Jumamosi ya Septemba 04, 2021 Msemaji Mkuu wa Serikali alizungumza na Waandishi wa habari na kutoa taarifa ya wiki kwa Watanzania. Huu ni ufafanuzi wake kuhusu maendeleo ya miradi yetu mikubwa na ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchini:-
"Yote kwa yote shughuli zote za Serikali zinaendelea vizuri, Serikali inaendelea kugharamia shughuli mbalimbali za kuhudumia Watanzania na miradi inaendelea vyema.
Wiki hii Serikali imefanya malipo ya awali ya bilioni 212.959 kwa ajili ya ndege zingine 5 ambazo Serikali imeagiza. Serikali imefanya malipo ya bilioni 50 wiki hii kwa ajili ya mradi wa reli, malipo mengine ya bilioni 50 kwa mradi wetu wa kufua umeme kule Julius Nyerere, imetoa bilioni 20 kwa ajili ya elimu bure, kwenye mfuko wa barabara wiki hii Serikali imetoa bilioni 55.4 kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa barabara. Umeme vijijini mpaka mwezi Disemba 2022 tunataka tumalize kabisa kila Kijiji kiwe na umeme na tayari wiki hii Serikali imetoa bilioni 25 kwenda REA kwenye mradi wa umeme vijijini na mijini, ununuzi wa nafaka kwenye mahindi na mazao mengine. Serikali imetoa bilioni 14 kwa NFRA kwa wakala wa hifadhi ya chakula na bilioni 5 kwa Bodi ya mazao mchanganyiko ili kununua mazao ya Tanzania.
Zaidi Serikali iliahidi, badala ya madiwani kulipwa posho zao kupitia Halmashauri, sasa zitalipwa kutoka hazina na tayari Serikali imetoa bilioni 1.686 kwa ajili ya kulipa posho na mishahara ya madiwani. Kwahiyo mambo yanakwenda na hakuna kilichoharibika na Watanzania tuendelee kuunga mkono Serikali yetu mambo yanakwenda vizuri msiwe na wasiwasi na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan anawahakikishia kwamba mambo yanakwenda vizuri. Tuchape kazi, tujenge nchi yetu na tulipe kodi.
#KaziInaendelea.