MAPEMA wiki hii vyombo vya habari viliandika habari za kukwama kwa wanafunzi wa Kitanzania waliokwenda nchini Ukraine katika bara la Ulaya kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu katika fani mbalimbali.
Safari hii, habari hizo zilihusu wanafunzi hao kujisalimisha katika ubalozi wa Uingereza katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev baada ya kuhangaika kwa zaidi ya miezi sita wakitafuta fedha kwa ajili ya kujikimu pamoja na kulipa ada katika vyuo wanavyosoma.
Hii si mara ya kwanza kwa vyombo vya habari kuripoti juu ya kukwama kwa wanafunzi hao, baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuwakana, ikisema haina mkataba nao na kwamba walikwenda katika nchi hiyo bila kufikia makubaliano yoyote ao.
Lakini wanafunzi hao wamekuwa wakisisitiza kwamba waliondoka nchini kwenda Ukraine baada ya makubaliano na Bodi ya Mikopo pamoja na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwamba wangetumiwa fedha hizo baada ya kufika huko.
Wanafunzi hao wanadai kuwa ni kutokana na makubaliano hayo ndiyo maana waliamua hata kutumia nauli kutoka mfukoni mwao kwenda Ukraine kwa ajili ya kuwahi masomo, wakiamini kuwa huku nyuma, Bodi ya Mikopo ingeendelea kushughulikia mikopo yao na kisha kuwatumia fedha kupitia akaunti zao.
Vijana hao wa KItanzania wapatao 29, walipata kibali cha kukopeshwa fedha za masomo nchini Ukraine katika mwaka 2005/2006, lakini kutokana na matatizo yaliyokuwapo wakati ule, walishindwa kwenda katika vyuo walivyoomba na kupata nafasi.
Wao wanadai kuwa baada ya kukosa masomo katika muhula huo, waliwasiliana na Bodi ya Mikopo na wakakubaliana kuwa waanze masomo katika muhula wa mwaka 2006/2007 kwa kuwa maombi yao ya mikopo yalikwisha kukubaliwa na Bodi ya Mikopo na kwamba wangetumiwa fedha zao mara baada ya kufika huko.
Lakini Bodi ya Mikopo imewakana kabisa wanafunzi hao ikisema kuwa kila mwaka, Bodi hiyo imekuwa ikiingia mikataba mipya na wanafunzi wanaoomba kwenda kuanza masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Bodi inadai kuwa maadam wanafunzi hao hawakwenda kuanza masomo katika muhula waliokubaliana katika mkataba, basi mikataba yao inahesabaika kuwa imeharibika na hawamo katika bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wanaotakiwa kuanza masomo katika mwaka 2006/2007.
Mbaya zaidi ni kwamba bodi inataa kabisa kuwa na mawasiliano na wanafunzi hao kabla ya kuondoka hapa nyumbani kwenda Ukraine kwa ajili ya kuanza masomo ya elimu ya juu.
Matokeo yake, tangu wafike huko, wanafunzi wamekuwa wakitumia muda mwingi kuhangaika mahali pa kula, huku wakisumbuliwa na utawala wa vyuo husika kwa kuwa wote hawajalipa ada. Ilifika mahali wanafunzi hao wakawa wanashinda mitaani kujaribu kupata fedha za kujipatia mahitaji muhimu, ikiwamo chakula.
Hata wizara pia imeshindwa kulitolea ufumbuzi tatizo hilo na hadi sasa haijulikani serikali inafanya nini ili kuwasaidia wanafunzi hao angalau waweze kurejea nyumbani baada ya kufukuzwa katika vyuo vyao kutokana na kukosa ada.
Ndiyo maana mwishoni mwa wiki, wazazi wa watoto hao walikutana jijini Dar es Salaam na kumwomba Rais Jakaya Kikwete aingilie kati suala hilo ili ama wanafunzi wapewe kopo huo, au aserikali ifanye utaratibu wa kuwarejesha nyumbani.
Tunachukua nafasi hii kuungana na wazazi wa wanafunzi hao ambao bado wamejisalimisha katika ubalozi wa Uingereza mjini Kiev. Tunasema hivyo kwa kuwa vijana hao walikwenda huko kwa ajili ya kupata elimu ambayo kwa bahati mbaya wameikosa.
Kwa watu walioishi maisha magumu kiasi hicho katika nchi ya kigeni, ni wazi wamepata mateso ambayo pengine hawajawahi kuyashuhudia maishani na kuna uwezekano mkubwa wakaanza kujishughulisha na vitendo viovu ikiwamo biashara ya dawa za kulevya au hata ujambazi.
Tunaamini kwamba ni jukumu la serikali kuwasaidia raia wake waliokwama ugenini kama ilivyo kwa vijana hawa ambao walifuata taratibu zote za uhamiaji kabla ya kuingia katika nchi hiyo na kwamba mateso waliyoyapata yanatokana tu na taratibu za kirasimu ndani ya serikali yetu.