MTUNZI: BEKA MFAUME
SEHEMU YA KUMI NA NNE
John aliteremka kutoka kwenye teksi iliyokuwa imesimama sawia kwenye mlango unaoingia moja kwa moja ndani ya jengo la hoteli ya Masai Shield. Teksi ikaondoka na yeye akageuka kuangalia mlangoni. Wahudumu wawili wenye sare za kazi wanaopokea wateja waingiao, walikuwa wamesimama ndani ya mlango wa kioo unaojifungua wenyewe pindi unapokaribiwa na mtu anayetaka kuingia au kutoka. Wote walimwona John alivyoteremka kwenye teksi na wakawa wanamwangalia.
Mara tu mlango ulipojifungua, John akaisikia harufu nzuri kutoka humo ndani; ni harufu ya aina moja ambayo duniani kote utakumbana nayo mara tu ukiingia kwenye hoteli za kifahari kama hizo. Alipokuwa akiingia aliwasalimia watu wale na wote waliitika kwa nidhamu na kumkaribisha.
Mteja ni Mfalme! John aliwaza baada ya wahudumu wale kumuinamishia vichwa wakati walipokuwa wakisalimiana. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia kwenye hoteli hiyo ingawa alikuwa akiiona na kuipita kwa mbali wakati wa siku za nyuma alipokuwa akija Arusha. Aliingia ukumbini kulikokuwa na mandhari ya kupendeza iliyokuwa ikimulikwa kwa taa zenye nuru hafifu ambayo miali yake ilichomoza kutoka kwenye matundu madogo na membamba yaliyopo kwenye dari iliyonakshiwa kwa ujenzi wa kisanii.
Kwenye ukumbi huo ambako kulikuwa na ukimya uliovunjwa na mziki mororo wa ala tupu uliosikika kwa sauti ndogo, eneo hilo lilikuwa na sofa za kupendeza ambazo baadhi zilikuwa zimekaliwa na wateja; wengi wao wakiwa ni Wazungu. Pia kulikuwa na matangazo ya huduma mbali mbali yaliyokuwa yakiwaka kwa kunakshiwa na taa za rangi kwenye baadhi ya kuta zilizomo humo ndani. John akaliona eneo alilokuwa akilihitaji; eneo la mapokezi ambalo lilikuwa lipo mbele yake. Kwenye meza ndefu iliyojengwa kwa muundo wa upinde kulionekana baadhi ya wateja waliokuwa wakihudumiwa na wafanyakazi watatu wa idara hiyo mapokezi. Wafanyakazi wote watatu walikuwa ni wasichana warembo wenye sare za kazi zilizofanana.
John alikwenda kusimama kwenye meza hiyo na kusubiri mmoja wa wafanyakazi hao amaliziane na baadhi ya wateja waliokuwepo hapo. Akapatikana mmoja aliyemwendea John.
"Karibu; nikusaidie nini?" msichana huyo wa mapokezi alimwambia John kwa lugha ya Kiingereza.
"Nataka kuonana na mgeni wangu, kati ya Richard Ken au Dina," John alisema kwa kujiamini kwa kutumia lugha ya Kiingereza ambayo hakuwa na umahiri nayo sana.
Msichana akainua simu na kupiga, akaonekana kusikilizia kwa makini. Akairudisha.
"Hawapo chumbani, nadhani watakuwa restaurant wakila chakula cha jioni," msichana alisema.
Hawapo chumbani! John alishangaa.
"Naweza kwenda kuwaona? Mimi ni mfanyakazi mwenzao," alisema na kujaribu kuificha taharuki aliyoipata.
"Unaweza kwenda kuwaona," msichana alisema na kuonyesha kumalizana na John, akataka kuondoka kwenda kuhudumia mteja mwingine aliyefika hapo ambaye alikuwa ni Mzungu.
"Unaweza ukanielekeza? Siijui restaurant yenu ilipo," John aliwahi kusema kabla msichana yule hajaondoka.
Msichana akamwelekeza. "Ahsante," John alisema.
"Unakaribishwa!" msichana alisema na kuonyesha tabasamu bandia la kikazi kisha akamfuata yule mgeni akiyekuwa amewasili.
Pamoja na kuwa alitarajia kitu kama hicho kingeweza kutokea, lakini ule ukweli uliojitokeza kutokana na kauli ya yule msichana wa mapokezi kutoa kauli iliyoonyesha kuwa, Richard na Dina hawakuwepo chumbani, ilimdhihirishia John kwamba, Richard na Dina walikuwa wakikaa kwenye chumba kimoja, ikawa kama vile jambo hilo hakuwahi kulifikiria kabla!
Udhihirisho huo uliomdhihirishia kuwa Richard na Dina walikuwa wakitumia chumba kimoja ulimchanganya. Hasira na wivu vilimjia kwa wakati mmoja na alijishangaa jinsi alivyoweza kujizuia mbele ya yule msichana kutoonyesha kuchanganyikiwa alikokupata. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yakimwenda mbio wakati alipokuwa akielekea katika lifti itakayompeleka kwenye ghorofa ulipo mgahawa ambako ndiko alikoelekezwa waliko Richard na Dina. Mkanganyiko uliokuwa kichwani mwake ulimfanya alijihisi kutamani kumuua yeyote kati ya Dina au Richard! Akili yake ilimtuma kutoukubali uzoba aliokuwa akifanyiwa na watu hao.
Akiwa amesimama nje ya mlango kuisubiri lifti iwasili, John alirudia kama mara mbili au zaidi kushusha pumzi za hasira kama vile afanyavyo mtoto mwenye hasira aliyetoka kulia kwa ghadhabu. Alijaribu kuituliza akili yake na kujihisi kama anayeshindwa kuidhibiti. Subira yake ya kuisubiri lifti ilimfanya asitulie sehemu moja, alizunguka huku na kule na kuiona lifti hiyo ikichukua masaa kadhaa kuwasili. Lifti ikawasili, akaingia.
Lifti ilimchukua na kwenda kusimama kwenye ghorofa yenye mgahawa. John alitoka akiwa na baadhi ya wateja wengine waliokuwa wakienda kula kwenye mgahawa aliokuwa akielekea. Yeye na wale wateja kwa pamoja walikaribishwa na msimamizi wa huduma za mgahawani.
"Nataka kuonana na Richard Ken, nimeambiwa yuko huku anakula," John alimwambia mkuu wa mgahawa aliyekuwa ameanza kumwonyesha meza ya kwenda kukaa.
* * * * *
"Yesu wangu!" Dina alisema na papohapo kuonyesha kushituka wakati uso wake akiwa ameuelekeza mlangoni ambako wateja walikuwa wakiingia.
"Kitu gani?" Richard aliuliza na kuangalia alikokuwa akiangalia Dina. Akaonekana kutokigundua kilichokuwa kimemshitua Dina. "Vipi?" aliuliza tena huku akiurudisha uso wake kumwangalia Dina.
Dina alikuwa bado akiangalia mlangoni, kisha kwa sauti ndogo kama vile alikuwa anaongea peke yake akasema kwa kifupi, "John!"
Ndipo Richard akapata mshituko ulioungana na kitendo cha kuangalia tena mlangoni. Kauli yake ikapotea baada ya kumwona mkuu wa mgahawa akimwonyesha John mahali walipo!
John akawa kama aliyezubaa huku akiangalia upande walipo Richard na Dina.
"Wacha nimfuate kule kule!" Dina alisema ghafla na kuinuka. "Mwache aje hapa hapa!" Richard alisema na kumzuia Dina kwa
kumshika mkono. Richard alishaingiwa na wasiwasi kunaweza kukatokea patashika kati ya Dina na John endapo wangebaki peke yao na ndio sababu ya kumzuia Dina. Lakini pia alikifanya kitendo hicho kwa sababu alikuwa akijiamini kupigana, aliwahi kuchukua mafunzo ya karate wakati alipokuwa akisoma Uingereza. Hata hivyo alishakuwa na zaidi ya miaka miwili tokea aliposimama kuendelea na mafunzo hayo na hakuwa na mazoezi ya aina nyingine yoyote tokea alivyorudi nchini, hata hivyo aliamini angeweza kumdhibiti John asimfanyie fujo yoyote Dina kama angewafuata hapo.
"Niache nikazungumze naye," Dina alisisitiza kwa kujiamini. Richard akamuachia! Dina akaondoka na kuharakisha kwenda
kumkabili John kabla hajaingia eneo la ndani zaidi la mgahawa lenye wateja waliokuwa wakila chakula.
Akiwa amesimama huku akimwangalia Dina aliyekuwa akimjia, John alishindwa kuamini kama anayemwona hapo alikuwa ni Dina yule yule aliyekuwa akimlia viapo vya uaminifu. Alijiona kama aliyekuwa akimwangalia Dina mpya mwenye uzuri ulioongezeka ghafla kiasi kwamba hata baadhi ya wateja waliokuwemo humo mgahawani walikuwa wamegeuka kumwangalia.
Dina alipokuwa akielekea kule alikosimama John, hatua zake ziliufanya ule mkufu wa dhahabu wenye kito cha thamani aliouvaa shingoni, kidani chake kichezecheze na kutoa miali ya kung'ara kila kilipokuwa kikitikisika kifuani kwake, na wakati huo huo hereni za dhahabu zilizokuwa mfano wa bangili kubwa nazo zilikuwa zikiyumba masikioni mwake wakati akitembea. Mwonekano wa Dina ulimfanya John apigwe na ganzi huku akishindwa kuamini kama yeye ndiye mmiliki wa mapenzi wa msichana huyo anayekuja mbele yake. Akili yake ilikuwa imepumbazwa na uzuri wa binti huyo aliyeonekana kuwa kwenye daraja la juu la kimaisha. Hasira iliyokuwa imemvaa wakati akiwasili hapo ikaanza kunywea taratibu!
Ghafla akaiona fahari ya kummiliki msichana mzuri wa aina hiyo, tukio hilo likamfanya akumbuke kuwa ni msichana huyo ndiye anayemfanya aingie kwenye ushindani wa kumgombania kati yake na Richard! Na ndiye aliyekuwa akimhangaisha kwenda kwa waganga kwa ajili yake ili afanikiwe kumrudisha kwenye himaya yake!
Siwezi kumuachia Richard! aliapa ghafla. Akayakumbuka madawa aliyojipaka usoni kuwa yalikuwa na uwezo wa kuipumbaza akili ya Dina pindi atakapoangaliana naye machoni! Na hicho ndicho kilichomleta hapo Arusha; aje amchukue na kurudi naye Dar es Salaam!
"Vipi?" Dina aliuliza alipomkaribia John huku sura yake ikiwa kwenye mshangao na nusu kwenye kuchanganyikiwa.
Kitendo cha Dina kumwangalia sawia John kwenye macho yake wakati alipomwuliza swali hilo, ndicho John alichokuwa akikihitaji. Alihitaji Dina ayaangalie macho yake kwa kuamini madawa aliyojipaka ndipo yatakapofanya vyema kazi yake. Na yeye akayatuliza macho yake machoni mwa Dina na kupoteza sekunde kadhaa kama sehemu ya kukoleza ufanyaji kazi wa dawa hizo kabla ya kulijibu swali la aliloulizwa.
"Nimekufuata turudi Dar es Salaam!" John alisema baada ya kujitosheleza na muda alioutumia kuangaliana na Dina, na hata aliposema hivyo, alisema kwa kujiamini. Akatarajia Dina angegwaya.
Lakini badala ya kugwaya, Dina akashangaa!
"Hebu njoo huku!" alimwambia John kwa sauti ya upole lakini yenye amri. Alikuwa akijielewa jinsi anavyoweza kumdhibiti John na alikuwa na uhakika John angefuata alichosema.
John akamfuata! Wakaenda ulipo ukumbi wa baa, wakakaa kwenye sofa. Mhudumu akafika muda huo huo na kuwauliza wanachohitaji kunywa.
"Utakunywa nini?" Dina alimwuliza John.
John akazitambua fikra za Dina kuwa zipo kwenye kumwongoza kama alivyokuwa amezoea siku zote. Kwa kuwa na yeye alikuja hapo kwa imani ya kuleta mapinduzi ya kuyageuza mazoea hayo kwa kuamini dawa alizojipaka, akaona sasa ilikuwa zamu yake kuchukua utawala wa kumtawala Dina kimapenzi.
"Sihitaji kinywaji chochote Dina!" John alisema kwa sauti aliyotaka Dina aione ni amri.
"Nimekuja kukuchukua turudi zetu Dar! Kwa hiyo tuondoke!"
Dina akatengeneza tena mshangao usoni na kumwangalia John. "John umelewa?" aliuliza kwa kujiamini na kuonyesha kiburi kidogo kwenye sauti yake ili kuonyesha ni yeye ndiye mwenye turufu ya utawala wa kumtawala John.
"Ni mzima na akili yangu!" John alijibu kifedhuli huku mikono akiwa ameituliza juu ya magoti yake. Ghafla akajiona ana nguvu za kupambana na Dina kimazungumzo, akaamini dawa alizopewa na mganga zilikuwa zikimpa nguvu hizo!
Jibu la John likamfanya Dina amwangalie mhudumu aliyekuwa bado amesimama akisubiri maagizo.
"Nikikuhitaji nitakuita," alimwambia mhudumu kwa lengo la kumwondoa.
Mhudumu akaondoka.
"Umekuja kunichukua wakati unajua nimekuja huku kikazi?" Dina alimwuliza John kwa utulivu baada ya mhudumu kuondoka.
"Nimeamua! Kwa hiyo tunaondoka pamoja hadi hotelini nilikofikia!" John alisema kwa sauti yenye ushari.
"Na kesho asubuhi tunarudi Dar es Salaam!"
Dina hakujibu haraka. Alitulia kwa sekunde chache huku akimwangalia John kwa dalili zile zile za mtu aliyemzoea huku akionekana kama anayetaka kuisoma akili ya John.
"Unajua John sikuelewi!" alisema na safari hii sauti yake ilikuwa na ukali fulani.
"Hunielewi kwa sababu lugha niliyoizungumza huijui? Au hunielewi kwa lipi?" John aliuliza.
Hata hivyo, John alikuwa ameanza kushangazwa kumwona Dina akiwa bado anaonyesha aina fulani ya ubishi. Alitarajia Dina hadi muda huo angekuwa tayari amekwishapumbazwa na dawa alizojipaka na angekuwa anatii kila analoelezwa. Alitarajia endapo Dina kama angetokea kuhoji, basi angehoji maswali madogo madogo yasiyoashiria aina yoyote ya kuleta ubishi; lakini mwonekano uliokuwepo hapo ulianza kuwa tofauti na matarajio hayo. Dina alikuwa bado akionyesha kuwa na akili zile zile za utawala dhidi yake! John akaanza kuuhoji uwezo wa dawa alizojipaka kama zilikuwa na uwezo wa kumbadilisha Dina.
"Utakujaje ghafla bila ya kuniarifu?" Dina aliuliza kwa sauti iliyoonyesha kukerwa na kuonekana joho la utawala wa kumtawala John likiwa bado maungoni mwake.
"Halafu kufika tu unaniambia umekuja kunichukua unipeleke hotelini kwako! Hakuna kunisalimia, hakuna kuulizana! John umechanganyikiwa?"
"Nadhani nina haki ya kukwambia hivyo! Dina, mimi ni mchumba wako!" John naye alisema kwa ukali wa kujibu mapigo.
Dina akatoa kicheko kidogo cha dharau.
"Haki ya kunikokota unavyotaka? Bado hujawa na haki hiyo John!' alisema kwa utulivu huku akitingisha kichwa chake kuonyesha kusikitika. "Hata mahari yenyewe hujanilipia unaanza kusema hivyo! Je, ukinioa itakuwaje?"
John akamkumbuka mama yake Dina na kauli hiyo ya mahari. Akanywea kiaina, lakini akajipa matumaini ya kuyatawala mazungumzo hayo. Bado alikuwa akiamini dawa zake zingefanya kazi.
"Lakini mimi bado ni mchumba wako Dina!" alisema kwa ajili ya kuendeleza ligi ya ubishi. "Kuna makosa gani kukwambia hivyo?"
"Najua kuwa ni mchumba wako, lakini ndio uamue kunifuata huku Arusha bila ya kunifahamisha kama unakuja?" Dina alisema, kisha ghafla akaonyesha kukerwa na kitendo hicho.
"Kwa nini hukuniambia kama unakuja wakati mchana wa leo tulizungumza kwenye simu? Ulikuwa na mawazo gani kichwani mwako? Huniamini? Lengo lilikuwa ni kunifumania?"
John akapigwa na butwaa! Lakini halikuwa butwaa lililoletwa na kauli hiyo kali ya Dina; bali lilitokana na kule kutomwona Dina kutokuwa na dalili za kulainika! Alijiona bado akizungumza na Dina yule yule ambaye siku zote yuko juu yake.
"Kwa hiyo hatutakwenda hotelini nilikofikia?" John aliuliza swali ambalo alikuwa na uhakika sio jibu la swali aliloulizwa.
"Nakuomba kitu kimoja John!" Dina alisema kiukomavu na kumwangalia John machoni. "Naomba urudi Dar! Kama unalo lolote la kuniambia hata kama nimekuudhi, basi unisubiri hadi nitakapokuja Dar. Samahani kwa kukwambia hivyo, lakini sikudanganyi John; kweli umeniudhi!"
John akapoteza mhimili wa kujizuia, akaonyesha kuanza kuchanganyikiwa. Alizirudisha nyuma nywele zake kwa kuzisukuma na vidole vyake vya mkono. "Dina, bado unanipenda?" aliuliza huku akiwa amekiegesha upande kichwa chake. Swali lake halikuulizwa kimahaba, lilikuwa na aina ya ushari.
"John bwana! Maswali gani hayo unayoniuliza?"
John akagundua alikuwa akipoteza muda kusubiri nguvu za dawa alizojipaka zifanye kazi. Yule mshenzi amenitapeli! aliwaza. Akaachana na mawazo hayo ya kishirikina ambayo yalikuwa yamemjengea subira kwa wakati wote. Akairudisha akili yake kwenye uhalisia wa jambo analokabiliana nalo kuwa, Dina na Richard walikuwa wanalala chumba kimoja humo hotelini! Na isitoshe pia, amewafumania wakiwa kwenye meza moja wakila chakula wakionekana dhahiri ni wapenzi!
Wivu ukarudi upya na subira ikamtoka!
"Mimi najua kila kitu Dina! Usifikiri miye zoba!" John alibwata huku akionekana kuchachamaa ghafla. "Nina habari zenu zote kuhusu wewe na yule mshenzi wako uliyekuwa naye pale mezani!" alisema na kunyoosha mkono kuelekeza upande uliko mgahawa ambako yuko Richard.
"Kwa taarifa yako, najua kama ulisafiri naye kwenye ndege moja! Isitoshe vilevile, najua kama unalala naye chumba kimoja!" alinyamaza na kutweta huku macho yake yakitambaa mwilini mwa Dina.
"Ni nini kilichokubabaisha Dina? Au ni hiki kijiguo pamoja na hizi dhahabu alizoanza kukununulia? Hukuwanavyo hivi wakati ulipoondoka Dar! Uwongo? Kwa muda huu mfupi wa kuja hapa Arusha tayari umeamua kunisaliti? Umeisahau ahadi uliyoniahidi kuhusu huyu jamaa? Umesahau kama uliapa Miungu yote kunihakikishia kuwa hutotembea naye? Umesahau yote niliyokutendea? Umesahau tulikotoka? Unanifanyia haya ukiwa na pete yangu ya uchumba kidoleni mwako Dina?"
Dina aliganda. Akaonekana kama mlemavu asiyeweza kuzungumza. Alikuwa amenywea kama aliyenyeshewa. Akaonekana kama sanamu lenye kupepesa macho. Kiburi na kule kujiamini kukatoweka. Aligwaya!
John alikuwa tayari ameghadhibika!
"Tunaondoka pamoja kwenda hoteli nilikofikia!" alisema na kuukamata mkono wa Dina.
Dina akaufyetua mkono wake kutoka mkononi mwa John.
"Bwana tutakuja kuongea Dar!" Dina alisema na kuonekana kurejewa na fahamu. Akasimama kutaka kuondoka.
John akawahi kumzuia Dina kwa kumshika tena mkono.
"Huwezi ukazungumza na mimi halafu ukataka kuondoka kienyeji, rudi kwenye kiti!" alisema kwa sauti ndogo kujaribu kuwafanya watu wasifuatilie kinachoendelea hapo.
Dina akanywea tena, safari hii macho yake yakawa yameingia woga! Na yeye naye akazungukwa na kiwingu cha hofu kama ya mwenzake ya kuogopa watu wasilifuatilie tukio lao. Akarudi kwenye sofa.
"Mimi nazungumza na wewe halafu unaondoka!" John alisema,
munkari ulikwishaanza kumpanda. "Sasa mimi nakwambia, kwa yule mshenzi wako hurudi! Na utaondoka na mimi!"
"John mimi nipo kazini! Sasa mambo gani haya unayonifanyia? Utaniharibia kazi…" Dina alilalamika kwa sauti ya kujitetea, alikuwa hajawahi kumwona John akiwa katika hali ya hasira kama anayomwona nayo hapo na hali hiyo ilianza kumwogopesha.
"Kazi ya kuja..!" John alitaka kutukana, lakini na yeye akashindwa kumalizia alilotaka kulitamka. "Nitakutukana Dina!" alisema kwa hasira. "Sijawahi kukutukana hata mara moja! Tafadhali Dina!"
Dina hakujibu!
John akasimama.
"Twende!" alisema kwa jazba. Dina hakujibu wala hakuinuka!
Hasira na wivu vikampagawisha John! Akamuinamia Dina na kuukamata mkono wake karibu na kwapa, akaanza kumuinua kwa nguvu. "Nadhani ulikuwa hunijui!" alisema na kuanza purukushani ya kumvuta Dina ambaye alikuwa akigoma kuinuka.
Tukio hilo likaanza kuwavutia wateja na wafanyakazi waliokuwepo eneo hilo. Wahudumu wawili wa kiume wakaenda eneo walilokuwepo Dina na John, wote kwa pamoja wakamvaa John ili amwachie Dina huku wakimsihi aache vurugu. Kitendo hicho kikamfanya Dina apate upenyo wa kuchomoka. Akafyetuka kama mtego ulioteguka, akakimbia kurudi mgahawani alikomuacha Richard!
John alikuwa mtu wa kufanya mazoezi mara kwa mara hasa ya kuogelea na kukimbia, akatumia nguvu za kushitukiza kuwasukuma wahudumu wale wawili waliokuwa wamemzuia na kuwabwaga chini. Akaitumia nafasi hiyo kumkimbiza Dina aliyekuwa nusu anakimbia nusu anatembea!
* * * * *
Richard alikuwa amekosa amani muda wote tokea Dina alivyokuwa ameondoka. Aliwaona Dina na John wakiongozana kuelekea ulipo ukumbi wa baa na kupotea machoni kwake, tokea wakati huo kukawa na ukimya! Alikuwa na uhakika, John alikuja hapo Arusha ghafla kwa kushitukiza na alikusudia kumshitukiza Dina. Hakujua ni nini kilichomleta ghafla, lakini alihisi huenda kuna kidudu mtu aliyemvujishia mahusiano yake na Dina yalivyo hapo Arusha.
Hakutaka Dina akakabiliane na John kama Dina alivyokuwa amesisitiza wakati John alipokuwa ameingia hapo mgahawani. Alikuwa na wasiwasi Dina asingekuwa salama kuwa peke yake na John. Kitendo hicho cha kuondoka pamoja na kwenda kuzungumzia baa na ukimya uliokuwa unazidi kuendelea kukamfanya akose amani. Kuna kipindi alijikuta alishawishika kutaka kumtuma mhudumu wa humo hotelini ili afuatilie nyendo za watu hao wawili, kisha aje kumripotia. Lakini alijikuta akikwama kuutekeleza uamuzi huo kwa hofu ya kuruhusu watu wengine waingilie mambo yasiyowahusu.
Wasiwasi aliokuwa nao kuhusu Dina aliyekuwa mikononi mwa John akiwa peke yake, ulimfanya ajikute akiinywa pombe ya mvinyo kwa kasi iliyomshitua hata yeye mwenyewe. Aliliona jukumu la kumtetea na kumlinda Dina lilikuwa ni lake endapo John ataamua kufanya lolote la kumdhuru. Kwa hiyo, kitendo cha kuendelea kuwepo hapo akiendelea kumsubiri Dina arudi kikawa kinamtia kwenye hali hiyo ya kupoteza umakini wa unywaji wake. Ghafla akawaona wateja waliokuwa wakiendelea kula chakula humo mgahawani walioko upande ambao wanaliona eneo la ukumbi wa baa, wakigeuza sura zao kwa mpigo na kuliangalia eneo hilo.
Richard akatambua kuna walakini unaotokea kati ya John na Dina!
* * * * *
Hakusubiri! Richard aliinuka na kuanza kujitoa katikati ya meza na kiti alichokuwa amekalia. Akawaona wahudumu wakitaharuki, kisha wote kwa pamoja akawaona wakielekea eneo la baa. Tukio hilo likamfanya Richard afanye papara ya kutoka, na alipokuwa akitoka miguu yake ikakisukuma kiti kilichokuwa nyuma yake, kikapiga mwereka na kutoa sauti ya kuanguka. Akiwa hajali tukio la kuangusha kiti kutokana na akili yake kutekwa na kule watu wanakoangalia ambako ndiko waliko Dina na John, ghafla akamwona Dina akitokeza huku akikimbia kumfuata kule aliko! Baadaye akafuatia John aliyekuwa akimkimbiza Dina! Richard hakufikiri mara mbili, alijua Dina yuko hatarini na lilikuwa jukumu lake kumtetea. Akachomoka, lakini hakumfuata Dina!
Alimkabili John!
Wakavaana katikati kama fahali wawili wenye hasira. Wakashikana na kuzoana kimzobemzobe, wakaangushana kwa kishindo kwenye meza iliyokuwa jirani yao ambayo ilikuwa haina wateja. Nyenzo za kulia chakula zilizokuwa zimepangwa kwenye meza hiyo zikaanguka kwa kishindo cha kelele na kutawanyika chini. Hali ya vurugu ikawa imetawala kwa watu hao wawili. Wote walikuwa wameangukia sakafuni na kila mmoja akitaka kuwahi kuinuka kabla ya mwenzake. Wakakikirishana huku kila mmoja akionyesha misuli yake, lakini akawa ni Richard ndiye aliyewahi kutupa ngumi iliyompata John kwenye paji la uso. John alisukumwa chini na nguvu ya ngumi hiyo, Richard akawahi kupanda juu ya mwili wa John ambaye alianza kutoka damu sehemu aliyopigwa ngumi na kuanza kuikaba shingo ya John kwa mikono yake huku akitumia nguvu zote, kama vile alipania kumuua!
Wahudumu ambao walikuwa wakipiga kelele ya kutaka walinzi wa hoteli waitwe, walikwenda kwa pamoja kwenye ugomvi uliokuwa ukiendelea huku Richard akionekana amemdhibiti vyema John katika ile hali ya kumkaba koo. John akaonekana anapoteza nguvu!
"Mtoeni anamuua mwenzake!" kelele za wahudumu na wateja hasa wanawake zilisikika zikihimizana. Baadhi ya wahudumu wa kiume wakamvamia Richard na kuanza kumvuta kumwondoa kutoka mwilini mwa John na kufanikiwa kuwaachanisha. Kitendo hicho cha kuwaachanisha kikampa nafasi John ya kuokota kisu kabla ya Richard hajapata mhimili mzuri wa kujiinua. Kilikuwa kisu cha kulia chakula kati ya nyenzo zilizokuwa zimeeanguka chini, John akazitumia nguvu zake zote kumchoma kisu hicho Richard sehemu ya ubavuni!
Richard alipiga ukelele na kuangukia ubavu uliochomwa kisu na kukishikilia kisu hicho kilichojikita ubavuni mwake. Wakati huohuo damu ikachukua nafasi yake kutoka! Tukio hilo liliwachanganya watu wote waliokuwepo eneo hilo, sura zilizohamanika kwa hofu na taharuki iliyowatawala mioyoni mwao wakaonekana kuanza kuhaha kutafuta eneo la kukimbilia. Baadhi yao wakakimbilia kwenda kusubiri lifti.
Wakati vurugu za kila mmoja aliyekuwepo hapo akisema lake, John aliinuka na kuokota kisu kingine. Uso wake uliopigwa ngumi ukiendelea kuchirizika damu kwenye sehemu iliyopigwa, alianza kutamba kwa kuzunguka kama Sokwe na kuonekana kupagawa. Sura yake iliogofya, macho yake yaliyotapakaa damu aliyokuwa akijaribu kuifuta mara kwa mara kwa kutumia eneo la mkono karibu na bega lake yalionekana kuingiwa na woga. Akaanza mkwara wa kuwatisha kuwachoma kisu wateja wa hoteli waliokuwa wamesimama mbele yake. Wateja hao wakaanza kurudi nyuma huku wakitoa nafasi ya kumpisha John apite.
Kelele za kushakiziana zikaanza, "Jamani mkamateni anakimbia huyo!"
John alikuwa bado akitamba na kisu chake mkononi, aliupindisha mgongo wake kama anayepigana miereka. Alikuwa na mwonekano wa kutisha, alikuwa kama mwendawazimu aliyepandwa na kichaa, aliyazungusha macho yake yaliyoonekana kuwa makubwa ghafla, akawa kama aliyekuwa akitafuta kimbilio. Akawaona baadhi ya wateja waliokuwa wakiwahi kuingia kwenye lifti kulikimbia eneo hilo. Naye akatimua mbio kuelekea huko huko kwenye lifti!
Kelele za taharuki zikasikika! "Huyo anakuja!"
Watu waliokuwa wamekwishaingia ndani ya lifti ambayo ilikuwa haijafunga mlango wakapagawa walipomwona John akikimbilia kwenye lifti walipo wao!
"Jamani huyo anakuja!" kelele za kutaharuki zilisikika kutoka ndani ya lifti.
****WIVU umezua vita!!! vita ya kumuwania DINA....DINA asiyekuwa na msimamo!!!
***NANI ATAIBUKA MBABE????
culbbymlynAnalyseprincetxslim5MUSSOLIN ram Mphamvu ICHANA