Mtoto Patrick ameshatangulia mbele za haki lakini huku nyuma, moto unawaka. Mama yake, Muna Love amesababisha kizaazaa kabla hata mwanaye hajapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele, machozi jasho na damu vinachuruzika.
Muna anadai mtoto ni wa Casto Dickson, yule mtangazaji wa Siz Kitaa (Clouds), Casto anadai mtoto ni wake lakini upande wa pili, yupo baba halisi, Peter Zacharia ambaye anavyo vithibitisho vyote vya kisheria kwamba Patrick ni mwanaye.
Muna anataka yeye ndiye achague wapi anamzika mwanaye, Zacharia anadai yeye ndiyo baba halisi wa mtoto kwa hiyo ndiye atakayechagua wapi pa kumzika mwanaye na azikweje. Muna anasisitiza kwamba mtoto ni wake na msiba ni wake kwa hiyo yeye ndiye atakayemzika mwanaye.
Kuna misiba miwili kwa maiti ya mtoto Patrick, Muna ameweka msiba nyumbani kwake, Zacharia pia ameweka msiba nyumbani kwake. Waombolezaji wamechanganyikiwa, hawaelewi waende kwa Muna au kwa Zacharia.
Zacharia anasema mwanaye akizikwa bila ridhaa yake, yupo tayari hata kufuata sheria ili mwanaye akafukuliwe na azikwe anapopataka yeye, kwa sababu yeye ndiye baba halisi. Anavyo vithibitisho, kikiwemo cheti cha ndoa na Muna na anaeleza kwamba hajawahi kumuacha mkewe huyo, ile yeye ndiye aliyekimbia nyumbani kwao, mtoto akiwa na miaka mitatu.
Nini hatma ya malaika Patric ambaye maskini ya Mungu hana hatia katika hili? Maiti yake inagombewa na kuna hatari akizikwa kabla ya hizi tofauti hazijapatiwa ufumbuzi, mwili wake utafukuliwa na kuzikwa upya.
Yajayo yanahuzunisha sana!
Habari zaidi, soma=>
TANZIA: Mtoto wa Munalove Patrick Peter Zacharia Komu almaarufu Partsmartboy Afariki dunia