Mh. Rostam, mtu mzima hatishiwi nyau'
Lula wa Ndali-Mwananzela
Mei 7, 2008
KUNA watu wanaitwa mashujaa na majasiri; kuna watu wanaojidhania kuwa ni mashujaa na majasiri; na kuna watu ambao ni mashujaa na majasiri.
Wale wa kundi la kwanza huitwa hivyo na watu wengine kwa sababu mbalimbali za ukweli na za uongo, zenye msingi na zile za kutunga. Wale walio kundi la pili ni wale ambao wanajivisha ushujaa na ujasiri na kujitungia sifa za ukuu huo ili kuwavutia watu au kutisha watu.
Wale wa kundi la tatu ushujaa na ujasiri unathibitishwa na vitendo vyao ambavyo havihitaji kupigiwa panda na mtu yoyote kwani ni dhahiri kuviona.
Mwandishi wa makala ya "Tusimbeze Rostam, hatikisi kiberiti" kwenye toleo lililopita la gazeti hili amejaribu kutupatia Watanzania shujaa wa kundi la kwanza. Joseph Wambura akijibu makala yangu ya wiki mbili zilizopita iliyokuwa na kichwa cha habari "Sipendi Rostam Aziz atikise kiberiti bungeni" amejaribu kwa jitihada kubwa kuonyesha kuwa nilichokisema kwenye makala yangu ya awali hakina msingi, ni cha kutunga na hakina msingi katika ukweli.
ROSTAM Aziz
Jaribio hilo la kujibu hoja zangu japo dhaifu, halina budi kupongezwa kwani bila ya shaka baada ya kuacha magazeti yote aliyokuwa anayasoma na kuvutiwa na makala yangu kiasi cha kuamua kuijibu kunaonyesha ni jinsi gani makala hiyo ilimgusa Wambura (kwa uzuri na kwa ubaya).
Hivyo najihisi ni heshima ya pekee kwangu kuchaguliwa kati ya makala nyingi zilizoandikwa habari za Rostam wiki ile kujibiwa kwa kina na kiufundi namna ile. Pia nimefurahishwa sana na jitihada zake za kujenga hoja zenye nguvu badala ya kulazimisha hoja kwa kutumia nguvu kama alivyosema yeye mwenyewe "Sina sababu ya kutumia nguvu kuonyesha ukweli umelala wapi katika kueleza Rostam alipata kuchangia nini akiwa bungeni."
Na mimi, basi, kwa heshima kubwa na taadhima naomba nisitumie nguvu niweze kujibu hoja zake kama vile nimefumbwa macho na mkono mmoja ukiwa umefungwa nyuma yangu niweze kuonyesha ni jinsi gani hoja za Wambura hazina mantiki, ni dhaifu, na ukiziangalia kwa ukaribu hazina msingi kwani ni jaribio dhaifu la kumjenga Rostam kama shujaa na mbunge jasiri ambaye anaweza kutikisa nchi.
Kwanza kabisa niseme kile nilichosema kwenye makala yangu ya awali; sipendi tena sitaki (nimeongeza hilo) Rostam atikise kiberiti bungeni. Nasema hivyo kwa sababu naamini kama nilivyoandika kwenye makala hiyo kuwa "Hofu ambayo Spika ameijenga kuwa Rostam akisema basi kutazuka "vurugu bungeni" au kwa namna fulani kutafanya taifa liyumbe ni hofu isiyo na msingi na ni hofu ambayo inaongeza nguvu za kimungu za Rostam. Rostam ni mwanadamu mwenzetu na hana nguvu zozote zile ambazo zinaweza kusababisha mvua inyeshe au jua lichomoze!"
Kitu pekee ambacho Wambura amejaribu kujibu ni swali langu ambalo niliuliza "Hivi ni lini mara ya mwisho kwa Rostam kutoa mchango bungeni na alichangia nini? Ni kitu gani ambacho watu wanakumbuka ambacho Rostam Aziz alisema bungeni katika mijadala ya bajeti au mingineyo ambayo inaweza kukumbukwa? Kama huko kote hajasema jambo lolote la kukumbukwa iweje leo tugwaye kama Taifa ati Rostam anataka kusema?"
Katika kujibu hoja zangu Wambura anatoa mifano ya kuonyesha jinsi gani Rostam ni shujaa na jasiri akiwa bungeni. Anasema kuhusu hilo kuwa "matukio haya aliyotenda kwa ufasaha wa hali ya juu na kutikisa nchi akiwa bungeni." Hebu tuangalie mifano hiyo na tuone kama kweli ni ya "ufasaha wa hali ya juu" na ya kuwa Rostam aliweza "kuitikisa nchi akiwa bungeni".
Mfano wa kwanza ni ule anaosema "Mwaka 1994 Taifa lilikumbwa na mfumuko wa bidhaa kutoka Zanzibar. Bidhaa hizo zilikuwa zikipita kwa njia ya panya, maarufu kama ‘Zanzibar Route.' Zilikuwa zikiingia nchini bila kulipa kodi na kufurika madukani. Rostam alisimama bungeni, akajenga hoja na Serikali ikachukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo…Hapo alionyesha ujasiri wa kwanza akiwa mbunge kijana kuliko wote wakati huo."
Ningefurahi kama Wambura angetuwekea alichosema Rostam bungeni na ambacho hakikusemwa na mbunge mwingine yoyote kabla yake kuhusu suala hilo. Wambura anasema Rostam alijenga hoja lakini hatuambii hiyo hoja ilisemaje na Rostam alisema nini. Angeweza kutuambia ni kwenye hansadi gani ili na sisi wengine tuende kuangalia.
Katika hoja yangu ya awali niliuliza ni kitu gani ambacho Rostam alisema bungeni ambacho kinaweza "kukumbukwa"? Hivi msomaji unakumbuka alichosema Rostam kuhusu "njia za panya"? Mimi ni mfuatiliaji wa masuala ya kisiasa na kumbukumbu yangu ni nzuri. Alichokisema Rostam hakikumbukwi na kwa hakika hakikuitikisa nchi.
Mfano wa pili ni ule anaosema "Mwaka 1997 kwani ndio wakati sheria ya madini ya 1998 ilikuwa imeanza kujadiliwa) Rostam alikuwa mbunge pekee aliyekataa kuunga mkono muswada wa Sheria ya Madini. Alisema muswada huo ulikuwa na upungufu mkubwa wa msingi na akaonya kuwa iwapo ungepitishwa, vizazi vijavyo vingewahukumu wabunge kwa uamuzi huo. Leo, kamati ya Madini ya Rais, chini ya Jaji Mark Bomani, imeipitia sheria hii. Si ajabu matokeo yatakuwa sawa na alivyokuwa amependekeza Rostam."
Ingawa hili linawezekana kuwa ni kweli, lakini Rostam hakumbukwi kwa alichosema (ndiyo hoja yangu). Hivi ubaya na mapungufu ya sheria ya madini tulisikia toka kwa Rostam au kwa Zitto Kabwe? Kwa nini, wakati ule hatukumuona Rostam mtu jasiri akisimama na kutetea msimamo wake hata kutengwa na chama chake au kupewa adhabu na Bunge? Hata kama alipinga muswada huo, je, ulipoletwa wakati wa kupiga kura ya Bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba au ule wa madini, Rostam alipinga na kuondoa Shilingi au aliunga mkono hoja?
Kwa hakika, huko kupinga kwake sheria ya madini si kitendo cha kishujaa kwani ni wajibu wake na kwa hakika sidhani kama kuna Mtanzania anakumbuka, na zaidi ya yote haikutikisa nchi kama kina Zitto walivyotikisa nchi mwaka jana!
Mfano wa tatu Wambura anasema "Mwaka 1999 Rostam huyu huyu ambaye mwandishi hakumbuki iwapo aliwahi kusema lolote bungeni, aliweka historia katika chama tawala. Akiwa mbunge wa chama tawala, aliongoza kundi la wabunge 50 kupinga iliyoitwa kesi ya uhaini dhidi ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF).
Kumbuka CUF ni chama cha upinzani. Kesi hii ilikuwa imepandikizwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, akidai wabunge hao walikuwa na njama za kumpindua. Baada ya hoja ya Rostam, muda mfupi baadaye watuhumiwa wote waliachiwa."
Hapa nianzie na hili la mwisho. Wambura anadai kuwa kesi ya Uhaini ilikuwa "imepandikizwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya nne wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour".
Wambura anataka kuacha taswira kwa msomaji kuwa bila Rostam kuongoza kundi la wabunge 50 wa Bara, basi, kesi ya uhaini ingeendelea kuwapo na wale wabunge wa CUF wangeendelea kusota. Huku ni kujipa ujiko usio na msingi. Kuachiliwa kwa wabunge wale hakukutokana na juhudi za Rostam pekee na wala hastahili hata kidogo kubeba sifa za juhudi za mamia ya watu, vikundi na asasi mbalimbali.
Kushikiliwa kwa wabunge wale wa CUF lilikuwa ni doa kubwa kwa Tanzania na Zanzibar, na hasa watu wengi walipinga kushikiliwa kwao. Sekretariati ya Jumuiya ya Madola na viongozi wastaafu na wenye kuheshimika Afrika walishikiri katika kuishawishi Serikali ya Zanzibar kuwaachilia wabunge hao.
Kwa kumkumbusha tu Wambura ni kuwa Januari 2000 Rais Benjamin Mkapa alifanya mazungumzo na Rais Salmin kuhusu sakata la wabunge hao wa CUF. Na hilo lilitokana na shinikizo toka ndani na kutoka nje hasa baada ya kesi ya uhaini kuanza.
Ni siku hiyo hiyo ndiyo wabunge hao walipoandika barua yao ambao hawakuungwa mkono na Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye ambaye aliwaambia kuwa hawakuwa na baraka ya Chama.
Walichofanya wabunge hao ni kudandia treni ambalo wengine walishalianzisha akiwamo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ali Mohammed Ali Omar ambaye alisema kuwa kesi hiyo ilikuwa ya "kisiasa" kitu ambacho kiliashiria kuwa haishindiki mahakamani. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wenyewe kabla ya G50 walisema hilo hilo na asasi nyingine zisizo za kiserikali.
Hivyo kumpa ujiko Rostam kwa kazi ya watu wengi zaidi ya kundi hilo la G50 na kumfanya kuwa ndiye shujaa aliyesababisha wabunge wale kuachiliwa si haki na si kweli. Na zaidi ya yote kutoa madai bila ushahidi kuwa "Baada ya hoja ya Rostam, muda mfupi baadaye watuhumiwa wote waliachiwa" ni kutulaghai kwa kutudhania kuwa hatujui historia ya miaka michache tu iliyopita.
Watanzania wangapi wanakumbuka jina la Rostam juu ya hoja hii? Je, Rostam aliitikisa nchi kwa hilo? Msomaji hukumu mwenyewe.
Lakini kwa ujanja wa kujaribu kuchomea hoja Wambura ameongeza: "Mwaka huo huo, kwa ujasiri mkubwa, Rostam aliongoza mapambano dhidi ya Dk. Salmin aliyetaka kubadili Katiba ya Zanzibar na kuongeza muda wake wa kuwa madarakani."
Yaani, aliyesimama kati ya Dk. Salmin na kubadilisha Katiba ni Rostam! Sasa hapa naamini Wambura alikuwa anafanya mzaha. Yaani Rostam ndiye aliyeongoza mapambano dhidi ya Dk. Salmin? Hili nitawaachia wachambuzi wengine kwani itabidi michango ya Mwalimu Julius Nyerere, na Watanzania wengine itupwe katika kiza cha historia na tuanze kuimba nyimbo za kumtukuza Rostam kwa kuiokoa Zanzibar kutoka utawala wa Komandoo! Nani anakumbuka jinsi Rostam aliongoza "mapambano" dhidi ya Dk. Salmin? Je aliweza kuitikisa nchi?
Mfano wake mwingine anasema kuwa "Yapo mengi, ila nikumbushe hata hili. Rostam huyo huyo anayebezwa, mwaka 2001, alisimama kidete kupinga mabadiliko ya Katiba yaliyokuwa yakimpa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mamlaka makubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kuteua wabunge 10."
Kwa mara nyingine Wambura ameshindwa kutuonyesha alichosema Rostam na ambacho hakikusemwa na watu wengine. Kimsingi Wambura ametoa maelezo ambayo hayana msingi katika ukweli na yanaendeleza jaribio lake la kumpamba shujaa wake ambaye anaamini kuwa anaweza kuitikisa nchi.
Hakuna mahali ambapo amenukuu alichosema Rostam na hakuna mahali ambapo ameonyesha ni wapi na sisi wengine tunaweza kuangalia.
Lakini bado nasimamia maneno yangu ya awali. Rostam hana cha kuitisha nchi hii; na yeye kama raia mwingine yeyote yule hana nguvu yoyote ya kuifanya Tanzania itetemeke mbele yake ati kwa sababu anataka kusema kitu fulani. Aendelee kuwatetemesha anaowatetemesha na wale wenye kugwaya mbele zake wagwaye. Wale ambao wanaamini kuwa yeye ndiyo shujaa wake basi na wambebe juu juu ili nasisi tujue wamempata shujaa wao.
Vinginevyo, Rostam anayo haki ya kusikilizwa na chochote anachotaka kusema anaweza kusema bila kupigwa mkwara na mtu yeyote. Si Spika, si CCM na wala si waandishi wa habari.
Kama madai ya Wambura kuwa "Rostam alikuwa akidai kutotendewa haki na kwamba kamati ilifanya kazi nje ya muda wake, hivyo aliamini kuwa ilifanya kazi kisiasa. Kama kweli wangekuwa na nia ya kumhoji wangeweza kumhoji, ila kumhoji kwao kungeweza kuvuruga mchezo wa kisiasa ulionuiwa" yana ukweli basi Rostam aandike makala au amtumie mwandishi kuandika makala na aweke hoja zake hadharani badala ya kulalamikia pembeni.
Hofu ya kuwa ati akisema nchi itatikisika ni hofu ya nchi ya wenye hofu. Kama mada yangu inavyosema leo kuwa mtu mzima hatishiwi nyau na ncha ya mkuki haipigwi konzi. Lolote alilonalo Rostam litamtikisa yeye na chama chake na watu wake wa karibu. Linaweza kumtikisa Spika, Rais, wabunge, mawaziri na waandishi wa habari! Lakini kwa hakika haliwezi kuitikisa Tanzania!
Majuzi Waziri Mkuu wa nchi hii alijiuzulu na kesho yake watu waliamka na kwenda zao sokoni! Waziri wa Miundombinu ameanguka kama lumbesa na saa chache waliokuwa na harusi zao waliendelea. Sasa huyu Rostam hiyo nguvu ya kuweza kuitikisa nchi ataitoa wapi.
Tunaweza kushtushwa, tunaweza kupigwa na mshangao, na tunaweza kusikitishwa lakini nawahakikishia Watanzania wamekomaa kiasi cha kuweza kuhimili jambo lolote kama Taifa. Anayedhania kuwa Rostam anaweza kuitikisa nchi basi huyo aende kupiga magoti na kumbembeleza asiseme.
Kwa upande wangu narudia nililosema kama analo lake la kusema na anafikiri ameonewa asimame ajitetee; wenye kutikisika watatikisika na Tanzania haitotishika. Wale walio mabua ya mitete ambao wanatetemeka akikohoa na kukosa pumzi akipita waende kupanga foleni na kumlilia asiseme.
Mimi nasema Rostam anatikisia kiberiti ambacho akikiwasha vitakavyoungua ni yeye na nguo zake na za marafiki zake. Sisi wengine tutakaa pembeni kuwachora wanavyoumana na kutafunana kama mchwa. Kama haamini na asubiri.
Mashujaa wetu bungeni wapo na tunawajua, Rostam si mmoja wao.
Niandikie:
lulawanzela@yahoo.co.uk