RIWAYA: Wivu-Beka Mfaume

RIWAYA: Wivu-Beka Mfaume

MTUNZI: BEKA MFAUME



SEHEMU YA KUMI


"Hata hivyo, bado ukifika unayo haki ya kukataa kukaa naye hoteli moja!Hakuna sheria itakayo kulazimisha kukaa naye hoteli moja!"

"Mohsein,"Dina aliita kwa utulivu, kisha akaendelea, "Pamoja na kwamba mimina Richard tuna uadui wetu, lakini bado ni bosi wangu. Kuna mambo ambayo naweza kumkatalia, lakini sio ya kikazi! Safari tunayokwenda ni ya kikazi na hata kama tutakaa hoteli moja bado litakuwa ni sualala kikazi. Lakini pale atakapotaka kunilazimisha kukaa chumba kimoja na yeye, hilo litakuwa sio suala la kikazi tena na nitakuwa na haki ya kumkatalia!"

Kauli hiyo angalau ikampa matumaini Mohsein,wivu wake ukashuka kwa asilimia fulani, lakini kitendo hicho cha Richard kutaka kusafiri na Dina bado kilikuwa kikimteketeza!Akatamani achukue ruhusa ya dharura ili naye aende Arusha kivyake vyake, akiamini kuwa karibu na Dina ndio njia pekee yakumlinda.

Hadhari aliyopewa na Dina kuwa amechumbiwa,ikaonekana kusahaliwa na Mohsein, akajiona yeye ndiye mwenye haki ya kummiliki Dina kuliko mtu mwingine yeyote!



***


JOHN aliwasiliana na baba yake na kumtaarifu kuwa, lile kusudio lake la awali la kutaka ndoa yake na Dina ifungwe mapema, sasa halipo tena.Sababu ile ile ya barua ambayo Dina alimwonyesha kama kikwazo kinachozuia kufunga ndoa mapema, ndio aliyoitumia kumwambia babayake.
"Kwa hiyo mmekubaliana?" baba yake alimwuliza.

"Alikuwa tayari tufunge ndoa mapema, lakini ni sababu hiyo ya barua ndio imeleta kikwazo," John alijitetea.
"Kwa hiyo sikumwambia tena kama ulikuwa ukimhitaji."

"Hakukuwa tena na ulazima,hata mimi nilitaka kuzungumza naye kwa suala hilo hilo. Lakini vipi kuhusu suala la upelekaji mahari, si bado liko pale pale?"
Kuulizwa swali hilo kukamkumbusha John kusudio lake la kutaka kwenda kijijini kwao kwa ajili ya kumfanyia ushirikina Dina. Akahofu pesa ambazo angekwenda nazo zisingetosha baada ya kuambiwa mganga atakayekwenda kumwona huwa anatoza gharama kubwa kutokana na sifa kuwa, wateja wake wengi ni vigogo wa Serikali. Taarifa hizo zikamuweka kwenye hitaji lakuongeza pesa ili aweze kuikabili gharama atakayotajiwa. Kwa kuwahakuwa na pesa nyingine za ziada ya akiba zaidi ya zile za mahari zilizokuwa zikisubiri kupelekwa kwa wazazi wake Dina, John akaamua alisimamishe kwanza zoezi la kupeleka mahari na pesa hizo zikafanyekazi ya ushirikina!

"Kwa kuwa ndoa yenyewe itafanyika baadaya miezi mitatu, nadhani hakuna haraka ya kupeleka mahari mapema,"John alimwambia baba yake.

"Ni wewe tu, hata ukisema zipelekwe leo au kesho ni wewe mwenyewe na maamuzi yako!" baba yakealimjibu.

Safari ya kupelekwa mahari ikaahirishwa! Umuhimu wakutaka kumdhibiti Dina kwa kumfanyia ushirikina ukachuku anafasi.

Kuchelewa kuyapeleka mahari hayo hakukuisumbua akili yake kwani aliamini, endapo Dina atatengenezwa na kuinamishwa kwa imani za kishirikina, basi kutampa uwezo wa kumwambia Dina waanze maisha ya kuishi pamoja kama mtu na kimada wake kisha ndoa ingefuata baadaye.

Aliamini hilo lingewezekana kwa sababu madawayangemdhibiti Dina na atakuwa akizipokea amri zake kwa kila atakachomwambia.
Huo ungekuwa ni ushindi mkubwa kwake wa kumsambaratisha Richard!

Siku ya pili, John alionana na Dina,akamuaga kwa kumwongopea kuwa anatarajia kusafiri kwenda kijijini mwishoni mwa juma kwa ajili kuwapelekea taarifa za harusi wazee wake wengine walioko huko na kuahidi angerudi Jumatatu.

Jumatatu hiyo ikamkumbusha Dina kuwa ndio siku ambayo yeye na Richard watasafiri kwenda Arusha!

Awali, Dina alikuwa amepanga amtaarifu John safari yake hiyo ya kwenda Arusha. Alipanga amwambie siku ya Jumapili asubuhi, siku ambayo ni kawaida yake kuitumia akiwa nyumbani kwa John hadi jioni kabla ya kurudi nyumbani kwao. Lakini hakupanga kumwambia kuwa angesafiri na Richard, alijua kauli hiyo ingemchanganya John. Badala yake angemwambia kuwa anasafiri kwenda Arusha kikazi kwa muda wa wiki moja. Lakini baada ya John naye kumwambia alikuwa akitarajia kusafiri, Dina akabadili azma yake yakutaka kuaga. Akaamua asubiri hadi John atakaposafiri, kisha ampigie simu huko kijijini atakakokuwa amekwenda amfahamishe kuwa na yeye amepata safari ya ghafla ya kikazi kwenda Arusha! Alijua kwa kufanya hivyo angekuwa ameondoa bugudha ambayo ingempata kutoka kwa John kama angemuaga wakiwa Dar es Salaam, aliamini John angeleta ligi yakuuliza maswali lukuki yenye mrengo wa wivu ambayo yangemhusisha Richard na kutaka kujua kama naye angesafiri, lakini kwa kupitia kwenye simu aliyaona maswali hayo yasingempa wakati mgumu kuliko kama ingekuwa ni ana kwa ana!

Alikwishaanza kukerwa na tabia za wivu zilizoanza kuonyeshwa na John alizokuwa akizielekeza kwa Richard dhidi yake tokea aanze kazi kwenye kampuni ya mzee Ken!

* * ** *

Hadi ilipofika siku ya Ijumaa mchana, Dina alikuwa hajaambiwa lolote kuhusu kujiandaa na safari aliyoambiwa. Alitarajia kuambiwa mapema mipango ya kujiandaa na safari itakavyokuwa, lakini hadi kufika siku hiyo hakukuwa na dalili zozote kutoka kwa Richard zilizoonyesha kuwa angelizungumzia jambo hilo.

Alishangaa kuona, tangu Richard alipomzungumzia kuhusu safari hiyo, hajawahi tena kulizungumza jambo hilo japo kwa kumdokeza muda wa kuondoka au safari hiyo itaanzia kituo gani. Ukimya wa kutoambiwa ulimuweka njia panda kwa sababu siku hiyo ya Ijumaa ndio siku ya mwisho ya wikikufanya kazi, siku zinazofuata za Jumamosi na Jumapili ni siku za mapumziko. Aliamini hata kama wangeondoka siku hiyo ya Jumatatu kama alivyokuwa ameambiwa na Richard, pengine kwa kuondokea ofisini kwagari la ofisi au la Richard mwenyewe, bado alistahili kuarifiwamapema ili hiyo Jumatatu aweze kuja kisafari.

Ukimya huo wa Richard haukuwa ukimsumbua Dina peke yake, lakini hata Mohsein ulikuwa ukimgusa, tena kwa kiasi kikubwa kutokana na kuteswa na wivu.Safari ya Dina kuondoka akiwa na Richard ilikuwa ikimuuma kila alipokuwa akiifikiria. Mawazo ya wivu yalikuwa yakimteketeza kila alipokuwa akiijenga picha ya uwepo wa peke yao kwa watu hao wawili watakapokuwa Arusha. Sononeko la kuchukuliwa kwa Dina kwenye mikono yake na kutenganishwa naye lilikuwa likimwadhibu. Bila ya kujijua,hali hiyo ikamfanya Mohsein apoteze uzito ndani ya siku hizo chacheza kusubiri Dina na Richard waondoke kwenda Arusha.

Safari hiyo ya Dina na Richard kwenda Arusha ilikuwa kama chachu iliyomzindua Mohsein kuujua uzito wa penzi lake lilivyozama kwa Dina.Awali alivyokuwa ameambiwa na Dina kuwa awe mwangalifu ili Richard asiyajue mahusiano yao kutokana na sababu zilizoelezwa, fikra za Mohsein zikamuweka kujiona kama shujaa aliyebahatika kumpata Dina nakuhisi burudiko la kumuwazia bosi wake anavyohangaika kupapata mahali alipopata yeye kiulaini na kumwona Richard kama ---- fulani aliyekuwa hatakiwi kimapenzi na Dina!

Lakini tokea Richard alivyorudikutoka Morogoro na kumjulisha Dina kuwa atasafiri naye kikazi kwendaArusha, upepo wa kumwona Richard kuwa ni '---- fulani' ukawaumegeuka! Wivu ukajitengeneza, ufala ukamgeukia yeye! Akaanzakumlalamikia Dina kwa kumtuhumu Richard kuwa anatumia madaraka yakekumlazimisha kusafiri naye kama njia ya kwenda kumlazimisha kufanyanaye mapenzi! Ingawa Dina alimpa moyo na kumhakikishia kitu kamahicho hakiwezi kutokea kwake, bado Mohsein alikosa imani.
Lolotelinaweza likatokea kati yao! Fikra hizo zikaendelea kumtafunaMohsein.

Lakini ukimya uliokuwa ukiendelea kujitokeza kuhususafari hiyo huku Dina akidai kuwa, Richard hajamwambia lolote jinginelinalohusiana na maandalizi ya safari hiyo huku wiki ikiishiakukatika, Mohsein akaanza kupata aina fulani ya faraja kuwa huendasafari hiyo haipo tena. Yeye kwa upande wake na kama ilivyokuwa kwaDina, wote kwa pamoja walitaka safari hiyo ivunjike, na ukimya huoulivyokuwa ukiendelea wakaanza kupata matumaini kuwa, pengine upouwezekano wa safari hiyo kutokuwepo tena na huenda ikawa ndio chanzocha ukimya huo!

Wivu, chuki na husda, Mohsein alikuwaamemuwekea Richard, akawa anaomba Richard afikwe na mabaya, kama vilekuumwa ghafla au kutokee jambo lolote litakalomzuia asiweze kusafirisafari hiyo na badala yake safari hiyo imwangukie yeye! Wakati akiwana mtafaruku wa msongo mkali wa mawazo na kukiri kumpenda Dina kwakasi ya ajabu na kujiona ndiye mwenye uhalali wa kummiliki, Mohseinakawaza kuwa, endapo safari hiyo itakuwepo kama Richard alivyopanga,basi ni vyema akafanya mpango kati ya Jumamosi au Jumapili amwombeDina aje nyumbani kwake ili awahi kufanya naye mapenzi angalaukuondoa usongo aliokuwa nao kabla ya Dina hajasafiri. Aliaminikufanya mapenzi na Dina kungekuwa ni aina ya faraja ambayoingempunguzia kukabiliana na machungu wakati Dina atakapokuwa hayupo,na angeitumia nafasi hiyo wakati wa kufanya naye mapenzi kumsisitizaDina asikubali kabisa kumpa penzi Richard watakavyokuwa wapoArusha!

Wakiwa ofisini mchana huo katika hali ile yasintofahamu ya uwepo wa safari hiyo ya Arusha, Mohsein akaona boraautumie wakati huo kumshawishi Dina aje nyumbani kwake sikuinayofuata kwa kusudio alilokuwa amelipanga la kufanya nayemapenzi.

"Dina," John aliita kwa kujiamini.
"Unaonajekesho…" akasita kuendelea baada ya kuusikia mlango wa ofisinikwao ukigongwa. Akaonekana kuchukizwa, "Karibu!" alisema kwahasira.

Akaingia msichana ambaye ni mfanya usafi na mpika chaiwa ofisini. Akasimama na kumwangalia Dina.
"Dada Dina,"alisema. "Bosi Richard anakuita ofisini kwake!"

Mohseinakahisi mfano wa kisu kikali kikichana katikati ya moyo wake!Akashindwa hata kumwangalia Dina wakati Dina alipoinuka. Dina akaionahali iliyomkuta Mohsein, akaamua kuondoka bila ya kusema lolote kwaMohsein. Mohsein akamwangalia Dina alipokuwa anauvuta mlango waofisini kwa ajili ya kuufunga wakati akitoka, akatamani kumuita nakumwambia asiende!

Dina akaufunga mlango nyuma yake baada yakutoka, Mohsein akabaki anasaga meno huku akiuangalia mlango huoukimsuta!
Dina alimkuta Richard akizungumza kwenye simu wakatialipokuwa akiingia ofisini kwake. Safari hii Richard aliupunga mkonowake kumkaribisha kwenye kiti huku akiendelea kuzungumza na simu.Dina akaenda kukaa na kubaki kimya huku akijiangalia kucha zake zamikono na wakati mwingine kuyazungusha macho yake kuziangalia kuta zaofisi hiyo kama kwamba ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia ofisinihumo.

Richard alimaliza kuzungumza kwenye simu na kumwangaliaDina huku akiirudisha simu juu ya meza. Akafanya tabasamu dogo."Nilikwambia safari ni Jumatatu vile?" alisema.
Dinaaliitikia.

"Ulishawahi kufika Arusha?"

"Bado,"Dina alijibu kwa sauti ya chini. Ghafla alijiona anazungumza na mtualiyemzoea.

"Tiketi yako," Richard alisema huku akimpaDina bahasha yenye rangi mchanganyiko buluu na nyeupe iliyokuwa nanembo ya kampuni yao.
Dina aliipokea na kuiweka mapajani mwakebila ya kuifungua.

"Na hizi pesa ni za teksi," Richardalisema tena na kumpa Dina bahasha nyingine iliyofanana na ile yakwanza.
Bahasha hiyo nayo, Dina aliipokea na kuiunganisha na ileya kwanza kwa kuiweka pale pale mapajani mwake, nayohakuifungua.

"Hakikisha unawasili Uwanja wa Ndege saa kumina mbili na nusu asubuhi, utanikuta nikikusubiri."
Lilikuwea nishambulio jingine ambalo Dina alikuwa hakujiandaa nalo!

Alikuwahajawahi kupanda ndege! Uelewa wa kuwa atasafiri kwa ndegeulimyumbisha akili yake. Kila kitu alikiona ni kigeni kwake, alikuwahajui teksi itakayompeleka Uwanja wa Ndege itamgharimu kiasi gani naatakapofika uwanjani hangejua angeanzia wapi. Akili yake ikawategemezi kwa wazazi wake ambao walikuwa na uzoefu wa kusafiri kwandege miaka ya nyuma kabla ya kustaafu kazi kwa baba yake aliyekuwaakisafiri kikazi kwa usafiri huo ambapo wakati mwingine alikuwaakisafiri na mama yake.

Lakini pia kuwepo kwa Richard katikasafari hiyo na uwepo wake wa kutangulia kufika Uwanja wa Ndege kwaajili ya kumsubiri yeye nako kulimpa matumaini ya kuwa atakuwa na mtumzoefu kwenye safari hiyo.
Wazo la kumuwazia Richard kuwa nisehemu ya msaada atakaokuwa akiuhitaji wakati wa kuingia na kuwepokwake kisafari ndani ya ndege, likamfanya akiri kuwa lingeuleta tenaukaribu wa mahusiano yao binafsi yaliyoasiana kwa muda mrefu.
Wazohilo likamfanya alikumbuke onyo la Mohsein!

* * * * *

Kujuakuwa Dina atasafiri kwa ndege kulimtia wazimu Mohsein! Bao lakisigino! Alikiri kufungwa bao hilo. Aliiona kete iliyotumiwa naRichard ilikuwa ni ya aina yake, kete yenye ushawishi kwa mtu kamamwanamke, au mwingine yeyote mwenye kupatiwa huduma kama hiyo! Yeyemwenyewe alishawahi kusafiri na Richard kwa safari za kikazi kamahizo na kwa mikoa tofauti, lakini hakuna hata safari moja aliyowahikusafiri kwa ndege. Safari zote Richard alizowahi kusafiri kwa ndegeza ndani au nje ya nchi, alisafiri peke yake.

Kwa mara yakwanza uelewa ukaanza kumjia kuwa, vita aliyokuwa akijaribu kupiganailianza kumuelemea mapema. Mwanzo huo uliofanywa na Richard kwakumkabidhi Dina tiketi ya ndege, zilikuwa dalili za wazizinazomthibitishia kuwa, alikuwa anashindana na mtu mwenye fedha naaliyepania kuitumia kuhakikisha anaununua ushindi kwa hali yoyoteile! Hali hiyo ilimchanganya na kujikuta akishindwakujizuia.

"Unaona!" Mohsein alibwata mbele ya Dina nakuonekana kupoteza kabisa mhimili wa akili kichwani mwake na kujikutaakisimama. "Mimi nimeshasafiri naye mara kibao, hakuna hata sikumoja aliyowahi kunisafirisha kwa ndege! Mi nakwambia hii safari sioya kikazi, ina lengo lake! We utaniambia!" akamwangalia Dina kwasura iliyojenga wasiwasi. "Kwa nyie wanawake..!" akasita, kishaakasema. "Sijui!"

"Nakuomba uondoe presha Mohsein,"Dina alisema kwa utulivu. "Unajipa presha za bure, miminimekwishakwambia atakuwa anajisumbua! Au huniamini?"

"Kukuamininakuamini," Mohsein alisema kwa sauti yenye kujitilia mashaka nakauli yake mwenyewe. Alikuwa hamwangalii Dina usoni, hasira ilikuwabado ikitawala usoni mwake na alikuwa amenuna!

"Sasa kwanini unapandisha presha?"

Mohsein akasikitika. "Inauma,Dina!" alisema kwa sauti iliyomwonyesha ni kweli alikuwa akiumizwana maumivu aliyokuwa akiyasikia. Kisha akakiangalia kiambaza chaukuta wa ofisini, akaganda kama aliyezubaa, na kubaki hivyo.

Dinaakakosa la kuzungumza, alikwisha kumwona Mohsein akiwa kwenye kiwangocha juu cha wivu.

"Nataka kesho uje nyumbani!" Mohseinalisema ghafla huku akimwangalia Dina. "Saa ngapi utakuja?"

Dinaakaonyesha mshangao usoni mwake.
"Kuna nini?"aliuliza.
"Uje tuagane!"

Dina akawa mwepesi kukijuakilichomo kichwani mwa Mohsein. "Kesho sitokuja!" alisema bila yakumwangalia usoni Mohsein.

"Basi fanya Jumapili!"

"Nayopia itakuwa ngumu kuja!"

Mohsein akajenga ndita kwenye pajilake la uso.
"Kwa nini?" aliuliza akionekana kuwa na aina yakisirani.

"Nitakuwa bize na kujiandaa kwa safari!"

Jibuhilo likamrudisha Mohsein kwenye kiti, akakaa kwa unyonge nakujiinamia. Akapiga kite huku akitingisha miguu yake. Akauinua usowake na kumwangalia Dina usoni.
"Unajua kuwa nakupenda?"alisema.
"Najua," Dina alijibu kwa sauti ya chini.

"Sidhani!"Mohsein alisema kulikana jibu la Dina. Nadhani unahisi kamanakupenda, lakini hujui ni kwa kiasi gani nakupenda Dina, labdapengine sijawahi kukutamkia neno hilo na ndio sababu ya kutoujuauzito wa mapenzi yangu kwako. Lakini, laiti ungeingia kwenye moyowangu na kuujua uzito wa kukupenda kwangu, usingenifanyiahivi!"

Dina akaonyesha aina ya mshangao huku akimwangaliaMohsein. "Kwani nimekufanyia nini?"

"Usingenikatalia!"

Dinaakafumba macho. Akataka kutamka neno, lakini akaishia kutanua papi zamdomo bila ya kuongea lolote.

Mohsein akaonekana kuwa mnyongeghafla na mwenye kukata tamaa. "Ungekuwa unanipenda, ungekujanyumbani tukaagana. Lakini huoni umuhimu huo kwa sababu badohujanikubali!"

Imeshakuwa kero! Dina aliwaza. Ghaflaakamfikiria John na safari yake ya kwenda kijijini kwao kwa ajili yakutoa taarifa za harusi yao. Akapanga jioni baada ya kutoka kazini,aende kwake kwa ajili ya kuagana naye na mengineyatakayofuatia!

****

JOHN alikuwa amekaa upande wenyedirisha kwenye basi alilopanda asubuhi hiyo ya siku ya Jumamosiakielekea kwao kijijini. Upepo uliokuwa ukiingia kupitia dirishaalilokuwepo ulimfanya alirudishe kwa kulifunga kidogo kwa lengo lakuupunguza upepo unaoingia. Akatulia kwa kujiegemeza kwenye kiti nakufumba macho kama aliyekuwa akihitaji kulala. Akaanza kuyakumbukamapenzi aliyofanya na Dina jana jioni baada ya Dina kuja nyumbanikuagana naye. Kisha akaifikiria hiyo safari yake…

Alijikutaakimlaani Richard na kumwona ndio chanzo cha safari hiyo, lakini piaakaamini safari hiyo ndio ya kukata mzizi wa fitina wa vita iliyopokati yao. Kuifikiria vita hiyo kukamfanya amuwazie mganga anayemfuatahuko kijijini ambaye kwake alikuwa kama silaha ya maangamizianayoiendea. Akajenga matumaini jinsi mganga huyoatakavyolishughulikia tatizo lake kwa ukamilifu, na aliamini matundaya safari hiyo ni kurudi na ushindi wa kuja kumdhibiti Dina kwakumuweka kwenye kiganja chake! Aliyawazia madawa yenye nguvu za ajabuatakayopewa na mganga jinsi yatakavyoweza kumdhibiti Dina na kumfanyaasiwe anavutiwa na mwanamume mwingine yeyote zaidi yakeyeye!

Alikuwa na uhakika baada ya kurudi kutoka hukoanakokwenda, juhudi za Richard za kutaka kurejeana na Dina zitakuwazimefikia ukingoni! Dina angekuwa haoni wala kusikia la mtu; wakuonekana angekuwa ni yeye na wa kusikilizwa angekuwa ni yeye!Wengine wote wangeonekana ni wajinga fulani, mmoja wao akiwa niRichard! Richard asingekuwa tena mwiba wa kuwa tishio la ndoa yake,na utajiri wake usingekuwa mali kitu kwa Dina!

Akalikumbukatukio la kusindikizwa na Dina asubuhi ya siku hiyo hadi Kituo chaMabasi yaendayo Mikoani cha Ubungo. Akaamini alikuwa akipendwa naDina kwa dhati, lakini pia akakiri Richard alikuwa kidudu mtuanayetaka kuliharibu penzi hilo!

Aliiona safari hiyo ilikuwana umuhimu kuliko hata ile ndoa aliyotaka kuiwahisha. Uamuzi wakwenda kumwona mganga kwa lengo la kujihami ulikuwa wa maana na wenyemanufaa kwake, kwa sababu lengo ni kumdhibiti na kummiliki Dina.Alitaka awe mmiliki pekee wa kummiliki, hakuhitaji mshirika kwenyeumiliki huo. Hiyo ndio ilikuwa dhamira yake ambayo endapoitafanikiwa, suala la kufunga ndoa na Dina lisingekuwa na harakatena. Angeweza kuichelewesha kidogo ili ajipange upya endapo pesaaliyokuwanayo mfukoni itaishia kwa mganga anayemwendea. Alikuwa nauhakika Dina asingeulalamikia uamuzi huo wa kuichelewesha ndoa kwasababu angekuwa hana kauli ya kuipinga kauli yake!

Matumainihayo yalimpa furaha wakati akiwa ndani ya basi, akaihisi furaha yaushindi wa kumdhibiti msichana mzuri kama Dina ikielekea kwake!

Johnalijikuta akitabasamu peke yake; tabasamu la ushindi!

* * * **

John baada ya kuwapa taarifa baadhi ya wazee wake wanaoishikijijini kuwa anatarajia kufunga ndoa, akawaomba siku inayofuatawampeleke kwa mganga aliyewatajia jina ambalo alipewa na jamaa zakewa Dar es Salaam. Aliwadanganya wazee hao kuwa anataka akafanyiwetiba ya kuimarisha mwili wake kwa kuogeshwa na kufukizwa madawa kablaya kufunga ndoa. Wazee hao wakamhadharisha kuwa, mganga anayemtakaana gharama kubwa kwa sababu haishi kwa kutegemea uganga kama wagangawengine walivyo, mganga huyu ni mfanyabiashara mwenye biashara zake.Wakamshauri wampeleke kwa mganga mwingine ambaye hayupo mbali na eneowanaloishi.

"Lakini huyu niliyemtaja si ndio yuleanayewashughulikia hadi Mawaziri waliopo Serikalini?" John aliulizakwa lengo la kutaka kuupinga ushauri aliopewa.

"Hizo nihabari tunazosikia juu juu kuwa, anapokwenda Dar es Salaam huwaanakwenda kuwafanyia Mawaziri, lakini kwa hapa kijijini hatujawahikumwona Waziri yeyote aliyewahi kuja kwa ajili yake. Labda ndiosababu inayomfanya atoze gharama kubwa kwa wateja wanaomwendea.Lakini kwa sisi wakazi wa hapa kijijini huwa hatumtumii, wotetunakwenda kwa mganga tuliyekwambia," ulikuwa moja ya ushaurialioambiwa.

John hakukubaliana na ushauri aliopewa,akamg'ang'ania mganga aliyesifiwa na watu wa Dar es Salaam.Akapelekwa!

Gharama alizoambiwa zikawa kubwa mara mbili yavile alivyofikiria baada ya kuelezea shida yake. Akahakikishiwa kaziatakayofanyiwa ni ya uhakika na yeye mwenyewe atarudi hapo kijijinikuja kutoa mkono wa pongezi kwa mganga huyo. Ikamlazimu John alitumiefungu la mahari alilokuwa amelichukua kama akiba endapo pesaalizokwenda nazo zisingetosha. Akafanyiwa shughuli aliyoihitajiambayo ilichukua siku mbili, akapewa masharti ya kufanya, menginealiyaanzia hapo hapo kijijini na mengine akatakiwa aende akayamalizieakifika Dar es Salaam.

Ilipofika usiku wa Jumapili akijiandaakutaka kulala ili asubuhi asafiri kurudi Dar es Salaam, akamfikiriaDina, akaona ni vyema amjulishe kuhusu safari yake hiyo ya kurudi Dares Salaam, lakini badala ya kupiga, John akawahiwa kupigiwa naDina!

Dina akamfahamisha John kuwa anaondoka kesho asubuhikwenda Arusha kikazi itakayomchukua wiki moja huku akiilalamikiasafari hiyo ilikuwa ni ya ghafla ambayo hakuitarajia.

Habarihizo zilimshitua John na kumchanganya baada ya kumkumbukaRichard!
"Unakwenda na Richard?" aliuliza.

"Badosijajua, lakini sidhani kama na yeye atakwenda!" Jibu hilolikashusha presha za John.

"Kwa hiyo unasafiri peke yako?"John aliuliza.

"Bado sijajua. Nilichoambiwa, kesho asubuhiniwahi kufika ofisini kuna safari ya kwenda Arusha!"


* * * **

***MOHSEIN amechomolewa na DINA kuhusu kuagana....RICHARDanamchanganya DINA kwa kumweleza kuwa atasafiri na ndege...jeatamnasa???
*** JOHN ameenda kwa mganga ....vipi atafanikiwa shidazake??
 
Habari wanajukwaa, kuna softcopy kadhaa nnazo za hadithi tofauti nkaona si vibaya ku-share ikizingatia watunzi wake wameziweka public hivyo kutohesabika kama wizi wa kazi za watu au kuharibu mapato.. Kila siku nitaweka sehemu moja, watakuwepo ambao wameshazisoma lakini pia kutakua na wengi ambao hawajahi kuzisoma,



sijui nilikuwa wapi, ndiyo naiona leo, naomba uskose kuniita Casuist!
 
Last edited by a moderator:
  • Thanks
Reactions: ram
MTUNZI: BEKA MFAUME

SEHEMU YA KUMI NA MOJA


Dina akamfahamisha John kuwa anaondoka kesho asubuhi kwenda Arusha kikazi itakayomchukua wiki moja huku akiilalamikia safari hiyo ilikuwa ni ya ghafla ambayo hakuitarajia.

Habari hizo zilimshitua John na kumchanganya baada ya kumkumbuka Richard! "Unakwenda na Richard?" aliuliza.

"Bado sijajua, lakini sidhani kama na yeye atakwenda!" Jibu hilo likashusha presha za John.

"Kwa hiyo unasafiri peke yako?" John aliuliza.

"Bado sijajua. Nilichoambiwa, kesho asubuhi niwahi kufika ofisini kuna safari ya kwenda Arusha!"

* * * * *

Dina aliwasili Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa kwenye teksi na alisindikizwa na mama yake. Walimkuta Richard akiwa amekwishafika kama alivyokuwa ameahidi.

Kitendo cha kuwepo kwa Richard mapema hapo uwanjani kwa ajili ya kumsubiri Dina kilionekana kumfurahisha mama yake Dina na kuamini Dina alikuwa kwenye mikono salama. Alimchukulia Richard kama mwanae na alimwona Dina kama yuko na kaka yake. Kwenye maamkizi kati ya mama huyo na Richard, mama yake Dina alionyesha upendo kwa kijana huyo. Dina na Richard wakamuaga, akawaombea heri kwenye safari yao. Baada ya mama huyo kuondoka, Dina na Richard wakajikuta kwenye muunganiko wa pamoja na wakawa karibu kama vile hawakuwa na tofauti zao.

"Ulishawahi kusafiri kwa ndege?" Richard alimwuliza Dina mara tu baada ya mizigo yao kukaguliwa kwenye mashine za usalama wakati walipoingia ndani ya jengo la Uwanja wa Ndege.

"Bado," Dina alijibu na kucheka kicheko kidogo cha kuondoa aibu kutokana na swali aliloulizwa. Kilikuwa kicheko cha kwanza na cha wazi kumchekea Richard baada ya kipindi kirefu cha uhasama wao!

Richard akamfahamisha Dina kinachotakiwa kufanywa hatua inayofuata wakati walipokuwa wakikaribia kujiunga na moja ya foleni inayoelekea kaunta ambako kulikuwa na vitenganishi vya majina ya mashirika tofauti ya ndege yenye kuashiria utoaji huduma wa wasafiri wa ndege zao.

"Watakuwekea namba ya kiti, kwa hiyo unatakaje? Tuchague kukaa pamoja au tukae viti tofauti?" Richard aliuliza wakiwa wanaikaribia kaunta.

Dina akafumba macho na kujenga tabasamu.
"Mi sijui chochote, mambo yote nakuachia wewe!" alijibu na kumtazama Richard.

"Basi tukae pamoja au unasemaje?"

"Yaani bado unaniuliza mimi?" Dina alisema na kumwangalia Richard kwa ncha za macho yake.

"Poa, nitamwambia karani atuweke pamoja."

Walipoingia ndani ya ndege kabla ya kukaa kwenye viti vyenye namba walizoandikiwa, Richard akamwuliza Dina, "Utapenda kukaa dirishani?"
"Mi naogopa kuangalia nje!" Dina alisema kwa sauti ndogo ambayo hakutaka asikiwe na abiria waliosimama jirani ambao walikuwa wakihangaikia kuiingiza mizigo yao kwenye majaluba ya kuhifadhi mizigo ya ndani ya ndege.

Richard akakaa sehemu ya dirishani, Dina akakaa kando yake.

Dina alikuwa mwepesi kuiangalia hali iliyomo kwenye ndege na kuwaangalia baadhi ya abiria waliokuwa wakiendelea kuhangaika kupandisha mizigo yao kwenye majaluba na wakati huo huo wahudumu wa ndani ya ndege wakiwasaidia kuwaonyesha abiria mahali vilipo viti vyao. Akakumbuka kujifunga mkanda. Akadhani angeufunga mkanda huo kama vile ajifungavyo kwenye gari. Akaukamata mkanda uliopo kwenye kiti chake na kutaka kujifunga, akagundua uko tofauti na ule wa kwenye gari, hali hiyo ikamfanya aanze kubabaika kujifunga.

"Niangalie mimi ninavyojifunga mkanda!" Richard alisema ghafla baada ya kumwona Dina akijaribu bila mafanikio kuufunga mkanda huo.
Dina akamwangalia Richard alivyokuwa akijifunga, kisha na yeye akajaribu kuiga. Akapatia!

Richard akatabasamu na kumwangalia Dina. Dina akalirudisha tabasamu na kumwangalia Richard kwa ncha za macho yake.

"Itabidi uzime simu yako, hawaruhusu matumizi ya simu kwenye ndege!" Richard alisema huku tabasamu likiwa bado lipo mdomoni mwake.
Dina akaizima simu yake!

* * * * *

Upweke uliosababishwa na kutokuwepo kwa Dina ofisini ulianza kumtesa Mohsein baada ya kuwasili kazini. Tokea Dina alivyoanza kazi, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kutokuwepo pamoja. Kutokuwepo kwake kulikuwa kama kipimo kilichompa jawabu kuwa Dina alikuwa ni sehemu muhimu ya maisha yake ya kila siku hapo ofisini. Aligundua Dina alikuwa akimwongezea furaha ya kuipenda kazi yake kila alipokuwa naye.

Kutokuwepo kwa Dina kulimfanya ashindwe kuifanya kazi yake ipasavyo asubuhi hiyo na kujikuta mnyonge wakati wote. Ule uelewa wa kujua Dina hatokuja kazini kutokana na kusafiri kulimpa wakati mgumu na kuiona asubuhi iwe chungu kwake. Penzi lilikuwa likimuadhibu na wivu ulikuwa ukimwandama.

Kadri muda ulivyosogea kwenda mbele hali ya kujiona ni mgonjwa iliongezeka, kila kitu humo ofisini kikawa kinamkumbusha uwepo wa Dina. Tafakuri za mazoea ya kumwona Dina akifanya hiki au kile humo ofisini zilimwelemea. Alikikumbuka kicheko cha Dina chenye maringo, na uangaliaji wake wa kupenda kumtazama mtu kwa kutumia ncha za macho yake. Hali hiyo ilimfanya awe na hisia zilizomwumiza na kuhofu kama vile, Dina asingerudi tena! Akili yake haikuwepo kabisa ofisini, ilikuwa imetekwa na fikra za kumuwaza Dina na kumfanya atumie muda mwingi wa kuduwaa kuliko kufanya kazi. Dina alikuwa amemkaa akilini mwake kama muhuri wa moto ukaavyo kwenye nyaraka!

Siku hiyo pia, ilitumika kama mzani wa kugundua jinsi alivyotokea kumpenda msichana huyo kwa kasi ya ajabu. Alijishangaa kujiona akimlilia wivu hali akijua msichana huyo yuko njiani kuolewa! Lakini, alijishangaa zaidi kujiona akimwona Richard kuwa ndiye adui yake namba moja badala ya John ambaye ndiye mume mtarajiwa wa Dina!

Mohsein alijaribu mara kadhaa kujipa ujasiri wa kuachana na fikra za kumuwaza Dina na kumwonea wivu Richard, hasa akizingatia hata yeye ana rafiki yake wa kike wa muda mrefu wanaoheshimiana na kupendana na pengine wakaja kufunga ndoa! Alikiri huyo ndiye aliyestahili kupewa upendo wote badala ya kubabaishwa na Dina aliyejipenyeza ghafla kati kati ya penzi lao. Ushawishi wa kujipa ujasiri huo wa kumwondoa Dina mawazoni mwake aliuona ukikubalika akilini, lakini ukikataa moyoni.

Akiwa mwenye kujihurumia, Mohsein alijionya kuwa, upendaji aliojiachia nao wa kumpenda Dina kwa nguvu kiasi hicho unaweza ukaja kumzindua rafiki yake wa kike kugundua kuwa anamsaliti. Mawazo yake yakarudi nyuma na kukiri kuwa, siku ambayo moyo wake ulipenyezwa sumu ya kumpenda Dina na kumuingiza kwenye ufala wa kupenda kibwege uliomkuta hapo alipo, ni ile siku ambayo alifanya mapenzi na Dina wakiwa stoo. Kitendo hicho ndicho kiliingiza sumu kwenye mfumo mzima wa mzunguko wake wa damu na kuivuruga sehemu kubwa ya ubongo wake. Lakini pia, baada ya kitendo hicho ukawepo mwendelezo wa vitendo vya kuonyeshana kuwa wanapendana kila walipokuwa pamoja ofisini.

Siku ambayo Richard alirudi kutoka Morogoro ndio ikawa siku ya kuihitimisha fungate yao na furaha ya penzi lao kusambaratishwa baada ya Richard kumpa Dina taarifa ya safari!

Siku hizo ndizo ambazo zilikuwa na sumu iliyomwangamiza kiakili, sasa aliziona akizitumikia kwa kifungo cha mateso yanayomtesa huku akitawaliwa na donge la kumwonea wivu Richard kwa kuondoka na Dina. Akakiri kuwa, amezama kichwa kichwa kwenye penzi la Dina.

Nimekwisha! alijisikitikia peke yake!

* * * * *

Waliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na Dina alishangaa pale alipokuwa kwenye gari lililowachukua kutoka uwanjani kugundua kuwa, uwanja huo wa Kimataifa ulikuwa mbugani na ukiwa mbali kabisa na jiji la Arusha ikiwa ni tofauti na Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ambao haukuwa mbali kutoka katikati ya jiji.

Waliwasili Arusha, gari walilopanda likawapeleka moja kwa moja kwenye hoteli kubwa ya kimataifa na ya kifahari ya Masai Shield iliyokuwepo kando kidogo kwa kilomita chache kutoka katikati ya jiji la Arusha. Wakiwa mapokezi, Richard alijiandikisha, hali kadhalika kwa Dina naye ikawa ni hivyo hivyo, na walipokuwa wakijaza maelezo yao kwenye kadi ya hoteli ya kujisajili upangaji, kuna maeneo ambayo Richard alimwelekeza Dina namna ya kujaza kwenye kadi yake.

"Tungependa kwenda kustafutahi kabla hatujakwenda vyumbani kwetu," Richard aliyeonekana sio mara yake ya kwanza kuwepo kwenye hoteli hiyo alimwambia mtumishi wa mapokezi.

"Mnakaribishwa. Restaurant yetu bado inahudumia kifungua kinywa," mtu wa mapokezi alisema huku akiiangalia saa yake ya mkononi.

Waliruhusiwa kwenda kwenye mgahawa wa hoteli wakiwa na mizigo yao. Huko Richard alimsaidia Dina kuagiza kifungua kinywa kwa kumchagulia baadhi ya vitafunio kutokana na uzoefu wake. Wakati walipokuwa wakistafutahi, Richard aligundua Dina alikuwa na tatizo linalowakabili wasichana wengi warembo wa kutokuwa na uzoefu wa namna ya kukamata uma. Dina alikuwa akiikumbatia badala ya kuikamata wakati akikita kuchoma kitu anachotaka kula. Richard hakusema lolote! Baada ya kumaliza kustafutahi, walikwenda kwenye vyumba vyao na Richard akamwonyesha Dina chumba chake kilipo. Kilikuwa jirani na chake.

"Kesho ndio tutakwenda kuanza kazi, vipi baadaye utapenda kuuzunguka mji wa Arusha na kuujua?" Richard aliyekuwa amemsindikiza Dina hadi mlangoni mwa chumba alichopangiwa kukaa alimwuliza Dina kabla hajaingia chumbani humo.

"Mi nakusikiliza wewe!" Dina alijibu na kumwangalia Richard kwa ncha za macho yake.

"Basi pumzika, baada ya masaa mawili nitakuja kukugongea mlango ili ukatembee kuuona mji."

"Sawa," Dina alijibu kwa upole.

Richard akamsaidia Dina kumfungulia mlango wa chumbani kwake kwa kutumia kadi na kumwelekeza matumizi ya kadi hiyo ambayo hutumika badala ya funguo ya kawaida.

Akiwa chumbani peke yake na kushangazwa na uzuri wa chumba alichomo huku akijiona kama yuko ndotoni akiwa haamini yale yanayomtokea, Dina alikuwa tayari amechanganyikiwa! Hadhi ya kusafiri kwa ndege kikazi, kulala kwenye hoteli ya kifahari kama hiyo, kilikuwa ni kitu ambacho hakikuwahi kumtokea kwenye fikra zake. Alikiri huduma anayopewa haikuwa hadhi yake kikazi, ilikuwa ni hadhi ya mtu mwenye elimu inayoanzia na Shahada! Hakutaka kujidanganya kuwa alikuwa na bahati ya mtende kupewa hadhi hiyo kutokana na kazi aliyokuwa nayo. Hakuwa na elimu ya kazi wala ujuzi wa kazi hiyo! Alitambua yote hayo yalikuwa yakifanywa na Richard kwa sababu moja ya wazi; Richard alikuwa akimpenda na alikuwa akiuonyesha upendo wake kwake!

Aliwazia jinsi alivyokuwa akimkataa Richard kwa kipindi kirefu, kipindi ambacho Richard alikuwa akimbembeleza kwa kila hali ili warudiane. Akafikiria jinsi alivyomkatisha tamaa baada ya kumchagua John kuwa chaguo lake na kumteua kuwa mchumba wake! Alikuwa na uhakika maamuzi hayo yalimwumiza Richard, lakini yeye hakujali wakati huo; kwa sababu aliamini ni John pekee ndiye aliye moyoni mwake na ndiye mwenye haki ya kuutumia mwili wake. Lakini bila ya kutarajia, alijikuta akimsaliti John kwa kutembea na Mohsein, tena kwa hiari yake! Ulikuwa ni kama uamuzi wa ajabu kukubali kufanya kitendo hicho cha kumsaliti John, lakini aliukiri udhaifu uliomkuta wa kuvutwa na mvuto wa Mohsein, udhaifu ambao unaweza kumkuta yeyote! Sasa amejikuta akiwa na mabwana wawili, na kuwa tayari kila mmoja ampende kwa sababu yake. John kwa ajili ya ku-make love, na Mohsein kwa ajili ya ku-make sex!

Lakini sasa hapo alipo kwenye chumba cha hoteli ya kifahari, Dina alikiri yupo kwenye mtihani mwingine aliokuwa akipewa na Richard. Mtihani aliouona ukimchanganya kichwa, ulimchanganya kwa sababu ni mtihani ulioingia takrima ya mapenzi. Alikuwa na uhakika matendo aliyofanyiwa hadi sasa na Richard kama angeyaeleza kwa rafiki yake yeyote wa kike, rafiki yake huyo asingesita kumshauri kumkubali Richard! Na angemshawishi kuwa, takrima anayofanyiwa na Richard ni yenye upendo wa dhati kwa sababu Richard alishamuahidi kutaka kumuoa!

Aliyafikiria matendo yote aliyotendewa na Richard na kuamini hata ule mshahara aliopangiwa ulitokana na juhudi za Richard kumshawishi baba yake, na kwa mara ya kwanza alijikuta akiamini, hata kazi aliyoajiriwa ilitokana na Richard! Akaifikiria safari iliyofanyika asubuhi hiyo kutoka Dar es Salaam hadi hapo Arusha, matendo yaliyotokea kati yake na Richard katika safari nzima hakutaka kujidanganya nayo, alikiri yalikuwa ni matendo yaliyowezesha kuwaweka tena karibu na kujikuta wakiurudisha uhusiano wao kwa njia moja au nyingine. Alitakiwa airudishe fadhila hiyo ili kuonyesha uungwana wake!
Mtihani ulikuwa kwake!


****

SIMU yake ndio iliyomshitua, alijishangaa kujikuta kumbe alikuwa amepitiwa na usingizi akiwa amelala na suruali yake ya jeans iliyomshika vema mapajani. Awali kabla ya kupitiwa na usingizi alizungumza kwa simu na wazazi wake wote wawili, akawajulisha kuwa alikwishafika salama mjini Arusha. Pamoja na kuwakumbuka John na Mohsein lakini hakuwapigia simu kuwajulisha kuhusu kuwasili kwake jijini Arusha. Akiwa ameshituliwa na simu ambayo ilikuwa ikiendelea kuita akaiweka dhana ya kuwa huenda simu hiyo ilikuwa inapigwa na mmoja wapo kati ya John au Mohsein. Akaichomoa simu yake iliyojibana kutoka kwenye mfuko wa mbele wa jeans alikokuwa ameiweka. Akashangaa kuziona namba za mpigaji badala ya jina la mmoja wao kati ya John au Mohsein. Akashindwa kuijua simu hiyo ilikuwa ikipigwa na nani.

"Haloh," alisema kivivu.

"Mimi Richard, nifungulie!" sauti kutoka kwenye simu ilisema. Akashituka baada ya kutambua ni Richard ndiye aliyekuwa akiipiga
simu hiyo, akakumbuka namba ya Richard alikwishaifuta muda mrefu kwenye simu yake, lakini pia akakumbuka siku chache zilizopita Richard aliiomba namba yake wakiwa ofisini na alimpa. Akakurupuka kutoka kitandani, akajifuta uso haraka haraka na kwenda kuufungua mlango. Akamkuta Richard amesimama mlangoni.

"Karibu," Dina alisema.

"Siingii," Richard alisema kwa upole.
"Nakusubiri Mapokezi, gari limeshafika."

Dina akaikumbuka safari ya kwenda kuzunguka kuliangalia jiji la Arusha.

"Nakuja!" Dina alisema.

Walitumia muda mwingi kuzunguka mjini, Richard alimwonyesha Dina baadhi ya maeneo yenye umaarufu hapo Arusha, waliingia kwenye maduka tofauti na Richard akaitumia nafasi hiyo kumnunulia Dina zawadi mbalimbali, kisha alimuagiza dereva wa gari walilokuwemo ambalo ni mali ya kampuni yao kuwapitisha kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na kampuni ya baba yake. Walipofika hawakuteremka, Dina akaonyeshwa kituo hicho cha mafuta kuwa ni hapo ndipo ambapo kesho watakuja kufanya kazi. Dina akakiangalia kituo hicho ambacho kilikuwa kikubwa chenye Super Market pamoja na mgahawa wa Kimataifa.

Waliporudi hotelini, walikuwa wamechoka na njaa zilikuwa zikiwauma.

Richard alimsaidia Dina kubeba baadhi ya mizigo aliyomnunulia hadi chumbani kwa Dina.

"Richard," Dina alisema wakiwa chumbani kwake baada ya kuiweka mizigo waliyoiingiza. "Mungu akubariki!"

"Amen," Richard alijibu na kuunganisha alilokuwa anataka kulisema. "Unaonaje ukiagiza chakula kiletwe humu chumbani? Kuna kitu nataka kukuonyesha."

Dina akamwangalia Richard kwa ncha za macho yake.
"Kuna kitu unataka kunionyesha?" aliuliza huku akionyesha kushangaa.

"Ndiyo. Nitakuonyesha wakati chakula kitakapoletwa," Richard alisema na kuifuata kadi yenye orodha ya vyakula kwa ajili ya huduma maalumu ya chumbani huku akimuacha Dina akiwa bado yupo kwenye mshangao. Alirudi alipomuacha Dina, akamkabidhi kadi hiyo.
"Chagua, chakula gani utapenda uletewe?" alisema.

"Samaki," Dina alisema alipokuwa akiitazama kadi hiyo.
"Naona kuna aina tofauti ya mapishi, unaweza ukanichagulia?"

"Nakuchagulia Poached fish, naamini utafurahia."
"Wewe huagizi?"
"Kama utaniruhusu nile chumbani kwako, nitaagiza."

Dina akamwangalia Richard. "Agiza!" alisema kwa sauti ya chini yenye maringo.

Richard akaagiza kwa kutumia simu ya humo humo chumbani, naye pia aliagizia samaki kama aliomchagulia Dina. "Itachukua sio chini ya dakika ishirini hadi kutuletea, wacha niende chumbani kwangu kuna kazi kidogo nakwenda kuifanya, nitarudi kabla ya chakula hakijaletwa," Richard alimwambia Dina.
Wakaagana.

Ni kweli aliwahi kurudi kabla ya chakula kuletwa! Dakika tano baada ya kufika, chakula nacho kikaletwa. Richard akasaini kwenye stakabadhi ya malipo, kisha alitumbukiza mkono mfukoni na kutoa noti aliyompa mhudumu aliyeleta chakula ikiwa sehemu ya bakshishi. Mhudumu akashukuru na kutoka.

"Nionyeshe ulichotaka kunionyesha!" Dina alisema kabla ya kuanza kula.

"Kula kwanza…" Richard alisema huku akitabasamu.

Dina akagoma kula. "Sili mpaka unionyeshe hicho kitu!" alisema. Ikawa kama sehemu ya utani kwao ambao haukuwa rasmi. "Nitakuonyesha," Richard alisema huku akiinuka kivivu kwa kujishika magoti wakati akisimama, akaenda kumsimamia Dina mgongoni.
"Nataka kukufundisha namna ya kukamata uma," alisema huku akimuinamia Dina juu ya mabega yake.

"Khaa!" Dina alishituka.
"Yaani mimi sijui kushika uma?"
"Hujui kuushika wakati unapokula!"

"Haya makubwa!"

Richard akauchukua uma uliovingirishwa na kisu kwenye karatasi ya kujifuta mdomo iliyokuwa pembeni mwa sahani ya chakula, akaukamata kama alivyokuwa ameukamata Dina asubuhi walipokuwa wakistafutahi.
"Wewe unashika uma hivi," akamwonyesha Dina.
"Uma haukamatwi hivi, unakamatwa hivi. Hebu jaribu," akaurudisha kwa Dina.
Dina akasikitika kisha akafanya alivyoambiwa.

"Na kisu kikamate kama ulivyoukamata uma. Ukite uma juu ya samaki, kisha kata kwa kisu."

Dina akafanya vile alivyoambiwa.

"Sasa endelea kula. Huo ndio ukamataji wa uma na kisu. Tatizo hili sio lako peke yako, nimeshuhudia vijana wengi, pamoja na kuupenda Uzungu, lakini wengi wanashindwa namna ya kukamata uma unavyotakiwa wakati wa kula."

Walipokuwa wakiendelea kula, ghafla Richard alichukua kipande cha samaki alichokikata na kukiinua kwa uma.

"Nataka kukulisha," Richard alisema huku akimwangalia Dina usoni. Dina akawa kama aliyeshangaa, akamwangalia Richard usoni bila ya kutoa jibu la haraka. Wakaangaliana kwa makini kama waliokuwa wakisomana akili zao. Hatimaye Dina akaufungua mdomo bila ya kutamka
lolote, akamruhusu Richard amlishe!

* * * * *





***DINA mtegoni AMEFUNDISHWA KUTUMIA UMA na sasa anataka kulishwa…..je atanasa????
**Nini hatma ya wivu wa JOHN SAILAS na MOHSEIN
 
Ni kweli Mphamvu, ndiye yeye huyu huyu! Namkubali sana huyu jamaa!

Wa ukweli, pamoja na kuwa mwandishi wa riwaya pendwa lakini anaiandika katika namna ambayo inavutia hata wapenzi wa riwaya dhati.
 
Last edited by a moderator:
MTUNZI: BEKA MFAUME


SEHEMU YA KUMI NA MBILI


Walpokuwa wakiendelea kula, ghafla Richard alichukua kipande cha samaki alichokikata na kukiinua kwa uma.

"Nataka kukulisha," Richard alisema huku akimwangalia Dina usoni. Dina akawa kama aliyeshangaa, akamwangalia Richard usoni bila ya kutoa jibu la haraka. Wakaangaliana kwa makini kama waliokuwa wakisomana akili zao. Hatimaye Dina akaufungua mdomo bila ya kutamka
lolote, akamruhusu Richard amlishe!

* * * * *
Jioni ya saa kumi na moja, Dina akiwa ameamka sekunde chache zilizopita na kabla hajakiweka vyema kichwa chake kutafakari, akausikia mlango wa chumbani kwake ukigongwa. Moja kwa moja akahisi ni Richard ndiye angekuwa anaugonga mlango huo. Akakumbuka wakati alipoachana naye mara tu baada ya kumaliza kula chakula cha mchana walichokula pamoja, Richard alimuaga na kumtaka apumzike, akisema wataonana baadaye. Ndipo naye alipoamua kulala na kupata usingizi mzuri hadi alipoamka na kusikia mlango ukigongwa.

Alipoufungua, akashangaa kumwona mhudumu wa vyakula akiwa amesimama na tray iliyobeba birika mbili, zote zilikuwa ndogo zenye ukubwa uliotofautiana, na kijaluba cha sukari, pembeni kukiwa na sahani iliyofunikwa na kitambaa.

"Sijaagiza!" Dina alisema, usoni akiwa na mshangao.
"Mzee Richard ameniagiza nikuletee," mhudumu alisema.

Mzee Richard! Dina alishangaa na kutaka kujiuliza mtu huyo ni nani. Ghafla akapata jibu kuwa ni heshima aliyokuwa akipewa Richard. Akatabasamu na moyoni kukasuuzika baada ya kukiri, Richard alikuwa akimjali.
"Karibu," alimwambia mhudumu na kumpa nafasi ya kuingia.

Mhudumu aliingia chumbani na kuangaliwa na Dina aliyekuwa amesimama mlangoni kwa ajili ya kumsubiri atoke.
"Nakwenda," mhudumu aliaga baada ya kuviweka kwenye meza vitu alivyoingia nao.
"Yeye yuko wapi?" Dina aliuliza wakati mhudumu akiwa mlangoni anatoka.
"Yupo duka la kahawa akinywa chai," mhudumu alijibu.
"Ahsante na karibu tena," Dina alisema kisha akaufunga mlango nyuma ya mgongo wa mhudumu aliyetoka.
Dina aliiendea tray iliyoletwa na mhudumu na kuvipekua vitu vilivyoletwa. Birika kubwa ilikuwa na chai, birika ndogo ilikuwa na maziwa na alipokifunua kitambaa kilichofunika sahani, akaiona keki iliyomtamanisha, akatengeneza tabasamu dogo. Huduma ya V.I.P! aliwaza.

Akiwa anakaribia kumaliza kunywa chai aliyoletewa, simu ya chumbani kwake iliita. Alishituka na kuiangalia. Ilikuwa ni mara ya kwanza kuisikia ikiita tokea alivyoingia asubuhi. Hakuwa na uhakika kama alikuwa akipigiwa yeye au simu hiyo iliingia kwa makosa. Aliamini kama angekuwa ni Richard ndiye anayempigia basi angempigia kwa simu yake ya mkononi kama alivyofanya asubuhi.

Akaifuata simu hiyo na kusimama kando yake, badala ya kuiinua, akasita. Akaiangalia kama vile kilikuwa kitu cha ajabu kilichojenga uhai na kutoa mlio. Kisha kama vile anategua bomu, aliinua simu hiyo kwa uangalifu na polepole, akaiweka sikioni.
"Haloh," alisema kivivu baada ya kuipokea huku akiamini sio yeye anayepigiwa.

"Umekwisha kunywa chai?" sauti ya kiume kutoka upande wa pili wa simu ilisema.

Dina akatabasamu kwenye simu baada ya kuigundua sauti ya Richard.
"Nimeshakunywa," alisema.
"Nasikia uko duka la kahawa ukinywa chai?"

"Ni kweli. Utakuja?"
"Labda nikishaoga."

"Basi nakuomba ufanye kitu kimoja," Richard alisema kwa utulivu. "Ukishaoga uvae lile gauni jeusi katika zile nguo tulizozinunua leo."

"Umelipenda?"

"Ni kati ya nguo zilizokupendeza mno wakati ulipokuwa ukizijaribu dukani, pia ni nguo ya jioni inayostahili kuingia nayo restaurant kwa chakula cha usiku."

"Sawa mkubwa," Dina alisema kiutani.
"Utanifuata nikishamaliza kuoga?"

"Utakapokuwa tayari njoo duka la kahawa."

Akiwa bado hajamaliza kuzungumza na Richard kwenye simu, simu yake ya mkononi ikaita. Akaiangalia pale kitandani ilipokuwepo, lakini hakwenda kuipokea, alisubiri hadi alipomaliza kuzungumza na Richard ndipo alipoifuata. Ilikuwa imekwishaita zaidi ya mara mbili, na alipokuwa anaichukua ikaita tena. Alikuwa John!

"Mbona umechelewa kuipokea simu?" John alianza na lawama. "Bado nipo kazini!" Dina alidanganya.
"Vipi mzima?"

"Mimi mzima, nilitaka kukufahamisha kuwa nimekwisharudi Dar, vipi huko Arusha?"

"Ni kipindi cha baridi na ni kali."
"Umefikia hoteli ipi?"

"Masai Shield."

"Masai Shield?" John aliuliza kwa sauti iliyojaa mshangao kuonyesha alikuwa haamini Dina kufikia kwenye hoteli kubwa na ya kifahari kama hiyo.
"Aisey, hiyo hoteli ni ya kifahari sana! Richard uko naye?"

Wivu! Dina aliwaza.
"Tumemuacha huko huko Dar. Nasikia anaweza akaja baada ya siku mbili au tatu," Dina alidanganya tena.
"John, nitakupigia baadaye nikipata mwanya, sasa hivi bado tuko bize sana."
"Poa, Dina. Baadaye."

"Baadaye John."

"I miss you!"
"I miss you too!"
Zikawa ni simu zilizofuatana! Mara baada ya kumaliza kuongea na John, simu yake ikaita tena. Safari hii alikuwa Mohsein!

"Dina, vipi mambo?" Mohsein alisema kwenye simu.
"Poa. Vipi, za huko Dar?"

"Huku poa. Wangu hata kunipigia simu kunifahamisha kama umefika salama?"

"Tumefika na kuingia kazini moja kwa moja na jamaa bado nipo naye karibu."

"Mmefikia hoteli gani?"

Dina akahisi na huyo naye atapigwa na mshangao kama aliopigwa nao John. "Masai Shield!" alisema.

"Eti wapi Dina?" Mohsein alipayuka kwenye simu kwa sauti iliyojaa mshangao.

"Masai Shield!"


"Unaona Dina? Huyo jamaa yupo kwenye kukupumbaza…" "Nitakupigia baadaye!" Dina alisema kwa mkato na kukata simu. Dina akakunja uso kwa hasira. Alitamani aizime simu yake ili asiwe na mawasiliano na watu hao wawili ambao wote alijua hoja zao zilianza kujikita kumjadili Richard, na yeye kwa wakati huo hakuwa tayari kulijadili hilo. Alihitaji amani, na kwa mara ya kwanza akakiri kuwa, Richard ndiye aliyekuwa akimpa amani aliyokuwa akiihitaji tokea alivyowasili hapo Arusha. Akatamani awe karibu naye kwa wakati huo, kuliko kuwa na mazungumzo na watu hao wawili yanayomjadili Richard!

Dina alikwenda kuoga huku akihisi watu hao wawili wakiwa kama mzigo kwake. Alipomaliza kuoga, aliiva nguo aliyoambiwa na Richard aivae.

Alipendezwa na nguo hiyo! Akaenda duka la kahawa kumfuata Richard. Alipokuwa akitoka kwenye lifti kuingia duka la kahawa, kila aliyekuwepo eneo hilo kuanzia wafanyakazi na wateja ambao wengi wao walikuwa ni Wazungu walimwangalia. Alionekana kama mlimbwende aliyekuwa akitembea juu ya jukwaa la mashindano ya urembo. Akamwona Richard, akatengeneza tabasamu dogo lililopokewa na Richard aliyekuwa amekaa peke yake mezani.

"Umependeza!" Richard alisema wakati akiwa amesimama na kumvutia kiti Dina.

"Ahsante," Dina alisema wakati akikaa. "Utaongeza chai?"

"Hapana." Mhudumu akafika.

"Hapana, sihitaji chochote," Dina aliyekuwa akitabasamu alimwambia mhudumu kabla ya kuulizwa.

"Ningependa tuzunguke zunguke nje ya hoteli uiangalia mandhari iliyoizunguka hoteli, lakini baridi iliopo huko nje ni balaa!" Richard alisema baada ya mhudumu kuondoka.

"Mchana kulikuwa na baridi vile, sasa hivi kutakuwaje huko nje! Lakini hii hoteli ni nzuri nje hadi ndani Richard, utadhani upo kwenye pepo! Na yale mandhari ya nje yanatamanisha uzunguke zunguke kama ulivyosema."

"Mwezi wa Novemba tutarudi tena, hali ya hewa itakuwa imebadilika na tutaweza kutembea tembea kwa miguu. Au unasemaje?"

Kikazi au kibinafsi? Dina alijiuliza. Mazingira halisi ya siku moja hiyo yalikwisha kuonyesha kuwa, wameurudisha uhusiano wao, kwa hiyo ujio mwingine wa kuja tena Arusha hakuujua ungekuwaje. "Sawa," alijibu kwa sauti ya chini huku akiiangalia meza. Alikiri kwa hatua ambayo wameifikisha kwa siku hiyo, kamwe asingeweza kukataa chochote atakachoambiwa na Richard!

"Unaonaje tukienda baa kupata kinywaji cha kuvuta muda ili baadaye tukale chakula cha usiku?" Richard alisema.

"Sawa," Dina alikubali.

Wakaenda! Wakati wakisubiri mhudumu aje awaulize na kuwahudumia vinywaji watakavyoagiza, Richard akakumbuka kinywaji alichomwona nacho John wakati akimpelekea Dina alipowakuta kwenye hoteli ya BBH eneo la bwawa la kuogelea. Richard akajiuliza kama Dina angekiagizia tena kinywaji kile alichopewa na John?

Crème de Menthe! alikikumbuka kinywaji hicho.

* * * * *

Usiku walikula chakula ghali na Richard aliagiza kinywaji cha Champagne. Mhudumu alipowahudumia kwa mara ya kwanza kuwatilia kinywaji hicho kwenye glasi zao na kisha kuondoka, Richard akawa wa kwanza kuinua glasi yake juu na kumwambia Dina, "Tunywe kwa furaha ya kuurudisha uhusiano wetu. Cheers!"

Kauli hiyo ya Richard ikawa imemwingiza Dina ili akiri kwa kauli yake mwenyewe kuwa, hatua ya kukubali kuigonganisha glasi yake na ya Richard na kutamka neno ‘cheers' atakuwa tayari amekubali kuurudisha uhusiano huo!

Kwanza Dina alionekana kusita na kujikuta akimfikiria John, kisha akamfikiria Mohsein! Tuhuma ya kuongeza mwanamume wa tatu ilimtuhumu, akauona ni uhuni usiokubalika kwake. Akakiri moyoni lazima amteme mmoja wao. Mohsein akawa kafara, akalengwa kuachwa yeye!

"Cheers!" alisema na kuigonganisha glasi yake na ya Richard, akanywa funda moja kabla ya kuirudisha glasi mezani.

Richard naye akafanya hivyo hivyo.

Baada ya kumaliza kula, hawakuondoka mapema mezani. Waliendelea kuagiza Champagne na kuzungumza, walionekana kutulia na mazungumzo yao yalitawaliwa na sauti za chini huku wakiwa wanaangaliana ana kwa ana. Mwanga hafifu wa mshumaa uliokuwa ukiwaka kwenye meza yao, ulionyesha sura zao zikiwa kwenye masikilizano na kuzingirwa na mandhari ya mahaba kwa kila mmoja wao.

Usiku huo, Dina hakulala chumbani kwake, alikwenda kulala chumbani kwa Richard!

* * * * *

Dina alihamia rasmi chumbani kwa Richard ilipofika siku ya pili baada ya kukubaliana chumba alichokuwa akilala kirudishwe. Wakaanza kuishi kama bibi na bwana. Walilala, waliamka na kwenda kazini pamoja huku uchipuaji wa penzi jipya ukishamiri kwa kasi. Kila jioni baada ya kumaliza kazi, walichagua pa kwenda kama hawakuhitaji kurudi mapema hotelini. Ikawa kama vile huko Arusha walikokwenda, walikwenda zaidi kama fungate kuliko kikazi.

***

MOHSEIN alibaki na kinyongo tokea siku aliyokatiwa simu na Dina! Kitendo hicho alikichukulia ni dharau aliyofanyiwa! Hakuamini kama kulikuwa na dharura iliyomfanya Dina aikate simu hiyo ghafla, tena bila hata kuomba samahani au kutoa neno lolote la kumtafadhalisha kabla ya kuikata simu hiyo. Moja kwa moja Mohsein akakichukulia kitendo hicho alichofanyiwa na Dina kilikuwa ni kiburi kilichoonyesha kumthamini Richard na kumdharau yeye!

Tukio hilo likawa limemdhihirishia kuwa, tayari Dina ameanza kuwa karibu na Richard! Ni mazingira ambayo alikuwa ameyatabiri awali kuwa, uendaji wa pamoja wa safari hiyo, lengo lake lilikuwa ni hilo, lakini Mohsein hakutarajia kama lingefanyika kwa haraka hivyo. Hofu iliyoingia wivu ikaanza kumtafuna, wasiwasi wa kuwa huenda Richard na Dina wamekwishafanya mapenzi ikampandisha jazba. Dhana hiyo ikamgubika kwenye wingu kubwa la wivu. Donge likamkaa kooni, akatambua kuwa, Dina ndio basi tena kwake! Kitendo cha kuhisi Richard amekwishaingiliana kimwili na Dina huko Arusha waliko kilikoleza moto wa wivu uliokuwa ukiuteketeza moyo wake. Akatamani kupiga kelele, akajizuia. Akaanza kumlaumu Dina moyoni kwa kujirahisisha kwake kwa Richard!

Kwa mara ya kwanza aliilaumu nafsi yake kwa kukubali kujiingiza kwenye penzi la kumpenda Dina, alikiri alikuwa akimpenda na alikuwa akimhitaji awe karibu naye wakati wote. Lakini pia, akamwona Dina kuwa ndiye aliyemwingiza kwenye penzi na baada ya muda mfupi ameamua kumwumiza moyo! Aliiona ilikuwa ni aina ya dhihaka aliyofanyiwa. Mohsein akaapa na yeye lazima amwumize Dina kama vile alivyoumizwa yeye!

Akaanza kufikiria njia za kulipiza kisasi za kumkomoa Dina. Akamkumbuka John!

Alikuwa hajawahi kumwona, lakini alikuwa na habari zake zote! Ni Dina ndiye aliyemwambia wakati alivyomjulisha kuwa ana mchumba! Dina alizungumzia mengi yanayomhusu John na kumjulisha hadi anakofanyia kazi. Akapanga amfuate John kazini kwake! Akaenda! Akamwulizia kwa mlinzi, mlinzi akamwambia yupo, Mohsein akaomba aitiwe.

John alipotoka akashangaa kumwona mtu asiyemjua!

"Naitwa Mohsein, najua hunijui, lakini mimi nakujua," Mohsein alisema huku akiangaliwa na John kwa makini. "Nadhani wewe ni mume mtarajiwa wa Dina? Au sivyo?"

Kwanza John alisita kujibu, akaonyesha wasiwasi wa kutojua kule anakopelekwa kimazungumzo. "Ni nani aliyekueleza kama mimi ni mume mtarajiwa wa Dina?" aliuliza.

"Dina!" Mohsein alijibu kiuhakika.

John akaganda na kuonekana kushitushwa na jibu alilopewa. "Ilikuwaje akakwambia wewe?"

"Tunafanya kazi pamoja. Alishanipa kadi ya mchango ya Send off ili nimchangie. Katika maongezi yetu ya kawaida alinitajia unapofanya kazi na ndio sababu nipo hapa kwa ajili yako. Swali langu liko palepale, wewe ndiye mume wake mtarajiwa?"

"Ndiyo ni mimi," John alijibu akionekana bado yuko kwenye wasiwasi.

"Sasa sikiliza, mimi ni mwanamume mwenzio!" Mohsein alizungumza kwa sauti ya kishari iliyokaza. "Hawa wanawake unatakiwa uwajue kabla ya kuamua kuwaoa. Uzijue tabia zao na ujue uadilifu wao. Je, una kifua cha kuzijua habari zake?"

John alianza kuonekana kuchanganyikiwa baada ya kuambiwa hayo. "Nipo tayari," alisema akijaribu kuifanya sauti yake imjengee taswira kuwa ni kweli alikuwa tayari. Hata hivyo uso wake ulijenga hofu ya kile alichokuwa akisubiri kuambiwa.

"Tatizo sio kuwa tayari," Mohsein alisema kama vile Mwalimu anayemwelekeza kitu mwanafunzi wake. "Kifua chako kipo tayari kuhifadhi siri ninayotaka kukwambia? Sio tena uende ukapayuke kwake, Ooh, Mohsein ndiye aliyeniambia!"

"Niamini, sitomwambia!" John alijaribu kusema kwa utulivu. Mohsein akawa na uhakika kwa wakati huo mapigo ya moyo ya John yalikuwa yakipiga kwa nguvu kifuani pake, na hapo ndipo alipokuwa akipataka! "Nadhani unajua kama Dina yuko Arusha?" alisema.

"Ndio nafahamu," John alijibu huku sura yake ikionekana kama aliyepigwa na msukule.

"Najua amekuaga kuwa anakwenda kikazi, lakini kwa taarifa yako hakwenda kikazi, bali amekwenda kustarehe na mtoto wa tajiri mwenye kampuni, anaitwa Richard!"

Kutajiwa jina la Richard, John akahisi aina ya kizunguzungu kikiwa kimemwandama. Mapigo ya moyo wake yakaanza kumwenda mbio, damu ikamchemka na uso wake ukawa mzito. Akajizuia ili asiyumbe au kuanguka.

"Najua amekwenda Arusha, lakini kikazi!" hatimaye John alipata nguvu ya kusema. "Unataka kuniambia hakwenda kikazi?"

"Kiofisi imetafsiriwa kikazi, lakini ni zaidi ya hivyo!"

John alijishika kiuno akauinamisha chini uso wake na kuviangalia viatu vyake, akaonekana kufikiri haraka haraka. "Namfahamu Richard, lakini sikujua kama wana mahusiano ya aina hiyo," alisema. "Kwa hiyo waliondoka pamoja?"

"Walipanda ndege moja kwenda Arusha!"

Ilikuwa ni habari mpya kwake! Dina alikuwa hakumwambia kama angesafiri kwa ndege. "Safari hiyo Dina alikuwa akiijua kabla?" aliuliza.

"Mbona aliambiwa mapema tu, siku tano kabla!" "Na alijua kama angesafiri na Richard?"

"Richard ndiye aliyemuita kumfahamisha safari hiyo na kumuahidi kuwa wangeondoka pamoja kwa ndege. Haikuwa safari ya ghafla!"

Dina alinidanganya! John aliwaza baada ya kukumbuka kuambiwa na Dina kwenye simu kuwa, Richard alibaki Dar es Salaam. "Naomba kukuuliza swali moja la msingi…" alisema na kumwangalia Mohsein machoni.

"Niulize," Mohsein alisema kwa kujiamini.

"Kwa nini umekuja kuniambia habari hizi?" John aliuliza na sura yake ikawa makini kumwangalia Mohsein usoni.

Swali hilo lilionekana dhahiri kumyumbisha Mohsein na akaonekana kukosa jibu sahihi. "Ina maana nimekosea kuja kukwambia?" alijikuta akiuliza badala ya kujibu.

"Sina maana hiyo! Nataka kukuuliza swali jingine…" Mohsein hakujibu!.

"Ulikuwa ukinijua?"

"Tatizo nilikuwa sijakuona, lakini nilikuwa nikijua kuna mtu kama wewe ambaye anataka kumuoa Dina! Kwani vipi?"

John alishusha pumzi kwa nguvu kama aliyechoka, kisha akasema, "Basi nimekusikia na nitazifanyia kazi habari ulizonipa."

"Wewe ni mwanamume mwenzangu na mimi hili jambo limeniumiza. Kwa nini akufanyie upuuzi wa namna hii? Dina atakuwa na maana gani ya kukubali kuolewa na wewe halafu papohapo atembee na mwanamume mwingine? Wewe chunguza hizi habari na mwenyewe utajionea. Lakini utakuja kunipa mkono kama nilichokwambia ni kweli!"

"Sawa nimekusikia," John alisema na kuonyesha hakuwa tayari tena kuendelea kuwepo hapo. "Nashukuru kwa taarifa yako!" akamuaga Mohsein na kabla ya Mohsein hajajibu, John akaondoka.

Mohsein akabaki ameduwaa huku akimwangalia John alivyokuwa akiondoka.

John alirudi kufanya kazi akiwa na mtafaruku wa mawazo, muda mwingi alijikuta akizubaa kuzifikiria tuhuma alizotuhumiwa nazo Dina. Moyo wake ulikuwa ukifukuta na mapigo ya moyo wake yalikuwa yakienda kasi. Wivu ulikuwa umetawala kila sehemu ya kiungo chake na hatimaye kujigundua kuwa, hata mikono yake ilikuwa ikitetemeka! Kila wakati alikuwa akisonya peke yake na kuna kipindi alitamani aipige ngumi meza yake ya ofisini!

Ingawa hakuwa na uhakika na sababu hasa zilizomfanya mtu aliyejitambulisha kwake kwa jina la Mohsein kumletea habari hizo, lakini alikuwa mwepesi wa kuziamini kutokana na ukweli kuwa, hata yeye mwenyewe kwa siku za hivi karibuni alijengwa na mashaka makubwa yaliyomtishia kuwa, huenda Dina na Richard wakaurejesha uhusiano wa mapenzi kati yao baada ya Dina kuajiriwa kwenye kampuni ya baba yake Richard ambako Richard anafanya kazi. Lakini, laiti asingekuwa na hofu hiyo tokea awali, kitendo cha Mohsein kumjia na kumpa habari hizo kingemuweka kwenye mashaka ya kutomuamini. Na pengine angemuwekea dhana kuwa, huenda Mohsein alimtaka Dina kimapenzi na baada ya kukataliwa ndipo akaamua kumfanyia fitina.

Lakini ni ile hofu aliyokuwa nayo awali dhidi ya ajira aliyopewa Dina kwenye kampuni ya baba yake Richard ndio iliyomfanya avutike na madai yaliyotolewa na Mohsein, ujio huo wa Mohsein akauona kama vile Mungu alimwelekeza aje amthibitishie mashaka aliyokuwa nayo dhidi ya ajira hiyo kuwa, yalikuwa ni ya kweli! Pamoja na kuziamini habari alizoambiwa na Mohsein, lakini mara kwa mara John alijikuta akiwa kama haamini kama ni kweli Dina angeweza kumfanyia usaliti wa aina hiyo.

Ni usaliti ambao awali walipeana viapo vya kutosalitiana. Mara kadhaa walikwisha kumjadili Richard, wakaapa kupambana naye kuhakikisha hafanikiwi kuwatenganisha huku Dina akichukua jukumu la kula kiapo kuwa, hata iweje, katu asingeweza kurudiana na Richard! Leo kusikia Dina amekiasi kiapo hicho na kukubali kumsaliti, John alijihisi akiteketea kwa maumivu aliyoshindwa kuyafananisha na mengine yoyote yaliyowahi kumtokea tangu ajitambue kuwa anaishi duniani!

* * * * *

WIVU wa MOHSEIN unampelekea kumuuza DINA kwa JOHN....Je nini kitatokea???
***RICHARD amemuweka DINA kimapenzi....je? Atamuoa???

culbby mlyn Analyse princetx slim5 MUSSOLIN ram
 
Last edited by a moderator:
Haya njoo uendelee basi

samahani, msaada wako pse, mimi huku napata vipande vipande vya hii stori, tena vingine vimerukwa, ram naomba msaada wa link yenye mtiririko full!
 
Last edited by a moderator:
duu ngoja nimbembeleze Judy kwanza kwa alichofanyiwa na Richard then niendelee na Dina & John
 
Back
Top Bottom