Watanzania kwa ujumla wetu tumejumuika katika tukio la kuomboleza kifo cha mkurugenzi wa Clouds media, Ruge Mutahaba. Nawapa pole ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu.
Tukiweka unafiki pembeni, tukio la kifo cha Ruge limekuzwa mnoo. Ruge hakuwa mtu maarufu sana Tanzania (japokuwa amefanya mambo mengi makubwa), hakuwa mwema sana na wala hakuwa mtu muhimu sana kwa watanzania walio wengi.
Kila kitu kuhusu maombolezo ya msiba wake kinaonekana kupangwa, kuratibiwa na hata kugharamiwa kwa karibu mnoo na serikali. Tunaambiwa hata tangazo la kifo chake ilibidi itifaki ya ikulu itumike ili rais atangaze kifo chake. Ndugu, jamaa na marafiki wa karibu naye waliopata taarifa za kifo chake waliambiwa wakae kimya kwanza (walifichwa taarifa?) mpaka rais alipotangaza.
Sote tunajua Ruge alikuwa ni mfanyabiashara na kila alichokuwa akikifanya kwenye jamii kilikuwa kimelenga biashara zake kwa 100% hata kama alikuwa akikifunika kwa koti la kijamii. Waliowahi kufanya kazi naye wanajua hilo, na hakuwa na mchezo mchezo katika kufanya biashara zake. Huo ndio ukweli.
Watanzania wote wanalazimishwa kusema mema ya Ruge, kushiriki kuomboleza kifo cha Ruge na kulipia gharama za mazishi yake kama msiba wa kiongozi mkubwa wa kitaifa. Sidhani kama jambo hili lina afya sana kwa taifa letu huko tuendako, maana nadhani kila mtanzania angetamani naye siku moja ndugu, jamaa au rafiki yake atakayefariki njia hii hii itumike kwake ili kufuta majonzi na kumpa faraja.
Bado sijajua kwanini hili la kufa na kuzikwa kwa Ruge limelazimishwa kuwa tukio kubwa la kitaifa, lazima kuna sababu, nadhani huenda ipo siku tutaambiwa kinagaubaga.
Ruge hayupo tena, tuliompenda na waliomchukia tumeendea kuwepo, tukishamaliza kumzika turudi na kuendelea na maisha yetu.