Safari ya kurudi Dar es salaam kutoka Chato kwa ndege ya Air Tanzania ilichelewa kwa saa moja. Kati ya mapungufu niliyoyaona kwenye shirika ni kutokutoa taarifa kwa abiria kuhusu uchelewaji na ofisi ya wakala wa Air Tanzania pale Chato kufungwa asubuhi tu.
Taratibu za upekuzi pale uwanjani zilifanyika vizuri na kwa haraka. Kulikuwa na abiria wapatao Kumi, idadi ambayo inatia matumaini kwa kiwanja kidogo vile na hasa ukizingatia kuwa ilikuwa inakwenda kushusha na kupakia abiria wa Mwanza.
Ndege ilijaa hadi kuvuka nusu ya viti, kulikuwa na mapengo machache. Ndege iliyotumika TC-TCB kwenye njia hiyo inaonyesha uchakavu kwa kiasi fulani kwenye viti na vishikio, rangi pia zinaanza kufifia kwa ndani, nje safi. Nashauri matengenezo madogo madogo yafanyike na sisi abiria tutunze mali zetu vizuri. Wahudumu wote waliokuwa kazini jana wako vizuri na walitoa huduma iliyotukuka.
Marubani pia wako vizuri nawapongeza kwa weredi na umakini katika kufanya kazi yao. Kuruka Chato safi kutua Mwanza safi sana, hakukuwa na mkito!.
Abiria wa Mwanza walikuwa wengi hadi kujaza viti karibu vyote, nyomi ya uhakika kabisa ilitamalaki. Kuruka Mwanza kama ilivyokuwa Chato safi ila kutua Dar, yumba yumba kidogo mkito ulisikika...lakini safi.
Kwa ujumla Air Tanzania imeishaingia kwenye Ligi ya usafiri wa anga na mashirika ya kimataifa, hadi sasa wanafanya vizuri,waongeze bidii zaidi katika kazi ya kuwahudumia watanzania. Marubani waongeze umahiri na weredi wakati sisi watanzania tukiwajibika kutunza mali hii ya umma.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Air Tanzania.