JK USE YOUR PRESIDENTIAL POWER NOW
Habari Tanzania
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Richmond Development iliyoahidi kuingiza megawati 20 za umeme katika gridi ya Taifa mwishoni mwa wiki iliyopita, imeshindwa kufanya hivyo na sasa imeendelea kukaa kimya.
Ahadi za kampuni hiyo kwa mara ya tatu zimeshindwa kutimia, baada ya Desemba 2 uongozi wa kampuni hiyo kuahidi kuwasha mitambo kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita lakini ahadi hiyo haikutimia.
Meneja Mkazi wa Kampuni ya Richmond, Naeem Gire, alikaririwa na gazeti hili Jumamosi Desemba 9, mwaka huu akisema kuwa walikuwa wanafanya jaribio la mwisho kabla ya kuruhusu umeme kuingia katika gridi ya taifa.
"Tunatarajia leo tutafanya majaribio ya mwisho ya kiufundi kwa kuiwasha mitambo hii, baada ya hapo ndio tunaweza kuiwasha moja kwa moja endapo haitaonyesha hitilafu ya kiufundi," alisema Gire.
Hata hivyo, vyanzo vya habari ndani ya kampuni vimesema kuwa hadi jana mitambo hiyo ilikuwa haijawaka na mafundi wa kampuni ya hiyo walikuwa wanaendelea kutoa jasho kuhakikisha umeme huo unaunganishwa katika giridi, lakini hadi jana jioni, walikuwa bado hawajafanikiwa.
Chanzo cha habari kilicho karibu kampuni hiyo kilisema jana kuwa huenda umeme huo ukapatikana baada ya saa 72 kuanzia jana jioni, hii ikiwa na maana kuwa huenda ukapatikana kuanzia kesho Jumanne.
Kama kawaida, eneo la mitambo hiyo jana lilikuwa na ulinzi mkali na watendaji wa kampuni hiyo hawakupatikana wala kujibu simu ili kuelezea hatua waliyofikia na kueleza ni lini hasa umeme wao utapatikana na kuingizwa katika gridi ya taifa.
Umeme huo wa Richmond unaosubiriwa kwa muda mrefu ni sehemu ya kwanza ya kiwango kinachotakiwa kuzalishwa na kampuni hiyo, kabla ya kuleta mitambo mingine ya kuzalisha awamu ya pili ya mewagawati 80 ili kutimiza kiwango cha megawati 100 zilizokubaliwa katika mkataba wake na serikali.
Hii ni mara ya tatu, umeme wa Richmond kushindwa kuingia katika gridi ya taifa kama ilivyoahidiwa baada ya mara ya kwanza kuahidiwa na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha kuwa ungeingia Oktoba 20, na baadaye Waziri wa sasa, Nazir Karamagi kuwa umeme huo ungepatikana kabla ya Desemba.
Kuzidi kuchelewa kwa kampuni ya Richmond kuingiza umeme katika gridi ya taifa, kunazidi kukaza kitanzi cha karamagi ambaye aliahidi kuwa megawati zote 100 za Richmond, zitakuwa zimeingizwa katika gridi ya taifa kabla ya Januari mwakani.
Waziri Karamagi alitoa ahadi hiyo Novemba 23, mwaka huu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ambapo aliahidi kuwa mgawo wa umeme ungekwisha kabla ya Januari mwakani.
Karamagi, Waziri mwenye dhamana na masuala ya umeme, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta hiyo, ilikuwa katika jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa tatizo hilo, ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa zaidi ya miezi sita sasa, linamalizika kabla ya Januari.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa waziri anayeshughulika na masuala ya umeme kutoa ahadi kama hiyo. Mtangulizi wa Karamagi, Dk Ibrahim Msabaha, pia aliwahi kutoa ahadi kama hiyo, akisema makali yangepungua mwishoni mwa Oktoba lakini hali haikuwa hivyo.
Badala yake, makali ya umeme yakazidi kuongezeka na ingawa haikuwekwa wazi, inaelezwa kuwa ni moja ya sababu zilizomfanya Rais Kikwete amhamishie katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa kujiamini siku hiyo, Waziri Karamagi alisema jitihada mbalimbali za dharura zinafanywa kwa lengo la kumaliza mgao wa umeme uliopo sasa.
Alisema jitihada hizo ni pamoja na kuhakikisha kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Richmond, yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100, inafungwa haraka ili hadi kufika mwezi huu, iwe imeanza kuzalisha umeme kikamilifu.
Alisema kazi ya kufunga awamu ya kwanza ya mitambo ya kampuni hiyo, yenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 ambayo iliwasili mwezi uliopita kutoka Marekani, inakaribia kukamilika akisema mafundi wamefikia asilimia 80 ya ufungaji wake, hali inayotia matumaini kuwa megawati hizo 20 zingeanza kuzalishwa mapema mwezi huu.
Alisema awamu ya pili ya mitambo ya kampuni hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 80 ipo katika maandalizi ya mwisho kuletwa nchini wakati wowote kuanzia sasa, ili iweze kufungwa na kufanya jumla ya megawati zitakazozalishwa na kampuni hiyo kuwa 100.
Hata hivyo, wasiwasi uliopo ni kwamba huenda ufungaji wa mitambo ya awamu ya pili usikamilike katika kipindi anachokitaja Waziri Karamagi, hasa ikizingatiwa kuwa mitambo yenyewe bado haijawasili nchini.
Wasiwasi huo unatokana na ukweli kwamba mtambo wa kwanza wa Richmond uliwasili nchini Oktoba 21, 2006 na jana, Desemba 10, bado kazi ya kufunga na kufanya majaribio, ilikuwa bado ikiendelea. Watu wengi wanahoji kuwa iwapo mtambo wa megawati 20 unachukua zaidi ya mwezi mmoja kufungwa na kuanza kazi, ni wazi kuwa kazi itakuwa ngumu zaidi kwa mtambo wa kuzalisha megawati 80.
Mchanganuo unaonyesha kwamba ili mgawo wa umeme uishe ni lazima Richmond wakamilishe kujenga mitambo yote kabla ya Desemba 31, mwaka huu.
Alisema lengo la mgao ni kupunguza matumizi ya maji katika maeneo ya kuzalisha umeme ambako kina kimepungua na kwamba utaratibu huo utawezesha maji kidogo yaliyopo yaendelee kuendesha mitambo hiyo hadi Desemba wakati mitambo ya dharura ya kuzalisha umeme itakapoanza kufanya kazi
JK use your power now to strip this dubious contract.