China kwa sasa inageuza soko lake kuwa chachu ya ushirikiano, hali ambayo inaonekana ni tofauti kabisa na nchi za magharibi ambazo zinatoa mapendekezo yanayoambatana na masharti kemkem.
Nchi za Afrika zimekuwa zikijiuliza kwa muda mrefu, ya kwamba ni nani hasa anayefungua soko lao, kwa masharti gani na kwa kasi gani? Mapema mwezi Februari, China ilitoa jibu wazi lisilohitaji tochi wakati iliposema kwamba kuanzia Mei 1, haitatoza ushuru wowote kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi 53 za Afrika ambazo zinadumisha uhusiano wa kidiplomasia nazo.
Kwa miaka mingi, serikali za nchi za magharibi ziliahidi kufikiria upya ushirikiano wao na wenzao wa Afrika, zikitoa maneno matamu ya kuzishawishi nchi hizo kuhusu usawa kwenye mifumo tata ya biashara. Hata hivyo China imechagua njia tofauti kabisa. Imegeuza soko lake kuwa chachu ya ushirikiano. Kwa mataifa mengi ya Afrika, njia hii ni thabiti zaidi kuliko makubaliano yoyote ya nchi za magharibi.
Matokeo yake mjadala katika miji mikuu ya nchi za Afrika unabadilika sasa. Badala ya kujiuliza kama wajiunge na China au Magharibi katika ushindani wa siasa za kijiografia, maafisa wanafanya hesabu rahisi kabisa yaani mshirika gani anayepunguza vizuizi halisi vya mauzo ya nje, anayesaidia kubadilisha uchumi na kuichukulia Afrika kama mshirika mkubwa wa kibiashara badala ya kuonekana kama eneo la mradi tu? Katika vipimo hivyo, China inaonekana msingi wa aina tofauti ya uhusiano.
Hatua hii ya Beijing inapaliliwa na makubaliano mbalimbali ya ushirikiano baina ya China na Afrika yaliyofikiwa huko nyuma. Viongozi wa China walitoa ahadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na katika vikao vya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), lililoanzishwa mwaka 2000, kupanua huduma za kutotoza ushuru kwa bidhaa za Afrika na kufanya uhusiano wa biashara kuwa na usawa zaidi.
Hatimaye ilipofika mwaka 2025, China ilitangaza habari njema kwa nchi za Afrika kuwa itaondoa ushuru kwa karibu bidhaa zote kutoka Afrika ikitoa jibu zuri juu ya mvutano wa biashara duniani. Hatua hii ya ushuru sifuri kwa nchi 53 inaonekana zaidi kama kuongeza kasi na uimarishaji wa ajenda hiyo.
Takwimu za biashara ya pande mbili zinaelezea waziwazi kwa nini Beijing imenuia kwenda mbali zaidi. Katika miezi minane ya kwanza ya mwaka 2025, biashara kati ya China na Afrika iliongezeka kwa asilimia 15.4 hadi dola bilioni 222 za Marekani. Bidhaa zinazoagizwa na China barani Afrika ni mafuta kutoka Angola, shaba kutoka Zambia, na cobalt kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na kahawa, chai, matunda na bidhaa zilizotengenezwa kutoka kwa wauzaji wa Afrika. Wakati huohuo China inauza nje kuanzia mashine na magari hadi vifaa vya mawasiliano na bidhaa za walaji.
Katika ulimwengu ambao umekuwa na simulizi nyingi za ushindani juu ya thamani na mifumo, hoja inayoshawishi zaidi mara nyingi inakuwa rahisi zaidi. Beijing imechagua kusema: soko hili hapa, na sheria zetu hizi hapa na kuanzia mwezi Mei, ushuru hautakuwa kikwazo kama ilivyokuwa hapo awali.
Wahenga wanasema “hayawihayawi mwisho huwa”, Kenya ikiwa imeazimia kuchangamkia fursa hii ya ushuru sifuri iliyotolewa na China, wiki kadhaa zilizopita, shehena ya kwanza ya bidhaa zake zitakazonufaika na sera hiyo tayari zimesafirishwa zikipitia bandari ya Mombasa kuelekea China kwa njia ya baharini. Kabla ya hapo, Kenya ilifanya maonesho ya bidhaa za Kenya zitakazonufaika na sera hii mjini Nairobi, ambapo makampuni 25 ya Kenya kutoka sekta mbalimbali yalionesha bidhaa zao zimepata ruhusa ya kuingia kwenye soko la China bila ushuru.
Kwa mataifa ya Afrika yanayoweka uwiano wa mahusiano mengi, uwazi wa namna hiyo ni vigumu kuupuuza. Katika enzi iliyogubikwa na sintofahamu, China ni moja ya nchi chache zinazoweza kukuwekea pendekezo lenye mashiko mezani. Kwa watu wengi barani Afrika, jambo hilo lina maana zaidi kuliko kusubiri ahadi za Magharibi zisizojulikana zitatimizwa lini.