Maulid Ahamed, Dodoma
HabariLeo; Friday,February 02, 2007 @00:06
WABUNGE wa chama tawala, CCM, jana walikutana kwa faragha mjini hapa, kujadili masuala mbalimbali, huku suala la kampuni iliyokuwa imepewa tenda ya kuzalisha umeme, Richmond iliyouzwa kwa Dowans, likichukua nafasi kubwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambacho Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, Edward Lowassa, zilibainisha kuwa suala la Richmond lilizungumzwa kwa kina, huku waziri wa sasa wa Nishati na Madini, na aliyemtangulia, wakitakiwa kutoa maelezo kuhusu kilichosababisha kampuni hiyo kukwama kuzalisha umeme, kwa mujibu wa mkataba.
Mawaziri hao ni Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa waziri wa wizara hiyo kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika mabadiliko ya Oktoba mwaka jana, na aliyemrithi, Nazir Karamagi.
Hata hivyo, mtoa habari ndani ya kikao hicho alieleza kuwa suala hilo lilionekana kuwakera wabunge wengi wa CCM, na baadhi yao wakaonyesha wasiwasi wao kuhusu kwa nini Dk. Msabaha atoe maelezo wakati amekwisha kuondoka katika wizara hiyo inayosimamia nishati nchini.
Wabunge wengi waliuliza kwa nini Msabaha ajieleze wakati amekwisha kuondoka wizara ile. Wanahoji kuwa kwa utaratibu wa Serikali, Waziri anapoondoka, anayemrithi ndiye anayewajibika kwa suala husika kwa wakati uliopo.
Wanahoji kuwa kama Msabaha hakupaswa kulizungumzia suala hilo na badala yake, Karamagi pekee ndiye mwenye jukumu la kulielezea. Je, leo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, aitwe kujieleza kwa mambo yaliyofanyika wakati wake? alieleza mmoja wa wabunge wa CCM aliyeshiriki kikao hicho.
Inaelezwa kuwa Dk. Msabaha alipewa fursa ya kueleza hali ilivyokuwa hadi kampuni hiyo ikashinda tenda ya kuzalisha umeme huo, lakini ikakumbwa na matatizo na kusababisha minongono mingi kuwa kampuni hiyo inahusika na baadhi ya vigogo katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Hata hivyo, licha ya wabunge hao wa CCM kuwa na shauku ya kutaka kujua ukweli kuhusu kampuni hiyo ambayo ilipaswa kuzalisha megawati 100, lakini ikazalisha megawati 20 tu, dukuduku lao litabidi lisubiri kwa muda ili kujua ukweli.
Imeelezwa kuwa sasa suala hilo linasubiri ripoti ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo (CCM), ambayo iliamua kulivalia njuga kutaka kujua ukweli. Hata hivyo, haijajulikana ni lini wabunge hao watakutana tena kuzungumzia ripoti hiyo, ingawa inaelezwa kuwa itakuwa kabla ya kumalizika kwa kikao cha sasa cha Bunge, Februari 16, mwaka huu.
Tumeelezwa kuwa suala hili tusubiri ripoti ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara, na baada ya hapo, tutakutana tena kabla ya kumalizika kwa kikao hiki cha Bunge. Inaweza kupangiwa siku za Jumamosi au Jumapili, au muda mwafaka ukipatikana, alisema mmoja wa wabunge hao wa CCM aliyehudhuria kikao cha jana mchana. Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya mradi huo jana jioni, Waziri Karamagi alisema tatizo lililoikumba kampuni hiyo ni mvua, hali iliyofanya ishindwe kuweka mitambo hiyo.
Kutokana na sababu hiyo, Kampuni hiyo haitapewa adhabu ya kulipa fidia.