Wabunge wazozana kuhusu Richmond
Mgaya Kingoba, Dodoma
Daily News; Thursday,April 17, 2008 @08:57
SUALA la Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM) kuzuiwa kutoa maelezo binafsi kuhusu Richmond, jana lilisababisha wabunge wa upinzani na wa CCM wazozane. Wabunge hao walikuwa wakihoji ni kwa nini hakupewa nafasi ya kutoa maelezo yake ndani ya chombo hicho kama alivyoahidi Spika.
Mjadala huo uliibuka baada ya Naibu Spika, Anna Makinda, kuwasilisha tamko kuhusu utaratibu wa kuwasilisha hoja binafsi; na ingawa katika maelezo yake hakuna popote alipomtaja Mbunge huyo wa mkoani Tabora, baadaye ilidhihirika kuwa ni kutokana na suala la Rostam.
Ijumaa iliyopita, Spika Samuel Sitta aliliambia gazeti hilo kwamba Mbunge huyo wa Igunga hataweza kutoa maelezo yake kwa mujibu wa Kanuni ya 54, kifungu kidogo cha nne, ambacho kinaeleza kuwa suala likisha kujadiliwa bungeni na kutolewa maamuzi, halitajadiliwa tena.
Baada ya maelezo ya Naibu Spika jana, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisimama na kuhoji kama shauri la Mbunge likizungumzwa ndani ya Bunge linaweza kuzuiwa na chama chake.
Naibu Spika alimtaka Hamad ambaye ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, kutoa mfano katika suala kama hilo na Mbunge huyo wa CUF alilitaja suala la Rostam, ambaye alisema licha ya Spika kuahidi kuwa Mbunge huyo atatoa maelezo yake ndani ya Bunge, chama chake kimemzuia kufanya hivyo.
Baada ya kupewa mfano huo, Naibu Spika alisema amefurahi kuulizwa kwa hoja hiyo, na hivyo kuanza kutoa darasa kwa wabunge na waandishi wa habari kuhusu Kanuni zinazoongoza chombo hicho cha kutunga sheria, akivitaja vifungu vya 55, 109 na 110 kuhusu suala la Hoja Binafsi.
Kwa mujibu wa Naibu Spika, utaratibu wa kuwasilisha Hoja Binafsi unaelekeza kuwa suala hilo ni lazima kwanza Mbunge aliwasilishe kwa chama chake na kisha ndipo lipelekwe kwa Katibu wa Bunge.
"Kutokana na utaratibu huo uliowekwa na Kanuni za Kudumu za Bunge, hoja yoyote binafsi inayokusudiwa kuwasilishwa bungeni inapaswa kuzingatia utaratibu ulioainishwa kwenye Kanuni za Kudumu za Bunge, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa hoja husika kupitia kwanza kwenye Kamati ya Chama cha Siasa kinachohusika, kabla ya kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge," alisema Makinda.
Aliongeza: "Ieleweke wazi kwamba Bunge haliwajibiki kuzuia hoja yoyote itakayokuwa imetimiza masharti yaliyoainishwa katika Kanuni za Kudumu za Bunge.
"Utaratibu huu unakusudia kuepusha fikra potofu kuwa hoja binafsi za wabunge zinakwamishwa na viongozi wa Bunge na vile vile kuepusha migongano inayosababishwa na hoja hizo kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge kabla hazijapitishwa na Kamati za Chama cha Siasa kinachohusika".
Hata hivyo, Makinda alisema maelezo ya sasa ya Rostam, yalizuiwa kwa sababu yalionekana yote aliyoyasema yalikuwamo katika mchango wake wa maandishi katika Mkutano wa 10 wa Bunge, Februari 15 mwaka huu alipochangia mjadala wa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya Richmond chini ya uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe.
Naibu Spika alisema kutokana na hilo, Kanuni ya 54, kifungu kidogo cha nne, kinamzuia Mbunge huyo kuwasilisha maelezo yake, kama alivyoeleza Spika alipozungumza na gazeti hili Ijumaa iliyopita alipoeleza ni kwa nini hoja hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu, haitafikishwa mbele ya Bunge.
Jibu la Naibu Spika halikumridhisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), hivyo akataka Mwongozo wa Spika, akitumia Kanuni ya 68, kifungu cha saba.
Mbunge huyo alimtaka Naibu Spika kueleza kwa nini Kamati ya Uongozi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ilimzuia Rostam wakati suala hilo ni la Bunge; na akamtaka Naibu Spika atoe ufafanuzi wa masuala mawili; atangaze msimamo wake kwa sababu ni mjumbe ndani ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM na pili, kanuni zinaelekeza kuwa Mbunge atawasilisha hoja zake bungeni kwa njia za maswali, maswali ya nyongeza, maelezo binafsi na maelezo ya mawaziri.
Hivyo, alimuomba Naibu Spika kuwa suala hilo la Rostam lilirudi kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo inao wajumbe kutoka upinzani, kwani alidai CCM inataka kuwabana wabunge wake ndani ya chombo hicho kikuu cha kutunga sheria nchini.
Naibu Spika akijibu alisema: "Zitto hauko sahihi. Suala hilo ni la Kanuni na kwa maandishi ambayo tayari yako katika Hansard. Hili ni suala la taratibu na Kanuni, halina uhusiano na chama. Tuwe wakweli. Waandishi wa habari na wabunge wanazifahamu vizuri Kanuni zetu.
"Lipo Azimio la Musoma ambalo limeeleza wazi kuwa wabunge wa CCM watakuwa huru kutoa maoni yao ndani ya chama chao na katika Bunge. Watu wasishindane kwa maneno na ufundi wa kusema," alisema Makinda ambaye kauli zake zilishangiliwa na wabunge wa CCM.
Ilionekana kama malumbano yanaweza kuchukua nafasi yake, kwani Zitto alisimama tena na safari hii alianza kwa kuwataka wabunge wa CCM kunyamaza; kisha akamueleza Naibu Spika kuwa suala la Rostam ni Hoja Binafsi na alisisitiza nia ya kutaka suala lake likajadiliwe na Kamati ya Uongozi.
Naibu Spika alisimama na kueleza kuwa asingependa iwe malumbano, na kueleza kuwa suala la Mbunge huyo wa Igunga, limejadiliwa kwa kuzingatia taratibu za Hoja Binafsi.
Mbunge pekee wa CCM aliyesimama kuchangia hoja hiyo alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah ambaye alikuwa na hoja mbili; akihoji kwa nini Zitto 'amedandia' hoja hiyo wakati hakuwa muulizaji wa kwanza na akahoji wapinzani hao wana maslahi gani katika suala hilo.
Naibu Spika alifunga mjadala huo kwa kusema, "Sisi sote interest yetu ni wananchi."
Suala la Rostam ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wahusika wa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, liliibuka tangu kuanza kwa Mkutano wa 11 wa Bunge, Aprili 8, mwaka huu, na lilishika kasi na kutawala mazungumzo yasiyo rasmi ya wabunge baada ya kubainika kuwa Mbunge huyo amezuiwa na Kamati ya Uongozi wa CCM kutoa maelezo yake bungeni.
Mwenyewe alikuwapo Dodoma kwa siku tatu za kwanza za mkutano huo, lakini baadaye akatoweka, na alipozungumza na gazeti hili Ijumaa iliyopita, alisema anamheshimu Spika, anakiheshimu chama chake na akasisitiza kuwa hahusiki na kashfa ya kampuni hiyo inayodaiwa ni ya kitapeli.
Katika mchango wake wa maandishi ulioko kwenye Hansard ya Februari 15, mwaka huu, Mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa Mweka Hazina Mkuu wa CCM na sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya CCM, alisema:
"Napenda kulihakikishia Bunge lako kuwa sina hisa wala umiliki wa aina yoyote katika kampuni hizi mbili (Richmond na Dowans) na nina hakika Kamati Teule, inafahamu ukweli huu. "Mheshimiwa Spika, kaulimbiu yako ya kasi na viwango, haijadhihirika katika utekelezaji wa majukumu ya Kamati Teule.
Ulipobaini Kamati haijatoa mapendekezo kwa sababu ya muda kutotosha, uliwaongezea muda na upo ushahidi kuwa Kamati ilikuwa ikiendelea kumalizia kazi zake mpaka wiki ya kwanza ya Bunge.
"Inashangaza kwamba Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe na wewe Mheshimiwa Spika, ambao kwa pamoja mlikuwa na wajibu wa kuhakikisha kila mtuhumiwa anatendewa haki, kwa kupewa haki ya kusikilizwa, mlipuuza haki hii ya msingi kabisa ya raia."
Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo hatajibu maswali ya papo kwa papo ya wabunge kwa sababu atakuwa Kenya ambako atashuhudia kuapishwa kwa Baraza la Mawaziri la nchi hiyo lililotangazwa Jumapili iliyopita na Rais Mwai Kibaki.