PCB yaisafisha tuhuma za rushwa Richmond
Jonas Songora na James Magai
TAASISI ya Kuzuia Rushwa nchini (TAKURU) imeisafisha kampuni ya Richmod Development Company dhidi ya tuhuma za rushwa zilizokuwa zikiikabili katika uingiaji wa mkataba wa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kwa TANESCO.
Akizugumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Takuru , Upanga jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takuru, Edward Hosea alisema kuwa hakuna ushahidi wowote uliopatikana kuthibitisha vitendo vya rushwa, uzembe, au upokeaji wa kamisheni kwa watendaji wa serikali.
Kusafishwa huko kwa tuhuma za rushwa dhidi ya kampuni hiyo, serikali na wadau wengine kunakuja baada ya kuwepo mingong'ono ndani ya jamii na hata serikali na bunge.
Alisema kuwa uchunguzi huo ulithibitisha kuwepo kwa mapungufu ya kawaida katika utendaji na ambayo hayakuhusisha rushwa au manufaa ya aina yoyote ile kwa upande wa watendaji na hakuna hasara iliyosababishwa na mapungufu hayo.
Katika ushahidi uliopatikana kufuatia uchunguzi huo, Hosea alisema kuwa kampuni ya Richmond Development Company, LCC ambayo ni kampuni mama ya kampuni ya Richmond Development Company (T) Limited inayomilikiwa na Naeem Gire ambaye ana uraia wa Tanzania na Mohamed Gire ambaye ni raia wa Marekani, ilifanikiwa kushinda zabuni iliyotangazwa na TANESCO baada ya kuyashinda makampuni mengine manane yaliyojitokeza.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo ilishinda zabuni hiyo baada ya Kamati ya tathmini yenye watu kumi na mbili, wakiwemo wajumbe wanane kutoka TANESCO, mjumbe mmoja mmoja kutoka Wizara za Fedha, Nishati na Madini, na wajumbe wawili kutoka Kampuni ya ushauri ya Laymeyer International ya Ujerumani ambayo ni kampuni ya ki- ufudi kwa TANESCO.
Hata hivyo kutokana na hali ya dharura na uharaka wa kutatua tatizo la umeme, alisema kuwa serikali iliamua kuingilia kati na Waziri Mkuu aliamua kuunda kamati ya watu watatu ilio kuharakisha zoezi hilo baada ya kuona kuwa utaratibu wa kutumia soko la kimataifa la wazabuni ungezidi kuchelewesha upatikanaji wa umeme.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Katibu Mkuu Hazina ilipewa jukumu la kuishauri serikali kwa uharaka zaidi, na kuweka vigezo ikiwemo mzabuni kuthibitisha uwezo wake kiufundi, uthibitisho wa bei kutoka kwa mzabuni, na kueleza muda atakaotumia hadi kuanza uzalishaji, ambapo kampuni ya Richmond ilithibitika kuwa na sifa zinazotakiwa.
Aliongeza kuwa Richmond ilithibitisha kuwa na sifa zinazotakiwa kwa kushirikiana na kampuni kubwa ya Pratt and Whitney yenye uzoefu mkubwa katika utengenezaji na uzalishaji wa umeme na pia kuthibitisha kuwa inaweza kuingiza umeme ndani ya wiki kumi na nne.
Akizungumzia kuhusu kushindwa kutekeleza kwa mkataba ambao Richmond iliingia na serikali, Hosea alisema kuwa baada ya kuthibitishwa Richmond kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba, serikali haikuilipa kampuni hiyo hadi ilipouza kazi zake kwa kampuni ya Dowans Holding SA Disemba 21, 2006 ambayo ndiyo inastahili kupewa malipo ya usafirishaji mtambo.
Aliongeza kuwa Richmond ilipaswa kuilipa TANESCO fidia ya ucheleweshaji huo kiasi cha dola za Kimarekani 10,000 kwa siku kuanzia Februari 20, 2007 kwa vile shughuli za Richmond ziliuzwa kwa Dowans, adhabu ambayo kwa sasa italipwa na kampuni hiyo.
Taarifa hiyo ya uchunguzi imekuja kufuatia malalamiko yaliyojitokeza kufuatia mchakato mzima wa utoaji zabuni ambapo serikali iliingia mkataba wa kukodi mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kufuatia kina cha maji kupungua katika mabwawa ya kuzalishia umeme ambapo serikali iliingia mkataba na Richmond kupitia TANESCO mwezi Juni 23, 2006.
Hata hivyo baadhi ya watendaji wa serikali walishutumiwa kuwa wamiliki wa kampuni hiyo ambayo ilishutumiwa sana kutokana na kuchelesha uletwaji wa majenereta hayo ya kuzalisha umeme wa dharura.
SOURCE:
http://www.mwananchi.co.tz/habari/habari1.asp