Seti 2 za treni ya kisasa inayotumia nishati ya umeme - EMU (Electric Multiple Unit) na vichwa 8 vya treni ya umeme vimewasili tanzania kutoka Korea Kusini.
Serikali kupitia TRC ilifanya manunuzi ya seti 10 za treni za EMU zinazotengenezwa na kampuni ya Hyundai Rotem Korea Kusini, seri moja ua EMU ina jumla ya mabehewa 8, yakijumuisha kichwa kimoja mbele na kingine nyuma ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 589 na kutembea kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa.
Seti mbili za EMU zinafikisha idadi ya seti tatu zilizowasili nchini mpaka sasa, seti ya kwanza iliyowasili mwezi April 2024 inaendelea na majaribio.
Shirika la Reli Tanzania limeshapokea jumla ya mabehewa 65 ya abiria, vichwa 17 vya umeme na seri 3 za EMU. Upokeaji wa vifaa vya uendeshaji vya reli ya kiwango cha SGR unaendelea kwa awamu tofauti, vifa vipya vinavyowasili vitaendelea kufanyiwa majaribio kwaajili ya kujiridhisha kabla ya kuanza kutoa huduma.
Shirika linaendelea na uendeshaji wa awali na utoaji huduma ya usafiri wa treni za umeme kupitia reli ya kiwango cha kimataifa kati ya Dar es Salaam na Morogoro, uendeshaji rasmi kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma unatarajiwa kuanza Julai 25, 2024.