Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,513
Pinocheti anasema kuwa tabia hiyo huweza kusababisha taasisi husika kupoteza dira, yaani kuanguka kwenye mtaro mchafu unaoitwa "mission creep,".
Anasema kuwa hili ni jambo ambalo hatimaye huyumbisha taasisi kwa kuzalisha maagizo yanayokinzana yakielekezwa kwa viongozi ambao ni watendaji wa ngazi za chini, yaani "antinomic delegation."
Hii ndio sababu Kanuni za Maadili za Chadema, zinakataza uchonganishi, kuzua migogoro, kutoa tuhuma juu ya viongozi pasipo kupitia vikao halali, kukaidi maagizo ya viongozi na maamuzi ya vikao halali, kukashifu Chama, kufanya upinzani dhidi ya chama, kufanya uasi, kufanya mapinduzi, kuvujisha siri za chama, kufanya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama, na kufanya makosa mengine kama hayo.
Makatazo haya yanatamkwa kanuni namba 3(a), (b), (c), (f); Kanuni namba 10.1(iii), (ix), (x), (xi), (xii); na Kanuni namba 10.3(iv) kwenye Kanuni za Chadema Toleo la 2019.
Na sasa ni wazi kwamba kwa kuzingatia ukweli huu, leo tarehe 05 Aprili 2025, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Tundu Antipas Lissu, ameanza hatua za kutekeleza Kanuni hizi.
Ametengua uteuzi wa Catherine Ruge kutoka kwenye nafasi ya Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema.
Ruge alikuwa anakitumikia Chama kwenye Sekretarieti kama Mtaalaam wa Dawati la Jinsia.
Catherine Ruge ni kiongozi wa pili kutenguliwa ndani ya siku mbili, wa kwanza akiwa ni Julius Mwita, aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Chadema.
Mwita amekuwa anapinga msimamo wa Chadema kuhusu ajenda ya “No reforms, no election” na amekuwa akiwahamasisha viongozi wengine kupinga ajenda hiyo.
Ajenda hii inalenga kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ili kuleta usawa na haki.
Kwa mujibu wa kauli ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, aliyoitoa tarehe 03 Aprili 2025 wakati anaongea na watia nia wa Ubunge na Udiwani, "No reform No Election" ni ajenda yenye Baraka rasmi za Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema na inatekelezwa kwa kutumia "constitutionally protected tools of protest".
Mara tu baada ya kutenguliwa Mwita aliongea na waandishi wa habari na kuthibitisha tuhumhidhidi yake.
Tarehe 03 Aprili 2025, John Mrema na wenzake 55 walijibatiza jina la G55 kisha kuandika, kusaini na kusambaza “Waraka Maalum” wenye kubeba kilichotajwa kama “Ushauri kwa Chama” cha Chadema.
Katika waraka huu kina Mrema wanadai kwamba Chadema itenganishe madai ya mabadiliko ya kimfumo yatakayoleta chaguzi huru na zenye kuaminika (reforms) na ajenda ya kuzuia uchaguzi kwa kusogeza ajenda ya mabadiliko katika kipindi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025;
Julius Mwita na Catherine Ruge ni miongoni mwa watu waliosaini waraka huo, wenye kupinga msimamo wa chama.
Hivyo, uamuzi wa kuwaweka pembeni kina Mwita na Ruge ni hatua mwafaka, na hasa kama tukitumia ubovu wa hoja zao zilizomo kwenye waraka wao, ulioambatanishwa hapa chini, baada ya kufupishwa na kuhakikiwa.
Sababu za Kina Mrema kuunga mkono uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025
Waandishi wa Waraka wanadai kwamba wanapinga mpango wa Chadema wa kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 kabla ya mabadiliko ya kimfumo kwa sababu zifuatazo:
- Ajenda ya "No Reforms, No Elections" iliyoasisiwa na vikao vya Chadema haijumuishi kipengele cha kuzuia uchaguzi mkuu, bali inalenga kutengeneza shinikizo la kisiasa bila kudhamiria kuzuia au kususia uchaguzi.;
- Chadema haina uwezo kuzuia uchaguzi wakati iko nje ya mchakato wa uchaguzi;
- Tumekwishafeli kuzuia uchaguzi maana tayari mchakato wa kutekeleza uchaguzi umeshaanza na uandikishaji wapiga kura pamoja na kugawanya majimbo;
- Mpaka sasa vyama vyote vya siasa, madhehebu makubwa ya dini na asasi za kiraia hawaungi mkono ajenda yetu ya kuzuia uchaguzi mkuu; na
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi ni mkakati ulio kinyume cha katiba ya nchi na unapingana na sheria za Tanzania.
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi ni mkakati ulio kinyume cha katiba ya Chadema na unapingana na kanuni zake.
- Kususia uchaguzi kutaifanya Chadema kukosa ruzuku, ambao ni mkakati wa uhakika wa kuinua mapato ya chama kuliko ulivyo mkakati wa tone tone, na hivyo chama kushindwa kujiendesha.
- Mazingira ya uchaguzi yasiyo rafiki kwa vyama vya upizani, yaliyopo sasa hivi, yanaweza kutumiwa na Chadema kuishinda CCM katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
- Mkakati wa "No Reform No Election" utainyima Chadema fedha kutoka kwa baadhi ya wagombea ambazo zingetumika kujenga chama wakati wa uchaguzi, maana watia nia watakata tamaa ya kuwekeza kwenye chama.
- Hakuna uwezekano wa kutekeleza ajenda hii kwa ufanisi katika muda mfupi uliobaki kabla ya Oktoba 2025.
- Kwa ajili ya kulinda uhai wa Chadema, mabadiliko yanao umuhimu lakini hayana uharaka, wakati uchaguzi unao umuhimu na uharaka, kwa maana kwamba Chadema inapaswa kutekeleza mkakati wa "Ama Kupigania Mabadiliko au Uchaguzi" lakini sio kutekeleza mikakati yote miwili kwa mpigo.
- Japo lengo kuu la Chadema ni kushiriki uchaguzi ili kuitoa CCM madarakani bado tunapaswa kuwa tayari kushiriki uchaguzi ili kupigania hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Mabarza ya Madiwani.
Hoja zote za Kina Mrema zimeshajibiwa na Lissu, hasa kupitia mkutano na watia nia uliofanyika makao makuu ya Chadema tarehe 03 Aprili 2025. Majibu ya Lissu yako hivi:
- Ajenda ya "No Reforms, No Elections" iliyoasisiwa na vikao vya Chadema inajumuishi kipengele cha kuzuia uchaguzi mkuu, kwani maneno "no elections" yanamaanisha "hakuna uchaguzi" na ili uchaguzi usiwepo inabidi uzuiwe;
- Chadema inao uwezo kuzuia uchaguzi wakati iko nje ya mchakato wa uchaguzi kwa sababu ipo ndani ya Tanzania mahali ambako uchaguzi unapaswa kufanyika;
- Ni kweli hatujazuia uandikishaji wapiga kura wala kugawanywa kwa majimbo lakini bado tunayo nafasi ya kuziia hatua za mchakato wa uchaguzi zinazofuata;
- Mpaka sasa Chadema tunaendelea na mkakati wa public engagement kwa njia ya mikutano ya nje na ndani tukivilenga vyama vyote vya siasa, madhehebu makubwa ya dini na asasi za kiraia, na hivyo sio sahihi kwa sasa kusema makundi haya hayaungi mkono ajenda yetu ya kuzuia uchaguzi mkuu; na ushahid wa kuungwa mkono unaanza kuibuka, mfano ni chapisho katika gazeti la Pambazuko (Toleo la JUmatatu, 7 Aprili 2025) lisemalo "Bunge Lisifungwe."
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi sio mkakati ulio kinyume cha katiba ya nchi na unapingana na sheria za Tanzania, kwani mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani, kuwasiliana na wadau, na hatua kama hizo zinakubalika kikatiba na kisheria.
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi sio mkakati ulio kinyume cha katiba ya Chadema na haupingani na kanuni zake kwani kusogeza mbele ratiba ya uchaguzi kutatoa fursa bora zaidi ya kutekeleza katiba ya Chadema.
- Ni kweli kwamba kususia na/au kuzuia uchaguzi kutaifanya Chadema kukosa ruzuku, lakini sio kweli kwamba kwa sasa ruzuku ni mkakati wa uhakika wa kuinua mapato ya chama kuliko ulivyo mkakati wetu wa tone tone, maana yamkini ya kushinda uchaguzi katika mazingira ya sasa ni karibu na zero.
- Kwa mujibu wa ushahidi kutokana na uchaguzi wa 2015, 2019, 2020 na 2024, mazingira ya uchaguzi yasiyo rafiki kwa vyama vya upizani, yaliyopo sasa hivi, hayawezi kutumiwa na Chadema kuishinda CCM katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
- Kweli, Mkakati wa "No Reform No Election" utainyima Chadema fedha kutoka kwa baadhi ya wagombea ambazo zingetumika kujenga chama wakati wa uchaguzi, lakini chama hakijengwi kwa siku 70 za uchaguzi, wala sio sera ya chama kwamba tutatumia fedha za wagombea kujenga chama, maana kazi ya mgombea ni kunadi sera jukwaani.
- Ni kweli hakuna uwezekano wa kutekeleza ajenda hii kwa ufanisi katika muda mfupi uliobaki kabla ya Oktoba 2025, lakini kanuni za uendeshaji wa mradi wa ujasiriadola zinaonyesha kwamba kuna uwezekano wa kusogeza mbele ratiba ya uchaguzi;
- Kwa ajili ya kulinda uhai wa Chadema, mabadiliko yanao umuhimu na yanao uharaka, kama ambavyo uchaguzi unao umuhimu na uharaka, kwa maana kwamba Chadema inapaswa kutekeleza mkakati wa "Kupigania Mabadiliko Pamoja na Uchaguzi" wa mpigo.
- Japo lengo kuu la Chadema ni kushiriki uchaguzi ili kuitoa CCM madarakani bado tunaweza kuamua kuwa tayari kushiriki uchaguzi ili kupigania hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Mabarza ya Madiwani, lakini mfumo wa sasa hauturuhusu hata kupata hadhi hiyo.
Tunafahamu kuwa, uwezekano wa kushinda uchaguzi hutegemea vigezo (determinants) sita, yaani: (1) mgombea bora, (2) ajenda bora, (3) mtandao wa rasilimali watu wenye kuongea lugha moja kabla na wakati wa kampeni, (4) rasilimali fedha za kutosheleza mahitaji ya kibajeti, (5) wapiga kura wenye kiu ya haki na amani na (6) mfumo wa uchaguzi ulio rafiki kwa wadai wote.
Vigezo hivi sita, vinayo michango yenye uzito tofauti katika kufanikisha ushindi.
Kwa mujibu wa tunayoyajua kuhusu chaguzi za Tanzania tangu 2015 hadi 2024, michango hiyo, katika asilimia zilizo kwenye mabano, ni kama ifuatavyo:
Mgombea bora (5%), ajenda bora (5%), mtandao mpana wa rasilimali watu wenye kuongea lugha moja kabla na wakati wa kampeni (5%), rasilimali fedha na rasilimali vitu za kutosheleza bajeti ya kampeni ya angalau dola moja kwa kila mpiga kura (5%), wapiga kura wenye kiu ya haki na amani (5%), na mfumo wa uchaguzi rafiki (75%).
Kwa hiyo, ni ndoto za mchana kufikiria kwamba, mfumo wa uchaguzi unaoweza kubatilisha ushindi kwa yamkini ya 75%, unairuhusu Chadema kwenda kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba ikiwa na matumaini ya ikaambulia kitu chochote. Hivyo, Lissu yuko sahihi na kina Mrema wanakosea.
==KIAMBATANISHO==
John Mrema, Mwandishi wa "Waraka Maalum"
WARAKA MAALUM: USHAURI KWA CHAMA CHA CHADEMA
John Mrema, Mwandishi wa "Waraka Maalum"
WARAKA MAALUM: USHAURI KWA CHAMA CHA CHADEMA
KUTOKA KWA: John Mrema, Kwa Niaba ya Watiania 55 wa Chadema wa 2025 na Baadhi ya Viongozi wa Juu wa Chadema.
KWENDA KWA: Katibu Mkuu, Chadema Taifa, S.L.P 31191, Dar-es-Salaam.
TAREHE: 3 Aprili 2025.
I. UTANGULIZI
Kichwa cha Waraka hapo juu chahusika.
Pia rejea wito uliotolewa na Ofisi yako kwa tuliokuwa wagombea ubunge wa CHADEMA 2020 na watia nia wa ubunge 2025, ukitutaka kushiriki kikao maalum pamoja na viongozi wakuu wa Chama, kilichopangwa kufanyika tarehe 3 April, 2025, kujadili hali ya kisiasa na mwenendo wa Chama katika kudai chaguzi huru na zenye kuaminika (No Reforms, No Elections)
II. MADHUMUNI YA WARAKA HUU
Pamoja na kupokea wito wa kushiriki mkutano huo maalum, sisi, wagombea ubunge wa 2020 na watiania wa ubunge wa 2025, tumeona kuna viashiria vya kutopewa au kutopata nafasi ya kutosha kusikilizwa katika mkutano huo maalum, na kwa hiyo, tumeamua kukuandikia Waraka huu, kwa sababu zifuatazo:
1. Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe Tundu Lissu, akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Iringa ametamka wazi kuwa, wote wanaoona, "No Reforms, No Elections" haiwezekani ni wana-CCM pamoja na vibaraka wao.
Kauli hii ya Mwenyekiti tayari imezuia uhuru wetu wa kutoa maoni au ushauri mbadala dhidi ya "No Reforms, No Elections", kwani, kwa mujibu wa Mwenyekiti wetu, watu wa namna hiyo ni wana-CCM au vibaraka wao.
2. Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Kamati ya Chama ya kuchangisha fedha kwa ajili ya "No Reforms, No Elections", Mhe Godbless Lema, akihutubia mkutano jijini Arusha, amenukuliwa akisema kwamba wote wanaotaka ubunge au udiwani bila reforms waondoke CHADEMA.
Kauli hii ya Mhe Lema ya kufukuza watu wenye maoni mbadala ndani ya Chama, haijakanushwa na Chama, na inazidi kuondoa mantiki ya mkutano huo maalum wa kujadili mwenendo wa No Reforms, No Elections, kwani tayari washiriki tumewekewa mipaka na vitisho katika kujadili suala hilo.
3. Hivi karibuni, Mwanaharakati, Maria Sarungi, aliandika katika ukurasa wake wa "X" akikitaka Chama kiyaweke hadharani majina ya wote wanaotaka ubunge kwa udi na ubani bila reforms, na akatuhumu kuwa watu hao wanataka kufanya "blackmail" (kutishia) eti watahama chama.
Pia, Maria Sarungi, bila kujali mamlaka ya Ofisi yako, ametaka ajulishwe ni nani amewaita watiania kwenye mkutano huo maalum maana uongozi mzima upo field. Na akataka Chama kisiwahusishe watiania (do not engage them), bali waachwe waende CCM.
Kauli hizi za Maria Sarungi, ambaye si mwana Chadema, zinafanana na kauli za Mhe Lissu na Mhe Lema. Aidha, kauli hizi zinaingilia mamlaka ya ndani ya Chama, na Ofisi yako imezinyamazia kimya, huku kukiwa na taarifa kuwa Mwanaharakati huyo ana mgongano wa kimaslahi wa kutaka Chama kisishiriki uchaguzi wa mwaka huu kwa maslahi yake binafsi.
Kauli za Maria ambaye ni swahiba wa karibu wa baadhi ya viongozi wetu wakuu zinazidi kuongeza vitisho na kufinya uhuru wa maoni kuelekea katika kikao hicho maalum.
Kwa msingi huo, tunawasilisha mchango wetu wa mawazo kwa njia ya maandishi kama ifuatavyo:
III. TUNAUNGA MKONO MADAI YA MABADILIKO (REFORMS)
Tunaunga mkono na tupo tayari kuongeza nguvu zaidi katika jitihada zote za Chama za kudai mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi (reforms) ili kuwa na chaguzi huru na zinazoaminika.
IV. MAONI MBADALA DHIDI YA MPANGO WA KUZUIA UCHAGUZI
Tunasita kuamini katika mpango wa Chama wa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2025 (iwapo mabadiliko hayatopatikana), tukiwa na sababu kuu zifuatazo:
1. Tunaona kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya uchaguzi. Kujaribu kuzuia uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi itakuwa ni sawa na kufanya jinai.
Uwezekano pekee wa kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi wenyewe kwa kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi.
Ni rahisi kwa wagombea kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi katika vituo mahsusi vya uchaguzi, katika kata au majimbo yanayoelekea kufanyiwa hujuma kuliko kujaribu kuzuia uchaguzi wote huku tukiwa nje kabisa ya uchaguzi wenyewe.
2. Dhana ya "No Reforms, No Elections", ilianza kama kampeni mnamo mwezi Januari mwaka 2020 baada ya "retreat" ya Kamati Kuu iliyofanyika Makueni, nchini Kenya, na haikuwa na tafsiri ya kuzuia uchaguzi bali ilikuwa inalenga kuhamasisha uungwaji mkono wa kudai reforms.
3. Kwa muda mfupi uliosalia, hatuoni uwezekano wa kutekeleza kwa ufanisi mkakati wowote madhubuti wa kuzuia uchaguzi.
Tayari, uchaguzi wenyewe umeshaanza kupitia zoezi la uandikishaji wapiga kura ambalo limeshafanyika kwenye mikoa mingi nchini na mchakato wa uchaguzi unaendelea kwa hatua ya mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
4. Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, ibara ya 4 inayohusu madhumuni ya Chama, dhumuni kuu la Chama ni kuongoza dola na kutekeleza madhumuni mahsusi ya kisiasa kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 4.1, madhumuni ya kiuchumi yaliyopo kwenye kifungu 4.2 pamoja na madhumuni ya kijamii kama yalivyoainishwa katika kifungu 4.3. Kwa hiyo, kushiriki uchaguzi ili kuongoza dola ni sharti la kimsingi la kikatiba.
5. Ibara ya 5.2.2 ya Katiba ya Chama imetamka haki ya mwanachama wa CHADEMA kuwa ni pamoja na kuchaguliwa kuongoza na kuwakilisha Chama katika ngazi yoyote kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa ya sifa za uongozi.
Mpango wa kuzuia uchaguzi unaweza kukosa uhalali wa kutosha kikatiba kwa kuathiri haki za wanachama wa CHADEMA wanaotaka kugombea.
6. Ukiondoa chama chetu, mpaka sasa hakuna chama kingine hata kimoja cha siasa kinachounga mkono mpango wa kuzuia uchaguzi ikiwa reforms hazitopatikana.
Kinyume chake, kuna Chama kimoja tu cha upinzani ambacho kinapigania "reforms" lakini huku kikiendelea kujipanga kushiriki uchaguzi. Vyama vingine hususani vile vyenye kawaida ya kutumika na CCM, vimeendelea kutangaza nia zao za kushiriki uchaguzi.
7. Viongozi wa dini na madhehebu yenye waumini wengi hapa nchini, tayari wamehimiza na wanaendelea kuelimisha na kuhamasisha waumini wao kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi.
Hali hii inaashiria kuwa ama Chama chetu kimechelewa au tayari kimekwama kupata uungwaji mkono wa wadau muhimu katika mpango wa kuepuka uchaguzi usio na reforms.
8. Uchunguzi na uchambuzi wetu unaonesha kuwa wadau wengi wa demokrasia wanaunga mkono madai yetu ya "reforms", lakini wanasita kuunga mkono mpango kamili wa Chama chetu wa kuzuia uchaguzi iwapo "reforms" hazitopatikana, kwani hali hiyo kwao inatafsiriwa kuwa ni karibu sawa na kufanya uasi au kuvunja katiba na sheria zilizopo licha ya ubaya wake.
Kwa maneno mengine, msisitizo wa kuzuia uchaguzi unaathiri au kupunguza kasi ya uungwaji mkono katika madai ya msingi ya reforms.
9. Kushindwa kuzuia uchaguzi katika dakika za mwisho (ikiwa jitihada za kupata reforms zitakwama), kunamaanisha kuwa Chama hakitokuwa tena na muda wa kujiandaa na hivyo hakitoshiriki kabisa uchaguzi huo.
10. Mhe Katibu Mkuu, matokeo ya kushindwa kuzuia uchaguzi yatakuwa ni kutoshiriki uchaguzi. Katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari, Makamu Mwenyekiti wa Chama, Mhe John Heche, alithibitisha ukweli huu pale alipojibu swali la Chadema itafanyeje iwapo haitofanikiwa kuzuia uchaguzi.
Mhe Heche, aliweka bayana kuwa "ikiwa hivyo basi Chama hakitoshiriki uchaguzi".
V. ATHARI ZA KUTOSHIRIKI UCHAGUZI
Ni maoni yetu kuwa Chama kitafikwa na athari zifuatazo iwapo hakitoshiriki uchaguzi:
1. Chama kinaweza kuondokewa au kupoteza viongozi na wanachama wenye nia ya kuwania urais, ubunge, udiwani pamoja na nafasi za viti maalum vya ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini.
2. Chama kitapoteza mvuto kwa umma, kitadhalilishwa kwa propaganda na hata kudhohofika.
Hadi sasa Chama kimekatika katika vipande viwili vinavyosigana kuhusu jambo hili.
Ikitokea tukashindwa kushiriki uchaguzi, mkatiko huu utakuwa ni wa wazi na athari zake zitakuwa mbaya zaidi.
3. Chama kitapoteza kabisa ruzuku baada ya uchaguzi na hivyo kuathiri uhai na uendelevu wa shughuli za Chama.
4. Ari na hamasa ya wanachama kukichangia Chama itazidi kushuka kwani wananchi hawatoona faida ya kukichangia Chama kisichoshiriki uchaguzi.
5. Kutoshiriki kampeni na uchaguzi kutakipotezea Chama fursa ya kujijenga zaidi maana haitokuwa rahisi kwa watiania kuwekeza kwenye Chama ambacho hakiingii kwenye uchaguzi maana hawatopata fursa ya kugombea.
6. Kwa ujumla, kutoshiriki uchaguzi kutasababisha Chama kupoteza uhusika na umuhimu wake kwa umma (relevance), hali inayoweza kufuatiwa na kuporomoka kisiasa na hatimaye kudhohofika kabisa.
VI: USHAURI WETU: TUJIANDAE KWA UCHAGUZI
Kwa kuzingatia msingi wote huo, sisi tuliokuwa wagombea ubunge 2020 na watiania wa ubunge 2025, tunakishauri Chama chetu (CHADEMA) kwamba tuendelee na tuongeze kasi na nguvu ya kudai mabadiliko yatakayoleta chaguzi huru na zenye kuaminika (reforms), lakini bila kuchanganya madai hayo na ajenda ya kuzuia uchaguzi.
Badala yake, Chama kiruhusu kuanza mara moja kwa maandalizi ya chini kwa chini ya kujipanga kwa ajili ya kushiriki uchaguzi hata kama “reforms” zitakuwa zimekawia kupatikana.
Tunatoa ushauri huu tukiwa ni wana Chadema makini, wenye mapenzi mema na uaminifu wa hali ya juu kwa Chama chetu, huku tukisukumwa na maslahi mapana na endelevu ya Chama na nchi yetu. Katika ushauri wetu huu, tumetilia maanani masuala ya msingi yafuatayo:
1. Upo uwezekano wa kushinda uchaguzi wa 2025 na kutangazwa katikati ya vikwazo vingi vya kikatiba, kisheria na utamaduni mbaya wa CCM wa kubaka demokrasia.
Pamoja na hujuma na uonevu wote tuliofanyiwa katika chaguzi zilizopita, bado yapo madhaifu ya ndani ya kirasilimali na kimkakati yanayoweza kuondolewa na hivyo kukifanya Chama kiingie katika uchaguzi huu kikiwa na nguvu mpya na mikakati madhubuti ya kukabiliana na hujuma za CCM na serikali yake kwa kiasi kikubwa.
Zipo nchi nyingi duniani na ndani ya Bara la Afrika ambazo vyama vya upinzani viliweza kupambana na kushinda chaguzi katikati ya mazingira onevu na kandamizi ya katiba na sheria za uchaguzi.
Wakati tukipigania reforms, tuchukue vile vile wajibu wa kuandaa mkakati kabambe wa kuikabili CCM katika mazingira magumu ikiwa reforms hazitopatikana kwa wakati.
2. Tukijipanga vizuri kimkakati, kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa kubwa na nzuri zaidi ya kuuzuia uchaguzi kirahisi kwenye vituo na maeneo mahsusi yanayoelekea kufanyiwa hujuma.
Tunasisitiza kuwa ni ngumu na kwa kweli haiwezekani kuuzuia uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi.
3. Kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa ya ziada ya kuyatumia madhila ya uchaguzi katika kuwaunganisha, kuwachochea na kuwaongoza wananchi kuendeleza vuguvugu la kudai reforms kwa kishindo kikubwa zaidi.
4. Kushiriki uchaguzi kutasaidia kuimarisha na kuendeleza umoja na mshikamano wa Chama, wanachama na wananchi, kutahuisha uhai na kuendeleza nguvu, hamasa na harakati za Chama (mabadiliko ni mchakato)
5. Ikumbukwe kwamba, pamoja na mapungufu makubwa ya katiba na sheria za uchaguzi, bado si hujuma zote tunazofanyiwa katika chaguzi zimetamkwa au zimehalalishwa katika kisheria.
Vitendo vya mawakala wetu kutoapishwa, mawakala wetu kuzuiwa kuingia vituoni, wagombea wetu kunyang'anywa fomu, wasimamizi kukimbia ofisi ili kukwepa kupokea fomu za wagombea wetu na kura feki kuingizwa vituoni, si matendo ambayo yamehalalishwa na katiba wala sheria bali ni uhuni tu unaofanywa na CCM na serikali yake na ambao upo kinyume pia na sheria zilizopo.
Kwa hiyo, mbali na kupigania reforms kwaajili ya kuleta chaguzi huru na zenye kuaminika, kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa ya kuja na mikakati madhubuti ya kukabiliana moja kwa moja na vitendo vya kihuni vilivyo kinyume kabisa na sheria zilizopo.
VII. HITIMISHO
Mheshimiwa Katibu Mkuu, tunaomba uzingatie kuwa tumetoa maoni na ushauri wetu huo baada ya Ofisi yako kutualika kujadili ajenda ihusuyo hali ya kisiasa na mwenendo wa Chama katika kudai chaguzi huru na zenye kuaminika.
Kwa muhtasari, maoni na ushauri wetu, vimejikita katika kuunga mkono madai ya reforms lakini wakati huo huo tukikisihi Chama chetu kione haja ya kujiandaa na hatimaye kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 hata kama “reforms” hazitopatikana kwa wakati.
Kwamba, kushiriki uchaguzi kutatuepusha na athari nyingi na za muda mrefu za kudorora kwa Chama, huku tukiwa pia na uwekezakano wa kushinda au kuzuia uchaguzi kwenye maeneo au mazingira mahsusi ya kiuchaguzi yatakayoelekea kufanyiwa uhuni au hujuma dhidi ya demokrasia.
Tunaomba Chama kiyazingatie, kiyape kipaumbele katika tathmini na tafakari zake na kiyafanyie kazi maoni na ushauri wetu huo kwa kina, kikiongozwa na fikra chanya, maslahi mapana na endelevu ya Chama, pamoja na nafsi zilizojaa upendo, umoja na mshikamano kwa wanaChadema wote.
Tunapenda kusisitiza kuwa maoni na ushauri wetu huo si wa kupinga msimamo wa Chama, bali ni wa kupendekeza namna bora zaidi ya kuziendea reforms huku tukilinda ustawi endelevu wa Chama chenyewe chini ya imani kuwa "change is a process" (mabadiliko ni mchakato).
Tunapenda ieleweke kuwa iwapo Chama hakitakubaliana na maoni na ushauri wetu, basi tutaendelea kuheshimu msimamo na mwelekeo wa Chama kwa uaminifu na mapenzi yetu yote.
VIII. SAHIHI ZA UTHIBITISHO
Pamoja na salaam za "Stronger Together"
Mungu ibariki Chadema, Mungu ibariki Tanzania.
Tunaomba kuwasilisha.