Riwaya: Wahuni Wote Peponi

Riwaya: Wahuni Wote Peponi

SABA



KUFA KUFAANA!

Ama kweli, kufa kufaana.

Habari mbaya husambaa mapema kama upepo, tena kwa bila gharama kuliko habari njema. Kuanguka kwa Sijali kukawa gumzo Buza nzima. Uhasama baina yake na mke mwenza ikawa tamu na chungu kwa wambeya kutoka Buza kwa Lulenge. Kaka wa mtu mwenye miradi yake mbalimbali, akasikia habari za kuanguka ghafla kwa mdogo wake—akawahi kwenda kumtazama ili kuona nusura inapatikana vipi.

Alimkuta Amina akigaagaa na kilio kikiwa ndio wimbo wa Sijali, povu likimtoka mdomoni.

“We Amina, embu jikaze kwanza, tumwinue tumpeleke sehemu kwa mtaalamu wangu,” alisema Abdi, kaka wa Sijali na Amina. Kijasho kikamtoka katika kumkukulusa Sijali. Mwembamba lakini uzito wa reli una husika.

Wakamtoa mpaka nje, kwa bahati, Bajaj ikawa inapita. Wakaisimamisha na kumpakia.

“Tupeleke Mwanagati upesi,” alisema Abdi huku akihema kwa wasiwasi. Povu liliendelea kumtoka polepole Sijali huku jicho likiwa leupe likitazama mbingu. Amina asiseme kitu wala kuuliza, alikuwa akichezesha mikono yake kwa wasiwasi wa kumpoteza dada, kipenzi, shoga na mshauri wake mkuu wa maisha—Sijali. Kutoka Kwa Lulenge hadi Mwanagati si mbali kwa safari ya chombo. Baada ya dakika 15, walifika sehemu waliyokusudia. Mzee maarufu kwa uaguzi wa kilozi aliyetambulika kama Mkuu Kimbulaga. Naam, walikaribia kilingeni, utaratibu hakuna kupiga hodi. Kurupu tii, ndani.

“Mkuu tumekuja, dada yangu huyu ameanguka ghafla na kuanza kutoa povu mdomoni na puani,” alisema Abdi aliyeonekana kuchanganyikiwa. Mkuu akatulia, akaanza kumsaili Sijali kuanzia kichwani hadi miguuni. Akashika usinga wake, akauweka kichwani kwa Sijali.

Akautoa na kuuchopeka katika maji aliyokuwa nayo pembeni yake. Maji yenye mchanganyiko wa madawa mbalimbali ayajuaje bwana mganga, akanyunyiza kichwani mwa Sijali. Bado jicho liliendelea kuwa legelege, mikono imelegea, haeleweki kama anapumua au la. Jicho mbiruko wake mithili ya kuku mdondo.

Mkuu akaanza kuimba nyimbo za kiaguzi,

‘N’sebo-n’sebo nchike imwana!’

‘N’sebo-n’sebo nchike imwana!’

‘N’sebo-n’sebo nchike imwana!’


Hakuwang’amua kitu, Mkuu aliendelea.

‘N’sebo-n’sebo nchike imwana!’

‘N’sebo-n’sebo nchike imwana!’

‘N’sebo-n’sebo nchike imwana!’


Akachopeka tena usinga majini, akauinua juu kabisa kisha akauchapa kichwani kwa Sijali. Pigo hilo likatoa cheche, angalau tumaini la uhai wa Sijali kubaki maungoni likionekana. Sijali akatikisika. Akaanza kuchezesha vidole.

Mwili ukaanza kutetema. Kasi ya kutetema ikazidi, akatetema kiasi cha kuanza kutoa mapovu hata yule aliyemshika—Amina akazidiwa nguvu. Sijali akaanza kubidukabiduka na kugaagaa chini kama samaki aliyeopolewa kutoka majini. Mganga akamsogelea, akachota dawa kutoka katika kibuyu chake na kumlambisha Sijali.

Hakuwa na hali ya kurejesha mlambo wa Bwana Mganga. Akachopeka tena usinga katika chungu chake, safari hii kilikuwa kimepata moto barabara, mwaah! Maji kichwani mwa Sijali. Kutetema kuliendelea, akamshika vilivyo Sijali kiunoni.Akamimina maji aliyoteka na usinga wake kwa nguvu—Sijali akatulia tuli.

Asicheze tena, akamwinua na kumuweka kitako. Dera alilovaa lilikuwa limelowa maji ndembendembe. Kitako akakaa, pumzi anahema lakini macho yangali yamefungwa. Kufungua hawezi. Kifua kimejaa pumzi, panda shuka.

Mkuu akaweka kibuyu kichwani cha Sijali, kikakaa bila kuanguka. Akachota unga mweupe na kuutapakaza mwilini mwa Sijali. Akanywa maji kisha akamtemea Sijali. Ndani yake kulikuwa na ugoro, mauchafu mengine ya kutia kinyaa, lakini Sijali ni kama jina lake, hakujali. Hakuwa na uwezo wa kung’amua yaliyokuwa yakiendelea mwilini mwake.

Mkuu alicheza ngoma zake huku akiimba;

Kinyamkera, genda-genda kumwenu, genda!

Kinyamkera, genda-genda kumwenu, genda!

Kinyamkera, genda-genda kumwenu, genda!


Aliyacheza mayenu ya kiganga ipasavyo, akachota maji yalokuwa chunguni kiasi na kuchanganya mengine yalokuwamo ndani ya kidoo cha plastiki kidogo. Akatia na unga mweupe alioumwaga mwilini mwa Sijali, akachanya na majani mengine kisha kuyavuruga kwa mwiko.

Akachukua majimaji mengine yasiyoeleweka kisha akachanganya katika kile kidoo. Mvurugo ulivyokubali, akainua kidoo na kumwaga maji yote mwilini kwa Sijali huku kibuyu kikiendelea kubaki imara kama hakuna lolote lilitokea.

Dakika moja baadaye, tangu maji kumwagiwa maungoni mwa Sijali, akaanza kupiga kelele sasa. Babu akachota unga mwingine wenye mwonekano wa maziwa akachanganya na asali kisha akamlambisha tena Sijali kwa nguvu safari hii.

Sijali akameza, Mkuu akamwamuru Abdi akae nyuma ya Sijali. Amfunge kiunoni kwa mikono yake miwili kulia na kushoto. Akamtaka ambinye kwa nguvu. Sijali akaanza kuhisi kusukuma, msukumo ulitokea tumboni.

“Mbinye kwa nguvu,” alisema Mkuu. “Mbinye bila huruma, hii ndiyo tiba yenyewe. Hii ndiyo tiba yenyewe,” aliongeza Mkuu. Abdi akahamanika. Uamuzi ukawa haukuchukua mkondo wake.

“Unashangaa nini?”

“Unashangaa nini?”

“Unashangaa nini?”

Alisema kwa kurudia maneno Bwana Mganga. Abdi akaamka, akaanza kumbinya kwa nguvu Sijali. Sijali akatoa upepo sana hadi hapo vijiko, vikombe, misumari na visu vilivyoanza kutoka tumboni mwake. Viliingizwaje, hajui. Amina akaanza kuogopa.

“M’binye!”

“M’binye!”

“M’binye!”

“M’binye!”


Bwana Mganga aliendelea kuchochea mambo. Abdi hakusita, akaendelea kum’minya dadaye huku akitikisika. Vitu vya ajabu-ajabu vilitoka katika tumbo la Sijali. Baadaye akaanza kutapika mavitu meusi kama oili chafu, ilimwagika mpaka damu zikatoka.

Sijali akaanza kukohoa kwa nguvu sana, Abdi akashindwa kumshika, matokeo yake akamwachia. Sijali akaenda chini, mikono imeshika ardhi, akaanza kuunguruma kama simba, kikohozi kikaendelea. Alikohoa hadi akatema kifaranga cha kuku cheusi kilichokosa macho.

Baada ya kukitoa tu, akenda chini mithili ya gunia lililomshinda m’bebaji.

Udenda ukamtoka kama wote. Akaanza kufumbua macho polepole, vidole vikaanza kuchezacheza kama mtoto mwenye degedege. Kidogokidogo akaanza kuinua kichwa, mara mwili, hatimaye akajiweka sawa. Akafungua jicho lake kwa upole, akamtazama Bwana Mganga, kushoto kwake alikuwapo Amina.

“Loh! Kuna nini tena? Mbona nimeloa mwili mzima… Mbona kama vile…” Hakumaliza kusema Sijali Bwana Mganga akadakia, “Tulia kwanza, ‘ebu tulia. Utafahamishwa upo wapi, shaka-ondoa!” Alisema Bwana Mganga na sauti yake ya mkwaruzo.

Sijali akashusha pumzi ndefu. Akaanza kuishikashika shingo yake, akajinyosha huku na huko. Akautingisha mwili mno kila alipoweza.

“Mbona kama vile nimetoka kubeba mizigo mizito sana, ilikuwaje jamani?” Sijali alisema tena. Abdi na Amina wakawa kimya. Hawakutia neno kwa sababu hilo lilimuhusu zaidi Mkuu Mganga.

“Tazama mbele yako!” Mkuu alisema. Sijali akatazama lakini asielewe chochote alichoambiwa akitazame. “Nd’o nini hizi—takataka, au?” Sijali alijibu kwa mshangao badala ya kujibu swali kwa swali. “Mzigo wote ulikuwa tumboni mwako huu,” Mkuu alijibu. Sijali akaziba mdomo wake kwa kutumia kiganja cha mkono. Akastaajabu viliikaje tumboni.

“Kweli vimetoka tumboni mwangu hivi?” Sijali alisema.

“Ndiyo, vimetoka tumboni mwako wewe hapo!”

“Inawezekanaje?”

“Vivyo-hivyo, si unaona vimetoka?”

“Mmmh, hata siamini hichi ninachokiona machoni pangu,” Sijali alisema kisha akajiegesha ubavu huku mhemo ukiwa mkubwa. “Tulia sasa kwanza maana ulipotea katika viunga hivi vya ulimwengu. Nimekurudisha kutoka mbali sana nikiwa na makomandoo wangu. Huwezi kuwaona. Wapo hapa wametuzunguka!” Alisema Mkuu kisha akawa anatoa pumzi, psssiiii! Mara chungunzima.

“Samahani, hivi ni nani aliyenitenda hivi?” Sijali aliuliza kwa kitetemeshi, akajiweka sawa tena kwa mara pili huku akisubiri jibu la Mkuu. Mkuu akainua kichwa juu, akamtazama vyema Sijali.

“Usitake kunitia ubayani, ukweli unaujua. We kaa, jitafakari una ugomvi na nani… Ugomvi hasa na si kiji gomvi. Jibu ukilipata ndiye aliyehusika,” Mkuu alisema kisha akaweka tuo. Sijali hakusema kitu. “Nitakupa dalili au alama za mbaya wako… Ni mwanamke, ametokea mahali ambapo juwa linachelewa kuzama. Asili ya watu wa huko, wengi huzihofia huenda wakawa watu wa mataifa mawili. Aaaah, ahaaaah,” Mkuu aliendelea kuunguruma, akaweka tuo kisha akaendelea.

“Ukifanya mchezo, utapotea! Inabidi upambane hasa. Upambane vilivyo—vinginevyo gari la bure litakuhusu!” Alisema Mkuu na kunyamaza. “Mmmhh! Kama nd’o hivyo basi nikubali tu kushindwa—nje ya hapo ni kujitafutia kifo,” alisema Sijali huku kijito cha machozi kikianza kutiririka mashavuni kwake.

Mkuu hakusema kitu. Akainuka pale alipo na kumfikia Sijali.

“Shika hii!” Alisema Mkuu. Sijali akanyoosha mikono yote miwili. “Inua juu kabisa mikono yako. Kinga” Aliongeza Mkuu. Sijali akatii bila shuruti. Mkuu akaweka kibuyu juu chake juu ya viganja vilivyokunjwa mithili ya bakuli vya Sijali.

“Toa mfuniko wa kibuyu kisha kunywa fundo moja dawa iliyomo humo,” alisema Mkuu. Sijali akafuata maelekezo.

“Mmmmhh!!!! Chuuuuunguuu balaa!” Alisema Sijali.

“Naam, nd’o dawa! Iwe tamu imekuwa jojo hiyo,” Mkuu alijibu. Sijali akaendelea kuvumilia machungu yaliyosafiri hadi ubongoni mwake. “Sasa hakuna shida. Nimekukinga dhidi ya machawi. Uwende salama. Hutosumbuka, ila tu, kwa sasa, ungeachana na yule mwanaume kwa muda ili kupisha upepo wa dhiki,” alisema Mkuu.

“Sawa, nitafanya hivyo!” Sijali alijibu.

****​

Siku tele zikapita kama kimbunga, Sijali akawa anajituliza nyumbani kwao bila kuwa na shughuli ya msingi. Siku moja alikuwa kwao akimsuka mtu nywele za rasta za kupendeza, akapita mdada mmoja aliyependezewa na ujuzi wa kusuka misuko mtindo mvuto ya Sijali.

“Dada, hii nd’o ofisi yako?” Aliuliza dada mpita njia. “Hapana. Hapa ni kwetu tu—sina ofisi kama ofisi,” Sijali alijibu.

“Daah, nimependezewa sana na ujuzi wako, hasa uchakataji nywele,” alisema yule dada.

“Ahsante, karibu na wewe usuke!” Sijali alijibu kimashauzi.

“Lakini…” Alisema yule dada bila kumaliza maneno yake. “Basi, wacha tu. Haya, kwaherini,” aliaga yule dada.

Kabla hajapiga hatua ya pili, Sijali akamwita, “lakini nini dada—mbona hujamalizia sentensi yako?”

Dada akahamanika. Akashusha pumzi kiasi na kutuliza mchecheto wake. “Nina Saluni pale karibu na Buza, kwa Mama Kibonge, sina fundi wa nywele mwenye ubora wako—ningependa uwe mmoja wa mafundi zangu,” alisema yule dada kisha akaweka tuo.

“Kama hutojali, lakini!” Aliongeza yule dada. Sijali akatuliza kichwa chini kwanza, ili akili imkae sawa. Akakiinua kichwa na kumtazama dada aliyemsimamia mbele yake. Mwenye kimo chake, sura ndefu ya Kisomali, nywele za gharama zilizompendeza na jinzi ya rangi ya samawati mpauko. Nguo imeshikana na nyama za mwili, ukimwona lazima shingo igeuke.

“Kwa hiyo unataka kuniajiri au?” Sijali aliuliza.

“Unaweza kusema hivyo, lakini zaidi kama mwenza wa kibiashara—kwa maana ujuzi wako utavutia watu kuja saluni kwangu, hivyo tutakachopata, basi tutagawana kwa namna yoyote ile itakavyokuwa,” alijibu yule dada.

“Haya, sio mbaya. Lini nije?” Sijali alijibu.

“Hata leo twende ukapaone!”
“Basi ngoja nim’malize huyu kisha twende, dada,” alijibu Subira. Yule dada akaketi chini na kusindikiza mazungumzo aliyoyakuta wakizungumza wenyeji wake. Mambo ya kike karibia sawa tu. Alimaliza, wakachukuzana mpaka ofisini kupaona. Akaoneshwa wafanyakazi wengine, utambulisho na kadhalika.

Siku iliyofuata alifika ofisini mapema baada ya kupelekwa jana, uenyeji umepamba moto. Kama haitoshi, akaja na shogaye maarufu wa mtaani, Bi. Avijawa. Mboni ya jicho la Sijali, msiri wake na mshirika mwenza katika mambo mbalimbali.

Kazi iliendelea na mwitiko ukawa mkubwa sana kwa saluni ya huyo dada. Ikawa habari ya Buza, mambo kwa ‘Mama Eliza Hair Dressing Saloon,’—masiku yakasafiri, Sijali akasahau maumivu ya nafsi yaliyosabishwa na mumewe, akajiona mpya katika dunia ya kale. Mafanikio yakapatikana, fedha zikawa nyingi. Maisha ya dhiki yakamtoka. Furaha ikatawala na majonzi yakazikwa mazima.

Urafiki ukawiva baina ya mwenye saluni, ‘Madam Rehema Mshindo’ na Sijali. Utamwambia nini mtu na fundiye, kila kona wote, kila baa wote, sijui kupika dada, wote! Urafiki mpya umestawi na kusimama wima vilivyo. Hata wale waliotangulia hawakupata bahati hii. Bahati ya kupendwa na mwenye mali kama mmezaliwa tumbo moja.

Furaha ya milele, si mali ya mwanadamu.

Siku moja asubuhi na mapema, aliamka kama ilivyoada, majipambo kawaida kwa wasichana, safari ya kazini ikaanza. Akiwa anaikaribia ofisi, mapigo ya moyo yakaanza kwenda tofauti na ilivyo kawaida. Wasiwasi ukamwingia. Hata kasi ya kutembea ikapungua, akawa anatafuta cha kukishika walau aamini alichokiona katika ofisi yake.

“Nini tena jamani hii?” Sijali alisema, mara hali ya kumwaga chozi ikabisha hodi. Kashindwa kuzuia machozi yake. “Sasa dhiki inaondoka, faraja inatawala, kumbe lilikuwa suala la muda tu? Ama kweli ng’ombe wa maskini hazai,” alisema Sijali huku akishika kichwa na mkoba mkononi.

Kufuli la mlango wa geti la saluni lilikuwa chini, kama haitoshi, geti lote lipo wazi cheeekwaa! Ndani yake hakuna kitu. Wamesomba mpaka makopo ya dawa. Walichoweza kuwaachia ni mbao za shelfu za kuwekea vitu na vioo vidogo, maana hata vile vikubwa vya kujiona, wamekwiba.

Kilio kisichosikika kikafanikiwa kumkamata, Sijali. Muda huo, shogaye Bi. Avijawa alikuwa hajafika, punde akafika, akakumbana na madhila haya. Sijali akamwelezea kila kitu, mbaya zaidi, eneo lao fremu iko moja, moja tu kama roho, kama haitoshi, iko katika nyumba ya mtu.

Kajenga nyumba yake, lakini mbele kuna fremu. Avijawa akamsihi Sijali kutulia, washikamane vyema ili kulimaliza tatizo. “Em twende tukaulize kwanza huko ndani,” Avijawa alisema. Sijali akajibeba, wakagonga kigeti kidogo cha nyumba hiyo, nukta chache mlango ukafunguliwa. Akatoka binti mdogo wa umri kati ya miaka 14 hadi 16.

“Eti mmesikia chochote kinatokea nyakati za usiku?” Avijawa alihoji, Sijali hakuwa na hali. Hata kuinua mdomo kulimshinda. Alikuwa akijivutavuta huku midomo akiibana vilivyo. Kwa hakika uchungu usiomithilika ulishika hatamu.

“Hata sijui, labda nimwite mama mumwulize,” alijibu yule binti. Akaondoka na mlango akaufunga nyuma yake. Nukta chache tena mbele, mama akatoka. Alikuwa wa makamo hivi, makunyanzi yalishaanza kubisha hodi. Huhitaji digriii kujua mtu wa makamo, “niwasaidie nini,” aliuliza yule mama aliyetoka.

Avijawa akamwamkia, maana mama hakutoa hata salamu ya asubuhi. “Jana usiku tumeibiwa hapa saluni kwetu, je, mlipata kusikia pilipilika zozote zile?” Aliuliza Avijawa. Mama akakunja kidomo chake, akajiseti uzuri, akamtazama Avijawa kuanzia juu mpaka chini kisha akasema.

“Hapana, sijasikia pilika zozote zile!”

“Kabisa, hata kidogo?”

“Ulitaka jibu gani zaidi ya hilo?”

“Lakini mama tupo katika shida, ndiyo maana tunaulizana, sa’ si tumwulize nani kama si nyinyi majira zetu?”

“Hainihusu. Kifupi, sijasikia kitu, usinichoshe kwa maswali yako ya kijinga,” alijibu yule mama akisindikiza na sonyo kama nukta ya maongezi yake. Lango likabamizwa mpaka upepo wa m’bamizo ukampungia hewa yake Avijawa.

“Maswali ya kijinga tena?” Avijawa alisema polepole kwa kujiuliza.

“Mmmh, mi’ kisirani, lakini huyu mama nambari nyingine!” Avijawa aliongeza. Wakabebana na shoga’ke mpaka saluni kwao. Wakaketi chini kubawabu yaliyowasibu ni kitu gani? Wakiwa katika ukumbi mzito wa mawazo, kidogo mwenye mali akatokea. Akawakuta nje mlangoni kabisa mwa saluni, huku lango likiwa wazi na wao wamezama katika dunia ya mawazo.

Sijali kauzika uso wake na mikono, maana chozi lilikuwa likimtoka mmwago wake sawa na bonde la mto Mzinga.

“Kuna nini hapa? Mbona vilio tena?” Madam Rehem aliuliza. Sijali hakujibu kitu, Avijawa akadakia. “Tazama saluni ndani.” Madam akasogea kuchungulia. Hakumaliza hata ngazi za kuingia ofisini, pochi ikamponyoka. Mikono akaitwisha kichwani.

Yowe likamtoka, lile lisiloezeka kama ni vigelegele au sauti ya kuchanganyikiwa. Akapiga kimya, nguvu zikamwisha. Akabwagika chini pasipoumiza. Ngazi zikawa kiti chake. Hakusema neno lolote kwa takriban dakika 15, kwa hakika mawazo yalichachamaa.

“Nendeni tu, ngoja nifuatilie hii kesi,” alisema Madam Rehema. Sijali na Avijawa wakainuka na kwenda zao. Bado Sijali hakuamini kilichotokea. Alihisi kuchanganyikiwa kama si kuvurugikiwa. Amekuwa malikia wa tabu, amejitafakari sana.

Masaa manne baadaye_

Sijali na Avijawa walikuwapo kibarazani kwao wakitafakari yale yaliyotokea, ghafla ubavuni mwa nyumba ya akina Sijali wakatokea polisi watatu. Wanaume wawili, mwanamke mmoja. “We’ nd’o Sijali?” Polisi wa kike aliuliza. Sijali akashangaa, hakujibu kwanza. “Kwani kuna nini?” Sijali alihoji. “Jibu swali, we’ nd’o Sijali?” Polisi aliuliza tena kwa ukali. “Eeeh, nd’o mimi!” Alijibu huku jicho lake likiwa limemtoka pima. Mikasa juu ya mikasa.

“Twende polisi tukachukue maelezo yako…” Alisema yule askari wa kike kisha akaweka tuo. “Lakini…” Kabla Sijali hajamaliza kuongea, askari wa kiume akamdakia, “Utaelewa kituo cha polisi,” alisema huku akimkazia macho.

“Lakini,”

“Eeeh, we mwanamke tumechoka na hizo lakini zako. Em twende kituoni,” alisema kwa hamaki yule askari wa kike.

“Mjumbe wangu hajui, ndo utaratibu gani huu? Sasa sitoki!” Sijali alijikakamaza katika kutaka itifaki izingatiwe. Askari wakatazamana, wakamsogelea wote kwa pamoja pale alipo.

Nukta chache baadaye, Sijali akaonekana kushikwa na butwaa. Hasira si hasira, hamaki si hamaki. Uso akaukunja kupita maelezo. Mkono shavuni. Alilambwa kofi na yule askari wa kike.

“Usinifanye niongeze lingine,” aliongeza yule askari wa kike. “Basi mama nakwenda,” Sijali alijibu. “Na wewe ongoza, ulidhani utakosekana katika hili?” Alisema askari wa kiume. Sijali na Avijawa safari ya kwenda chumba cha bure kuingia kutoka na hela ikawadia.

Hawakupelekwa tu kama malkia, bali watuhumiwa wa kuaminika. Masingi yalihusika kiasi kikubwa wakiwa njiani—achilia mbali masimango na maneno ya kukinaisha nafsi, yalitumika kama njugu. Walifungwa fundo madera yao na kutumika kama pingu.

*****​

Kijiweni, Buza Kanisani, mahali pa mgahawa, walikutana wasichana watatu wanaofanya kazi ofisi moja ya kupamba nywele. Ofisi ambayo Sijali na Avijawa wameitwa hivi karibuni.

“Hivi wenzangu hamjahisi mabadiliko yoyote yale pale ofisini?” Aliuliza Hamida ambaye awali alikuwa kiongozi wa saluni kabla madaraka yake kupokwa na Sijali.

“Kama yapi kwa mfano?” Aliuliza shogaye Hamida, mwenye jina la Rose. “Mabadiliko shoga, hamuoni bosi anavyowapetipeti wale wenzetu?” Hamida aliongeza. Akazua jambo la kupindisha midomo kwa wenzake. “Mmmh mwenzangu! Sina hata hamu!” Alisema shoga wa tatu mwenye jina la Upendo.

“Yaani, tunakubali vipi sisi kupigwa bao na mafolena?” Hamida alijazia juu yake. “Hata sielewi tunafanyaje. Bosi siku hizi hana mpango na sisi kabisa. Kwa mwenendo huu, shoga tutegemee kutokuwa na chetu muda wowote ule kuanzia sasa,” Hamida alisema.

“Kwa hiyo una mpango gani?” Aliuliza Upendo. Hamida akatulia kwa nukta chache kutafakari kwa kina. “We’ Rose yule bwana’ko mwizimwizi unasemaga sijui anakufikishaga ukikutana naye—bado una mawasiliano naye?” Hamida aliuliza.

“Kwanini umekimbilia huyo?”

“Nimeuliza tu kwanza, nijibu bado una mawasiliano naye?”

“Ndiyo, kwanini—nauliza tena?”

“Yule tumpe mchongo!”

“Mchongo gani?”

“Aibe pale kisha tuwasingizie wale akina Sijali. Hivyo vyombo tutaenda kuanzisha saluni yetu mahali kwingine, popote pale hata kama itakuwa Gongo la Mboto,” Upendo alihitimisha.

“Duh! Kumbe!” Rose alichagiza.

“Eeeh, mama, usizubae. Siuelewi upepo ujao mimi,” alisema Upendo.

“Ngoja nimtafute,” Rose alisema kisha akatoa simu yake kumpigia bwana’ke mwizi.

“Haloo!” Rose aliitikia simuni.

“Eh, niambie, Rose. Usiniambie umemisi mambo yangu. Afu n’likuwa nakuwazia ‘apa!” Ilisema sauti kutoka upande wa pili wa simu. Rose akatulia kwa sekunde kadhaa kupisha pupa ya maongezi ya bwana’ke.

“S’kia Stone Mdudu, kwanza!” Rose alisema.

“Enhee, nakusiliza!

“Nina dili kubwa sana! Upo tayari?”

“Dili gani tena?”

“Kuna mtu kazingua, sasa tunataka tumwoneshe ka’ si watoto wa mjini.”

“Unataka nikusaidieje katika hilo?”

“Kwenye simu itafaa kuongea au tuonane tu?”

“We’ uko wapi Bi. dada?”

“Niko Buza Kanisani, hapa katika kibanda cha Mama Kwini, nakunywa maziwa. Unaweza kuja?”

“Ndiyo naweza. Dakika sifuri tu n’takuwa hapo!”

“Sawa, wahi… chukua bodaboda n’talipa miye!”

“Sawa!”

Wakatulia kusubiri ujio wa Bwana Stone Mdudu.

Punde akafika. Akamkuta Rose akiwa na wenzake wawili. Macho kwake. Akataka kusita kusogea kibandani kwa Mama Kwini.

Rose akamnyooshea mkono kwamba yupo pale. Stone akasogea.

“Mbona inzi kibao—we’ Rose vipi we’? Stone alifoka kabla hata ya salamu. “Tulia basi kwanza,” Rose alimtuliza. Stone si mweledi wa ukali kwa watoto wa kike. Akatulia kusikiza kusudio la wito.

“Kaa basi,” Rose aliongeza. Stone akajivuta hadi karibu ya Rose. “Habari za asubuhi, shem!” Upendo alimsalimia Stote. Stone akaitikia kwa kichwa bila kutamka neno lolote. Ikawa ndiyo stopu kwa Hamida naye kumsalimia Stone.

Uso kaukunja mithili ya mtu aliyelamba ndimu. Kisirani kipo barazani kabisa mwa uso wa Stone.

“Nakusikiliza,” alisema Stone kwa kisirani.

Rose akashusha pumzi, akamtazama Hamida mwenye wazo. Hamida akamtaka Rose yeye nd’o amwelezee bwana’ke mpango wao. Rose akamwelezea kwa kirefu. Stone akawa mtu wa kutikisa kichwa. Akapewa ukomo wa tukio ni kwamba lazima liwe ndani ya masaa ishirini na nne tangu walipokutana.

“Neno la mwisho, ukivichukua, vihifadhi sehemu tutavifuata sisi halafu tutakupoza kiasi utakachotaka!” Alisema Hamida aliyeonekana mchora ramani mkuu wa tukio hilo. Stone akaitikia tena kwa kichwa bila kutia neno.

“Poa basi bebe, kesho au baadaye tutaonana!” Rose alisema. “Poa. Hakuna noma!” Stone alijibu.

*****​

Tukio likatukia.

Furaha zikatawala miongoni mwao. Vicheko vya shangwe ya kuyashinda katika maisha vikatamalaki. Walikubaliana wakutane mwembeni kwa Mama Mwambene huko Mokigo Barabara ya Mwinyi siku ya pili tangu tukio litokee.

Saa nne asubuhi walifika.

Furaha na vicheko, stori za udaku ziliendelea.

“Shoga, wale mbwa watajibeba. Madam Rehema alinipigia simu kuniuliza masuala ya wizi, nikatoa dukuduku langu kwamba huenda wageni wetu nd’o walotupiga!” Upendo alisema.

“Weeeeee!!! Niambie koma!” Hamida alichagiza.

“Nd’o nakwambia bibi koma, ukomae, kaa chini udumae!” Upendo alijibu.

“Heeheeee! Halooo! Shuntuuuuu!” Walisema kwa pamoja wakigongosheana mikono.

“Shosti, ‘ebu mpigie basi huyo bwana’ko,” alisema Upendo. Rose akachoropoa simu alikoiweka, hewani.

Rose akageuka kuwatazama wenzake. Akapiga tena na tena. Akainuka pale alipoketi. Akasogea pembeni, akapiga tena simu. Uso wake ukaanza kuingiwa na simanzi. Kifua kilimjaa kiasi wenzake waingiwe na wasiwasi.

Simu haipatikani.

“Vipi tena shoga, mbona sura imekengeuka?” Hamida aliuliza. Rose asijibu kitu. Akaanza kulia. “We’ vipi tena?” Upendo alihoji akienda alipo Rose.

“Stone hapatikani katika simu,” Rose alijibu huku akilia. Mwili wote uliloa kwa hofu. Hamida akarudi nyuma hatua moja. “Unatuchezea shere eh?” Hamida aliuliza akiwa midomo mikavu. Macho yamemtoka pima.

“Lakini hili lilikuwa wazo lako, naomba usinibebeshe mie!” Rose alisema kwa hasira. “We’ bwana’ko unamjua, usitutanie nakwambia,” Upendo aliongeza. “Nimjulie wapi? Zaidi ya namna kadhaa, sina nilijualo kuhusu yeye,” Rose alijitetea.

Haikutosha.

Wasichana wakamvaa Rose.

Kipigo.

“Niacheni washenzi nyie,” Rose alipiga kite huku akijaribu kujitoa mikononi mwa Upendo na Hamida. Wakamdhibiti nywele zake vilivyo. Vuta kisawasawa.

“Tulia! Unadhani sisi wajinga kiasi hicho eh?” Upendo alisema. Walimtandika vibaya mno, hata wasijue kwamba wanamwonea. Walioiba wameibiwa. Wakati ngumi zingali moto, simu ya Upendo ikaita. Wakasimamisha ugomvi.

“Madam huyu anapiga,” Upendo alisema huku akitweta. “Pokea basi,” alisema Hamida. Akatulia kidogo Upendo. Wakatazamana kwanza kabla ya kupokea. Akabonyeza kitufe cha kupokea, lakini simu ikawa ishakata tayari.

“Nimpigie?” Upendo aliuliza. “Mpigie,” walisema kwa pamoja Rose na Hamida. Wakati anataka kumpigia, simu ikaita.

“Yeye huyo,” Upendo alisema.

“Pokea!” Hamida alidakia.

“Halo, Mama. Shikamoo!” Upendo alisema.

“Marhaba, uko wapi?” Madam Rehema aliuliza.

“Nipo tu, mitaani nazurura, madam,” Upendo alijibu.

“Njoo basi tukutane Abyola tukanunue vifaa vingine vya saluni,” Madam Rehema alisema.

“Sawa nakuja!” Upendo alisema. Akafurahi kusikia habari hiyo. Kabla hajatia neno la pili, simu ikaita tena. Akaipokea.

“Uje na wenzako—maana vifaa vitakuwa vingi,” Madam Rehema alisema.

“Sawa!” Upendo alijibu. Rose akagoma kuongozana na wenzake. “Kwa jema lipi mlonifanyia hata nikaingia kundini mwenu,” Rose alisema. “Bibi wee! Tupishege huko,” alisema Upendo huku akirusha mikono iliyotua pajani kwake kwa kuchapa.

“Aaah, bure kabisa!” Upendo aliongeza. “Hata kama bure, potelea mbali, lakini siendi nanyinyi,” Rose alijibu.

Wakasonyana mithili ya mijusi hizo sauti za misonyo.

Hamida na Upendo, wakafika kwa Abyola Buza. Wakampigia simu Madam Rehema.

Akapokea, wakamwona kwa mbali amesimama katika fremu moja njia ya kuelekea Kebo na Malawi Yombo Vituko. Akawapungia mkono. Wakamfuata pale alipo.

Wakasalimiana tena kwa mara ya pili.

Maongezi mawili matatu, wakazubaishwa na vicheko bandia miongoni mwao. Muda ukayoyoma pasi jambo la maana. Hamadi! Nyuma yao wakatokea polisi kwa mtindo wa kubaka panzi kumbe wamebaka watu. Wakawashika, tayari kwenda kituoni. Hali hii ikazua mtanziko kwa wasichana.

“Madam vipi tena?” Upendo aliuliza.

“Tutajua hukohuko kituoni. Twendeni kwanza!” Madam alijibu.

ITAENDELEA...
Ohooooooo
 
Back
Top Bottom