Tusimbeze Rostam, hatikisi kiberiti
WIKI iliyopita nilikusanya magazeti yote ya wiki. Niliyasoma kijuu juu, ila nilipata fursa ya kuyapitia kwa ufasaha Jumapili nilipotoka kanisani.
Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wanahabari kwa kazi nzuri wanayofanya kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha jamii. Kimsingi nimekuta magazeti mengi kwa asilimia kubwa yakilifahamisha Taifa letu nini kinaendelea katika jamii.
Hata hivyo, wakati napitia gazeti la Raia Mwema, toleo namba 025, nilikutana na makala ndefu iliyochapishwa ukurasa wa nne na kuendelea ukurasa wa 22. Mwandishi wa makala hii ni Lula wa Ndali Mwananzela.
Makala hii ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho: Sipendi Rostam Aziz atikise kiberiti bungeni. Alichambua na kuhoji Rostam alitaka kuzungumza nini bungeni hadi nchi nzima ikatetemeka.
Katika moja ya aya zake anasema: Kitu gani hasa alitaka kusema kiasi kwamba kwa nyakati tofauti imeonekana kana kwamba ana jambo kubwa ambalo lingeweza kuleta vurugu bungeni?
Anafafanua kuwa Rostam alitaka kupeleka maelezo ya ufafanuzi kuhusiana na mkataba wa Kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Makala hiyo inasema Rostam angetumia muda huo kujisafisha, na si ajabu angefika na vielelezo vyake zikiwamo fomu za BRELA zenye kuonyesha wamiliki halisi wa Richmond, na hivyo kujisafisha yeye na washirika wake.
Ameandika mengi, anayojua aliyatoa wapi, lakini pengine ninukuu aya ifuatayo iliyonifanya kuandika makala hii: Hivi ni lini mara ya mwisho kwa Rostam kutoa mchango bungeni na alichangia nini? Ni kitu gani ambacho Rostam Aziz alisema bungeni katika mijadala ya bajeti au mingineyo ambayo inaweza kukumbukwa? Kama huko kote hajasema jambo lolote la kukukumbukwa, iweje leo tugwaye kama Taifa eti Rostam anataka kusema? Huku ni kujifanya duni kusiko na sababu.
Nimeamua kuijibu makala hii baada ya kuona tabia inayoibuka katika jamii yetu inastahili kukemewa vinginevyo itatupeleka pabaya. Namchukulia Rostam Aziz kama raia yeyote wa nchi hii mwenye haki ya msingi ya kujitetea anapokuwa ametuhumiwa.
Ni wiki iliyopita tu, tumeshuhudia Spika wa Bunge Samuel Sitta akijikanyaga juu ya uamuzi muhimu unaohusu kanuni za Bunge. Spika ni mhimili wa kanuni hizi, akijua kuwa jambo lililoamuliwa na Bunge haliwezi kujadiliwa katika muda wa miezi 12, katika mkutano wa 10, akasema Rostam angelazimika kuthibitisha tuhuma dhidi ya kamati ya Dk. Harrison Mwakyembe.
Rostam alikuwa akidai kutotendewa haki na kwamba kamati ilifanya kazi nje ya muda wake, hivyo aliamini kuwa ilifanya kazi kisiasa. Kama kweli wangekuwa na nia ya kumhoji wangeweza kumhoji, ila kumhoji kwao kungeweza kuvuruga mchezo wa kisiasa ulionuiwa.
Bunge la Mkutano wa 11 Sitta alikubali kumpa Rostam nafasi ya kutoa maelezo yake, lakini akatoa sharti kuwa shurti yaandikwe. Rostam alipoyaandika, Spika akabadili milingoti ya goli. Akasema kanuni za Bunge haziruhusu jambo lolote lililoamuliwa na Bunge kujadiliwa upya katika kipindi cha miezi 12!
Mwandishi wa makala ile anakiri nguvu na umuhimu wa Rostam Aziz katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema kuwa nguvu kubwa aliyonayo ndani ya chama hicho ilimwogofya Spika Sitta,, pale anaposema: Sasa kama mmoja wa mashabiki wake (Rostam) naye ataanza kumtwanga mangumi, basi si tu inawezekana kupata ufa mkubwa, lakini yaweza kabisa kusarambatika.
Mwandishi huyu huyu anayekiri nguvu ya Rostam, ndiye anadiriki kuhoji Rostam angesema nini na aliwahi kusema nini bungeni.
Kilichonisikitisha zaidi, mwandishi wa makala hiyo naye ameangukia katika mkumbo. Anamwagia matope Rostam, bila kuchunguza na wala sijui kilichomtuma afanye hivyo.
Sitaki pia kuamini kama kweli mwandishi huyu anaishi nchini na ni mfuatiliaji mzuri wa masuala ya kisiasa.
Sina sababu ya kutumia nguvu kuonyesha ukweli umelala wapi katika kueleza Rostam alipata kuchangia nini akiwa bungeni. Kwa uchache niorodheshe matukio haya aliyotenda kwa ufasaha wa hali ya juu na kutikisa nchi akiwa bungeni.
Mwaka 1994 Taifa lilikumbwa na mfumuko wa bidhaa kutoka Zanzibar. Bidhaa hizo zilikuwa zikipita kwa njia ya panya, maarufu kama Zanzibar route. Zilikuwa azikiingia nchini bila kulipa kodi na kufurika madukani. Rostam alisimama bungeni, akajenga hoja na Serikali ikachukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo.
Alidiriki kuwatuhumu hata viongozi wa Zanzibar kuhusiana na biashara hiyo. Hapo alionyesha ujasiri wa kwanza akiwa mbunge kijana kuliko wote wakati huo.
Mwaka 1977 Rostam alikuwa mbunge pekee aliyekataa kuunga mkono muswada wa Sheria ya Madini. Alisema muswada huo ulikuwa na upungufu mkubwa wa msingi na akaonya kuwa iwapo ungepitishwa, vizazi vijavyo vingewahukumu wabunge kwa uamuzi huo. Leo kamati ya Madini ya Rais, chini ya Jaji Mark Bomani, imeipitia sheria hii. Si ajabu matokeo yatakuwa sawa na alivyokuwa amependekeza Rostam.
Mwaka 1999 Rostam huyu huyu ambaye mwandishi hakumbuki iwapo aliwahi kusema lolote bungeni, aliweka historia katika chama tawala. Akiwa mbunge wa chama tawala, aliongoza kundi la wabunge 50 kupinga iliyoitwa kesi ya uhaini dhidi ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF).
Kumbuka CUF ni chama cha upinzani. Kesi hii ilikuwa imepandikizwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, akidai wabunge hao walikuwa na njama za kumpindua. Baada ya hoja ya Rostam, muda mfupi baadaye watuhumiwa wote waliachiwa.
Mwaka huo huo, kwa ujasiri mkubwa, Rostam aliongoza mapambano dhidi ya Dk. Salmin aliyetaka kubadili Katiba ya Zanzibar na kuongeza muda wake wa kuwa madarakani.
Yapo mengi, ila nikumbushe hata hili. Rostam huyo huyo anayebezwa, mwaka 2001, alisimama kidete kupinga mabadiliko ya Katiba yaliyokuwa yakimpa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mamlaka makubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kuteua wabunge 10.
Lakini si vibaya nikakumbusha kwamba pamoja na mengi yaliyozungumzwa na Rostam bungeni, na ambayo yamekuwa na manufaa kwa Taifa ni pamoja na lile la mwaka 2004 bungeni.
Katika mkutano wa Bunge la Bajeti, Rostam alimbana vilivyo aliyekuwa Waziri wa Uchumi na Mipango, Dk. Abdallah Kigoda juu ya kazi za wizara hiyo.
Nakumbuka vizuri sana suala hili. Hasa kutokana na ujasiri wake wa kuzuia shilingi, akitaka apewe majibu ya hoja kadhaa. Mosi, ilikuwa akitaka ahakikishiwe kuwa wizara hiyo inaachana na mpango wa kukusanya takwimu za uchumi, badala yake ibuni mipango thabiti ya uchumi na kuisimamia ipasavyo.
Akapendekeza Wizara ya Uchumi na Mipango iunganishwe na Wizara ya Fedha, kwani kazi zake zilikuwa pacha na zilizohitaji kuwa chini ya kiongozi mmoja. Leo suala hilo limetekelezwa na Seriakali iliyo madarakani.
Akataka uwepo udhibiti wa hali ya juu ili shilingi isiporomoke kila uchao, kwani athari za kushuka kwa thamani kulikuwa kunayumbisha uchumi.
Mjadala ulikuwa mkali mno, na wote walioshuhudia wanakumbuka vizuri hoja za Rostam ambazo baadaye zimetekelezwa.
Sipendi kuendelea zaidi ya hapo. Natumaini mwenye macho haambiwi tazama. Wapo wabunge wa kubezwa, lakini Rostam Aziz si mmoja wao, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.
Nimjuavyo Rostam Aziz, kwa ujasiri aliouonyesha ni kweli angetikisa nchi. Hata hivyo, hoja zinazopenyezwa kuwa angeweza kukiumbua chama chake, Chama Cha Mapinduzi, inaelekea wanaozitoa hawamfahamu vilivyo.
Kwa jinsi anavyojulikana, Rostam atakuwa mtu wa mwisho kukiumbua chama chake, hofu inayoonekana inatokana na ujasiri uliowekwa wazi na sehemu ya historia niliyoonyesha hapo juu.
Kwa vyovyote iwavyo, Mwananzela hakumtendea haki Rostam. Uandishi wa aina hii ni hatari kwa ustawi wa Taifa. Ninashauri bora kutoandika pale tusipokuwa na taarifa sahihi, vinginevyo tunaishia kujiumbua na kulipotosha Taifa.
Na Joseph Wambura-RAIA MWEMA Aprili 23, 2008