Warithi wa Richmonds mahakamani
Wabunge kutembelea eneo la mradi leo
Na Waandishi Wetu
WAFANYAKAZI waliotimuliwa kampuni ya Dowans SA, wameenda katika Mahakama ya Kazi kuwasilisha malalamiko yao kuhusu stahiki zao kikazi, imebainika.
Wakati hayo yakijitokeza leo Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, inatembelea miradi ya dharura ya uzalishaji wa umeme ili kujionea hali halisi.
Kwa upande wa wafanyakazi, wameichukua hatua hiyo kutokana na kutoridhishwa na 'mafao' waliyopewa na jinsi haki ya ajira yao ilivyochukuliwa na wawekezaji hao, waliotwaa majukumu ya kampuni ya Richmonds Develepment.
"Tumeenda Mahakama ya Kazi na nadhani tutaenda kuchukua barua zetu (ya kuanza shauri)," alisema mfanyakazi mmoja alipozungumza na gazeti hili jana.
Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili imelipata, waajiriwa hao wa Dowans walienda mahakamani kutafuta haki, baada ya kulipwa sh. 80,000 kila mmoja ikiwa ni baada ya kutoa shinikizo la kudai haki yao.
Mfanyakazi huyo, alisema walichukua hatua ya kwenda mahakamani baada ya mmoja ambaye ni mlinzi kulipwa sh. 60,000 na mwingine ambaye aliongezewa majukumu ya uhudumu, alikuwa analipwa sh. 85,000.
Waajiriwa hao walianza ajira tangu zama za kampuni ya Richmonds, ambapo iliuza shughuli na mali zake kwa Dowans.
Haijajulikana maudhui ya mkataba wa mauzo ya Richmonds kwa Dowans na mkataba mkuu na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) uliowezesha Richmonds kupewa kandarasi.
Pia, mmoja wa wafanyakazi hao kabla ya kuchukua hatua, alisema walimfuata mwajiri wao wa zamani, aliyekuwa Meneja Mradi wa Richmonds, Naem Gire, ambaye aliwapa baraka kwamba wana haki ya kwenda kwenye sheria, iwapo wataona kuna haja ya kufanya hivyo. Gire yupo nchini tangu mwisho wa wiki iliyopita.
Hii ni mara ya pili kwa Gire kutoa kauli ya kuitaka Dowans iwalipe wafanyakazi aliowaajiri Septemba mwaka jana. Mara ya kwanza alifanya hivyo mwezi uliopita akiwa nje ya nchi na uongozi wa Dowans ulitii.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, leo inatembelea miradi ya dharura ya uzalishaji wa umeme ili kujionea kama kuna kazi yoyote inayofanyika kwa mujibu wa mkataba.
Wakati kamati hiyo imeamua kufanya ziara hiyo, wajumbe wake pia wametaka kuundwa kwa tume kuchunguza kwa nini Richmonds ilipewa kazi ya kuzalisha umeme wa megawati 100 wakati haikuwa na uwezo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema jana kuwa uamuzi wa kutembelea miradi hiyo unafuatia kikao cha jana baina yake na Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO.
Alisema kamati itafanya ziara hiyo katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam ambako kampuni ya Dowans SA inaendeleza miradi hiyo baada ya kampuni ya Richmonds kushindwa.
"Baada ya kujadiliana kwa muda, kamati imeona ni vyema ikaenda kujiridhisha na kazi inayoendelea na hatimaye kupata jibu la uhakika, tofauti na ambavyo imekuwa ikielezwa," alisema.
Richmonds iliingia mkataba na serikali kwa ajili ya kuzalisha umeme wa megawati 100 lakini ilishindwa kufanya hivyo na ilidai kufanikisha kuzalisha megawati 20 tu.
Kampuni hiyo iliuza kazi kwa Dowans ambayo pia imekuwa ikisuasua kutekeleza mradi huo ambao kwa mujibu wa ahadi unatakiwa kukamilika takriban wiki tatu zijazo.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati walitaka kuundwa kwa kamati ili kuchunguza sababu zilizofanya Richmonds kupewa kazi ya kuzalisha nishati hiyo wakati wa mgawo mwaka jana.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo, zilieleza kwamba wajumbe hao ambao ni wabunge, walionyesha nia hiyo wakati wa mjadala uliodumu kwa zaidi ya saa nne kati ya kamati na TANESCO.
Wakizungumza kwa masharti ya kutokutajwa majina, wabunge hao walisema katika kikao hicho walichachamaa na kuibana bodi ya TANESCO kujua ni kwa nini ilikubali kuingia mkataba na kampuni hiyo huku ikijua haina uwezo wa kuzalisha hata megawati moja.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wajumbe hao, TANESCO ilidai ilifanya hivyo kwa kufuata maagizo kutoka kamati ya majadiliano ya kimataifa ambayo inajumuisha makatibu wakuu wa wizara kadhaa, akiwemo wa Wizara ya Nishati na Madini.
Vile vile, wajumbe wa kamati waliibana TANESCO kueleza kwa nini imeamua kupandisha bei ya umeme ambapo ilijibiwa kuwa ni kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na ununuzi kutoka kwa kampuni zinazozalisha nishati hiyo.