Uchaguzi 2020 Sababu za kushindwa upinzani Uchaguzi Mkuu 2020

Uchaguzi 2020 Sababu za kushindwa upinzani Uchaguzi Mkuu 2020

Kiokote

Member
Joined
Nov 9, 2010
Posts
86
Reaction score
42
Ni dhahiri shahiri kwamba kutokana na mwenendo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020 zinazoendelea Upinzani unakwenda kuendeleza kushindwa vibaya kwa mara nyingine. Sababu za kushindwa vibaya uchaguzi huu katika ngazi zote (Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani) ni nyingi ila mimi nitagusia chache:

1. Marufuku ya kutofanya siasa tangu 2016-2020: Hii ni moja ya sababu kubwa kwa sababu kwa miaka takribani vyama vya upinzani havikupata nafasi ya kujieneza na kujitangaza katika ngazi za Kitaifa mpaka mashinani. Hili linaongezewa uzito na susia susia ya chaguzi ndogo za Siha, Kinondoni na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24, 2019. Wakati uchaguzi huu unafanyika unavikuta vyama vya upinzani vikiwa havina Mwenyekiti wala mjumbe hata mmoja katika ngazi ya mitaa, vijiji na vitongoji.

2. Kutokuwa na Ukwasi: Vyama vingi vya upinzani vimeingia kwenye uchaguzi huu wa 2020 vikiwa na ukata mkubwa. Leo Lissu amesikika akisema amekuwa 'akiomba omba' michango kwenye mikutano ya Kampeni kwa sababu yeye binafsi na Chama chake hawana uwezo wa kumudu gharama za kampeni. Hii itufikirishe, kama Chadema chama cha pili kwa ukubwa nchini kinalia ukata Chama cha CHAUMA cha ndugu "Ubwabwa" Wakili Hashimu Rungwe kitakuwa na hali gani.

Ukata huu una athari za aina kadhaa. Mosi, unawapunguzia wagombea uwezo wa kufika maeneo mengi ya nchi--CCM kama chama tawala na kinachotumia rasilimali zake na zile za serikali kina wigo mpana wa kufika kila kona ya Nchi hii; hata mkakati wao wa kampeni umekuwa na mafanikio makubwa. Wameamua kuchora pembe tatu: Mgombea yuko Geita, Mgombea mwenza yuko mikoa ya Pwani, na huku Waziri Mkuu yuko mikoa ya Arusha, K'njaro n.k.

Pili, ukosefu wa fedha unavikosesha vyama uwezo wa kugharamia matangazo na mabango kwenye maeneo mbalimbali ya nchi--hivi sasa huko mitaani matangazo yanayoonekana ni ya chama Tawala tu. Tatu, ukosefu wa fedha unafanya iwe rahisi kwa wagombea wengi wa upinzani kurubuniwa kwa kununuliwa au kujitoa kwenye uchaguzi.

3. Kutokuwa na Chombo cha Habari: Siasa zozote duniani huendeshwa kwa sera na propaganda, na vyote hivyo lazima visafirishwe kupitia vyombo vya Habari. Leo hii vyombo vyote vya habari vilivyokuwa vinaaminika kuunga mkono upinzani ama havifanyi kazi au vimefungiwa na mamlaka za serikali.

Gazeti kama Tanzania Daima ambalo lilikuwa nguzo muhimu ya uenezi wa Chama Chadema liko korokoroni huku Chama tawala kikiendelea kutumia vyema utitiri wa vyombo vyake kama gazeti la Uhuru, Radio Uhuru, Chanel 10 na vyombo vya serikali kama TBC zote. Hii inaathari kubwa. Ndio sababu pia hata mapinduzi makubwa duniani huanza kwa utekaji wa vyombo vya habari. Mwalimu Nyerere alipokwenda League of Nations kwa mara ya kwanza miaka 1950s alitumia nafasi hiyo kuomba msaada wa wadau wa huko wasaidie uanzishwaji wa gazeti la The Nationalist ili ije iwasaidie kama nyenzo ya kupambana na utawala wa Kikoloni.

Mawasiliano ya mitandaoni (facebook, twiter, whatsap, youtube n.k) yanawafikia wapiga kura wachache sana kiuhalisia--wengi wao ni kundi la wasomi ambao hawajawahi kuwa nguvu ya mabadiliko popote duniani. Vyombo vya habari vya nje kama BBC, DW havitasaidia vyama vya upinzani.

4. Kutokubali kukiri udhaifu na kujiaminisha kupita kiasi: Umejengeka utamaduni wa muda mrefu miongoni mwa wadau wa vyama vya kujiaminisha kuwa havikosei na wala havihitaji kukosolewa. Mfano wa hivi karibuni ni kile kitendo cha Mhe. Freeman Mbowe kuwafukuza waandishi wa TBC na kuendelea kujiaminisha kuwa hajakosea mpaka pale alipotafutiwa suluhu. Katika nyakati kama hizi kugombana na TBC ni kama umewapa sababu ya kutumika na Chama Tawala kuliko ilivyokuwa awali.

5. Maonevu ya mfumo wa Uchaguzi: Kutokana na utamaduni kandamizi uliowekwa na mamlaka za uchaguzi na serikali vyama vya upinzani vimekuwa vikifanyakazi zake kwa mazingira ya mashaka na hofu kubwa. Kitendo cha karibu robo tatu ya viongozi wakuu wa upinzani kushinda kwenye mahakama kwa kesi hii ama ile umevidhoofisha vyama hivi.

Kushambuliwa na kuumizwa kwa viongozi kama Tundu Lissu, Mbowe n.k. Faulo za kuenguliwa na Tume na mapingamizi ya kubumba kumefanya vyama hivi kuendelea kunyong'onyea.

Ubashiri wangu ni kuwa upinzani utapoteza robo tatu ya viti vyote vya Ubunge na Udiwani ilivyoingia navyo katika uchaguzi Mkuu huu. Kwa upande wa Urais JPM atawashinda wenzie kwa mbali sana, haitarajiwi vyama vyote vya upinzani kwa pamoja kufikisha hata kura milioni 3 za Urais.
 
Back
Top Bottom