Habari. Nimepata wasaa sasa wa kuendelea pale nilipoishia mwanzo. Kumbuka kuwa habari hii ni simulizi za kweli kwa asilimia 100% hivyo unaposoma hapa jua kwamba unasafiri pamoja na mimi katika kila njia ya kweli niliyopitia. Ahsante na karibu sana hapa😊
Tunaendelea.... Baada ya kufika katika jiji la Mwanza, nikiwa katika standi ya mabasi ya Nyegezi nilipiga picha mbili tatu za kumbukumbu na kisha kutoka nje na kutafuta sehemu kwaajiri ya malazi. Hiyo haikuwa shida sana kwani kwa msaada wa dereva bodaboda niliweza kufanikisha hilo.
Mwendo wa takribani dakika mbili tu tulikuwa tayari mbele ya lodge moja iliopo karibu kabisa na standi hiyo. Nililipia nauli ya bodaboda na kisha kufanya malipo ya siku tano nitakazokaa hapo. Baada ya malipo yangu bodaboda alipewa tena pesa yake ya kupeleka mteja hapo na kuniacha eneo hilo.
Sikuwa na muda wa kupoteza tena hapo, kwani niliifadhi begi langu ndani ya chumba na safari kuelekea Bujora culture Centre ikaanza. Unajua nilikuwa na siku chache jijini Mwanza na katika siku hizo chache nilitamani nitembelee maeneo mengi hata kumzidi mtu mzaliwa wa mkoa huo😄😁.
Kwa kuwa muda ulikuwa umeshasogea sana niliamua kukodi pikipiki hadi Bujora culture Centre. Nilihofia kuchelewa kufika hapo kutokana na umbali kati ya nilipofikia na eneo hilo na pia jioni ilishaanza kuingia.
Kwa ghalama ya 8000 tu niliweza kufika kwa wakati na bila kupata usumbufu njiani.
Naagana na bodaboda, kisha moja kwa moja naelekea eneo la mapokezi na nakutana na mkuu wa makumbusho hayo yenye historia ya kanisa na utamaduni wa wasukuma kwa pamoja. Baada ya maelezo kidogo, kujiandikisha na kulipia kiingilio cha shilingi 3000 nakaa nasubili utaratibu.
Msimamizi mkuu wa makumbusho anamwita kijana mmoja mweupe na mrefu kunizidi mimi, mcheshi na anaependa kazi yake, na moja kwa moja anamtambulisha kwangu nikiwa kama mgeni na kijana huyo atakuwa mwongozaji wangu katika kuzunguka eneo hilo na kunipa maelezo yote
Binafsi napendezwa sana na eneo hilo, eneo kubwa, zuri na lililopangiliwa vizuri. Pia siku hii ilikuwa nzuri sana kwani kulikuwa nq makundi mengi ya wanafunzi yaliyotembelea hapo na kufanya eneo kuwa bize sana na msongamano wa watu wengi hivyo kufanya eneo kuchangamka sana.
Basi baada ya kama saa moja hivi ya maelezo mazuri kutoka kwa muongozaji wangu hapa, nilitoa tip kidogo na tukapata picha ya pamoja kwaajiri ya kumbukumbu zangu. Na binafsi nilipendezwa sana na uwasilishaji wake wa taarifa kwa mgeni, ambapo unaweza kutamani kubaki hapo😁
View attachment 2791801
(Pichani nikiwa pamoja na kijana muongoza wageni katika Sukuma museum Bujora)
Unajua lengo langu kuu ni kuwahamasisha watanzani kufanya utalii wa ndani, kutembelea mikoa wanayoitamani na pia kukutana na watu wengi nje ya maeneo yao waliyoyazoea na mwisho kuwafanya wawe na uelewa mkubwa kuhusu nchi yao na tamaduni mbalimbali zinazopatikana hapa.
Basi baada ya kumaliza kufanya utalii wa ndani katika makumbusho hayo niliamua kuelekea moja kwa moja mjini kati kabisa. Hapa nilitaka kupata kuona tu ni kwa namna gani katikati ya jiji la Mwanza kunavyoonekana hasa kwa nyakati za usiku. Hii ni aina nzuri ya kutalii katika eneo geni😀
Aisee nilishangazwa na kukuta maduka makubwa huko, hongera Vunja bei, mji unamwonekano mzuri sana nyakati za usiku, japo barabara ni finyu lakini walau nilipotea potea na kwa msaada wa Google map 🤣 nilipata upya mwelekeo wa niendako. Watu ni wapambanaji sana huko.
Kwa ufupi nilipata kuzunguka eneo baada ya eneo hapo katikati ya jiji na kwa kuwa ilikuwa usiku sasa niliacha nimepata walau kumbukumbu ya location nilizopita. Ni mitaa mingi ilinivutia hapa, kwa kweli ilinivutia sana na hii ndio maana mji huu umekuwa kivutio kwangu.
View attachment 2791807
( moja ya kumbukumbu zangu kutoka Google)
Sasa muda ulishasogea sana na kichwani niliwaza kufanya hitimisho kwa kufanya utafiti wa aina ya vyakula wanavyopendelea zaidi wenyeji wa hapa. Hii ni aina yangu ya utalii ninayoipenda pia, nataka ninywe na nile kile wenyeji wanakipendelea sana. Basi nikasogea sehemu moja hivi na katika kuuliza uliza nikasikia habari za (FULU) Kama sijakosea ni hao dagaa wanaoitwa Fulu, maziwa ya mtindi, mbogamboga na Ugali.
Nilipenda chakula hicho, maana vingine vyote vinapatikana Dar es salaam na maeneo mengi ya nchi. Aisee hao Fulu ni wachungu chungu hivi, sikuwaelewa kabisa, mtindi ulikuwa sawa na Ugali sio mbaya sana. Lakini ki ukweli kuhusu swala la mapishi watu wa Mwanza nawatunzia siri😀😄
Baada ya hapo, nilirudi kwenye Lodge niliyofikia na kisha kupumzika kwaajiri ya mizunguko mingine mingi ya siku ya pili yake hapo jijini Mwanza, ambapo hadi muda huo nilikuwa tayari nimeshafika Bujora makumbusho, nimeshatembelea jiji nyakati za usiku na nimesha kula FULU😄😁
....Itaendelea hapa...