Sakata la Kashfa ya Richmond: The Facts

Je Kweli tutafika?


``Suala la Richmond tuanze kumuuliza Mkapa, sababu IPTL sio ya leo wala ya jana, tunawapa bilioni tatu, tunawalipia kodi ya jengo, kiwanja NSSF, kodi ya maendeleo... sasa TANESCO imekuwa kama mzambarau usiokuwa na mwenyewe, kila mtu anautingisha na kuvuna. Halafu wanatueleza shirika halina ufanisi vipi,``
 
Kwa ufupi katika nchi yetu inaonekana kiasi cha pesa kinachopotea kwa siku ambacho wavuja jasho wanazalisha kingeweza kukidhi 75% ya mahitaji ya watanzania, na cnhi ikatoka katika umasikini uliokithiri na kurudi katika maisha ya kawaida. Hali hii inatisha
 
Naona vidole vinazidi kuelekezwa kwa Rais Mstaafu, Mh. Mkapa. Is he the father of all big scandals as we know them today?!!

Moto ukipamba kwenye makampuni kama Tanesco na kutapakaa kwenye makampuni mengine makubwa nchini, nina imani nguvu ya Watanzania itakuwa imeunganishwa katika kuonesha kuwa maisha duni na gharama za maisha nchini zinasababishwa na viongozi wetu wenye uchu wa mali. Na ni nguvu na mshikamano kama huu ndiyo utakao weza kutetea maslahi yetu sote. Tusiwatenge Tanesco, tuwaunge mkono na kuendeleza harakati za kuikomboa nchi yetu.

Source: ippmedia.com


SteveD.
 
WAFANYAKAZI wa Shirika la Umeme (Tanesco) wamecharuka na kutaka viongozi na watendaji wengine serikalini walioliingiza shirika hilo katika hasara kwa kusaini mkataba na kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, washitakiwe haraka.

Wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wametaka Rais wa awamu ya tatu, Bw. Benjamin Mkapa, afikishwe mahakamani na kufilisiwa mali zake kwa madai kuwa yeye ndiye chanzo cha mikataba mibovu wakati alipokuwa madarakani.

Kama Taifa huru la Tanzania Lingepata nguvu ya umma ya Watanzania wafanyakazi kwenye mashirika muhimu kadhaa wakashinikiza "USAFI WA TAIFA" kwa ngazi ya mfano wa shirika la umeme nafikiri mwendo wa tunapotaka kwenda ungeshika kasi nzuri. Kwa kando vyama vya upinzani viongeze jitihada ya ufuuatiliaji wa yale ambayo wameshayaweka hadharani...bunge nalo mwendo uwe ule tulio uona..JF tuendeele kunganisha habari, vyombo vya habari viwe serious kwenye ukweli, uzalendo na utaifa ...Nafikiri huku "kusafishana" kunakofanywa na hawa viongozi kungekosa nguvu na kuonekana ni michezo ya kitoto iliyopitwa na wakati kwa taifa kama Tanzania. Tunahitaji nguvu ya umma kuovercome..Uongozi uliopo...Kinachoonekana hawa viogonzi wala hawajaamka ..kuhusu ufisadi...wote ni kama wanafikiri wameonewa..it really suprising,wanajidangaya, wameamua kushikana mikono watasaidiana...wafe pamoja...Hii iskubalike. Na dawa ya kuvunja huo mchezo ni kuwafanya wanachi waungane..na hawa viogozi waone kuwa hata wakijikusanya pamoja it wont work...Na wafanyakazi wa mashirika mbalimbali..ni Resource ya msingi! They should keep it up!
 
Na umeme wa MKapa wa Kiwira unakuja wa 300 milioni kwa siku. Yaani TANESCO ni chaka la mafisadi.
 
Mafisadi wa Richmond nao warudishe pesa haraka sana na TANESCO ijitoe katika mkataba wake na kampuni ya fisadi Mkapa, Kiwira Coal Mining ambao utaigharimu TANESCO shilingi bilioni 326

Richmond yaibua makubwa TANESCO

na Salehe Mohamed
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

WAFANYAKAZI wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), wametishia kuwaburuza mahakamani watu walioingia mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya shirika hilo na Kampuni ya Richmond.

Aidha, wafanyakazi hao wametaka kusimamishwa malipo kwa Kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba huo.

Wafanyakazi hao walitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa kujadili masuala mbalimbali ya shirika hilo na kueleza kushangazwa na kitendo cha kuendelea kuilipa kampuni ambayo msingi wake unatokana na mkataba uliohusisha kampuni hewa.

Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano ya wafanyakazi hao, Abdul Mkama, alisema hakuna sababu kwa Tanesco kuendelea kuilipa shilingi milioni 152 kwa siku, kampuni ambayo imedhihirika kuwa ilishinda zabuni kifisadi.

Sambamba na hayo, alisema ni vema watu waliojiuzulu wakarudisha fedha hizo kama inavyofanyika kwa watu waliochukua fedha katika akaunti ya malipo ya nje (EPA), na baada ya kufanya hivyo, wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Sisi wafanyakazi wa Tanesco, tunataka malipo yanayofanyika kwa Richmond yasimamishwe kuanzia leo (jana), na tunafanya taratibu, ili wahusika watulipe fidia, wasipofanya hivyo tutawaburuza kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mkama.

Naye, Balton Mwaifugile, alisema viongozi waliojiuzulu ni sehemu ndogo ya mafisadi, hivyo ni vema waliobakia nao wakaanikwa hadharani, ili kukomesha tabia ya kufuja mali za umma kwa maslahi binafsi.

Alisema wanachohitaji wao ni kulipwa fidia kwa hasara iliyopatikana, kwani fedha hizo ni nyingi na zingewasaidia kuboresha maisha yao na mitambo ya shirika hilo.

“Tunawalipa hawa jamaa wa Richmond milioni 152 kwa siku, Songas milioni 200 kwa siku na IPTL sh bilioni tatu kwa mwezi. Fedha hizi ni nyingi, na kuanzia leo tunataka tuanze kuwashughulikia kwa kutowapa fedha,” alisema Mwaifugile.

Alisema maisha ya wafanyakazi yamekuwa magumu na kupata majanga mbalimbali yaliyowasababishia ulemavu, huku wakilipwa fidia kidogo kwa madai shirika halina uwezo wa kuwalipa kutokana na fedha nyingi kuchukuliwa na mafisadi.

“Kabla ya ‘kuwanyonga’ mafisadi wetu, kwanza watulipe fidia kutokana na matatizo waliyotusababishia, ili na sisi tuishi kwa raha na kuendesha magari kama wanavyofanya wao na familia zao,” alisema Mwaifugile.

Kwa upande wake, John Mwandika, alisema hivi sasa kuna bomu kubwa linakuja nchini, kwani mradi wa kuzalisha makaa ya mawe ya Kiwira nao unatarajia kuanza kulipwa sh milioni 300 kwa siku utakapoanza uzalishaji.

Alisema mradi huo wa Kiwira utakuwa unatumia sh bilioni tisa kwa mwezi, gharama ambazo zinadaiwa zitabebwa na Tanesco, ambayo inaonekana mnyonge na sehemu ya kuchuma.

“Tanesco imefanywa mti wa mzambarau, kila mtu anakuja na kapu lake na kutingisha matunda, na kapu linapojaa huondoka na matunda,” alisema Mwandika.

Aidha, Thomas Njama, alisema wabunge wa Tanzania ni waoga, kwani suala la ubadhirifu katika Tanesco lilianza kwa menejimenti ya Net Group Solution ambayo kwa kiasi kikubwa ilivuruga muundo mzima wa shirika hilo.

Alisema uongozi huo kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, wamefanikiwa kuuza majengo mbalimbali ya Tanesco, ikiwepo kutoa Chuo cha Morogoro na kuuza kiwanda cha kukaanga nguzo kilichopo Mbeya.

Aidha, alisema ni vema kuanzia sasa Katiba ya Tanzania ikabadilishwa, ili kuweza kuwakamata marais ambao watakuwa wamefuja mali za umma kwa maslahi binafsi.

Alisema Mkapa alikuwa kinara wa kushinikiza mabadiliko katika shirika hilo kwa maslahi ya watu wachache, bila kuangalia athari kwa taifa.

“Hii katiba inayotoa kinga ya kutowashtaki marais pindi wanapondoka madarakani imepitwa na wakati, inafaa tuibadilishe, ili tuweze kumkaanga Mkapa,” alisema Njama.
 
Nimesikia na kusoma kwenye magazeti kadhaa ukisema kuwa umefunga Mjadara wa Richmond, Utajiletea matatizo mimi nafikiri ungetulia acha wananchi waseme hadi wachoke lakini kufunga hoja ambayo huku uraiani tunaiibua bila simile utakwazika Bure tuache tuseme hadi tuchoke pesa zetu milioni 152 kwa siku zinatuuma sana na tukikuona tunatamani tukutafune, na hasa hasa hao waliokupokea kwa kukushangilia maana mimi sipati picha walikupokea kama shujaa wa kula pesa yetu kwa siku au walikushangili kwa kurudi jimboni kwako salama bila kudhuriwa pale Bungeni na akina Anna Kilango Malecela? kwa nini wakushangirie wakati ulichokifanya ni makosa?

Wamasai Bwana ndio maana wanaitwa Richmond.
 


Mbona alishasema tayari kuwa suala la Richmond lilishafungwa na TAKUKURU na kina Mwakyembe waliendelea nalo. Wewe kama una data zimwage tu, usichechetuke na mpayuko wa EL.
 

http://www.newhabari.com/mtanzaniajumapili/habari.php?id=311&section=habari


Kuna maswali muhimu ya kujiuliza kuhusu mantiki ya habari hii.Moja la msingi ni WHY NOW?Jibu jepesi linaweza kuwa jitihada za makusudi za ku-downplay ishu ya Richmond kwa kuonyesha kiwa hiyo ni "cha mtoto" ukilinganisha na ufisadi wa Kiwira.Ni vema kukumbuka pia kuwa gazeti hili ni la Rostam,na kwa vile tunaambiwa kuwa nae ni member wa Agenda 21,basi pengine hii ni sehemu ya mkakati wa kundi hilo.Inawezekana kwamba pengine wameshindwa kumrubuni Mkapa kujiunga na kundi hilo,hivyo kilichobaki ni kummaliza.Well,though he deserves kibano kwa ufisadi wake,lakini sio thru mafisadi wengine ambao ajenda yao sio uchungu kwa nchi bali kupooza makali ya uanaharamu wao.

Tutaona mengi mno kati ya sasa na 2010,na iwapo Muungwana ataendelea na ubabaishaji wake katika kuchukua maamuzi ya haraka,basi asije shangaa nae akawa miongoni mwa wahanga wa jitihada za kuchafuliana majina.Na asipokuwa makini,atapigwa bao kwenye nomination ya mgombea wa CCM 2010
 

Watanzania wengi wana mawazo kama yale ya watu wa Kiteto ambao wameipa CCM ushindi juzi pamoja na dimbwi la uvundo na uozo .So be sure kwamba JK pamoja na uchafu wote huu anaweza kupeta vile vile .
 
Mlalahoi,

Nimevutiwa na analysis yako.

Ni kweli Taifa linapitia vuguvugu zito na kila mbinu zinatumika kwa wahusika kujijenga, kujiiimarasha na kujiosha ndani ya shamrashamra hizo.

Bado;

Mambo yafutayo yatabakia kuwa kweli hata katika mtikisiko na upotoshwaji kiasi gani.

1. Viongozi wote waliojiuzulu na walihusishwa na ufisadi wa RDC si viogozi bora kuliogoza taifa la Tanzania. Si haki wala sio sawa kabisa kuendelea kupewa nafasi za Uongozi wa Nchi ya Tanzania.

2. Raisi Mstaafa BW Mkapa na viogozi alioshirikiana nao walivunja maadili ya uongozi na hilo halimpi Mkapa sifa na wala sio la kuigwa na viongozi wengine duniani.

Ni kweli watakuja viongozi au mafisadi wengine kutumia hizo hatua mbili kwa maanufaa yao. Na hapo ndipo Wanahitajika good analysts kuona, kuchambua na kuisadia jamii kutokupotoshwa.

Na Hapo JF na vyombo vingine vya habari we have a lot to contribute!
 

Wasi wasi wangu ni kwamba kama hawa wadanganyika watachoka kusikiliza nyimbo wakaingia kudai haki zao kwa maandamano wakaja FFU na wao wasirudi nyuma itakuwaje ?
 
Tatizo la viongozi wetu ni kutojali hatma ya taifa hasa kwa kutofanya lolote (doing nothing) kwa matarajio kuwa upepo mbaya utapita tu na mambo yatarejea kuwa normal.Wasichojua ni kwamba Watanzania wengi wamechoshwa mno na ubabaishaji huu na wanakaribia breaking point.Mola epusha hilo,lakini ukweli unabaki kuwa pindi nguvu za umaa zitakapoingia mtaani hakuna cha ffu wala sungusungu wa kuzidhibiti.
 
*Waziri Nishati anaswa ofisini kwao usiku
*Katibu Mkuu akiri alionya, akapuuzwa


Na Hassan Abbas

HUKU wakionekana kuwa na ujasiri wa aina yake na uthubutu ambao chanzo chake kinapaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi, baadhi ya vigogo waandamizi serikalini sasa imezidi kuthibitika jinsi 'walivyoamua kufa,' kuhakikisha kampuni ya Richmond ya Kariakoo, Dar es Salaam, ikijinasibu kutoka Houston, Marekani, na kupata kila ilichokitaka katika zabuni ya umeme wa dharura, Majira Jumapili limebaini.

Kwa mujibu wa taarifa za mashahidi kadhaa walionukuliwa kwenye ripoti rasmi za Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dkt. Harrison Mwakyembe, nyendo za vigogo wengi serikalini wakati wa mchakato wa kuipa Richmond tenda, zilijaa mashaka.

Nyendo hizo zilistaajabisha na zilioonekana kulenga, kwa gharama yoyote, kufikia jambo moja adhimu; iwe isiwe, Richmond inapata ilichokitaka.

Saa tano usiku ofisi za Richmond

Akihojiwa na Kamati hiyo, gazeti hili limebaini, mmoja wa mashahidi muhimu walioifahamu Richmond, wakili Tahir Muccadam ambaye ni mmiliki wa jengo ambalo Richmond waliwahi kupanga na kuweka ofisi zao kabla ya kuvurumushwa kwa kushindwa kulipa pango, amemtaja Waziri Mwandamizi kuwa alikuwa akionekana mara nyingi kwenye ofisi za kampuni hiyo nyakati za usiku.

Waziri huyo ambaye wakili huyo alimtaja kuwa ni wa Nishati na Madini na alipoulizwa ni Msabaha (Dkt. Ibrahim), alifafanua kuwa ni yule aliyewahi kuingia matatizoni na aliyekuwa Marekani. Bw. Nazir Karamagi ndiye aliyechukua nafasi ya Dkt. Msabaha kwenye Wizara hiyo.

Bw. Muccadam akaiambia Kamati kuwa Waziri huyo alikuwa akifika kwenye ofisi hizo zilizokuwa Muccadam House, Upanga, Dar es Salaam akitumia gari binafsi na kwamba walinzi wa ofisi mbalimbali zilozoko kwenye jengo hilo walikuwa wakimuona na kumbaini.

Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Muccadam na wajumbe wa kamati hiyo ilikuwa hivi:-

Lucas Selelii: Lakini kuna habari nyingine tumezipata kwamba kwa influence ya kwako ya uanasheria na influence ya Mzee uliwapa contact kupita milango, mikubwa mikubwa ambayo siyo rahisi kuingia kwao, ndiyo ulisaidia kuwafungulia milango kwa maana ya wakubwa.

Tahir Muccadam: Mheshimiwa Mwenyekiti sijaelewa kwa vipi, make it more clear (fafanua).

Lucas Selelii: Kwa sababu ulimpokea Naeem (Gire, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Richmond upande wa Tanzania) na umekuwa naye siku zote (akiwa mpangaji) na unamfahamu(walicheza na kusoma pamoja).

Kwa kutumia ile hadhi uliyonayo ya uanasheria na ya mzee marehemu (Mzee Muccadam aliyekuwa wakili maarufu wa CCM na viongozi kadhaa), uliwasaidia kuwatambulisha katika maeneo makubwa makubwa ya watu wakubwa. Unakumbuka kitu cha namna hiyo?

Tahir Muccadam: Mheshimiwa Mwenyekiti, Naeem alikuwa ananiambia wanatafuta ofisi na kuna jenereta wanataka kuleta, sijui nasikia kuna watu mbalimbali watawapa commission sijui tenda kitu kama hivi.

Na wakadeal sijui na Mkurugenzi wa TANESCO lakini picha hasa ninavyoona mimi kutokana na maoni yangu mpaka kupata ile contract, nahisi probability, Im not so sure, lakini nahisi labda Waziri wa Nishati na Madini anaweza akawa ame-involve sana.

Lucas Selelii: Bw. Msabaha au huyu wa sasa (wakati huo Nazir Karamagi)?

Tahir Muccadam: Yule ambaye alikuwa katika zile problem, sijui alikwenda Marekani. Unajua Naeem alikuwa mtu wa kujisifu (proud). Nimepata tenda na hivi na nini, Waziri anakuja kunitembelea. Halafu kuna ushahidi Waziri alikuwa anakuja saa nne usiku, saa tano usiku pale kwetu, usiku mara nyingi.

Lucas Selelii: Pale kwako au kwa Neem?

Tahir Muccadam: Ofisini pale

Lucas Selelii: Upanga?

Tahir Muccadam: Upanga, na walinzi wapo ambao tulishuhudia, tulimwona watu wote. He has to come many times (alikuwa akija mara nyingi). Wanapigiana simu wenyewewe, wanakutana.

Lucas Selelii: Lakini wewe ni mwanasheria, hivi ni kitu cha kawaida kweli Waziri kwenda kwenye...!

Tahir Muccadam: Na mimi I a m also surprised, maana yake nashangaa na system mtu Waziri una ofisi yako mwenyewe... unakwenda katika ofisi kama ile ya Richmond, I am very surprised.

Waziri ataka kumwaga fedha

Mbali na ushahidi huo mzito wa wakili Muccadam, sakata la vigogo kuonekana kuwa tayari 'kufa na Richmond,' linaonekana kuwa na mtandao mpana unaorejea hadi enzi za utawala wa Awamu ya Tatu, ambapo ndipo kampuni hiyo ilipoingia rasmi nchini mwaka 2004 na kupewa katika mazingira tata, mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Aliyeanika zaidi ukweli juu ya Richmond kubebwa ni mmoja wa maofisa wa kampuni ya AFRICOMMERCE ambayo ndiyo iliyobuni na kupewa kazi ya awali ya mradi huo kabla ya kupokwa na kupewa Richmond, Bw. Eliapenda Chuwa wakati akihojiwa na Kamati ya Mwakyembe.

"Tulikwenda kumlalamikia (baada ya kupokwa mradi huo) Mheshimiwa Daniel Yona (wakati huo akiwa Waziri wa Nishati na Madini) ofisini kwake...Yeye akasema tutawapeni hela. Sasa utupe hela tumekwambia tunahitaji hela?

Akinukuliwa tena katika ukurasa wa 951 wa taarifa rasmi za Kamati hiyo, Bw. Chuwa aliiambia Kamati hiyo: "Waziri Danieli Yona tulipomwuliza kwa nini unafanya vitu vya namna hii akasema ninyi nendeni tutawapa hela, sasa hatujui kwamba zinatoka wapi."

Katika hatua nyingine yenye utata juu ya uadilifu wa watendaji serikalini na katika kile kinachoweza kusisitizwa tena kuwa mkakati mpana usioshikika wala kukamatika wa vigogo kuhakikisha Richmond inakipata kila inachokitaka.

Mkurugenzi Mkuu wa AFRICOMMERCE, Bw. Elisante Muro naye akitoa ushahidi wake kwenye Kamati ya Mwakyembe ananukuliwa akisema Bw. Yona alidiriki hata kuwapatia Richmond nyaraka zao za siri ili ziwasaidie.

Akinukuliwa katika ukurasa wa 952 wa taarifa za Kamati hiyo, Bw. Muro anakieleza kitendo hicho cha kutia shaka cha utendaji wa kigogo huyo akisema: "Kampuni moja inaitwa ENERGEM ya Canada tulikutana nao, wakatuandikia kwamba wana uwezo na wangependa kuuendeleza huu mradi wakishirikiana na AFRICOMMERCE.

"Out of our goodwill (kwa nia njema) tukamwonyesha Waziri Daniel Yona kwamba yupo mtu ambaye huu mradi utatekelezwa na kampuni iliyobobea. Akachukua ile barua akawapelekea Richmond, wakaenda kwa wale wawekezaji wetu Energem wakawaambia ule mradi ni wetu (wa wao Richmond) kwa hiyo kama mnataka pitieni kwetu."

Rutabanzibwa apuuzwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, ambaye aliwahi kuwa kwenye Wizara ya Nishati na Madini wakati Richmond waliposhindwa kutekeleza mradi wa bomba la mafuta na anayeijua vyema kuwa ni kampuni ya kisanii, Bw. Patrick Rutabanzibwa naye ametoa kauli mbele ya Kamati ya Mwakyembe inayozidi kuthibitisha kuwa kuna watu waliamua kufa na Richmond.

Akinukuliwa kwenye Kamati hiyo, Rutabanzibwa, alisema:
"...Nakumbuka nilipopata habari kwamba Richmond Development Company ndio wamepewa ule mradi mara moja nilimpigia simu Kamishna wa Nishati, Ndugu Bashir Mrindoko nikamwuliza nikisema nimesikia Richmond ni wale wale tuliokuwa nao au vipi?

"Akanieleza kwamba ni wale wale, nikasema sasa imekuwaje, lazima kuna matatizo huko kwenu."

Bw. Rutabanzibwa akaendelea kueleza juu ya suala hilo akisisitiza:

"Ninakumbuka taarifa ilipokuja (kwenye Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali), kwamba Richmond Development Company ndio wamepewa huo mkataba... Niliungwa mkono na wenzangu wengi kwamba tutafute kila njia kuachana nao,.." .

"...Na ushauri niliotoa kwenye kikao cha MCT (Makatibu Wakuu) ni kwamba hawa tunawajua hawana uwezo technically (kiufundi) au financially (kifedha)."Maoni hayo ya Rutabanzibwa yakapuuzwa, Richmond wakapewa mkataba na kukipata walichokuwa wakikitaka.
Mkurugenzi TANESCO naye anena

Akizidi kuongeza nguvu katika dhana kuwa kuna watu walikuwa tayari kufa ili Richmond ipate ilichokuwa ikikitaka, mmoja wa waliokuwa Wakurugenzi wa TANESCO wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo, Bw. Yohanes Hans, raia wa Afrika Kusini alisema kuwa madai kwamba Richmond ilipewa tenda hiyo kwa sababu ya kuwa na bei ya chini kuliko kampuni zote ni uongo.

Aliiambia Kamati kuwa kampuni ya Songas ilikuwa imeshakubali kuikodisha TANESCO mitambo ya umeme, kwa bei ya chini zaidi ya Richmond na ambayo TANESCO wangeiendesha wenyewe (bila kulazimika kulipa capacity charges kama sasa ambapo Richmond inalipwa sh. milioni 152 kwa siku; izalishe umeme, isizalishe).

Lakini, kwa mujibu wa taarifa ya Bw. Hans, wakati Songas pia walikubali kuuza umeme wao TANESCO kwa senti 3.84 kwa yuniti (tofauti na Richmond wanaouza kwa senti 4.99 kwa yuniti), kama kawaida, vigogo wa Serikali 'waliamua kufa na Richmond,' ili kuhakikisha, kama ilivyopangwa, kampuni hiyo inakipata ilichokitaka na Songas wakaachwa.

Mtoto wa Sokoine asaidia

Katika kuonesha kuwa wapo Watanzania ambao kwa upande mwingine wamepania kuhakikisha kuwa ubinafsi na uzembe Serikalini unakomeshwa, wakati vigogo kadhaa wakiumbuliwa kwa kuonekana walishiriki kuhakikisha Richmond inakipata kila ilichokitaka, wapo maofisa Serikalini ambao pia walihakikisha kampuni hiyo inajulikana ukweli wake halisi.

Mmoja wa waliosaidia hilo ni mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu na mbunge wa zamani wa jimbo la Monduli. hayati Edward Moringe Sokoine, Bw. Joseph Sokoine ambaye ni Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani anayeshughulikia masuala ya Siasa, Biashara na Utalii.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati, wakati baadhi ya wajumbe walipokwenda nchini Marekani kujua ukweli kuhusu Richmond, Bw. Sokoine alikuwa mmoja wa maofisa waliotoa msaada mkubwa na kuwaongoza wanakamati hao.

Kamati hiyo ilipokuwa nchini Marekani ndiko ilikofanikiwa kubaini kuwa Richmond haikuwa imesajiliwa na wala haikuwa na ofisi na wala haitambuliki miongoni mwa makampuni ya nishati yaliyoko Houston, Texas.

Hata hivyo, hivi karibuni Bw. Yona alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akikana kuhusika katika sakata hilo la Richmond.
 
Tunaomba ushahidi kwani sisi tujuavyo Mheshimiwa JK kalizungumzia hili juzi tu kwenye hotuba yake kwa wananchi ya mwisho wa mwezi (29-02-2008) na kasema hivi "Matukio ambayo yatapata nafasi yake katika historia ya nchi yetu. Jambo la kwanza ni lile linalohusu kikao cha Bunge kilichopita, ambapo utekelezaji wa maamuzi yake yanasimamiwa na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda."

Au hili si la Richmond? au una tamko jipya kuhusu Richmond kutoka Kwa Rais ambalo sisi hatujaliona? kama ni hivyo hebu tuwekee hapa na sisi tulione.
 
Hivi Lowassa unataka tukufanye nini?? Nafikiri bado anadhani ana madaraka...poor Lowassa
 
Dar Jazz waliiona Richmond zamani

Ibrahim Mkamba Machi 5, 2008



KINYUME cha matarajio yangu, makala yangu iliyohusu uoga wa wasanii wa leo katika kupambana na ufisadi katika jamii yetu (toleo namba 017, Februari 20-26,2008) ilipata napokezi mazuri kwa wasomaji wa gazeti hili.

Lawama, manung'uniko, masahihisho, pongezi vilitawala ujumbe mbalimbali wa barua pepe na simu niliopokea kuhusu mada hiyo.

Kilichofurahisha zaidi ni kwamba miongoni mwa waliochangia mada hiyo ni Mwana Hip Hop maarufu nchini Afande Sele mwenye makao yake mjini Morogoro.

Kutokana na michango hiyo, leo nimeona tuwekane tena sawa katika kuukabili ufisadi kwa njia ya sanaa. Kwa sababu hiyo, makala niliyoiandaa kuitoa wiki hii ya kuzungumza na dada zetu wanamuziki, itabidi isubiri hadi wiki ijayo.

Kwa ufupi sana, mwanamuziki Afande Sele anayetamba na vibao kama "Acha Kupiga Mayowe," "Darubini Kali" na "Uwanja Mpya wa Taifa," amesema kwamba Hip Hop, kama inavyojulikana, ni muziki wa mapambano na ukombozi.

Wana Hip Hop wa Tanzania, akiwamo yeye, wanalifahamu vizuri sana jukumu hilo lakini wanashindwa kutimiza vizuri wajibu wao kwa jamii si kwa uoga bali kwa kukwamishwa na mfumo wa biashara ya muziki nchini.

Amesema, mara zote wadau wakubwa katika biashara hiyo ambao ni mawakala na ma-DJ wa Redio hupendelea nyimbo za kuimba za mapenzi na za majisifu hata zisipokuwa na ujumbe wowote wa maana na kuiwekea vikwazo Hip Hop.

Hip Hop yenye ujumbe mzito huwekewa vikwazo siku zote kwa madai haina biashara nzuri wakati si kweli kutokana na jinsi inavyopendwa kuliko aina yoyote ya muziki.

Kimsingi Afande Sele anajitetea yeye na wana Hip Hop wenzake kwamba hakuna uoga wowote kwa upande wao katika kupigana vita dhidi ya ufisadi bali wanakwamishwa na watu wengine kwani mapambano ndiyo kazi yao.

Kwa upande wangu pia naomba nijitetee kwamba kwa mimi kutoitaja Radio One na ITV katika kuzungumzia uamuzi wao wa kuacha kutangaza habari za Simba Sports Club, si uoga kama wengi walivyonieleza bali ilikuwa ni njia ya kiungwana ya kumshauri mwenye akili timamu na busara ya kawaida abadilishe msimamo usio na tija.

Kama njia ya kutomtaja haisaidii, hapo ndipo tunapoweza kuambiana uso kwa uso kwamba wenzetu ITV na Radio One mnatuaibisha, hata kwenye msimamo wa ligi Simba haimo?!

Huu ni uhabarishaji wa wapi wa kupotosha hivyo? Ikitokea wakachukua ubingwa mtatangaza bingwa ni nani,wa pili yake? Ikitokea wakafanya makubwa sana katika mashindano ya vilabu barani Afrika, hamtasema chochote?

Wapenda soka hatujisikii vizuri vyombo hivyo kuitwa vya Yanga kwa kutoitangaza Simba ambayo kwa soka letu la hapa ni kama pacha wa Yanga. Jina hili la kibaguzi linaonekana ni jina sahihi hasa kwa Redio One inayotoa muda mwingi kwa habari za Yanga tangu waisuse Simba!

Uoga wangu ungesababishwa na nini katika kuvitaja vyombo hivyo wakati maajabu yao hayo yanajulikana na kila mtu isipokuwa labda kwa viongozi wao kama alivyohisi mwandishi mmoja mwandamizi wa habari?

Katika barua pepe aliyonitumia, mwandishi wa habari huyo alieleza kwamba huenda viongozi wa vyombo hivyo hawalijui hilo kwa hiyo vitakapotajwa, viongozi hao wataamshwa.

Naamini sasa watakuwa wameamka kama kweli walikuwa wamelala na kama kweli hawana mkono kwenye maamuzi hayo ya ajabu. Nasema hali hiyo ilifahamika na wengi kwani kila aliyenishutumu alivitaja vyombo hivyo na klabu hiyo.

Hakuna aliyeniuliza nilikuwa nazungumzia vyombo vipi vya habari na klabu gani ya soka.

Tukiachana na hilo, si suala la kubishana kwamba zamani sanaa ilitumika sana kupiga vita ufisadi. Kazi ya sanaa ilivyo ya kifasihi ni kazi ambayo kamwe haifi bali hujibadilisha umbo lake kutegemeana na mabadiliko ya matukio kwa nyakati tofauti kutegemeana na tafsiri ya matukio ya nyakati husika.

Kwa mfano, wimbo "Chawa" wa Jamhuri Jazz Band (Wanyama Wakali),Wana Dondola wa jijini Tanga uliorekodiwa mwaka 1971 unaoanza na maneno "Chawa umenisumbua kwa muda mrefu chawa, najitolea chawa leo sikutaki tena..."

Kwa wakati ule ungetafsiriwa kwamba Wanyama Wakali walikuwa wanamfukuza mnyonyaji katika kutekeleza siasa iliyokuwapo wakati huo ya Ujamaa na Kujitegemea lakini leo utatafsiriwa kumfukuza mgeni anayepora mali yetu kwa njia ya utapeli wa kimataifa ya uwekezaji.

Ni katika muktadha huo ndipo inapoonekana wazi kuwa utunzi wa Dar Jazz, wana Mundo, Majini wa Bahari wa mwanzoni mwa miaka ya 1970 uliyalenga vizuri sana matukio ya leo ya kifisadi kama wa Richmond.

Wimbo huo unaimbwa hivi: "Haifai kwenda kusimama juu ya milimaa,kupokea mapesa kwa mabepari, kwa kutaka kuiangamiza nchi yee, haifai. Tizameni nyie mambo mnayotakaa kuyafanyaa, ni mabaya sana, roho za watu zitakuja kupotea na wakati huo Mungu atakuja kaasirika, haifai."

Baadaye korasi inasema: "Tanzania itakuja chanika oo, na mambo yote yatakuja haribikaa, itakuja kuwa hasara ya nchi. Tanzania itakuja jaa motoo..."

Kifasihi, wana Mundo waliposema "Haifai kwenda kusimama juu ya milima" walimaanisha haifai kujikweza, kutumia madaraka vibaya na kufanya mambo kwa niaba ya umma kwa siri kama ilivyo siri mikataba ya kuuza rasilimali zetu kwa watu wa nje wanaoitwa Wawekezaji.

Waliposema "kupokea mapesa kwa mabepari" walimaanisha kuuza raslimali za nchi kwa rushwa, au kuingia mikataba ya "Ki-Richmond" kwa vipato binafsi visivyo halali. Waliimba "roho za watu zitakuja kupotea" wakimaanisha matendo hayo yataathiri vibaya sana uchumi wa nchi na kuwafanya baadhi ya wananchi kufa kwa kushindwa kuyamudu makali ya maisha kwa kukosa uwezo wa kupata chakula cha kutosha na pesa ya matibabu.

Majini wa bahari walipoimba "Mungu atakuja kasirika" walimaanisha Mungu hatafurahishwa na dhambi ya viongozi mafisadi dhidi ya sisi wanaotuongoza. Baadaye kwenye korasi waliimba "Tanzania itakuja chanika" wakimaanisha ufisadi utatugawa katika matabaka na kuibuka kwa chuki ya ajabu baina ya tabaka la mafisadi wanaoneemeka kwa mgongo wetu na tabaka la sisi waathirika wa ufisadi huo na hapo "mambo yote yatakuja haribika" kama walivyoimba na wakamaliza kwa kuimba:

"Tanzania itakuja jaa moto" wakimaanisha ufisadi huo utasababisha machafuko makubwa na amani tunayojivunia itatoweka vibaya sana baada ya kuimarika kwa matabaka yatakayojengwa na ufisadi huo. Hiyo ndiyo kazi ya Dar Jazz waliolizungumzia kifasihi suala la Richmond miaka zaidi ya 35 nyuma!

Mfano mwingine wa kazi za zamani za fasihi ambazo maudhui yake yanadumu hadi leo ni kidokezo kimoja, kati ya vingi, cha Radio Tanzania Dar es Salaam kabla ya taarifa za habari kwenye miaka ya mwanzo ya 1970 hadi katikati ya miaka hiyo kinachokwenda hivi: Zinaanza sauti kakamavu za kike:-"Chungua uchumi wao, hawawezi kuishi kama sisi".

Baadaye inafuata sauti ya kiume ikitamka neno moja moja: "Maisha ya kibepari ni maisha ya uhasama, maisha yenye dhuluma. Binadamu wazima na fahamu zao, huishi kama wanyama wa porini ambao uhai wa kila mmoja wao hutegemea ujanja wake wa porini, urefu wa makucha yake na ukali wa meno yake.

Ubepari ni unyama. Ujamaa, ujamaa, ujamaa ni utu, ni utu, ni utu."

Leo hii kidokezo hicho kinafaa kiwe hivi:-"Chungua matumizi yao ya madaraka, hawana chembe ya uchungu na sisi".Kisha: "Maisha ya kifisadi ni maisha ya uhujumu uchumi, maisha yenye dhuluma. Binadamu wazima na fahamu zao, huishi kama wanyama wa porini ambao uhai wa kila mmoja wao hutegemea ujanja wake wa porini, urefu wa makucha yake na ukali wa meno yake. Ufisadi ni unyama. Uadilifu, uadilifu, uadilifu ni utu, ni utu, ni utu."

Swali ambalo limekosa jibu, ukiondoa jibu la Afande Sele la mwanzo wa makala hii na ushujaa wa Dada Irene Sanga katika tunzi zake za ukombozi mamboleo, ni sababu gani inayofanya wasanii wa leo tuwe waoga. Katika kujadili hilo, kila mmoja alimnyooshea kidole mwingine kuwa muoga na hapo ndipo nilipoingizwa.

Wengine wakasema "mbona RTD na TvT wanaogopa kusoma magazeti ya Tanzania Daima, Raia Mwema na MwanaHalisi?"

Nikashangaa. Katika dunia ya sasa chombo cha umma kinafanya hivyo kwa maelekezo ya nani au uoga tu wa watendaji wenyewe! Kuna nini cha kuogopa kwenye magazeti hayo kisichoandikwa na yale yanayosomwa?

Hata hivyo, nilipolitafakari hilo, nikafikia kwenye hitimisho kwamba hiyo si sera ya uongozi wa vyombo hivyo bali ni uoga tu wa watangazaji wenyewe kwani TvT ina vipindi vingi vya watu mbalimbali kutoa maoni yao yoyote yale kwa uhuru.

Miongoni mwa vipindi hivyo ni "This Week in Perspective", "Bungeni Wiki Hii" wakati wa vikao vya Bunge na "Tuambie", hasa kilichorushwa Alhamisi ya Februari 28,2008 kuhusu matukio baada ya uchaguzi wa Kenya na funzo kwa Tanzania.

Kwa upande mwingine,Yussuf A. Marare wa Musoma mjini aliniomba niwaondoe washairi katika orodha ya wasanii waoga kwani wao huzungumza chochote cha manufaa kwa umma bila hofu.

Alitoa mfano wa shairi lililojibiwa kwa shairi bungeni na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa. Baada ya kunikumbusha hilo, alinipa zawadi ya shairi lifuatalo la beti nne:-


Tulimzika Mwalimu,pamoja na uzalendo
Wakabaki madhalimu, watu bila ya upendo
Nchi wanaihujumu, kwa uovu wa matendo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu


Nchi imekosa sudi, maadili na mwenendo
Imejaa mafisadi, wala rushwa na uvundo
Hatuendi tunarudi, kama ni huu mtindo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu


Tuliowapa dhamana, tena ya jembe na nyundo
Wamekosa uungwana, kwa kashfa lundo lundo
Kama hii si laana, mbeleni chaja kishindo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu


Wametoka haidhuru, maji yafate mkondo
Sheria itunusuru, wawekwe nyuma ya nondo
Mikataba ya kufuru, isirejee mtondo
Wako wapi wazalendo, mfano wake Mwalimu.

Tufuate nyayo za wasanii wa zamani, washairi wa nyakati zote na wana Hip Hop wetu wa leo katika kuupiga vita ufisadi. Kwa wanamuziki wote, hasa wa Bongo Flavour, tusidanganyane kwamba nyimbo za mapambano, zisizo za mapenzi, ni hasara na haziwezi kumfanya mtu atoke.

Wimbo wa "Ndiyo Mzee" ulimtoa Professor Jay wakati "Tanga Kunani" iliwatoa Wagosi wa Kaya ambapo sasa "Mr Politician" inamtoa Nakaay.

Tuwe wazalendo, tutumie sanaa zetu kuikomboa nchi yetu dhidi ya ufisadi. Hatuna sababu ya kuogopa kwani Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wake, Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Mkuu wetu Mizengo Kayanza Peter Pinda hawana hata harufu ndogo ya ufisadi, ni wasafi. Ni wazi watafurahia kazi zetu kwani hata wao wanauchukia ufisadi.Ufisadi ni unyama.



0713 297085
Barua pepe: ibramka2002@yahoo.com
 
Kabla ya shirika la umeme la Tanesco kuingia mkataba wa Richmond, liliingia pia mikataba mingine mingi na mbalimbali. Swali moja kubwa linaloulizwa na watu wengi ni jinsi gani mikataba hii ilikuwa mibovu kiasi hicho. Ni wazi kuwa mikataba iliyoingiwa ni matokeo ya Wanasheria Wakuu Andrew Chenge na Johnson Mwanyika. Je, wangepatikana Watanzania wengine wapate nafasi ya kuangalia mikataba hiyo kisheria na kuitolea maoni watasemaje?

CD hii inatokana na kazi ya Watanzania hao kwa niaba ya Kamati Teule ya Bunge ambao walipewa jukumu la kuangalia mikataba sita ya nishati iliyoingiwa na TANESCO ukiwemo huo wa Richmond. Yafuatayo ni maoni yao wakianisha mapungufu ya kisheria ya mikataba hiyo na hivyo kuonesha wazi kuwa Andrew Chenge ni Mtanzania aliyeligharimu Taifa lake mabilioni ya shilingi kwa kushindwa kusimamia vipengele vya kisheria kwenye mikataba hiyo. Na pia aliyemfuatia Bw. Johnson Mwanyika naye ameonesha anafuata nyayo za Chenge.

Ni kwanini watu hawa bado wanaendelea kuwa katika utumishi? Hili tunawaachia wengine waliamue. Lakini ushahidi wa uzembe wao na kutolijali taifa lao uko hapa kwa mwenye macho kuona.
 

Attachments

Nijulisheni basi kama huu mziki umewakolea ili wengi zaidi washaurike kuusikiliza.........



---------------------------------------------------------------
 
Enigma,
Kwa niaba ya wanaJF nasema TAWILE, CD nzito na jina album naona linauza vibaya sana. CD hii bila shaka inawanyima kazi mapromota kwani inajiuza yenyewe. Tatizo FM station za bongo wanaweza kuendelea kuibania, isisikike.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…