HABARI: Juni 11, 2024 - Sanamu ya Askari jijini Dar es salaam ikiondolewa leo kupisha mradi wa ujenzi wa barabara ya BRT unaoendelea sehemu mbalimbali jijini. Tunafuatilia Kinikia hili kujua endapo sanamu hio itarejeshwa tena eneo hilo au la.
Sanamu hiyo, iliyokuwa penye kitovu cha jiji la Dar es Salaam mahali ambapo mitaa ya Samora na Azikiwe (zamani: Maktaba) inakutana, ni ya askari katika sare ya kijeshi ya King's African Rifles wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) akishika bunduki yenye sime nje huku ikiwa inaangalia upande wa baharini.
Sanamu hiyo ni moja kati ya tatu zilizochongwa huko London na mchongaji James Alexander Stevenson kama kumbukumbu ya askari na wapagazi Waafrika waliopiga vita hivyo katika Afrika ya Mashariki hasa kati ya Uingereza na Ujerumani ambao wengi wao walikufa. Zilipelekwa Nairobi, Mombasa na Dar es Salaam. Hii ya Dar es Salaam ilisimamishwa mwaka 1927.
Chini yake pana maandishi ya kumbukumbu kwa Kiingereza na Kiswahili kilichoandikwa kwa herufi za Kiarabu na pia kwa herufi za Kilatini kama yafuatayo:
"Huu ni ukumbusho wa askari Waafrika wenyeji waliopigana katika Vita Kuu na ni ukumbusho pia kwa wapagazi ambao walikuwa miguu na mikono ya majeshi. Ni ukumbusho pia kwa watu wote waliotumika wakafa kwa ajili ya mfalme na nchi yao katika Afrika ya Mashariki kwenye Vita Kuu toka mwaka 1914 mpaka 1918 . Ukipigania nchi yako ujapo umekufa watoto wako watalikumbuka jina lako."
Sanamu hii ilichukua nafasi ya ingine iliyosimkwa mwaka 1909 kwa kumbukumbu ya meja Hermann von Wissmann, gavana wa pili wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, ambayo ilibomolewa na Waingereza walipoteka Dar mwaka 1916.