SEHEMU YA 85
Baada ya hapo nikajiandaa kutoka sasa kwaajili ya kutoroka.
Nilichukua mkoba wangu uliokuwa na baadhi ya nguo na vitenge kisha nikaubeba, nikachungulia nje bado niliona kupo kimya, nikatumia mwanya huo kutoka na kuondoka.
Nakumbuka njiani nilikutana na mama Vero akiwa anarudi nyumbani, alinishangaa kwa zile harakati nilizokuwa nazo, akaniuliza "vipi unasafiri?"
Nilimjibu hapana naenda kumpelekea nguo rafiki yangu mmoja hivi, akauliza tena kuwa mbona naenda usiku, nikamjibu kwavile mchana huwa yupo kazini.
Nikaenda hadi kituoni na kupanda daladala ila kiukweli sikujua pa kuelekea ila nilitaka kujificha kwani nilijua kwamba wakijua tu kuwa nimemkata mtu miguu lazima nitafunguliwa kesi bila kujali maumivu yangu na mimi juu ya mwanangu.
Sikuwa na pesa ya kuweza kufika Mwanza, kwakweli sikujua cha kufanya.
Kufika njiani na lile daladala nikashuka, yani nilikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa, sina pa kuelekea, sina ndugu Dar es salaam na hakuna wa kunisaidia.
Nikawa natembea bila ya kuelewa ninakoelekea, nikaona bonde, nikadhani itakuwa vyema nikienda kupumzika pale bondeni.
Kulikuwa na mti wa mwembe pale karibu na bonde, nilienda na kukaa chini ya ule mti kama vile najikinga jua wakati ulikuwa ni usiku.
Wakati nimekaa pale chini ya mti nikiwa na mawazo yangu ya pa kwenda, mara gafla nikasikia sauti ya mtoto akilia, nilidhani ni mawenge yangu juu ya Jasmine ila kadri nilivyokaa ndivyo sauti ya kitoto ilivyozidi.
Nikainuka na kuangaza huku na kule kuwa labda kuna mtu anapita na mtoto, ila eneo lile halikuwa na njia wala nini.
Ikabidi niangalie ni wapi sauti inatokea, wakati natafuta tafuta nikaona kitoto kidogo sana kimetupwa, kilikuwa kidogo kweli kimeviringishwa kwenye khanga.
Roro ya uchungu ikanishika, nikamuinua yule mtoto, nikachukua baadhi ya vitenge vyangu kumkinga na baridi. Alikuwa mdogo sana, nadhani alitoka kuzaliwa na mama yake kuamua kumtupa labda sababu ya ugumu wa maisha.
Nikakaa nae chini, alikuwa bado analia nikajua kuwa ana njaa pia.
Nikachukua ziwa langu ambalo bado lilikuwa linaendelea kutoa maziwa kwani Jasmine alikufa wakati bado sijamuachisha kunyonya. Nilipokamua chuchu yangu na kuona inatoa maziwa, nikamnyonyesha mtoto yule.
Alinyonya na kutulia, nikanyanyuka pale chini na kuendelea na safari, na sasa nilikuwa naenda kituo cha mabasi ya mikoani ili nikaombe japo msaada wa safari.
Nilikuwa naomba msaada kwa mtu yeyote aliyembele yangu huku nikimwambia kuwa nimetelekezwa na mume na kuachiwa mtoto mchanga yule niliyembeba.
Wengi walinionea huruma na kunipa pole za mdomo tu, ndipo nikakutana na huyu mzee mmoja hivi aliyejitambulisha kwangu kwa jina moja la Patrick.
Nikamuelezea tatizo langu, akanihurumia sana, akaniambia nisijari atanisaidia nifike niendako kwakuwa nilimwambia nataka kurudi kwetu Mwanza kutokana na kutelekezwa huko na mume.
Mzee huyo aliniambia kuwa kesho yake mapema yeye na familia yake wanasafiri wanaenda Sindida kwa usafiri binafsi kwahiyo nitasafiri nao kisha atanisafirisha kwenda Mwanza.
Akanipakia kwenye gari yake na kwenda nae kwake maeneo ya kimara.
Usiku kucha sikulala maana mtoto alikuwa ananisumbua sana, muda mwingi nilikuwa nambembeleza kwa kuhofia kuwakera walioko mule ndani ya ile nyumba.
Alfajiri na mapema safari ikaanza, na tulifika Singida usiku kutokana na ubovu wa barabara kipindi hiko.
Yule mzee alinitafutia nyumba ya kulala wageni na nikalala humo na mwanangu kwani yule mtoto alishakuwa mwanangu kwasasa, sikutaka kumpoteza kabisa, sikutaka atoke mikononi mwangu na kama kufa basi nilikuwa tayari afie mikononi mwangu ila namshukuru Mungu, yule mtoto alikuwa ni mkakamavu licha ya misukosuko ila bado alihimili vishindo vya dunia.
Asubuhi na mapema, yule mzee alikuja kunifata na kwenda kunipakia magari yaendayo Mwanza, kisha akanipa pesa kiasi ya kunisaidia nilimshukuru sana kwani si rahisi mtu kukusaidia hivyo wakati hakufahamu.
Safari ya kwenda Mwanza ikaanza, mawazo yangu ni vile ambavyo shangazi atanipokea, sikujua atanichukulia kwa njia gani ila nilienda tu.
Tuliingia Mwanza kwenye mida ya saa moja usiku napo ni kutokana na barabara mbona na kuharibika haribika kwa gari nililopanda na mvua iliyonyesha siku hiyo.
Nilienda moja kwa moja hadi nyumbani kwa shangazi, nikiwa mlangoni kabla sijaingia ndani nilimsikia shangazi akizungumza.
"watoto wa kuokota sio watoto kabisa, mtoto akishatupwa na wazazi wake ujue ana laana hafai kabisa. Kwakweli mimi mtu yeyote akileta mtoto wa kuokota humu ndani, nitaenda kumtupa jamani. Sitaki kabisa watoto wa kuokota"
Kwanza kabisa nilishtuka na kujiuliza shangazi amejuaje, ila sikuelewa mazungumzo yao yalihusu nini hadi shangazi kusema vile ila nikajipa moyo na kusema kuwa lazima niendelee na ileile stori ya kutelekezwa ili shangazi amuhurumie mwanangu.
Nikaingia ndani, wote wakashangaa kuniona kwani hakuna aliyetarajia kuniona kwa wakati ule.
Shangazi akauliza kwa hamaki,
"mbona gafla jamani!! Kwema huko kweli?"
Nilikuwa nalia tu, nikamwambia shangazi kuwa Jumanne kanifukuza na kunitelekeza na mtoto yule, nilijua shangazi atanielewa ila shangazi hakunielewa na hakutaka kunielewa kabisa.
"Kwa mila za kwetu, kijana anapochoka kuishi na binti inabidi aje yeye mwenyewe kukukabidhi kwetu. Kingine nimekuozesha bila mtoto halafu wewe unanirudia na mtoto kwa misingi ipi?? Haiwezekani kabisa na siwezi kukupokea, bora hata ungekuwa peke yako ila na mtoto hapana. Itabidi tu urudi kwa mumeo, leo utalala hapa ila kesho sitaki kukuona. Rudi tu kwa mumeo."
Nililia sana, nilimkumbuka baba na mama. Kweli mzazi ni mzazi, sidhani kama wazazi wangu wangekataa kunipokea kiasi kile.
Sikuwa na raha kabisa, niliwaza tu niende wapi na yule mtoto.
Wazo likanijia kuwa niende Arusha kwa bamdogo, nikamuombe msamaha labda atanipokea.
Kesho yake, nikaondoka nyumbani kwa shangazi walijua narudi Dar ila nilienda Arusha kwa bamdogo.
Mwili wangu ulikuwa unanuka sana, sikuwahi kuoga tena toka nitoke Dar kwa kuhofia kumuacha mtoto chini na kupatwa matatizo.
Kufika Arusha nyumbani kwa bamdogo, huko ndio ilikuwa balaa zaidi. Bamdogo hakutaka hata kuniona, akanifukuza kama mbwa huku akisema nitakula jeuri yangu. Bamdogo aliongea mengi sana kuwa alinikataza kuolewa na Jumanne ila kiburi changu kimeniponza.
Nilikaa nje ya nyumba ya bamdogo, chini ya ule mti ambao Jumanne alisimama kwa mara ya kwanza aliponifata Arusha kwa bamdogo.
Nilikumbuka mengi sana na kulia sana, nilijiuliza maswali mengi kuwa upendo ule wa Jumanne alionipenda Mwanzo uko wapi, maana aliniacha kabisa, hakunitaka tena wala kunitamani. Nililia sana wala sikufikiria kama Jumanne aliyenipenda kiasi kile angenitenda vile.
Mara akaja mtu na kunishika bega, kumuangalia alikuwa ni Maiko.
Akanishika mkono, akanipakiza kwenye gari yake na kunipeleka nyumbani kwake.
Kufika kwake, akaniambia nisijari. Atanilea, atanitunza mimi na mwanangu nisiwe na shaka yoyote.
Nilifurahi sana kupata msaada ila sikujua kitu kimoja, kumbe Maiko alikuwa na mpango wake kabambe juu ya yule mtoto.