Dar Jazz waliiona Richmond zamani
Ibrahim Mkamba Machi 5, 2008
KINYUME cha matarajio yangu, makala yangu iliyohusu uoga wa wasanii wa leo katika kupambana na ufisadi katika jamii yetu (toleo namba 017, Februari 20-26,2008) ilipata napokezi mazuri kwa wasomaji wa gazeti hili.
Lawama, manung'uniko, masahihisho, pongezi vilitawala ujumbe mbalimbali wa barua pepe na simu niliopokea kuhusu mada hiyo.
Kilichofurahisha zaidi ni kwamba miongoni mwa waliochangia mada hiyo ni Mwana Hip Hop maarufu nchini Afande Sele mwenye makao yake mjini Morogoro.
Kutokana na michango hiyo, leo nimeona tuwekane tena sawa katika kuukabili ufisadi kwa njia ya sanaa. Kwa sababu hiyo, makala niliyoiandaa kuitoa wiki hii ya kuzungumza na dada zetu wanamuziki, itabidi isubiri hadi wiki ijayo.
Kwa ufupi sana, mwanamuziki Afande Sele anayetamba na vibao kama "Acha Kupiga Mayowe," "Darubini Kali" na "Uwanja Mpya wa Taifa," amesema kwamba Hip Hop, kama inavyojulikana, ni muziki wa mapambano na ukombozi.
Wana Hip Hop wa Tanzania, akiwamo yeye, wanalifahamu vizuri sana jukumu hilo lakini wanashindwa kutimiza vizuri wajibu wao kwa jamii si kwa uoga bali kwa kukwamishwa na mfumo wa biashara ya muziki nchini.
Amesema, mara zote wadau wakubwa katika biashara hiyo ambao ni mawakala na ma-DJ wa Redio hupendelea nyimbo za kuimba za mapenzi na za majisifu hata zisipokuwa na ujumbe wowote wa maana na kuiwekea vikwazo Hip Hop.
Hip Hop yenye ujumbe mzito huwekewa vikwazo siku zote kwa madai haina biashara nzuri wakati si kweli kutokana na jinsi inavyopendwa kuliko aina yoyote ya muziki.
Kimsingi Afande Sele anajitetea yeye na wana Hip Hop wenzake kwamba hakuna uoga wowote kwa upande wao katika kupigana vita dhidi ya ufisadi bali wanakwamishwa na watu wengine kwani mapambano ndiyo kazi yao.
Kwa upande wangu pia naomba nijitetee kwamba kwa mimi kutoitaja Radio One na ITV katika kuzungumzia uamuzi wao wa kuacha kutangaza habari za Simba Sports Club, si uoga kama wengi walivyonieleza bali ilikuwa ni njia ya kiungwana ya kumshauri mwenye akili timamu na busara ya kawaida abadilishe msimamo usio na tija.
Kama njia ya kutomtaja haisaidii, hapo ndipo tunapoweza kuambiana uso kwa uso kwamba wenzetu ITV na Radio One mnatuaibisha, hata kwenye msimamo wa ligi Simba haimo?!
Huu ni uhabarishaji wa wapi wa kupotosha hivyo? Ikitokea wakachukua ubingwa mtatangaza bingwa ni nani,wa pili yake? Ikitokea wakafanya makubwa sana katika mashindano ya vilabu barani Afrika, hamtasema chochote?
Wapenda soka hatujisikii vizuri vyombo hivyo kuitwa vya Yanga kwa kutoitangaza Simba ambayo kwa soka letu la hapa ni kama pacha wa Yanga. Jina hili la kibaguzi linaonekana ni jina sahihi hasa kwa Redio One inayotoa muda mwingi kwa habari za Yanga tangu waisuse Simba!
Uoga wangu ungesababishwa na nini katika kuvitaja vyombo hivyo wakati maajabu yao hayo yanajulikana na kila mtu isipokuwa labda kwa viongozi wao kama alivyohisi mwandishi mmoja mwandamizi wa habari?
Katika barua pepe aliyonitumia, mwandishi wa habari huyo alieleza kwamba huenda viongozi wa vyombo hivyo hawalijui hilo kwa hiyo vitakapotajwa, viongozi hao wataamshwa.
Naamini sasa watakuwa wameamka kama kweli walikuwa wamelala na kama kweli hawana mkono kwenye maamuzi hayo ya ajabu. Nasema hali hiyo ilifahamika na wengi kwani kila aliyenishutumu alivitaja vyombo hivyo na klabu hiyo.
Hakuna aliyeniuliza nilikuwa nazungumzia vyombo vipi vya habari na klabu gani ya soka.
Tukiachana na hilo, si suala la kubishana kwamba zamani sanaa ilitumika sana kupiga vita ufisadi. Kazi ya sanaa ilivyo ya kifasihi ni kazi ambayo kamwe haifi bali hujibadilisha umbo lake kutegemeana na mabadiliko ya matukio kwa nyakati tofauti kutegemeana na tafsiri ya matukio ya nyakati husika.
Kwa mfano, wimbo "Chawa" wa Jamhuri Jazz Band (Wanyama Wakali),Wana Dondola wa jijini Tanga uliorekodiwa mwaka 1971 unaoanza na maneno "Chawa umenisumbua kwa muda mrefu chawa, najitolea chawa leo sikutaki tena..."
Kwa wakati ule ungetafsiriwa kwamba Wanyama Wakali walikuwa wanamfukuza mnyonyaji katika kutekeleza siasa iliyokuwapo wakati huo ya Ujamaa na Kujitegemea lakini leo utatafsiriwa kumfukuza mgeni anayepora mali yetu kwa njia ya utapeli wa kimataifa ya uwekezaji.
Ni katika muktadha huo ndipo inapoonekana wazi kuwa utunzi wa Dar Jazz, wana Mundo, Majini wa Bahari wa mwanzoni mwa miaka ya 1970 uliyalenga vizuri sana matukio ya leo ya kifisadi kama wa Richmond.
Wimbo huo unaimbwa hivi: "Haifai kwenda kusimama juu ya milimaa,kupokea mapesa kwa mabepari, kwa kutaka kuiangamiza nchi yee, haifai. Tizameni nyie mambo mnayotakaa kuyafanyaa, ni mabaya sana, roho za watu zitakuja kupotea na wakati huo Mungu atakuja kaasirika, haifai."
Baadaye korasi inasema: "Tanzania itakuja chanika oo, na mambo yote yatakuja haribikaa, itakuja kuwa hasara ya nchi. Tanzania itakuja jaa motoo..."
Kifasihi, wana Mundo waliposema "Haifai kwenda kusimama juu ya milima" walimaanisha haifai kujikweza, kutumia madaraka vibaya na kufanya mambo kwa niaba ya umma kwa siri kama ilivyo siri mikataba ya kuuza rasilimali zetu kwa watu wa nje wanaoitwa Wawekezaji.
Waliposema "kupokea mapesa kwa mabepari" walimaanisha kuuza raslimali za nchi kwa rushwa, au kuingia mikataba ya "Ki-Richmond" kwa vipato binafsi visivyo halali. Waliimba "roho za watu zitakuja kupotea" wakimaanisha matendo hayo yataathiri vibaya sana uchumi wa nchi na kuwafanya baadhi ya wananchi kufa kwa kushindwa kuyamudu makali ya maisha kwa kukosa uwezo wa kupata chakula cha kutosha na pesa ya matibabu.
Majini wa bahari walipoimba "Mungu atakuja kasirika" walimaanisha Mungu hatafurahishwa na dhambi ya viongozi mafisadi dhidi ya sisi wanaotuongoza. Baadaye kwenye korasi waliimba "Tanzania itakuja chanika" wakimaanisha ufisadi utatugawa katika matabaka na kuibuka kwa chuki ya ajabu baina ya tabaka la mafisadi wanaoneemeka kwa mgongo wetu na tabaka la sisi waathirika wa ufisadi huo na hapo "mambo yote yatakuja haribika" kama walivyoimba na wakamaliza kwa kuimba:
"Tanzania itakuja jaa moto" wakimaanisha ufisadi huo utasababisha machafuko makubwa na amani tunayojivunia itatoweka vibaya sana baada ya kuimarika kwa matabaka yatakayojengwa na ufisadi huo. Hiyo ndiyo kazi ya Dar Jazz waliolizungumzia kifasihi suala la Richmond miaka zaidi ya 35 nyuma!
Mfano mwingine wa kazi za zamani za fasihi ambazo maudhui yake yanadumu hadi leo ni kidokezo kimoja, kati ya vingi, cha Radio Tanzania Dar es Salaam kabla ya taarifa za habari kwenye miaka ya mwanzo ya 1970 hadi katikati ya miaka hiyo kinachokwenda hivi: Zinaanza sauti kakamavu za kike:-"Chungua uchumi wao, hawawezi kuishi kama sisi".
Baadaye inafuata sauti ya kiume ikitamka neno moja moja: "Maisha ya kibepari ni maisha ya uhasama, maisha yenye dhuluma. Binadamu wazima na fahamu zao, huishi kama wanyama wa porini ambao uhai wa kila mmoja wao hutegemea ujanja wake wa porini, urefu wa makucha yake na ukali wa meno yake.
Ubepari ni unyama. Ujamaa, ujamaa, ujamaa ni utu, ni utu, ni utu."
Leo hii kidokezo hicho kinafaa kiwe hivi:-"Chungua matumizi yao ya madaraka, hawana chembe ya uchungu na sisi".Kisha: "Maisha ya kifisadi ni maisha ya uhujumu uchumi, maisha yenye dhuluma. Binadamu wazima na fahamu zao, huishi kama wanyama wa porini ambao uhai wa kila mmoja wao hutegemea ujanja wake wa porini, urefu wa makucha yake na ukali wa meno yake. Ufisadi ni unyama. Uadilifu, uadilifu, uadilifu ni utu, ni utu, ni utu."
Swali ambalo limekosa jibu, ukiondoa jibu la Afande Sele la mwanzo wa makala hii na ushujaa wa Dada Irene Sanga katika tunzi zake za ukombozi mamboleo, ni sababu gani inayofanya wasanii wa leo tuwe waoga. Katika kujadili hilo, kila mmoja alimnyooshea kidole mwingine kuwa muoga na hapo ndipo nilipoingizwa.
Wengine wakasema "mbona RTD na TvT wanaogopa kusoma magazeti ya Tanzania Daima, Raia Mwema na MwanaHalisi?"
Nikashangaa. Katika dunia ya sasa chombo cha umma kinafanya hivyo kwa maelekezo ya nani au uoga tu wa watendaji wenyewe! Kuna nini cha kuogopa kwenye magazeti hayo kisichoandikwa na yale yanayosomwa?
Hata hivyo, nilipolitafakari hilo, nikafikia kwenye hitimisho kwamba hiyo si sera ya uongozi wa vyombo hivyo bali ni uoga tu wa watangazaji wenyewe kwani TvT ina vipindi vingi vya watu mbalimbali kutoa maoni yao yoyote yale kwa uhuru.
Miongoni mwa vipindi hivyo ni "This Week in Perspective", "Bungeni Wiki Hii" wakati wa vikao vya Bunge na "Tuambie", hasa kilichorushwa Alhamisi ya Februari 28,2008 kuhusu matukio baada ya uchaguzi wa Kenya na funzo kwa Tanzania.
Kwa upande mwingine,Yussuf A. Marare wa Musoma mjini aliniomba niwaondoe washairi katika orodha ya wasanii waoga kwani wao huzungumza chochote cha manufaa kwa umma bila hofu.
Alitoa mfano wa shairi lililojibiwa kwa shairi bungeni na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa. Baada ya kunikumbusha hilo, alinipa zawadi ya shairi lifuatalo la beti nne:-
Tulimzika Mwalimu,pamoja na uzalendo
Wakabaki madhalimu, watu bila ya upendo
Nchi wanaihujumu, kwa uovu wa matendo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu
Nchi imekosa sudi, maadili na mwenendo
Imejaa mafisadi, wala rushwa na uvundo
Hatuendi tunarudi, kama ni huu mtindo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu
Tuliowapa dhamana, tena ya jembe na nyundo
Wamekosa uungwana, kwa kashfa lundo lundo
Kama hii si laana, mbeleni chaja kishindo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu
Wametoka haidhuru, maji yafate mkondo
Sheria itunusuru, wawekwe nyuma ya nondo
Mikataba ya kufuru, isirejee mtondo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu.
Tufuate nyayo za wasanii wa zamani, washairi wa nyakati zote na wana Hip Hop wetu wa leo katika kuupiga vita ufisadi. Kwa wanamuziki wote, hasa wa Bongo Flavour, tusidanganyane kwamba nyimbo za mapambano, zisizo za mapenzi, ni hasara na haziwezi kumfanya mtu atoke.
Wimbo wa "Ndiyo Mzee" ulimtoa Professor Jay wakati "Tanga Kunani" iliwatoa Wagosi wa Kaya ambapo sasa "Mr Politician" inamtoa Nakaay.
Tuwe wazalendo, tutumie sanaa zetu kuikomboa nchi yetu dhidi ya ufisadi. Hatuna sababu ya kuogopa kwani Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wake, Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Mkuu wetu Mizengo Kayanza Peter Pinda hawana hata harufu ndogo ya ufisadi, ni wasafi. Ni wazi watafurahia kazi zetu kwani hata wao wanauchukia ufisadi.Ufisadi ni unyama.
0713 297085
Barua pepe:
ibramka2002@yahoo.com