Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Kuanza kwa safari hizo ni utekelezaji wa Mkataba wa Huduma za Usafiri wa Anga kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufalme wa Ubelgiji uliosainiwa Novemba 3, 2021 jijini Dodoma, ukilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga, biashara, utalii na uwekezaji.
Mhe. Millya alieleza kuwa safari hizo zitafungua fursa mpya za kiuchumi kwa kurahisisha usafiri wa wageni, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ulaya kuja Tanzania, sambamba na kuwapa Watanzania urahisi zaidi wa kusafiri kwenda Ulaya kupitia mtandao mpana wa safari za Brussels Airlines.
Aidha, kuanzishwa kwa safari hizo kunatarajiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini ikiwemo Zanzibar, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Hatua hiyo pia itasaidia kuongeza mapato yatokanayo na utalii, kuongeza ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.
Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali mabalozi, watendaji wa sekta ya usafiri wa anga, utalii na biashara, pamoja na wadau wengine wa maendeleo, akiwemo Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Balozi wa Tanzania nchini Belgium, Jestas Nyamanga, Balozi wa Belgium nchini Tanzania Mhe. Peter Huyghebaert na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Lufthansa Bi. Julia Hilenbrand ambao kwa nyakati tofauti wameeleza matumaini yao kuwa kuanzishwa kwa safari hizo zitachangia kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania, Ubelgiji na Bara la Ulaya kwa ujumla.