Mzee Mwanakijiji: Ile artilce yako imetoka katika gazeti la Tanzania Daima. Ila mwandishi kaibadilisha kidogo. The bad news is that the author did not even acknowledge the original source! Anyway, angalau itawafikia watu wengi zaidi. Here we go:
Richmond kiboko wa mazingaombwe!
Dennis Msacky
KUNA mjadala mkubwa ambao unaendelea hasa kwa raia wa Kitanzania wanaoishi katika nchi za Uingereza na Amerika.
Mjadala huu si mwingine ni sakata la umeme, tena si umeme wa Mtera na Kidatu, bali ni kuhusu Kampuni ya Richmond, ambayo ilitamba kwa makeke kwamba ingetatua angalau kwa kiasi fulani tatizo la umeme. Watu hawa ambao wameingia katika mjadala huu si watu wa mzaha, bali ni wasomi waliobobea katika masuala mbalimbali ya kijamii, wana uzalendo na nchi yao, wanasikitikia viongozi wetu walivyo na upofu wa kujua baya na jema, wanasikitika na kuhisi kwamba ujio wa kampuni hii ni ‘dili' la baadhi ya watu.
Mjadala huu umezua mengi, sasa wengine wanasema kwamba kama ni bingwa wa mazingaombwe, basi Richmond inakwenda kwa Kasi Mpya, Ari Mpya na Nguvu Mpya, yote hasa yanaashiria kwamba mambo si shwari kwa masuala kadhaa kwa viongozi wetu.
Watanzania wamefanyiwa mazingaombe, wana maswali kemkemu ya kuuliza, lakini hayupo wa kujibu, kila mmoja anapiga chenga. Kuna siku hizi chenga wanazopiga zitajulikana, hapo ndipo wataanza kusaga meno. Maana wahenga walisema, muosha naye huoshwa.
Msomaji hebu fuatilia kisa cha Richmond kuifanyia serikali mazingaombwe ya mwaka na baada ya hapo tafuta jibu la maswali yaliyo chini kabisa.
Sasa kwenye fani ya mazingaombwe kuna vitu vikubwa vitatu. Cha kwanza kinaitwa wepesi wa mikono (sleight of hand), cha pili ni viinimacho (illusion) na cha tatu ni kupoteza lengo (distraction).
Ili mazingaombwe yafanikiwe na kuwa na mvuto ni lazima vitu hivyo vitatu viende sambamba na kwa wakati muafaka.
Sasa mwanamazingaombwe aliyebobea atahakikisha kuwa watu wanashuhudia mtu anaingizwa kwenye sanduku (sleight of hand), sanduku linakatwa nusu kwa upanga (illusion), huku mwanamazingaombwe anawaeleza na kuwachangamsha watu kwa maneno na porojo (distraction).
Pindi lile sanduku likiunganishwa tena na yule mtu aliyewekwa humo akatoka mzima (restoration), basi watu watapiga makofi na kumsifia mwanamazingaombwe kwa onyesho zuri na mwanamazingaombwe huyo atachukua pesa zake na kuandaa onyesho jingine, na wale ambao hawataki kufikiri juu ya nini wameshuhudia wataendelea kupiga makofi na kuchekelea.
Alichofanya jasusi, ni kutoboa siri ya mazingaombwe! Watu wa Richmond wameleta mazingaombwe ya hali ya juu na nusura wafanikiwe kumrejesha mtu akiwa bado mzima kutoka kwenye sanduku.
Watanzania walitaka kuridhishwa na onyesho zuri la ‘Umeme'. Ndipo wanamazingaombwe kutoka Houston, Marekani walipotokea na vikolokolo vyao vya mazingaombwe. Wakawaambia Watanzania kuwa wana uwezo wa kuleta nishati (kumkata mtu nusu bila kumuumiza) tena kwa bei rahisi. Watanzania wakaamini na wakawapa nafasi.
Kwa vile wanamazingaombwe wetu hawakuwa na lengo wala uwezo huo, iliwabidi wafanye viinimacho. Ndipo wakaagiza ‘majenereta' ambayo hayakuweza kufika kwa muda muafaka. Wakaanza kuyatengeneza, na ‘kuyaseti' ili baadaye yazalishe umeme (ndiyo kumweka mtu kwenye sanduku kwa taratibu huku watu wakiangalia). Wakaleta na wapiga picha Uwanja wa Ndege wa Mwalimu J.K. Nyerere kuona majenereta yanavyoletwa na ndege kubwa zaidi duniani ya mizigo. Watanzania wakapiga makofi na kushangilia.
Wakati watu wanajiuliza hivi kweli wataleta umeme hawa (je, kweli mtu ataungika?), basi wanamazingaombwe wa Richmond wakaanza kutuhamasisha pamoja na washirika wao (serikali) wakilumbana na kukandiana hadharani (distraction).
Lengo likiwa kununua muda. Wakati watazamaji (Watanzania) wakiendelea kushangaa nini kinaendelea, tukatangaziwa kuwa jenereta liko tayari kuanza kazi, na kwamba wanasubiri Tanesco wakubali umeme wao. Wakati huo wote, Richmond walikuwa wanasubiri mvua.
Hatimaye, dua zao zikasikika na mazingaombwe ya mwaka yakafanyika. Mabwawa ambayo yanatumika kuzalisha umeme yakajaa maji, umeme wa Richmond haukutumika, mkataba wa Richmond na Tanesco ukauzwa kwa kampuni nyingine ya kigeni, ambayo tuliambiwa kuwa ina uwezo wa kuifanya kazi ya Richmond, mwenye kutengeneza pesa akatengeneza pesa, na Watanzania wakabakia kushangilia umeme wa kudumu.
Rais Jakaya Kikwete akashangilia na kuwapongeza viongozi wenzake majasiri, hodari na makini kwa jinsi walivyoshughulikia tatizo la umeme.
Onyesho la mazingaombwe la Richmond likafanyika kwa ufundi mkubwa. Kwa vile Watanzania hawajagundua kuwa wameshuhudia mazingaombwe, basi mwaka huu wanasubiri onyesho jingine lenye kuhusu mkataba mwingine, na gurudumu la mazingaombwe na viinimacho linaendelea kubingirishwa. Ndugu msomaji, ingawa makala hii imeonekana kuwa na mzaha kwa kiasi fulani, lakini hicho ndicho ambacho kimetokea.
Hata umeme wa Richmond usingekuwapo sasa, Watanzania tungepata umeme kwa kuwa Mungu amesikia kilio chetu na kuleta mvua, lakini pia lazima kujiuliza, kwanini Richmond wameuza kampuni yao kwa wengine, kuna nini? Watawala wanapaswa kutuambia.
Je, hawana uwezo? Au wanaogopa kwamba wanaweza kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria hapo baadaye? Je, ni Richmond ndio walitafuta hii kampuni ya kuinunua?
Kwanini Tanesco ilikubali kuiuza haraka haraka tena hivyo? Haya ni maswali mengi ambayo Watanzania wanapaswa kuambiwa na serikali yao waliyoiweka madarakani. Watanzania katika zama hizi za utandawazi hawataki tena kitu kinachoitwa mazingaombwe. Huu ni wakati wa sayansi na teknolojia. Mazingaombwe, hayatatufikisha kokote, na ndoto zetu zitabakia tu kuwa ndoto za alinacha.
Watawala hebu tuambieni kisa cha Richmond kukimbia dili za fedha za walipa kodi.
Haiingii akilini kwamba umeanza mradi, hata bado hujaona matunda yake na kuamua kuuza kwa watu wengine. Kuna jambo ambalo limejificha, Watanzania wanataka ukweli wa jambo hili, msipofanya hivyo hawatawaamini, na umaarufu wenu utaendelea kushuka kila kukicha, jinsi pia hali zao za kiuchumi zinavyoshuka kila kukicha.
Mwisho nawatakia mwaka mpya, na kuwaambia watawala wasikubali mazingaombwe ya aina hii, werevu watatucheka.
Dennis Msacky ni mwanahabari mwandamizi, na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa
Email:
msackyd@yahoo.com