaji. Cha msingi fikiria pesa tu Patrick.
Patrick akawaza sana, akaona akitumia nguvu atashindwa kumtetea Tusa kwamaana Maiko ana kundi kubwa sana, akaamua kutafuta njia nyingine ya kumuokoa nayo ni kuwa karibu na Maiko.
Pamela alikaa na kufikiria sana kuhusu mtoto wake, alikosa raha kabisa, muda wote aliona sura ya Tusa ikimjia kwa huzuni.
PAMELA: Mama, lazima nifanye kitu kuhusu mwanangu.
REHEMA: Utafanyaje sasa?
PAMELA: Naenda Arusha kumtafuta mama.
REHEMA: Mmh utaanzia wapi sasa?
PAMELA: Popote pale lakini lazima nikamtafute kwakweli.
REHEMA: Nakuhurumia mwanangu mmh! Ni kweli roho inauma kuhusu huyo mtoto, lakini wewe kwenda Arusha naona kama utahatarisha maisha yako vile.
PAMELA: vyovyote itakavyokuwa mama lakini lazima nikamtafute mwanangu, nimepanga kati ya siku mbili tatu niondoke, nitaongea na Tina atakuja kukaa na wewe hapa mama.
REHEMA: Lakini mwanangu....
PAMELA: Usinizuie mama, nimeshaamua.
Pamela hakutaka ushauri zaidi, alishaamua kwenda kumtafuta mwanae, akawa anapanga safari ya kwenda sasa.
Patrick akiwa amewaza sana, akaenda tena kwa Maiko huku akionekana kufurahia kile kitendo cha Tusa kuchukuliwa na mashaka.
PATRICK: Hivi safari yenyewe lini?
MAIKO: Ni kesho kutwa bhana.
PATRICK: Natamani hata iwe kesho.
MAIKO: Kwanini?
PATRICK: Aaah mi nawaza mkwanja bhana, nataka niongeze magari mengine.
MAIKO: Umekuwa mjanja sasa Patrick, huo ndo uanaume. Sio kufikiria hawa wanawake wasio na faida.
PATRICK: Hivi ataenda nae wapi?
MAIKO: Dubai bhana ila analalamika kuwa mwanamke mwenyewe anatapika tapika damu kila mara.
PATRICK: Kama anataka kufa si afe tu.
MAIKO: Akifa kabla ya kazi ataharibu bhana, huyu atamalizwa kazi ikiisha halafu atakuwa bonge la dili.
Patrick akaanza kutambua tambua nia ya Maiko kuwa ni kummaliza Tusa kabisa ili asiwepo tena katika uso wa dunia.
Patrick akaenda kumuona Tusa ambaye alikuwa anatia huruma sana, ingawa Patrick alikuwa na roho mbaya kipindi hicho ila alimuhurumia sana Tusa na hakuweza kumuangalia kwa muda mrefu.
Patrick akaenda kuzungumza na Mashaka kwa mara ya kwanza.
PATRICK: Umemuonaje yule binti? Anafaa sana eeh!!
MASHAKA: Tena sana, yani yule binti ana vivutio vingi sana kwenye mwili wake.
PATRICK: Kumbe umejaribu kumchunguza kidogo?
MASHAKA: Nimemchunguza ndio, kwanza ile michirizi yake ile saivi ndio dili, nimefurahi sana kumkuta nayo, halafu ule mwanya pia ni dili na ile shingo yake ya kujikata mmh! Alikuwa demu bomba sana, isingekuwa biashara hata na mimi ningemchumbia.
PATRICK: Michirizi ndio nini kwani?
MASHAKA: Mistari flani hivi kwenye mwili, wengine huwa wanasema ni mistari ya unene sijui ingawa si kila mwenye nayo ni mnene. Basi ile nayo wameagiza sasa.
PATRICK: Hii biashara ni nzuri sana, halafu mimi nawajua wengi tu wenye hiyo mistari.
MASHAKA: Tatizo ile imejificha, vipi unaweza kunilengeshea mmoja ili niondoke na viungo vyake wakati naondoka na Tusa?
PATRICK: Hakuna tatizo, kesho nitawapatia mmoja mkashughulike naye.
Patrick alitafuta njia ya kuweza kushughulikia kile anachokiwaza kwenye akili yake.
Akamfata na Maiko,
PATRICK: Nimeongea na Mashaka kasema kuwa mwanya nao ni dili saivi.
MAIKO: Sasa utasaidiaje kwa hili?
PATRICK: Kuna mdada nimemzoea huyo, nae pia ana mwanya. Unaonaje nikuunganishe naye ili tummalize na tujitengenezee pesa zaidi?
MAIKO: Wazo zuri sana, sasa itakuwaje?
PATRICK: Kesho kama vipi nitakuunganisha nae.
MAIKO: Hayo ndio mambo ya kufikiria, kitu pesa tu.
PATRICK: Ila wapo wengi tu.
MAIKO: Ni kweli, ila huwa poa kama mtu akiwaunganishia. Unafanya kazi haraka hapo.
Patrick akaonao ngoja ajaribu bahati yake.
Pamela akajiandaa kwaajili ya safari ya kwenda Arusha.
PAMELA: Mama, kesho asubuhi na mapema naondoka na Mtei kwenda Arusha, na tiketi nimeshakata.
REHEMA: Yani umedhamiria kabisa Pamela?
PAMELA: Yani hii ndio sirudi nyuma, najua Adamu atashangaa akirudi toka huko Bagamoyo ila ndio hivyo akija mwambie tu.
REHEMA: Kwanini usingemngoja mshauriane?
PAMELA: Mama, naona anakawia tu, ngoja niende itajulikana hukohuko Arusha.
Kesho yake asubuhi na mapema, Pamela akasafiri na kuelekea Arusha.
Patrick akaenda kuzungumza na machangudoa wawili na kuwanunua.
Akaenda kuwaweka hotel tofauti na kuwaahidi pesa nyingi baada ya huduma, walichotakiwa kufanya ni kumsubiri tu, aliwakabidhi pesa kidogo kama kianzio ili wasiondoke, kila changudoa mmoja aliamini kuwa Patrick yuko kwa mwenzake kwahiyo akawa anangoja amalize kule ili nae aje kufanya kazi yake.
Patrick alipofika karibia na nyumba ya Maiko, akampigia simu Mashaka kwanza na kumuelekeza alipoacha funguo, kitendo hicho kilimfanya Mashaka ajiandae na kuchukua baadhi ya vijana na kuondoka nao, halafu akampigia simu Maiko, nae ikawa hivyo hivyo kwa mawazo yao watamkuta Patrick eneo la tukio.
Patrick akaingia getini kwa Maiko na gari yake, chumba alichowekwa Tusa alibaki mlinzi mmoja tu, ikabi Patrick amlaghai mlinzi huo na kumtuma huku akidai kuwa atabaki yeye, yule mlinzi akaenda alipotumwa.
Patrick akaingia ndani na kumbeba Tusa begani akampakia nyuma ya gari na kuondoka, mlinzi wa getini hakujua lolote, kwahiyo alimfungulia geti na kutoka.
Patrick hakutaka kupoteza muda sehemu yoyote, akaendesha lile gari kwa mwendo wa ajabu ili mradi afike mahali ambapo ataweza kujificha na Tusa kwanza huku akitafuta usafiri wa haraka wa kuwaondoa kabisa eneo hilo.
Pamela akiwa ndani ya Arusha, hatambui hili wala lile.
Alipofika alilala nyumba za kulala wageni na kesho yake akaanza kumsaka Tusa, katika pitapita zake akakutana na mwanaume wa makamo ambapo Pamela alimuona ni mwanaume mwenye heshima zake kumbe alikuwa ni Maiko ambaye yupo katika harakati za kuwatafuta Patrick na Tusa.
Pamela akaamua kumuuliza kuhusu Tusa.
 
SEHEMU YA 24

Pamela akaamua kumuuliza kuhusu Tusa.
Akasalimiana nae kwanza na kumuuliza.
PAMELA: Samahani baba naomba nikuulize kidogo.
MAIKO: Bila samahani mama, uliza tu.
PAMELA: Nina binti yangu ameolewa huku Arusha ila sijui anapoishi halafu sina mawasiliano nae.
MAIKO: Sasa wewe hujui kama Arusha hii ni kubwa sana? Hujui anaishi wapi wala huna mawasiliano nae, unadhani utampata kweli? Au huyo binti yako ni mtu maarufu?
PAMELA: Hapana sio maarufu ila mi naulizia tu labda unaweza ukawa umewasikia sehemu.
MAIKO: Anaitwa nani kwani?
PAMELA: Anaitwa.....
Kabla hajataja, simu ya Maiko ikaita nae Maiko akaipokea.
MAIKO: Nipe taarifa Tulo.
TULO: Kuna mahali ambapo Tusa na Patrick walionekana ndio nataka nikaangalie.
MAIKO: Hebu nenda haraka na mimi nakuja, huyu Patrick ni mshenzi sana.
Pamela akashtuka kusikia hilo jina la Patrick, Maiko alipomaliza kuongea na simu akasahau kabisa kama kuna mtu alikuwa anaongea nae, alichofanya ni kufungua gari yake na kuingia, kitendo kilichofanya Pamela amfate dirishani na kumwambia.
PAMELA: Hata mimi, huyo mume wa mwanangu nae anaitwa Patrick.
MAIKO: Wee mama wewe hebu niondolee maswahibu mie, wakina Patrick wamejaa wengi sana hapa Arusha bhana.
PAMELA: Labda unaweza kumjua mkewe anaitwa Tusa.
Maiko alishaanza kuondoa gari, aliposikia jina la Tusa ikabidi asimamishe gari na kushuka, kisha akamfata Pamela.
MAIKO: Umesema anaitwa nani?
PAMELA: Mwanangu anaitwa Tusa na mumewe anaitwa Patrick.
MAIKO: Ooh!! Mama hao nawafahamu sana, panda kwenye gari nikupeleke kwao.
Pamela bila kutambua akapanda kwenye gari ya Maiko.
Tusa alikuwa akishindwa hata kutembea kwani damu nyingi ilikuwa inamtoka sehemu za siri ni bora walikuwa na gari.
Patrick hakujua afanye nini na Tusa kwani alikuwa ananuka damu mwili mzima, ndipo alipoomba mahali ambapo Tusa aliweza kuoga na Patrick akamtolea nguo nyingine ambapo Tusa aliweza kubadilisha, jambo zuri alilofanya Patrick ni kubeba baadhi ya nguo zake na nguo za Tusa kwenye gari kabla ya kutoroka kwao.
PATRICK: Haya tuondoke Tusa.
TUSA: Tungekaa kaa kidogo hapa kwakweli nimechoka halafu najisikia vibaya sana.
PATRICK: Twende bhana, utapumzika kwenye gari. Tatizo lako hujamjua vizuri Maiko.
TUSA: Kwani wewe na huyo Maiko mna tofauti gani? Mi naona mko sawa tu, wote mna roho mbaya tena za shetani.
Patrick akaona kubishana na Tusa ni kupoteza muda, alichofanya ni kumnyanyua kwa lazima na kumuweka kwenye gari halafu safari ikaendelea, baada ya muda kidogo tu Tulo alifika eneo lile akiwa na vijana wengine wawili, wakajaribu kuwaulizia wakaambiwa kweli walikuwepo eneo lile ila wameshaondoka, walichukia sana na kuendelea kuulizia maeneo tofauti tofauti yani pale panapoonekana uwepo wa gari ya Patrick.
Adamu alisikitishwa sana na habari kuwa mkewe kaenda Arusha kumtafuta Tusa.
ADAMU: Kwanini asingeningoja jamani?
REHEMA: Hata mimi nilimshauri hivyo ila hakutaka kunielewa.
ADAMU: Mama, hivi mimi ukiniangalia unaniona ni mtu wa ajabu sana?
REHEMA: Hapana, upo kawaida tu mwanangu.
ADAMU: Mbona hawa wanawake wananichukulia tofauti? Najua kwa yule mke wangu wa kwanza nilikosea sana, sikutaka kufanya makosa hayo kwa Pamela ila mbona nae ameniogopa hivyo? Ameondoka bila kusikia kauli yangu.
REHEMA: Mwanangu, swala ni kwamba ameumizwa na upotevu wa mtoto wenu. Usimlaumu sana na wala usimfikirie vibaya.
ADAMU: Sasa mimi nifanye nini kwasasa?
REHEMA: Hakuna la kufanya zaidi ya kusikilizia majibu ya Pamela tu.
ADAMU: Na akipatwa na matatizo je?
REHEMA: Tumuombe Mungu tu amuepushie mabalaa yote.
Kwakweli Adamu hakupendezewa kabisa na kitendo cha mkewe kuondoka bila ya kushauriana nae.
Patrick alipofika mbele zaidi akamuona mtu mwenye gari pia, akamuomba wabadilishane, yule mtu alikubali haraka kwavile gari ya Patrick ilikuwa ni mpya na ya gharama zaidi. Wakabadilishana kila kitu halafu Patrick akaondoka na gari ya mtu huyo.
Wakiwa njiani, Tusa akaanza kumlalamikia Patrick.
TUSA: Binadamu gani wewe una roho mbaya kiasi hicho, unashindwa hata kunipeleka hospitali!
PATRICK: Wee Tusa funga domo lako chafu hilo, mi nahangaika hapa kwaajili yako halafu wewe unataka kuniletea maneno yako machafu nitakubadilikia sasa hivi nakwambia.
Tusa ikabidi akae kimya kwani anamjua Patrick alivyo kwahiyo akahofia kubadilikiwa pale. Akaamua kuongea kwa upole tu.
TUSA: Ila Patrick damu zinanitoka nyingi sana.
PATRICK: Sasa hizo damu zako mimi zinanihusu nini? Kama zinatoka acha zitoke tu.
TUSA: Nadhani mimba itakuwa imetoka.
PATRICK: Kama imetoka, thanks to God maana hiyo mimba yenyewe hata haijulikani ni ya nani.
TUSA: Ni ya kwako Patrick.
PATRICK: Ya kwangu wapi bhana! Mwanamke mwenyewe umebakwabakwa hovyo, uzuri wote umekupotea Tusa, umekongoroka vibaya sana.
Tusa alichomwa sana na yale maneno, ingawa Patrick alikuwa akiyaokoa maisha ya Tusa ila Tusa aliendelea kumuona Patrick kama mtu mwenye roho mbaya sana duniani.
Maiko akampeleka Pamela hadi nyumbani kwake, Pamela akashangaa kufika humo ndani akawekewa kizuizi cha kutoka.
MAIKO: Nisikilize kwa makini wewe mwanamke, mwanao kajifanya mjanja na kutoroka hapa na mumewe kwahiyo wee hutoruhusiwa kutoka hapa hadi mwanao apatikane.
PAMELA: Lakini hukuniambia hivyo mwanzo, huku si kunitendea haki jamani.
MAIKO: Tena utulie kabisa, ukizingua nakufumua fumua.
PAMELA: Ila mi sina makosa.
Maiko akampokonya Pamela kila kitu alichobeba hadi simu.
PAMELA: Basi naomba simu nimwambie hata mume wangu kilichonipata.
MAIKO: Hivi wewe mwanamke una kichaa? Hapa mahali sio pa mchezo kabisa unatakiwa utulie tuli.
Maiko akaondoka na kumuacha Pamela na baadhi ya walinzi, yeye akaenda kuzungumza na Mashaka.
MAIKO: Yule malaya tumempata mama yake mzazi.
MASHAKA: Vipi wanafanana?
MAIKO: Labda makalio tu ila vingine hawafanani sana.
MASHAKA: Sasa itakuwaje?
MAIKO: Tumtumie huyu mama kuwapata Patrick na Tusa au kama vipi tummalize yeye bhana.
MASHAKA: Ila je tutapata chochote toka kwake?
MAIKO: Tutapata tu kwamaana hata na yeye ni mrembo pia, njoo badae umchek.
Maiko akarudi nyumbani kwake na kumkuta Pamela akifanya fujo za kutaka kutoka, Maiko hakuwa na huruma kabisa, alichofanya ni kumshindilia mingumi hadi Pamela akapoteza fahamu na kuanguka chini, mara muda kidogo Mashaka akafika kumuangalia Pamela kama analipa.
Mashaka alipomtazama Pamela alishtuka sana, kitendo hicho kilimshtua hata Maiko kuwa kwanini Mashaka kashtuka kumuona Pamela pale chini?
 
SEHEMU YA 25


Mashaka alipomtazama Pamela alishtuka sana, kitendo hicho kilimshtua hata Maiko kuwa kwanini Mashaka ameshtuka baada ya kumuona Pamela?
Mashaka akainama chini, kama vile akimkagua Pamela mara gafla akainuka na kutoka nje. Bado Maiko hakumuelewa Mashaka kwanini amebadilika gafla, akashindwa kumuuliza kwa muda ule, akangoja atulie kwanza ndipo amuulize.
Maiko nge akatoka nje na kumuona Mashaka amekaa mahali akiwa na mawazo sana, akaona asimsogelee kwanza. Alichoamua kufanya muda huo ni kumpigia simu Patrick na kumpa habari za mama mkwe wake, ila simu iliita bila kupokelewa. Tangia Patrick alivyotoroka na Tusa, hakutaka kabisa kupokea simu ya aina yoyote.
Patrick akiwa na Tusa kwenye gari na baada ya kuona kwamba simu inaita sana, akamwambia Tusa aichukue ile simu na kuizima.
Tusa alipochukua ile simu na kuona mpigaji ni Maiko, akataka kujua kuwa Maiko anataka kusema, akapokea simu ile na kuiweka sikioni.
MAIKO: Umejifanya mjanja sana Patrick kuondoka na Tusa, sasa huku tumempata mama yake na Tusa na hatutamwachia mpaka pale utakapotuletea Tusa, tutamtesa na kumtumikisha huyu mama.
Maiko alikuwa anaongea huku anacheka sana, Tusa alijikuta akishusha simu chini na kusema "mamaaa!!"
PATRICK: Vipi wewe Tusa?
TUSA: Maiko anasema amempata mama yangu na atamtesa hadi pale nitakapopatikana.
Patrick akasimamisha gari na kumuuliza Tusa.
PATRICK: Umepata wapi hiyo habari?
TUSA: Nimepokea simu yako hapa wakati Maiko anapiga.
PATRICK: Haya lete hiyo simu.
Tusa akamkabidhi Patrick ile simu na Patrick akaizima kabisa, kisha akamgeukia na kumuuliza tena.
PATRICK: Nani kakutuma upokee simu Tusa?
TUSA: Sijui ila nimejikuta tu nimepokea.
PATRICK: Tatizo lako Tusa una akili ndogo sana, nilikuwa nakuangalia tu unapopokea hii simu. Unapenda mi nionekane mbaya kwako muda wote, siku zote ubishi wako ndio huwa unakuponza wewe.
TUSA: Jamani Patrick, sasa itakuwaje kuhusu mama?
PATRICK: Unataka iwaje? Unataka turudi tukamatwe?
TUSA: Siwezi vumilia kuona mama anakufa kwaajili yangu, ni vyema nirudi mimi ili yeye apone.
PATRICK: Ndiomana nyie wanawake huwa hamsaidiwi nyie, akili zenu ni fupi sana. Hapa nahangaika kukuokoa wewe halafu unaniletea habari za mama yako, unaugua nini wewe? Safari inaendelea hakuna kurudi nyuma.
TUSA: Jamani mama yangu atakufa, hakuna wa kumtetea.
PATRICK: Mungu atamtetea.
Patrick akawasha gari na kuendelea na safari.
TUSA: Nishushe Patrick, niache nirudi nikamsaidie mama yangu.
PATRICK: Ukitaka kuona nina roho mbaya ya kiasi gani endelea kufanya fujo ujute, nitakufumua fumua vibaya vibaya bila kujali nakupenda kiasi gani. Usinione fala kuwasaliti wenzangu kwaajili yako, nimeamua tu kukuokoa toka kwao sasa jitulize tufike salama.
Ikambidi Tusa atulie kwani alimjua wazi Patrick kuwa si mtu wa mizaha.
Deborah bado alikuwa na mawazo kuhusu mtoto wake.
DEBORAH: Sijui atafika lini?
SELE: Usiwe na shaka mamdogo atafika tu.
DEBORAH: Lazima atakuwa amepatwa na matatizo tu, najua Patrick hawezi kunifanyia hivi.
SELE: Hata na mimi naelewa mamdogo, tuendelee kumuomba Mungu tu amuepushe na mabalaa.
DEBORAH: Sawa mwanangu.
Sele akaamua kumuaga Deborah na kwenda kumtembelea bibi yake ambaye alikuwa ni shangazi yao na wakina Deborah.
DEBORAH: Utaenda kukaa siku ngapi huko?
SELE: Wiki moja tu mamdogo.
DEBORAH: Mmh! Mbona unaenda kukaa sana jamani? Nitakukumbuka sana.
SELE: Usijari mamdogo, nitarudi tu.
DEBORAH: Sawa basi, nakutakia safari njema.
Sele akajiandaa na kuondoka zake.
Tusa alikuwa akiumwa sana na tumbo njiani kote alikuwa akiugulia maumivu hayo, hakuweza kula wala kufanya chochote. Muda huo maumivu yalimzidia.
TUSA: Patrick, naumwa sana.
PATRICK: Vumilia tu, karibia tunafika Mwanza.
TUSA: Patrick, hata kama una roho mbaya kiasi gani nihurumie kidogo tu. Nipeleke hospitali Patrick, naumwa sana.
PATRICK: Tusa nishakwambia vumilia, mbona unakuwa huelewi wewe? Wangapi huwa wanaumwa matumbo na wanavumilia jamani!
TUSA: Tatizo Patrick huelewi ni jinsi gani naumia, hili ni tumbo la uzazi ndiomana linaniuma sana. Ungenipeleka hospitali nikapate matibabu kidogo.
PATRICK: Tafadhari Tusa, usinipigie kelele kwanza hapa nilipo nina mawazo mengi sana. Ngoja tukifika Mwanza utaenda huko hospitali ila kwasasa uwe mpole kabisa.
Tusa akabaki analia kwa yale maumivu makali ya tumbo aliyoyapata.
Pamela akazinduka na kuendelea kushangaa bila kuamini yanayomtokea.
Mashaka alipomuona Pamela kazinduka akamfata na kumuuliza.
MASHAKA: Unanikumbuka?
PAMELA: (Huku akitetemeka), hapana.
MASHAKA: Umefanana sana na mama yako wewe, yuko wapi sasa?
PAMELA: (Anashindwa kumuelewa huyu mtu amemfahamu vipi), alishakufa.
MASHAKA: Ooh!! Dada mzuri yule alikufa? Nini kilimuua?
PAMELA: Sijui ila alikufa gafla.
MASHAKA: Nikutajie aliyemuua?
PAMELA: (Akazidi kutetemeka), naogopa.
MASHAKA: Wewe na mtu mzima sasa hutakiwi kuogopa, sawa Pamela? Nimepatia eeh.
PAMELA: Ndio mimi ni Pamela.
MASHAKA: Vizuri sana Pamela, mimi ndiye niliyemuua mama yako na sababu ilikuwa ni ndogo sana, unajua ni ipi?
PAMELA: (Alizidi kutetemeka), sijui.
MASHAKA: Kwasababu alikataa kunitajia wewe na dada yako mlipo. Unajua kwanini niliwatafuta?
Pamela hakuweza kujibu sasa ila alitetemeka zaidi na kupoteza tena fahamu.
Tusa alikuwa amepatwa na usingizi mzito na ulala, hata walipoingia Mwanza hakuweza kushtuka hadi pale aliposhtuliwa na Patrick.
PATRICK: Tusa, hatimaye tumeingia Mwanza sasa.
Tusa alikuwa ametoa macho tu bila ya kuelewa chochote.
Patrick akafikisha gari hadi nyumbani kwao, akashuka na Tusa huku amemshika mkono, akaamua apite nae mlango wa nyuma ya nyumba yao ambapo aliingia nae hadi jikoni kisha akamuacha hapo na yeye kuingia sebleni, akamkuta mama yake akiwa na mama yake mdogo Anna wakizungumza, Patrick akaita "mama"
Deborah hakuamini macho yake kumuona Patrick, akamkumbatia kwa furaha kisha Anna nae akaenda kumkumbatia Patrick, halafu Patrick akawaambia.
PATRICK: Nimekuja na surprise mama.
DEBORAH: Nini tena mwanangu?
Patrick akarudi jikoni na kumvuta Tusa mkono hadi sebleni.
Cha kushangaza, Deborah alipomuona Tusa akapatwa na mshtuko mkubwa sana, akajikuta akitokwa na machozi mengi huku akilia kwa kwikwi wote wakabaki kumshangaa Deborah.
Tusa nae akaanguka chini na kupoteza fahamu.
 
Back
Top Bottom