Bila ya shaka inawezekana wewe kama watanzania wengine wengi, umeshindwa kuelewa ni nani anasema kweli kati ya vijana hawa 29 na serikali. Kutokana na mazoea yetu ni vigumu kwa watu kuwaamini watu wa kawaida na ni rahisi kuamini viongozi wa serikali. Mara nyingi tumezoea kuwa kiongozi akisema kitu basi tunachukulia (assume) kuwa ni cha kweli. Inakuwa rahisi zaidi kuamini serikali hasa kama anayetoa kauli ya uamuzi ni Rais, Waziri Mkuu au Waziri fulani. Hivi sasa kuna watanzania ambao hawaelewi kama serikali imewetelekeza vijana hawa au vijana wamejitakia wao wenyewe. Binafsi najikuta napigana vita ya Daudi na Goliathi kwani nimebahatika kupata habari toka pande zote nne, wanafunzi, serikali, vyuo, na wazazi. Na pia nimepata habari toka wa mawakala wa vijana hawa wa Tanzania na kule Ukraine.
Habari hizi siyo kazi kuzipata zinahitaji muda tu na mtu kujituma. Inasikitisha kuwa siyo Rais, Waziri au Mbunge aliyelipa uzito unaostahili kiasi cha kuamua kutafuta ukweliwake na kufuatilia bila kusoma magazetini. Ninapoendelea kuwaombea ufadhili vijana hawa, nikijua utata uliojaa miongoni mwa watu najikuta tena nasukumwa kujaribu kulieleza jambo hili kwa kina na hasa kwa wasikilizaji na wale ambao mko kwenye mailing list yangu. Niyaweke mambo yafuatayo wazi na kutoa utata wowote.
Je vijana hawa walipatiwa mikopo ya kwenda kusoma Ukraine?
a. Hakuna barua iliyotumwa kuwaambia vijana wamepatiwa mikopo ya bodi ya elimu kwenda kusoma Ukraine. Hata hivyo, majina ya waliopata mikopo 2005/2006 kwenda kusoma Ukraine (wakiwemo vijana 29) yalikuwepo kwenye website ya bodi hadi yalipoondolewa hivi karibuni. Majina hayo yalipotangazwa kwenye batch 6, 7, 8 yaliorodhesha kiasi cha mikopo walichopewa na wapi walikuwa wanaenda kusoma. Orodha ya walioshinda mikopo hiyo ipo bodi na wizarani, hivyo serikali wanayo. Vijana hawa walipewa mikopo na hilo halina mjadala.
Mbona serikali imesema vijana walijienda huko Ukraine wao wenyewe kivyao vyao?
b. Serikali inazungumzia suala la "wanafunzi kuondoka" na hata mara moja haijazungumzia kama walipatiwa mikopo au la. Hoja ya wanafunzi ni kuwa walishakubaliwa mikopo (angalia hiyo "a" hapo juu) kwenda kusoma. Kama walikubaliwa mikopo tayari na fedha zilikuwepo, na vijana hao hawakutumia mikopo hiyo ya 2005-2006 pesa hizo zilienda wapi na zilitumiwa na nani? Sasa ni kweli kuwa vijana hawa waliondoka "wenyewe" kwa maana ya kuwa walinunua tiketi wao wenyewe baada ya kuhakikishiwa kuwa mikopo yao (waliyokwisha kukubaliwa) iko njiani na hivyo wasiendelee kuchelewa (walikuwa wameshachelewa mara moja)
Je vyuo vikuu viliwatambua vijana hawa na ya kuwa walidhaminiwa na bodi hadi vikawapa nafasi?
c. Tunafahamu na ushahidi niliweka hapa
http://www.jambophotos.com barua toka Chuo Kikuu cha Kharkov waliandikia bodi na wizara kuwahakikishia kuwa kutokana na vijana kucheleweshwa kuja chuoni mwaka huo, nafasi zao zitashikiliwa hadi Septemba mwaka jana (kwa maana hawahitaji kutafuta nafasi upya). Barua toka vyuo vikuu ilitumwa Februali mwaka 2006. Katikati ya mwaka jana bodi ikabadlisha vigezo na utaratibu wa utoaji mikopo (kama walivyofanya tena mwaka huu). Vijana wakaenda kwenye bodi na kuulizia kama mabadiliko hayo yataathiri safari yao. Wakahakikishiwa kuwa mabadiliko ya 2006 hayakuwahusu wao (ingeshangaza kama yangewahusu wakati wao walishakubaliwa mikopo. Huwezi kutunga sheria itakayomuadhibu mtu kwa kwa kosa ambalo kabla ya sheria hiyo halikuwa kosa). Wakahakikishiwa na Bw. Mbegu na wenzake kwa mdomo kuwa mikopo yao haina tatizo wao wakipata tiketi waondoke. Wanafunzi 41 kati ya 65 waliondoka Tanzania kwenda kwenye masomo Ukraine. Barua toka Kharkov ipo Wizarani na kwenye Bodi.
Sasa vijana hawa 41 waliweza vipi kupata pasipoti bila kuonesha wanaenda wapi na kwanini? Kama walikuwa wanaenda vyuoni si lazima wangekuwa na barua za mdhamini?
d. Kabla ya kuweza kuondoka vijana walitakiwa kupata pasi za kusafiria. Huwezi kupata pasipoti Tanzania hadi uoneshe ni wapi unakwenda. Vijana hawa katika kuomba pasi zao vijana waliandikiwa barua za kukubaliwa vyuoni na bodi kuonesha ndio wadhamini. Barua hizi ziko (bado ziko???) uhamiaji na ndiyo zilizowezesha vijana kupatiwa pasi. Serikali inajua hilo na wanalojibu.
Vipi kuhusu zile Visa?
e. Ukraine haina ubalozi Tanzania na ubalozi unaotumika ni ule wa Nairobi. Pasi za wanafunzi zilikusanywa na kupitishwa ubalozi wa Tanzania Kenya kwenda kwa ubalozi wa Ukraine ili zigongewe Visa. Huwezi kupata Visa hadi uoneshe wapi unakwenda na udhamini wako ni upi. Ubalozi wetu na ule wa Ukraine wote walijua wazi kutokana na vielelezo vilivyoambatanishwa mdhamini wa vijana ni bodi, vinginevyo serikali ieleze ilikuwaje Ubalozi wetu kupitisha pasipoti zaidi ya 40 kwenda kwa ubalozi wa Ukraine bila ya wao kutambua hawa vijana wote ni kina nani, wanaenda wapi? Serikali inajua hili na wanalojibu.
Mbona tuliambiwa wanafunzi 17 walikubali maelekezo ya serikai na "wakaamua" kusoma nyumbani na mikopo yao ikahamishiwa katika vyuo vya nyumbani?
d. Kutokana na (c) hapo juu kati ya wanafunzi wote 29 , 2 walitangulia (ambao sasa wanalipiwa na serikali) wale 27 wengine walienda na ndege moja na kwa taratibu za Chuo cha Kharkov ni lazima uwe na tiketi inayoonesha kurudi pia vinginevyo hawakuruhusu kuingia
Return Ticket a Must. Hivyo hao 27 waliweza kuingia na kupokelewa vyuoni ikieleweka wazi kuwa bodi ya mikopo ndio wadhamini. Kumbuka kuwa hawa sio wanafunzi pekee wa kitanzania vyuoni hapo na mpango wa malipo ya shule haukuwa tofauti na wa wanafunzi waliotangulia. Wanafunzi 12 kati ya wale 17 waliweza kuondoka lakini walirudishwa kule kule Kiev baada ya tiketi zao kutoonesha "kurudi". Balozi Chokala alitumia ushawishi wote kuwasaidia ilishindikana. Hawa walirudi Tanzania na mikopo yao ikahamishiwa Tanzania na wanasoma kwenye vyuo vya Tanzania pamoja na wale wenzao 5. Hawa ndio 17 aliowazungumzia Gesimba kama na wao wangefanikiwa kuingia tungekuwa tunazungumzia vijana 41 waliokwama Ukraine!! Serikali inafahamu hilo na inajua hilo, na wanalo jibu.
e. Kutokana na (d) hapo juu hawa wanafunzi 17 waliporudi Tanzania hawakuomba mikopo upya kwani walishakubaliwa mwaka 2005-2006 (wakati ule ule na wale 29) na wenyewe walianza masomo hivyo hivyo kwa kuchelewa. Majina yao na vyuo vyao ninayo na nimeshayaweka hapa hadharani. Kama serikali iliweza kutumia mikopo ya 2005/2006 kuwasomesha vijana hawa hapo nyumbani bila kuhitaji waombe tena mikopo, iweje wale waliokwishaondoka wakataliwe na kutakiwa kuomba tena mikopo? Wale walioko Ukraine 3 walishaanza kupokea mikopo yao licha kuondoka wakati ule ule, kwa makubaliano yale yale na ahadi ileile na wale 26, majina yapo na nimeyaweka hadharani. Serikali ilitumia vigezo gani kuwalipia hawa 3 na kuwaacha hawa 26? Serikali inafahamu na inalojibu.
f. Serikali imedai kuwa "waliwashauri" vijana hawa wasiende huko kwa vile haina pesa (kumbuka walishakubaliwa mikopo-pesa zilikuwepo!). Hakuna wakati wowote serikali (wizara na bodi) iliwaandikia vijana au familia zao kabla ya kuondoka na kuwataka wasiondoke au kuwaambia wakiondoka basi hilo lwao. Hakuna barua, hakuna tangazo, hakuna taarifa kwa vyombo vya habari wala nini! Kama waliwaambia kwa mdomo tu bila kuwaandikia tutaamini vipi kuwa hawakuwambia kwa mdomo watangulie? Kumbuka serikali imesema "haiwatambui" baada ya vijana kufika na kuanza masomo Ukraine na baada ya mabadiliko ya 2006. Kabla ya hapo bodi wamekutana nao wamewasaidia kupata pasi na visa, na wakawahakikishia kuwa mabadiliko ya 2006 hayawahusu.
Mbona Rais amesema serikali haisomeshi wanafunzi tena nje kwani ni ghali na kuwasomesha huko ni sawa na kusomesha wanafunzi watatu nyumbani?
g. Kuhusu suala la serikali kuwasomesha wanafunzi nje, hili nalo ni kichekesho. Kama kweli serikali haina pesa za kuwasomesha watu, mbona hawajawarudisha wanafunzi wote wa kitanzania ambao wanasoma kwenye vyuo vya nje? Hapo Ukraine kuna wanafunzi wengine zaidi ya 80 wanaolipiwa fedha na serikali na hivyo ninavyozungumza wamepokea fedha zao siku ya jumanne na jumatano kupitia ofisa wa Ubalozi wetu Moskow Bw. Francis. Kama kweli serikali haitaki kusomesha tena nawafunzi nje kwanini wanafunzi hawa wamekubaliwa mikopo kusoma China. Vijana wa Ukraine mikopo yao ilikuwa ni ya dola 3000 kwa mwaka, linganisha na hawa wa wanaosoma China
Mikopo ya Wanaosoma China. Vijana hawa walikubaliwa kiasi cha dola 3000 kwenye mikopo yao wakati wale wanaoenda kusoma Uchina wamekubaliwa mara 3 zaidi, lipi gumu? Wale wanaosoma China kwa mwaka huu unaoisha sasa walikubaliwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia nane, 800,000.000/=! kwa mwaka. Vijana hawa 29 hawahitaji zaidi ya shilingi milioni 70 kwa mwaka!! Kama ni ghali hivyo kwanini wasisitishe mikopo yote ya nje na pale wanapowarudisha hawa 26 (wakifanikiwa) wawarudishe na wale wote wanaosoma US, UK, China, Urusi, India, Libya n.k!!
Kwanini serikali haiko tayari kukiri imekosea na kwa kutumia nguvu zao zote wanaendelea "kuwakana vijana hawa"?
Jibu siyo rahisi kiasi hicho lakini linalotarajiwa. Kwa maoni yangu, and I'll be very frank.
- Kwanza, Rais Kikwete hajaamua kutafuta ukweli bali yuko tayari kusikiliza wasaidizi wake ambao ndio watuhumiwa kwenye sakata hili. Rais anapoandika barua wizarani na kwenye bodi kuwataka wampe maelezo ya kuhusu vijana hawa, barua inamfikia Msolla, Kabaka, Katunzi, Gesimba, Mbegu, na Nyatega, hawa wote watoe jibu gani? Hawa hawana jinsi bali kukaza uzi ule ule yaani "mheshimiwa Rais vijana hawa tuliwaambia wasiondoke wakaondoka na sisi hatuna fedha za kuwasomesha". Kina Msolla na wenzake wanaficha na kutetea ajira zao!!
- Pili, viongozi wa bodi na wizara kama nilivyosema kule kwingine wameapa vijana hawa hawatawashinda, na wako tayari kusema na kufanya lolote lile kuhakikisha hawasomi Ukraine na hata wakirudi wasisome tena (kumbuka vigezo vya kupata mikopo vilibadilishwa pia).
- tatu Rais Kikwete licha ya kujua ukweli huu wote ambao ni rahisi kuupata ameamua kuwatetea wasaidizi wake kwani hayuko tayari kumwajibisha mtu yeyote anayeboronga au kuvuruga maisha ya wananchi. Utawala wa Kikwete kama iliyomtangulia ni rahisi kusema "tunathamini elimu" na wanapiga vita ufisadi lakini shoka likiwekwa kwenye mpini hawawezi kuukata mti! Rais Kikwete kama viongozi waliomtangulia hana nia, sababu, uwezo, na kusudi la kuhakikisha viongozi waliochini hawanyanyasi wananchi au kuwaonea. Pale wizarani kuna watu wamekaa kwenye "viti vyao vya enzi" kwa zaidi ya miaka kumi wakiendelea na biashara yao ya "elimu ya juu" huku wakiandika mikopo kwa wanafunzi hewa, huku mawakala wao walioko Urusi na Ukraine wakikata hizo fedha na kuzirudisha Tanzania. Ninapowaandikia hivi, kuna racket kubwa ya fedha za elimu ya juu inayowahusisha maafisa wa ngazi za juu wa wizara hiyo.
- Watu na waandishi kwa ujumla wamefikia mahali pa kuamini kuwa Rais wa Tanzania hadanganyi au hana uwezo a kudanganya, kuongopa au kulaghai. Watu wengi wanapomsikiliza Rais wanafikiri wanamsikiliza mfalme na hivyo neno lake ni amri, na matakwa yake ni sheria. Rais kasema "wameondoka wenyewe" so that settles it! bahati mbaya kwao, tupo watu kama sisi ambao tunaweza kunusu harufu ya uozo toka mbali.
Alichosema Rais hakina ukweli hata chembe na yeye na wasaidizi wake wanajua. Wametegemea kuwa kwa vile Rais kasema basi yote yatafikia mwisho. Rais aliposema watu hawali mapanki, tulitakiwa kunyamaza, aliposema silaha haramu hazipitishwi Tanzania tulitakiwa kunyamaza, aliposema tumwache Mkapa astaafu kwa amani, tumetakiwa kunyamaza, aliposema umeme utapatikana kwenye miezi miwili na ikapita tulitakiwa kunyamaza, aliposema ukame wetu ni mapenzi ya Mungu tulitakiwa kunyamaza, aliposema tutadai pesa zetu toka serikali ya Uingereza kwa kuachilia kampuni "yao" watutapeli, tulitakiwa kunyamaza, na sasa amesema "nimeambiwa wanafunzi waliondoka wenyewe na serikali haikuhusika" tunatakiwa kunyamaza!!!
Uamuzi ni wenu, lakini ningekuwa na uwezo na suala hili badala ya kususa wanafunzi na kukaza uzi ningechukua tahadhari.
a. Ningewasimamisha viongozi wa bodi na kuunda tume ya huru ya uchunguzi itakayosimamiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, ikiwa na wajumbe toka taasisi muhimu huru na isiyo na Mbunge au kiongozi yeyote wa kisiada ili kutafuta ukweli.
b. Wakati tume inafanya kazi, ningehakikisha deni la watoto hawa kwanza linashughulikiwa na wanaishi kwa amani bila hofu ya kupoteza nafasi zao au kufikishwa mahakamani.
c. Endapo inagundulika vijana "hawakuelewa" au walikosea kitu fulani, basi badala ya kuwarudisha tunahakikisha kosa kama hilo halitokea tena na wanaendelea na masomo baada ya kujaza fomu au chochote ambacho hawakukamilisha.
d. Endapo itaonekana kuna uzembe kwenye wizara na bodi wale wote wahusika wanafukuzwa kazi kudanganya na kuhataratisha maisha ya vijana wa kitanzania kama fundisho na wakati huo huo kuwaomba radhi vijana hawa na kuwaacha waendelee na masomo pasipo upungufu wowote ule.
e. Kuhakikisha suala kama hili halitokei tena.
Hata hivyo nina uhakika serikali haitabadili msimamo wake hata tukiweka kila kitu hadharani na nyaraka zote hadharani... wameshasema wao ni nani hata wabadili kauli zao? Rais kasema nani atamfanya abadilike..! Mfalme ameshaamuru nani atamhoji? Na watanzania tumeamua kukaa kimya isipokuwa sauti dhaifu za watu wachache. Ndugu zangu tuwasaidie vijana hawa kwenda shule. Michango yenu inahitajika. Tumebakiwa na very few options, tuliweza kuwashawishi shule kuwaombea muda hadi tarehe 10 ya mwezi huu. Sijui nini kitatokea. Lakini nitaisikitikia nchi yangu kwa kitendo hiki, na binafsi sitawasemehe, na nitahakikisha kuwa siku moja watalipa. Haiwezekani watu wachache watawale nchi kama wafalme au wana wa wafalme!