Mambo hayoo
Jina Richmond lazua balaa Dar
na Lucy Ngowi
KASHFA ya Richmond iliyosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wiki iliyopita, na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri, imeanza kuzua balaa katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam.
Balaa hilo limeanza kuwakumba wamiliki wa majengo mawili tofauti ya Richmond Hill na Richmond Tower ambao sasa wanalazimika kuanza kazi ya kungoa vibao vilivyoandikwa Richmond kwenye majengo yao hayo baada ya kuwapo kwa tishio la wazi dhidi ya biashara yao.
Tanzania Daima jana ilishuhudia mafundi wakimalizia kungoa maandishi yanayongara yaliyoandikwa Richmond Hill katika moja ya majengo hayo mawili, lililopo Mtaa wa Chake Chake, Masaki, Dar es Salaam.
Walipofika waandishi wa Tanzania Daima katika eneo hilo, mafundi hao waliacha kuendelea na kazi ya kumalizia kungoa maandishi mengine yaliyokuwa kwenye jengo la pili ambalo nalo lilikuwa na maandishi hayo hayo.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi wa Kampuni ya OMIMS Ltd inayomiliki majengo hayo pacha ya Richmond Hill, Sultan Mitha, alisema walilazimika kuyangoa maandishi hayo baada ya kubaini kwamba yamekuwa yakiwaletea matatizo yanayoathiri biashara tangu Kamati ya Teule ya Bunge iwasilishe ripoti yake bungeni wiki iliyopita.
Akitoa mfano, Mitha alisema siku tatu zilizopita, mmoja wa wateja wao ambaye ni Mzungu alikabiliana na usumbufu wa kutupiwa mawe na wananchi wakati akiwa katika gari lililoandikwa Richmond.
Tumeamua kufuta kwa sababu watu wanapiga mawe magari yetu wakati hawajui kuwa, hakuna uhusiano wowote kati ya Kampuni ya Richmond yenye kashfa na hii ya kwetu. Hili ni jina tu la kibiashara tunalitumia.
Tumeamua kufuta maandishi haya kwenye majengo yetu na magari ya wateja wetu, kwa sababu watu wanayapiga mawe, alisema mkurugenzi huyo.
Katika kuonyesha tofauti kati ya kampuni yao na ile ya Richmond Development Ltd, ndugu wa Mitha aliyejitambulisha kwa jina la Jaffary Mohammed, alisema wao hawawafahamu kabisa wakurugenzi wa kampuni hiyo yenye kashfa.
Kwa kweli tunasikitika kwa kuwa hatuna uhusiano wowote wa kibiashara, ila tunasoma tu kwenye vyombo vya habari, alisema Mohammed.
Alisema ujenzi wa majengo hayo ambayo ni makazi ya watu, ambayo hadi sasa zinaishi jumla ya familia 86, ulianza mwaka 2000 na ukakamilika mwaka 2004.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, jengo la Richmond Tower lililopo Mtaa wa Mindu, lina familia 62 wakati lile la Richmond Hill la Masaki lina familia 24.
Habari zaidi kutoka eneo la tukio zimeeleza kwamba, miongoni mwa watu wanaoishi katika majengo yanayomilikiwa na kampuni hiyo, ni watoto wa waliokuwa mawaziri wawili katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa wiki iliyopita ambao hawakuteuliwa katika serikali iliyotangazwa majuzi.