WAKALA WA SIRI 10
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300
ILIPOISHIA
Hatimaye alimaliza kununua bidhaa zote alizoagizwa, lakini alivutiwa na matunda Fulani yaliyokuwa na maganda ya rangi ya njano, alipouliza aliambiwa yanaitwa ‘Sambia’ aliyaonja, Dooh! Yalikuwa yana sukari na ukakasi, ndani yake yakiwa na mbegu za rangi ya huzurungi.
Muda ulikuwa umeenda sana, jua lilikuwa kali yapata mida ya saa sita. Sajenti akarudi Nkwini kwa Babu yake akiwa amefurahia safari yake, roho yake ilisuuzika, mji wa Makanya uliamsha chemchem ya uhai na ari moyoni mwake.
***************************
INAENDELEA
Usiku uliingia, giza nalo likafungua mdomo wake likaumeza mji wa Nkwini. Siku ile anga lilitawaliwa na Mawingu makubwa meusi yenye kutisha. Sajenti na Mzee Mkwizu walilala kama ilivyokuwa desturi ya wanadamu wote kulala usiku. Siku hiyo Sajenti alikuwa amechoka kuliko siku zote, alichoshwa na mizunguko ya mchana ya sokoni, Makanya. Leo alilala fofofo mithili ya pono. Hata angeota ndoto lazima ingekuwa ndoto yenye kutisha, yenye kufisha na kulegeza mwili na roho.
Huko nje Kajiru alikuwa akibweka Huu! Huuu! Wakati wengine wakiwa wamelala wasijue nje kuna zimwi linalokuja kuwala. Kajiru alibweka, sasa muda huu sauti ikiwa imeongezeka ikiwa na wehu ndani yake. Tayari mvua ilianza kunyesha hali iliyofanya sauti ya kubweka kwa Mbwa, ndiye kajiru kutosikika vizuri kutokana na bati kupiga kelele zilizosababishwa na matone ya mvua. Nje walikuwepo wanaume sita, waliovalia makoti makubwa meusi ya mvua, wakiwa wameshikilia bunduki aina ya SMG. Walishaingia kwenye uzio wa nyumba ya Mzee Mkwizu, Sauti ya Mbwa iliwafanya waongeze tahadhari, wakimtafutia shabaha ya kumlenga ili kumuua asiendelee kubweka kwani walihofia sauti yake ingewaamsha wakina Sajenti.
Wakwanza kushtuka usingizini alikuwa Mzee Mkwizu, akiwa kitandani alisikia kwa mbali Mbwa wake akilia huku Mvua kubwa ikinyesha. Aliamka kitandani na kuwasha tochi yake aliyokuwa kaiweka chini ya mto wa kitanda, kisha akachukua gobore lake, akatoka kwenda sebuleni.
Alipofika sebuleni alishtuka kuona mlango ukicheza cheza, ni kama kuna mtu alikuwa anataka kuvunja kitasa. Hapo akakoki gobore lake akimulika mlango. Mapigo ya moyo wake yalienda upesi mno, miguu na mikono yake ilianza kutetemeka. Muda huo Sajenti hana hili wala lile, kalala kwa starehe ungedhani dunia anaimiliki yeye. Asijue hatari inayowakabili.
Kitu pekee kilichowashinda ni ule mlango jinsi ulivyotengenezwa, pia ulikuwa ni mlango wa mbao ngumu ya mninga. Hivyo haikuwa rahisi kwao kuuvunja. Basi walichukua baruti ya kuvunjia wakaitega pale mlangoni, kisha wakasogea umbali wa mita kadhaa, wakati huo Mzee Mkwizu kasimama akiwa kajiandaa kumpiga yeyote atakayetangulia. Masikini, hakuwa na bahati. Mlango ulifumuliwa na baruti, Mzee Mkwizu alipigwa na kipande cha mbao kichwani akaanguka chini. Mshindo na sauti ya baruti ilimshutua Sajenti. Upesi akaamka akaichukua bastola yake.
Aliamka akiwa na kaptura, akachungulia sebuleni. Hapo macho yake hayakuamini, alimuona Babu yake akiwa kaanguka akiwa kashika tochi iliyokuwa inamulika mlangoni, alipagawa alipoona mlango umevunjwa. Hapo akajua kuna hatari kubwa inakuja. Akili yake ilimuonya, ikamuambia asifanye haraka kwenda kumuangalia Babu pale chini. Punde alishtuka kuona jitu kubwa lililovaa koti kubwa jeusi la mvua likiwa limenyeshewa likiingia kwenye ule mlango wa sebuleni. Jitu lile lilikuwa limebeba bunduki mkononi. Sajenti hakutaka kuwa na haraka kulipiga risasi, alisubiri aone kuwa lipo lenyewe ama lipo na wenzake. Punde akatokea mtu mwingine, huyu alikuwa mfupi mfupi, naye alikuwa kavaa koti la Mvua. Yule mtu wa pili aliingia akaichukua ile tochi na kuanza kumulika mulika. Kosa! Alifanya kosa ambalo hatajisamehe daima. Wote wawili walijikuta wakianguka chini baada ya Sajenti kuwapiga risasi. Jambo hilo lilifanya wale maadui wanne waliobakia nje kupiga risasi bila mpangilio. Sajenti akajua kuna maadui wengine lakini hakujua hesabu yao.
Sajenti alimuona Mzee Mkwizu akizinduka kichwani akiwa na jeraha lilokuwa linavuja damu, Mzee Mkwizu kabla hajafanya chochote wale watu walimtandika risasi tatu za kifuani wakiwa wapo kwa nje.
Sajenti aliumia sana. Alikumbuka maneno ya Babu yake siku alipofika aliyomwambia kuwa amekuja na mkosi. Sajenti roho yake ilizimia kwa maumivu. Alisikitika kuona maneno ya Babu yakitimia.
Akatoka kwenye ile kona akaenda kwa kunyata mpaka karibu na mlango wa sebuleni, akalala chini alafu akachungulia kwa nje, hapo akawaona watu watatu wakiwa wamesimama wakitazama ndani wakiwa wamebeba bunduki zao. Alichukua bastola yake kisha kwa upesi alijiviringa kama gunzi la mhindi na kuwapiga kwa mpigo, wote watatu wakadondoka chini. Awali niliwaambia kuwa hakuna mchezo anaoupenda na kuuweza Sajenti Warioba kama mchezo wa kutupiana risasi. Sajenti alikuwa na shabaha, hakuwahi kukosa pale atakapo kulenga mtu. Jeshini walimfahamu kama mkono wa Shabaha. Akipewa risasi kumi auwe watu kumi basi tambua kuwa kila risasi itaondoka na mtu mmoja kama alivyoagizwa. Sasa kulikuwa kimya kabisa, Sajenti akajua amemaliza kazi. Sajenti alisimama akaenda kwa Babu yake, alimkuta tayari ameshakufa. Alilia kama mtoto mdogo, alijiona yeye ndio chanzo cha kifo cha Babu yake. Kama si yeye kuja hapo basi Mzee Mkwizu asingekufa.
“Kweli mimi ni Mkosi, Babu mimi ni mkosi. Tazama sasa maneno yako yanatimia. Bora ningekuja kukuzika lakini sio kusababisha kifo chako. Babu yangu nisamehe” Sajenti alilalamika mwenyewe akilia kama mwendawazimu huku Mvua ikiendelea kunyesha.
Punde akiwa kapiga magoti akilia aliduwaa baada ya kisogo chake kuguswa na kitu kigumu, ndio alikuwa kawekewa bastola kisogoni na yule mtu wa sita, masikini Sajenti alijua amewamaliza wale watu wabaya lakini kumbe alikuwa amembakiza mmoja. Huyo ndiye sasa aliyemuweka chini ya ulinzi.
“Mikono juu, utulie hivyo hivyo, vinginevyo leo hii utamfuata Babu yako kuzimu” Yule Mtu aliongea kauli ya kibabe sana sauti yake ikikaribia sauti ya jinamizi mkatili asiye na chembe ya huruma.
Sajenti aliinua mikono yake juu bila ya ubishi, sauti ile aliielewa sana. Hakutaka kuleta ubishi ambao alijua ungegharimu maisha yake. Ghafla Mbwa alitokea akamvamia Yule mtu kwa nyuma na kuanza kumshambulia yuule jambazi akiwa kaanguka chini. Sajenti akaona ile ndio nafasi ya kujinasua, alinyanyuka chapuchapu kama umeme lakini alichelewa, kabla hajafanya chochote Yule mtu aliachia risasi ikampiga na kumuua Yule Mbwa, ndiye Kajiru. Sajenti hasira zilimpanda kama mbogo wa Mikumi aliyejeruhiwa, alimpiga Yule mtu risasi mfululizo hata alipopoteza maisha Sajenti aliendelea kumpiga risasi bila kuacha, Risasi ziliisha kwenye bastola ikawa ndio mwisho wa Sajenti kumpiga risasi.
Usiku huohuo Sajenti alitoka nje akaenda kuchimba kaburi la Babu yake karibu na Zizi la ng’ombe huku manyunyu ya mvua yakimdondokea. Mwanga wa jua la asubuhi ulimkuta akiendelea kuchimba, ng’ombe, mbuzi na kondoo walimtazama Sajenti wakiwa na nyuso zenye simanzi. Leo hii Bwana wao, Mzee Mkwizu amekufa kwa kuuawa na watu wabaya wasio na huruma. Ndama mmoja mweupe alikuja karibu na kaburi akawa anamtazama Sajenti akiwa ndani ya kaburi akichimba kaburi. Sajenti alimuona yule ndama, hapo akajikuta akipatwa na huzuni.
Alimaliza kuchimba Kaburi, hapo akarudi ndani jua lilikuwa limeshapanda juu kabisa. Maiti Saba ya watu pamoja na mzoga wa Mbwa, ndiye kajiru zilikuwa zimelala pale chini. Aliubeba mwili wa Babu yake kisha akaenda kuusafisha vizuri bafuni. Alafu akaenda ndani akachagua nguo nzuri aliyoiona itamfaa Marehemu Babu yake kumzikia. Aliona Suti nzuri mno ya rangi nyeusi, akamvalisha Babu yake. Kisha akaendelea kukagua lile sanduku la nguo, hapo akaona kanzu nzuri ya zambarau na kikofia cha kichifu. Akaivaa ile kanzu na kile kikofia.
Akaubeba ule mwili wa Babu yake, kisha akarudi kuuchukua mzoga wa Kajiru, baadaye akauingiza mwili wa Babu yake kaburini na mzoga wa Mbwa wake. Alipoiingiza kaburini hiyo miili, akaenda kufungulia ng’ombe. Mbuzi na kondooo. Hao ndio walikuwa mashuhuda wa mazishi ya Mzee Mkwizu Mifugo yote ililizunguka kaburi. Kisha Sajenti akiwa kavaa kanzu ya zambarau na kofia nyekundu akiwa kama Kuhani anayeendesha maziko hayo. Sajenti aliomba dua ya kumuombea Babu yake, kisha akamzika Babu yake pamoja na Mbwa wake.
Hivyo ndivyo shujaa Mzee Mkwizu alivyozikwa kwa heshima na Sajenti pamoja na mifugo yake. Akaliliwa na Mjukuu wake na mifugo yake kwa siku tatu. Sajenti akachukua maziwa aliyoyakamua kwenye ng’ombe na mbuzi na kuyamwagia kwenye kaburi lake. Kisha akachukua mafuta ya mkia wa moja ya kondoo zake akayamwagia katika kaburi lake. Mwisho akachinja kuku na kuchoma manyoya yake katika kaburi lake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa, na habari zake Sajenti akazichukua ili kuziandika kama alivyozikuta katika sanduku la kuhifadhia historia ya maisha ya Mzee Mkwizu.
ITAENDELEA
Usisahua ku-like na kushare.
Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.
Kitabu Tsh 15,000
0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel.
0758216209
M-PESA
Robert Heriel