KWA upande wa jamii ndio wateja wakubwa wa wasanii wa muziki na hata wale wa filamu, kwamba kama hawatanunua chochote ambacho kinatoka kwao au kuingia katika maonyesho ya wasanii hao basi sidhani kama kuna mwanamuziki au msanii ataendelea kufanya kazi hiyo.
Hataweza kuendelea kwa kuwa hatapata fedha, iko wazi kwamba kwa kipindi hiki muziki si sehemu ya ujiko tena kama ilivyokuwa miaka minne au mitano iliyopita badala yake ni kazi hasa inayoingiza fedha za kutosha kama mtu atakuwa makini.
Ni vigumu kwa msanii wa Tanzania kufanikiwa kuingiza mamilioni kama yale wale wa Ulaya, inawezekana ni athari za mipangilio ukilinganisha na hapa kwetu lakini hata hivyo inawezekana kabisa msanii akaingiza fedha za kutosha na akawa na kipato cha juu kama atakuwa na mpangilio na nidhamu ya juu ya kazi yake.
Kazi ya jamii ni kusikiliza, cha pili ni kuwaunga mkono wasanii kwa kununua kazi zao kama watakuwa ni watu ambao kweli wanaonyesha mapenzi ya dhati kwa wanamuziki wao na si ile tabia ya kuwaunga mkono kwa maneno mengi tu.
Jamii inaweza kuishia hapo lakini kuna mambo kadhaa wasanii yanaweza kubaki kwao kama majukumu ambayo wanatakiwa kuyafanya na kuhakikisha wanaongeza au kuboresha ubora wa kazi zao, kwanza ubora na baadaye kuwa makini katika masuala ya masoko.
Soko la muziki wa Tanzania si baya, hata kwa upande wa filamu za Kibongo unaweza kusema mambo si mabaya kwa mauzo kwa mujibu wa uchunguzi wangu lakini nakuhakikishia inawezekana kabisa wasanii huwa hawapati hata asilimia 25 ya mauzo ya kazi zao.
Tunajua mafanikio makubwa ya wasanii wetu ambavyo wamekuwa wakijiimba wao wenyewe kuwa gari aina ya Totoya Balloon na chumba kimoja Uswahilini inaonekana ni mafanikio makubwa sana kwa kuwa kabla msanii alikuwa akiishi nyumbani.
Tatizo kubwa lililonifanya niandike uchambuzi huu ni kuhusiana na malalamiko ya wasanii kuhusu suala la kulalama kuibiwa kazi zao na hao wasambazaji wanaojulikana kama Wahindi au Wadosi.
Utaona msanii amelalama jana, na leo akapeleka kazi zake pale pale halafu kesho tena akaanza kulalama anaibiwa. Jiulize, hawa watu ni wazima na nini wanafanya kujikomboa wenyewe kabla hata ya kutupa lawama hizo kwa serkali haiwasaidia. Nafikiri wanatakiwa kubadilika na kufanya kitu fulani kwa ajili yao na si kusubiri wafanyiwe.
Suala la mauzo na wasanii kuibiwa kazi zao ni sugu, wamekuwa wakilia kila kukicha na kilio chao ni wahindi, yaani wale wasambazaji wao ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
Lawama hizo si za jana au leo, kila ambaye amekuwa akizungumzia suala la usambazaji amezungumza suala la kuibiwa kazi zao zinapokuwa sokoni na imeelezwa Wahindi hao wamekuwa wakiwazunguka wasanii kimtindo na kuziuza kazi zao kwa wingi na wao kuwapa malipo kidogo tu kwa kisingizio kwamba haziuzi.
Mfano, msanii anapeleka kazi zake kwa msambazaji, wanaelewana zitauzwa kopi 10,000 na baada ya hapo wataingia mkataba wa kuuza nyingine kwa idadi hiyo. Lakini ambacho hutokea ni cha ajabu, msambazaji huyo hutengeneza kopi hata mara tatu ya hizo na kuziuza huku msanii akiendelea kuonyeshwa zile zake kwamba zimejaa kwa kuwa haziuzi.
Kuna wakati nilielezwa kuna wasanii wawili waliwahi kufanya uchunguzi na kuwanasa Wahindi hao kwenye mtego, lakini kitu cha ajabu wakakubali kulipwa fidia bila ya kuwachukulia hatua zaidi ili kufichua uovu wao. Leo lawama zinaendelea, serikali imetutupa, COSOTA haitujali na mambo mengi ambayo naweza kusema wakati mwingine hayana msingi.
Si vibaya nikisema, wasanii kutokuwa na ushirikiano ni chanzo cha Wahindi hao kufanya wanachotaka. Wanafanya wanavyotaka kwa kuwa wanajua wasanii na wanamuziki ni watu wasio na msimamo, wasiojiamini na wengi ni wanafiki kwa kuwa wamekuwa wa kwanza kupeleka taarifa kwa Wahindi hao kuhusu wenzao wanaolalamika au wanaopinga utaratibu huo mbovu.
Kama wasanii ndio wanakuwa wa kwanza kufikisha taarifa kwa Wahindi kwamba kuna wasanii fulani wanalalama na wanapanga kutoleta kazi zao kwenu. Sasa kuna haja gani wasanii hao hao kulalama wanaibiwa au serikali haiwasaidii. Ndio maana nawaita wanafiki!
Miaka zaidi ya nane leo lawama zinaendelea, mwisho wa hilo ni nini. je, wasanii wamewahi kutafakari angalau hata kuunda umoja wao ambao utakuwa na nguvu ya kutetea maslahi yao au kufanya mambo tofauti ili kuhakikisha jasho lao linawafaidisha wao. Najua hapana, kwa kuwa wanaamini kulalama na kuendelea kuupiga usingizi ndio ufumbuzi.
Kweli serikali inapaswa iwasaidie, lakini mnajua haki japo ni yako kuna wakati unalazimika kuisaka kwa nguvu zote. Ya kwenu mnaisaka, au mnasubiri serikali iwatafutie. Basi endeleeni kusubiri, mimi naamini itaendelea kuwa hivi ilivyo na mwisho mnaoumia wenyewe. Amkeni wajomba, kipindi cha usingizi kimepita!
Saleh Ally ni mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti. Email;
sulezetz@yahoo.com au
mwananchi@mwananchi.co.tz