Ni tafsiri ipi ya lugha inayokupa uhakika kwamba Eloi ni Allah,,,pili kama Yesu Alisema Mungu wangu una uhakika kwamba huyo Mungu ni Allah Subhana wataalah.???? Nataka uelewe kwamba uislam Una Mungu wake na Ukristo una Mungu wake.
SHK MUHSIN
anaendelea.....
A COMFORTER
Hebu sasa natulichungue hili neno lililofasiriwa Msaidizi katika Bibilia ya Kiswahili, na ambalo limeitwa "Comforter" yaani Mliwazi katika Biblia ya Kiingereza ya zamani ya King James, na likaitwa "Counsellor", yaani Mshauri katika Biblia ya Kiingereza ya Revised Standard Version, na likaitwa "Helper" yaani Msaidizi katika Biblia za Kiingereza mpya mpya kama New World Translation na Good News Bible, na "Mu'azzi", yaani Mliwazi katika Biblia ya Kiarabu ya Darul Kitabul Muqaddas ya Cairo.
Taabu inayotupata katika kuisoma Biblia ni kuwa asli ya maandiko yote yamepotea. Tumebakiwa na nakala za tafsiri tu. Na hata tukipata kwa mfano Injili ya Yohana iliyoandikwa kwa lugha ilioandikwa mwanzo, nayo ni Kigiriki, hatuna ushahidi wo wote kuwa ndivyo ilivyoandikwa hapo mwanzo. Injili hii iliandikwa mwanzo wake kiasi miaka mia baada ya Yesu. Lakini nakala zilio kongwe kabisa zinazopatikana si chini kuliko miaka mia mbili baada ya kuandikwa kwake.
Hali kadhaalika maneno aliyoyasema Yesu tunayapata kwa tafsiri tu, kwani Yesu hakusema Kigiriki wala Kilatini, bali lugha ya kawaida Palastina wakati ule ilikuwa ni Kiaramiya na lugha yao ya dini ni Kiebrania. Zote mbili hizo zina asli moja na Kiarabu. Injili ya Yohana ndio hiyo iliyotaja hiyo bishara ya Yesu kuwa atakuja huyo aitwae Msaidizi. Katika utangulizi wa nakla ya Biblia ya Revised Standard Version imeelezwa kuwa hata hiyo matini ya Kigiriki ilioko "imeharibiwa na makosa yaliyojumlika kwa kukosoea kosea kwa walionukulu muda wa karne kumi na nne." Wataalamu wa Biblia wakubwa kama Rudolf Bultmann (Mprotestanti) na Father John Lawrence Mackenzie (Mkatoliki) wanakubali kuwa sehemu nyengine za Injili si kweli kihistoria, na ya kwamba maneno fulani ya Yesu kwa hakika yamebuniwa na Kanisa la kale. Ye yote asomae maandishi ya wataalamu wa Kikristo wenyewe, bali hata mwenye kusoma hizi hizi tafsiri za Biblia mbili tatu ataona vipi maneno yanavyogeuzwa, yanavyoongezwa, na yanavyopunguzwa, hata kugeuza kabisa makusudio.Encyclopaedia Brittanica (nuskha ya 15) baada ya kueleza hayo imesema: "Ushahidi kuwa hayo hakika yametokea ni mwingi na wa namna mbali mbali." Qur'ani inasema:
Na kuna baadhi yao wanaopindua ndimi zao kwa Kitabu ili mpate kuyafikiri hayo kuwa ni ya Kitabu, wala si ya Kitabu, na wanasema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu; na hali hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu, na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na hali wanajua.
(Qur'ani) Al Imran 3.78
Je, ni neno gani hilo lilioandikwa Kigiriki kuwa Yesu kalitumia hata wengine wakalifasiri Mliwazi, wengine Mshauri, na wengine Msaidizi, kuwa ndiye wa kutarajiwa kuja? Nakla kongwe kabisa iliyopo ya hiyo Injili imetumia neno la KigirikiParakletos ndilo wanalolifasiri Msaidizi katika Injili ya Kiswahili. Katika Kamusi la Kigiriki neno Parakletos linafasiriwa kuwa ni "mwenye kuitwa kusaidia, mtetezi, mwombezi." Baada ya kuzingatia hayo tuliyoyasema hapo juu vipi yalivyogeuzwa geuzwa maneno, basi si jambo la kustaajabisha ikiwa neno hili Parakletos nalo wamelipotoa waandishi na wanaonukulu kwa karne na karne zilizopita, kama ilivyosemwa katika utangulizi wa Biblia ya Kiingereza ya Standard Revised Version. Tunajua vipi Wazungu walivyolipotosha jina la Muhammad, na kuliandika "Mahomet".
Hali kadhaalika neno la Kigiriki laPeriklitos ni wepesi kulipotoa na kuliandika Parakletos. Kwa dhaahiri khitilafu ni ndogo, lakini kwa hakika neno Periklitosmaana yake ni Msifiwa, ambalo kwa Kiarabu ndio khasa Muhammad au Ahmad au Mahmuud. Jambo la ajabu ni kuwa tangu wakati wa Yesu hapakutokea Mwaarabu mwenye jina hilo ila huyo Muhammad bin Abdullah, ambaye alipewa jina hilo na babu yake tangu kuzaliwa kwake bila ya kujua huyo mzee kuwa mjukuu wake atakuja kuwa Nabii ambaye amebashiriwa na Yesu. Na huyo babu hakuwa Mkristo bali alikuwa akifuata mila ya kishirikina na wala hakuijua Taurati wala Injili. Na wala hakutokea Giriki mwenye jina la Periklitos.
Ni makosa kusema kuwa huyo Periklitos (Msifiwa) aliyefasiriwa kwa kukosea Msaidizi, ni Roho Mtakatifu, ambaye Wakristo wanasema ni nafsi ya Mungu. Ushahidi wa makosa hayo umo humo humo katika Injili ya Yohana. Kama huyo Msaidizi ni Roho Mtakatifu yawaje basi Yesu kusema "yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo (Periklitos) hatakuja kwenu." Roho Mtakatifu twaambiwa ni Mungu wa milele. Je, kwani Mungu hatokuwepo maadamu Yesu yupo? Je, yeye Yesu na Manabii wote waliomtangulia na watakatifu wengine hawakuteremkiwa na Roho Mtakatifu? Hayo yamo katika Agano Jipya na Agano la Kale pia.
Huyo Periklitos (Ahmad au Muhammad) "atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu." Na ndio hivyo ilikuwa ni Muhammad aliyedhihirisha ukweli wote wa Mwenyezi Mungu mmoja, asiyezaa wala asiyezaliwa, na akawaokoa umma mzima wasimshirikishe Mwenyezi Mungu na kitu cho chote, wala mtu ye yote. Ni yeye ndiye aliyewarejesha Wakristo kwenye mafunzo ya Yesu na Musa kwamba Mwenyezi Mungu hana utatu, bali Mungu wao ni Mungu mmoja kama alivyofunza Yesu (Tazama Marko 12.29), na kama alivyoamrishwa Musa (Tazama Kutoka 20.3-4). Ni yeye ndiye aliyemtoa Yesu katika matusi ya Mayahudi walipomshutumu kuwa ni mdanganyifu, na matusi ya wanaojiita Wakristo kumzulia kuwa kafa kifo cha laana msalabani, na kuwa yeye ni mungu wa bandia kama walivyo miungu ya washirikina makafiri. Kweli yote imehakikishwa na huyo Periklitos, Muhammad, Roho wa Kweli. Huyo ambaye "hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena" hawezi kuwa Mungu,bali huyo ni Mtume wa Mungu, Mtume ambaye ametuachia Kitabu kizima ambacho kila neno liliomo humo ni neno alilolisikia kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe. Hicho ni Kitabu pekee duniani, nacho ni Qur'ani.
Na ni Mwenyezi Mungu katika Qur'ani ndiye aliyesema:
Na aliposema Isa bin Mariam: enyi wana wa Israili! Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kumbashiria Mtume atakayefika baada yangu, jina lake litakuwa Ahmad.
(Qur'ani) As Saff 61.6
Injili ya Mtakatifu Barnaba ambayo ilipigwa marfuku kwa amri ya Gelasius katika mwaka 496 B.K., karne nzima kabla ya kuja Nabii Muhammad s.a.w. inaeleza:
Tena Yesu akasema: Kwa maneno yenu siliwaziki, kwa sababu mnapotaraji mwangaza patakuja kiza; lakini maliwaza yangu ni kwa kuja Mtume ambaye ataivunja kila fikra mbaya juu yangu mimi, na dini yake itaenea na kutanda ulimwengu mzima, kwani hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyomuahidi Ibrahimu baba yetu. Na linalonipa maliwaza ni kuwa dini yake haitakuwa na ukomo, kwani itahifadhiwa na Mwenyezi Mungu. Kuhani akajibu: Baada ya kuja huyo Mtume wa Mungu watakuja manabii wengine? Yesu akajibu: Hawatakuja Manabii wa kweli baada yake waliotumwa na Mwenyezi Mungu, lakini watakuja manabii wengi wa uwongo, na hayo ndiyo masikitiko yangu. Kwani shetani atawanyanyua kwa hukumu ya haki ya Mwenyezi Mungu, na atawaficha chini ya udanganyifu wa injili yangu....Tena akasema kuhani: Huyo Masihi ataitwaje, na ishara gani itaonyesha kuja kwake? Yesu akajibu: Jina la Masihi ni Msifiwa, kwani Mwenyezi Mungu mwenyewe alimpa jina hilo alipoiumba roho yake na akaiweka katika utukufu wa mbinguni.
Injili ya Barnaba Sura 97
Imehaririwa na kufasiriwa kutoka Muswadda uliopo katika Maktaba ya Vienna, Austria, na Lonsdal na Laura, Oxford. Hii Injili ya Barnaba ndiyo inaaminiwa kuwa ni Injili ya pekee iliyoandikwa na mwanafunzi wake mwenyewe Yesu. Zilizobaki zimeandikwa na watu wengine baada yao hao wanafunzi kwisha kufa, lakini yakatumiwa tu majina ya hao wanafunzi. Injili hii ilikuwa inakubaliwa kuwa ni sahihi na Wakristo wa kwanza, na ikitumiwa katika kanisa la Alexandria mpaka mwaka 325 B.K. Mwaka huo ndipo Baraza la Nikaia likaamua kuzikubali hizi Injili nne za Mathayo, Marko, Luka na Yohana ziingizwe katika Biblia kuwa ni maandiko matakatifu, na likapiga marfuku Injili nyenginezo, na mojawapo ni hii ya Barnaba, kuwa ati si sahihi. Vitabu hivyo vilivyokataliwa viliitwa Apokrifa, yaani vinavyofichwa, na hapo zamani ye yote aliyeonakana navyo aliuwawa.
Injili iliyokubaliwa na Baraza kuwa ni sahihi, na iliyomo katika Biblia, Injili ya Mathayo, nayo inatueleza kuwa Yesu alibashiri kutokea kwa Muhammad, ambaye ni katika uzao wa Ismaili, anayefananishwa na jiwe liliokataliwa na wajenzi. Pia Yesu alibashiri kuinuka kwa Umma wa Kiislamu utakaopewa Ufalme wa Mungu, nayo yote hayo yakatimia:
Yesu akwaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko,Jiwe walilolikataa waashi,Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni;Neno hili limetoka kwa Bwana,Nalo ni ajabu machoni petu?Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.
Mathayo 21.42-44
Yesu kwa maneno hayo tuliyoyanukulu anawaambia Waisraili:
"Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake." Taifa la Israili halitazaa matunda tena. Yesu alililaani. Twasoma katika sura hii hii ya 21 ya Mathayo:
Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara.
Mathayo 21.18-19
Wataalamu wa Biblia wanakubaliana kuwa huo mtini ulionyauka, usioleta matunda yake, ni taifa la Israili. Na hatuna haja kutafuta maoni ya mtaalamu ye yote kutufasiria kuwa taifa lizaalo matunda lenye kubarikiwa ni taifa la Ismaili liliomzaa Mtume Muhammad. Biblia yenyewe inatwambia kuwa Mwenyezi Mungu alimwambia Ibrahim:
Na kwa khabari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu.
Mwanzo 17.20
Kwa hivyo tunaweza kusema bila ya wasiwasi kuwa Yesu alikusudia kuwambia Mayahudi: "Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu kwa kuwa nyinyi mmeacha amri za Mwenyezi Mungu alizozileta Musa na nilizothibitisha mimi, na ufalme huo watapewa taifa la Muhammad, mwana wa Ismaili, taifa liliobarikiwa na Mwenyezi Mungu, lenye kufuata maamrisho yake kama alivyofundisha Ibrahim na Musa na mimi na Manabii wote waliokuja kabla yangu mimi."
Kama alivyobashiriwa Nabii Ibrahim kuwa katika uzao wake kwa mwanawe Ismail utatokea umma uliobarikiwa wenye kuleta matunda, kadhaalika alibashiriwa Nabii Musa na Mwenyezi Mungu kwamba katika ndugu zao Wana wa Israili, yaani Wana wa Ismaili, atatokea Nabii, naye ni Nabii Muhammad, ambaye Mwenyezi Mungu anawataka viumbe wote wamuitikie na wamfuate. Na ye yote "asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake." Kwa ukamilifu Mwenyezi Mungu alimwambia Nabii Musa haya:
Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao (yaani Wana wa Israeli) mfano wako wewe (Musa), nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake. Lakini nabii atakayenena nena kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena kwa jina la miungu mingine, nabii yule atakufa. Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena Bwana? Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope.
Kumbukumbu la Torati 18.19-22
Zingatia vyema: maneno hayo anaambiwa Nabii Musa a.s., naye ni Nabii wa Wana wa Israili. Nabii anayebashiriwa hatotoka miongoni mwao Wana wa Israili, bali miongoni mwa ndugu zao, yaani Wana wa Ismaili. Lakini Nabii huyo hatokuwa kwa Wana wa Ismaili tu, bali hata wao Waisraili pia, kwani Mwenyezi Mungu anawaambia: "Nitawaondokeshea", yaani wao pia Wana wa Israili. Tena Mwenyezi Mungu anasema: "Mtu asiyesikiliza mananeo yangu atakayosema yule (Nabii) kwa jina langu, nitalitaka kwake." Ni dhaahiri kuwa yawapasa watu wote, mataifa yote, wampokee huyo Nabii atakyetokea katika ukoo wa Ismaili.
Mungu anasema: "Nitatia maneno yangu kinywani mwake." Kitabu gani ambacho kinadai, na madai yenyewe yakawa ya kweli, kuwa ni maneno khasa ya Mwenyezi Mungu isipokuwa Qur'ani? Muhammad alikuwa ni mkalimani wa Mwenyezi Mungu, akiyatamka tu yale yaliyokuwa yakifunuliwa kwake; na waandishi waliokuwepo miongoni mwa wafuasi wake wakiandika na wengine kuhifadhi kwa moyo maneno ya Mwenyezi Mungu wakati ule ule yeye Nabii Muhammad alipokuwa akiyatamka. Mwenyezi Mungu anamuamrisha katika Qur'ani:
Sema: Mimi si kizushi katika Mitume. Wala sijui nitakavyofanywa mimi wala mtakavyofanywa nyinyi. Sifuati ila yaliyofunuliwa kwangu; na mimi si cho chote ila ni Mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.
(Qur'ani) Al Ahqaf 46.9
Mwenyezi Mungu mwenyewe anawakabili kwa majadiliano wenye kutia shaka kuwa hii Qur'ani ni maneno yake au la:
Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomtermeshia Mja wetu, basi leteni sura moja katika mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli. Na mkitofanya - na hakika hamtafanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe ulioandaliwa kwa wakanushao.
(Qur'ani) Al Baqarah 2.23-24
Kwa muda wa miaka 1400 hapajatokea mwanaadamu wala jini aliyeweza kujibu hoja hiyo. Qur'ani ndio muujiza wa kudumu milele. Huu si muujiza wa kusimuliwa ya kwamba ulitokea, na watu wakazozana ulitokea kweli au haukutokea. Huu ni muujiza uliobaki na utabaki ukionekana tangu siku ulipoteremka mpaka leo na mpaka milele. Unaweza kuusoma leo, kesho, kesho kutwa na mtondogoo na daima dawamu, na ukuathiri kwa ufasihi wake uliokuwa hauna mfano, utamu wa maneno yake, ukakuongoza kwa ubora wa mafunzo yake, ukakusaidia kukabiliana na ulimwengu wako, ukaondoa matatizo yako ya kidunia na ya kiroho, ukatengeneza dunia yako na akhera yako.
Yamkinika kuwa mimi nikatuhumiwa kuwa imani yangu inanipelekea kuisifu hivi Qur'ani, lakini hebu natuiachie kalamu ya Muingereza Mkristo, Edward Gibbon, ambaye ni mtaalamu mkubwa wa historia, na bingwa wa uandishi, tuiache kalamu yake isiyo na khofu wala mapendeleo ituhukumie. Gibbon ameandika:
"Hapana kitabu duniani ambacho ndani yake Mwenyezi Mungu ameelezwa kwa utakatifu zaidi, kwa ubora zaidi, kwa usafi zaidi, kwa uzuri zaidi, kwa ukamilifu zaidi, kwa utukufu zaidi, na chenye kustahili zaidi Ungu kuliko Mungu huyu aliyekuwa Muhammad akimuabudu. Ruwaza hii haiwezi kutengenezwa kuliko ilivyo; sifa moja tu ikiondolewa italeta nuksani katika ukamilifu wake, na haiwezekani hata moja kuongezwa bila ya kuonekana kuwa imezidi na haina maana. Ni jinsi hiyo alivyo Mungu wa Muhammad kama alivyoelezwa katika Qur'ani. Kwa ujasiri kweli amepiga chapa isiyofutika kabisa juu ya sahifa za historia wazo la imani safi kabisa ya Mwenyezi Mungu Mmoja wa pekee; na kuliendea wazo hilo mwanaadamu mwenye akili, akitaka asitake, hawezi ila aliendee kwa yakini, hata ingawa pole pole."
Basi ni kitabu hichi ndicho kilichowafanya Waislamu wa zamani wa Vyuo vyao Vikuu vya Cordova (katika Uspania), Cairo, Damascus na Baghdad wakawa ndio waanzishi wa ilimu za Algebra, Alkimya (chemistry), Falaki (Astronomy) na utibabu wa kisasa. Peke yake ni jambo la kustaajabisha kuwa mtu ambaye mwenyewe alikuwa hajui kusoma wala kuandika, katika kaumu ya wajinga, amri ya kwanza iliyofunuliwa kwake - si kusali,wala kutoa zaka, wala kutazama wagonjwa na wazee, bali hata si kuamini Mungu mmoja, bali:
Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliyeumba, amemuumba mwanaadamu kwa tone la damu iliyotundikwa. Soma! na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote, ambaye amefundisha kwa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu yale aliyokuwa hayajui.
(Qur'ani) Al 'Alaq 96.1-5
Umma uliokuwa mjinga, mabedui wa jangwani - hali yao haikukhitalifiana sana na kabila yo yote ya Kiafrika yenye kutangatanga na mifugo yao, kama Wamasai, ambao ndani yake waliokuwa wakijua kusoma na kuandika wakihisabika kwa vidole vya mkono mmoja - Umma kama huo ukaamrishwa la mwanzo la kulifanya ni kusoma, na Mwenyezi Mungu mwenye kutoa amri hiyo hakutafuta sifa kubwa kuliko Aliyefundisha kwa kalamu, Aliyemfundisha mwanaadamu yale aliyokuwa hayajui. Kama huu si muujiza upi mwenginewe? Hii ni Ishara kuwa enzi mpya imekuja, enzi ya kusoma, enzi ya kalamu, enzi ya kutumia akili. Enzi za kugeuza fimbo kuwa nyoka, kufufua walioonekana kama wamekufa, kugeuza maji yakawa mvinyo na mazingaombwe kama hayo zimepita. Hayo labda yafanywe juu ya jukwaa katika majumba ya tamasha kwa kuwastarehesha vijana. Lakini katika mambo yaliyo na uzito kweli yahitaji masomo, kujifunza, na kufundisha kwa kalamu. Huu wakati wa muujiza wa hichi Kitabu kilichoandikwa kwa kalamu na kinachoweza kusomwa milele, na kila mwenye tatizo lake anaweza kulitatua kwa kusoma na kuzingatia vilivyo yaliyoandikwa humu na mwenyewe Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanaadamu kutokana na tone la damu, bali kutokana na mchanga khasa. Zama za muujiza wa kutumia akili na masomo umefika.
Bila ya Qur'ani ilimu zote za Warumi, za Magiriki, za Waajemi, za India, za China, za Misri, na za Iraq, zingelipotea kabisa, badala ya kuwa zimehifadhiwa, na zikazidi kukuzwa na kuendelezwa na zikakabidhiwa ulimwengu huu wa leo.
Kila tunapoona neema ya uvumbuzi wo wote ambao tukafikiri kuwa ndio wa kisasa na umetokana na Wazungu yafaa tushukuru kuwa lau kwamba ingelikuwa Qur'ani haikuamsha ulimwengu, na wakazindukana Waislamu wakatuhifadhia yaliyopita na wakayaongeza mengi sana yao wenyewe tunsingezipata hizi neema za leo, ikiwa ni katika matibabu, ikiwa ni katika vipando, ikiwa katika makaazi, ikiwa katika vyakula, ikiwa katika usafiri, na ikiwa katika fanni zo zote na ilimu zo zote za sayansi. Kitabu hichi ndicho kilichowageuza waliokuwa wakiabudu jua na mwezi na nyota na mawe na mito na miti na milima, kikawaambia kuwa vyote hivyo na vyenginevyo vyote vimeumbwa ili vimtumikie mwanaadamu.
Ni Kitabu hichi kilichokomboa akili za watu zichungue mpaka katika sehemu ambazo watu kabla yake hata hawajaziotea:
Enyi jamii ya majini na watu! Mkiweza kupenye kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni!
(Qur'ani) Ar Rahman 55.33
Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama, na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanaozingatia.
(Qur'ani) Al Baqarah 2.164
Vifungu hivi viwili tu tulivyovinukulu hapa vyatosha kukupa mawazo vipi Qur'ani ilizindua wanaadamu waliolala washughulikie ilimu, na uchunguzi, na utafiti na uvumbuzi. Uropa iliolala katika Karne za Giza (Dark Ages) ilizinduliwa na muamko wa Kiislamu katika kila ilimu. Katika vifungu hivi tunaona mahimizo na ishara ya kuanzisha ilimu za anga (Space Sciences), ilimu za matabaka ya ardhi na uvumbuzi wa maadini (Geology na Minerology), Jiografia, ilimu ya unahodha (Navigation), ilimu ya hali za hewa (Meteriology), na ilimu za zaraa (ukulima). Huu ni mfano mdogo tu; ni kama tone katika bahari. Mwenye kuisoma Qur'ani kwa moyo safi na akili kunjufu atagundua ndani yake uwongofu ambao haupati po pote kwengineko, atapata ilimu ambazo hazipati po pote, na atapata ukunjufu wa moyo ambao hawezi kuupata penginepo.
Katika bishara aliyopewa Musa na Mwenyezi Mungu juu ya kuja Nabii Muhammad aliambiwa: "Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii usimwogope."
Ikiwa Mtume Muhammad alikuwa na sifa yo yote ambayo ilizagaa zaidi kuliko nyengine basi ni hiyo sifa ya kubashiri jambo nalo likatokea kama alivyosema. Hayo yajuulikana kikweli kwa kuwa maisha yake, kinyume na waongozi wa dini zilizotangulia, yalikuwa katika zama ambazo zinajuulikana vyema na wanachuoni wa taarikh (historia). Yeye si mtu wa hadithini, lakini ni mtu wa hakika, anayejuulikana vilivyo, mtu aliyekuwa akikatibiana na kupambana na wakuu wa serikali na dola zilizokuwapo zama zake. Akikatibiana na Mfalme wa Uajemi, na Mfalme wa Rumi, na Wakuu wa Misri na Uhabeshi, na Wakuu wengineo walioko Arabuni na nje ya Arabuni. Kwa kutimia kauli zake, kama tulivyokwisha toa mifano kadhaa wa kadhaa, ndio akaitwa As saadiq, Msema Kweli, Al Amin, Muaminifu.
Bishara aliyopewa Nabii Musa a.s. inasema: "Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe." Hakuja Nabii baada ya Musa aliyefanana naye kama alivyofanana naye Nabii Muhammad. Musa na Muhammad walikuwa wakhubiri wa dini kwa mambo ya kiroho, na vile vile wakawa ni waongozi katika mambo ya dunia. Walikuwa wamekusanya dini na siasa, Unabii na utawala, uwalii na uamiri jeshi. Walikuwa ni maraisi wa kaumu zao, walikuwa mahakimu, walikuwa wapigania uhuru licha ya kuwa wanasiasa. Nabii Musa alipambana na Firauni na kaumu yake, Muhammad alipambana na Abu Jahli na kaumu yake. Musa ilimlazimu akimbie ahame Misri alikozaliwa ende Palastina. Muhammad pia ilimlazimu aongoze watu wake kukimbia adhabu za Makureshi Makka alikozaliwa ende Madina. Nabii Musa kapokea sharia ya Mungu katika Taurati, na Nabii Muhammad kapokea sharia ya Mungu katika Qur'ani. Wote wawili walioa wakawa na wake na wakazaa. Wote wawili walikufa kitandani ulipotimia mwisho wa maisha yao.
Mwenyezi Mungu alimwambia Nabii Musa: "Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa."
"Nabii yule atakufa." Nini maana ya haya? Kufa ni faradhi kwa kila kilio hai. Maana yake atakufa siku si zake, yaani atakufa ghafla naye kijana, au atauliwa. Nabii Muhammad alikufa na umri wake miaka 63, kiasi ya umri wa utuuzima wakati ule na mpaka hivi sasa. Juu ya misukosuko isiyokadirika, na vita alivyopambana navyo, na majaribio ya kumuua aliyofanyiwa katika maisha yake, Mwenyezi Mungu alimsalimu mpaka akafika wakati wake baada ya kutimiza na kukamilisha ujmbe wake aliyopewa, na akafa kitandani, na huku kazungukwa na ahali zake.
Yaliyosemwa katika Taurati pia yamesemwa katika Qur'ani:
Na kama (Mtume) angelizua juu yetu baadhi ya maneno tu bila shaka tungelimshika kwa mkono wa kulia - kisha kwa hakika tungelimkata mshipa mkubwa wa moyo; na hapana ye yote katika nyinyi angeweza kutuzuia naye.
(Qur'ani) Al Haqqah 69.44-47
Ama wanavyodai wengine kuwa bishara hii yamkhusu Yesu wamekosea sana. Yesu hakufanana na Musa ila katika kuwa ni Nabii na kuwa ni Mwana wa Israili. Kwa unabii wale wanaomdaia ungu Yesu wanamkatalia kuwa ni Nabii. Ikiwa Yesu kafanana na Musa, basi si Mwana wa Mungu wala si Mungu. Kwa hivyo wanajipinga wenyewe. Bishara inasema wazi kuwa huyo Nabii hatakuwa katika Wana wa Israili, bali miongoni mwa ndugu zao, nao ni Wana wa Ismaili. Yesu ni Muisraili. Kwa hoja hii pia Yesu siye aliyebashiriwa hapa. Nabii huyo aliyebashiriwa kama ni wa kweli hauliwi, wala hafi kijana. Yesu, kama wanavyodai Mayahudi na wakaamini Wakristo, aliuwawa msalabani, tena yungali kijana. Ikiwa bishara hii wanataka kumuambatisha nayo yeye Yesu, basi itakuwa wanamtuhumu kuwa Yesu ni nabii wa uwongo "aliyenena neno kwa kujikinai kwa jina la Mungu, ambalo hakuagizwa kulinena." Mwenyezi Mungu apishe mbali. Zaidi ya hayo Nabii Isa kinyume na Nabii Musa na Nabii Muhammad (rehema na amani ya Mungu iwashukie wote) hakuja na sharia yo yote. Yeye alifuata ile ile sharia ya Musa iliomo katika Taurati, na mwenyewe kasema yeye hakuja ila kutimiza tu. Wala yeye hakuongoza watu katika mambo ya kilimwengu, bali alimwachia Kaisari ulimwengu na yeye kashughulikia mambo ya akhera, ufalme wa mbinguni.
Miezi mitatu tu kabla ya kifo chake Mtume Muhammad s.a.w. aliyataja maneno ya Mwenyezi Mungu aliyoteremshiwa:
Leo waliokufuru wamekata tamaa katika Dini yenu, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.
(Qur'ani) Al Maida 5.3
Miaka mia sita kabla ya haya Yesu naye alisema: "Chakula changu ni kufanya mapenzi ya yeye aliyenituma na kutimiza kazi yake."
Wote wawili wamekutana kwenye kutenda apendayo Yeye aliyewatuma, na huo ndio Utume, na huo ndio Unabii, na huo ndio Uislamu. Kutenda mapenzi ya Mwenyezi Mungu ndio waajibu wa binaadamu, na katika hayo ndio hupatikana wema, na katika hayo ndio kuhisabiwa haki katika maisha haya na maisha ya milele ya baadaye. Huko ni kufuata mwenendo wa maumbile aliyowaumbia Mwenyezi Mungu wanaadamu wote kama mwenyewe asemavyo:
Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la mwenyewe Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu; hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa, walakini watu wengi hawajui.
(Qur'ani) Ar Rum 30.30